Ziara Ya Madiynah
Muhammad Faraj Salem Al Saiy
Ziara ya Madiynah ni jambo linalopendeza
sana. Kwa kawaida Mahujaji na wafanyao ‘Umrah huuzuru
mji huu mtukufu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
kabla au baada ya kwenda Makkah.
Hata hivyo kuna baadhi ya watu wanaojaribu kupunguza umuhimu wa ziara ya mji huu mtukufu kwa kuwaambia watu kwa mfano:
“Ukihiji bila ya kwenda Madiynah
Hijjah yako inakubaliwa", au
“Ziara ya Madiynah haihusiki na Hijjah", au
“Haina lazima kwa mwenye kuhiji kwenda
Madiynah", n.k.
Ingawaje maneno kama
hayo ni ya kweli, na kwamba mtu akienda Makkah na kutimiza shughuli za Hijjah
bila ya kwenda Madiynah, Hijjah yake huwa imekamilika na haina shaka yoyote na
inakubaliwa, lakini maneno hayo yanaleta maana ya kuwakimbiza watu mbali na mji
huo mtukufu ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
alikuwa akiupenda sana na kuutukuza.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
amesema:
((Madiynah ni mji mtukufu kuanzia (jabali) Ayrin mpaka (jabali)
Thawr.))
Haya ni majabali mawili, mojawapo lipo mwanzo wa Madiynah na la
pili lipo mwisho wa Madiynah.
Na akasema:
((Hakika Ibraahiym
ameutukuza mji wa Makkah na akauombea du’aa, na mimi
nautukuza mji wa Madiynah kama alivyoutukuza Ibraahiym mji wa Makkah. Mola
wangu mimi naitukuza ardhi (yote ya Madiynah) iliyo
baina ya majabali yake (Ayrin na Thawr), usikatwe mti wake na pasitendeke
maasi. Atakayetenda maasi katika mji huu, atapata laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika wake na ya watu wote kwa ujumla.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Wakati fulani palikuwa na shida kubwa sana hapo Madiynah na vitu
vikapanda bei na kuwa ghali kupita kiasi. Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema kuwaambia watu wa
Madiynah:
((Nakupeni
bishara njema. Mimi nimekubarikieni katika vibaba vyenu na katika magao yenu, chakula cha (mtu) mmoja kitawatosha
wawili, na cha wawili kitawatosha wanne, watano au sita. Kwa hivyo jikusanyeni
katika chakula kwa sababu baraka imo katika mkusanyiko
wa jamii. Atakayesubiri katika shida za mji huu (Madiynah) nitamuombea shifaa
siku ya Qiyaamah, na atakayeweza kufa katika mji huu,
basi afe, kwani mimi nitakuwa mwenye kumuombea shafa’ah siku ya Qiyaamah.)) [Imepokewa na
At-Tabaraaniy]
Hii ndiyo sababu
iliyomfanya Sayyiduna ‘Umarbin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) apende
kuomba du’aa ifuatayo:
“Mola wangu, mimi nakuomba nife shahidi katika njia yako na katika mji wa
Mtume wako (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)”. [Imepokewa na
Al-Bukhaariy]
Du’aa zote mbili hizo
za ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) zimekubaliwa, maana aliuliwa shahidi akiwa
anaswalisha Swalah ya Alfajiri ndani ya Msikiti wa
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na akazikwa
Madiynah tena karibu na kaburi la Sahibu yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam).
Hizi ni baadhi tu ya sifa mbali mbali za mji huu mtukufu ambao
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiupenda
sana.
Pana kundi
jengine ambalo hupindukia mipaka katika kuitukuza ziara ya mji huu mtukufu. Kundi hili
huwatuhumu wasiouzuru mji huu mtukufu kuwa wamemuasi Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wakitegemea Hadiyth zisizo
sahihi (Hadiyth Maudhu’i).
(Hadiyth Maudhu’i - ni zile ambazo Maulamaa wa fani hii wamezigunduwa kuwa ni
Hadiyth zilizopachikwa, zisizo za kweli na hazina asili wala msingi wowote.)
Mfano wa Hadiyth wanazozitegemea ni hizi zufuatazo:
Wanasema kwamba eti
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam) amesema:
“Atakayehiji na
asinizuru ameshaniasi.” au
“Atakayehiji na akalizuru kaburi langu baada ya kufa kwangu anakuwa mfano
wa aliyenizuru nilipokuwa hai”.
Zipo
Hadiyth nyingi za mfano huu.
Ni haramu kumsingizia
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam) uongo, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametoa onyo kali kwa
kila anayemsingizia uwongo aliposema:
((Atakayenisingizia
uongo makusudi, basi keshajitayarishia makazi yake Motoni.))
Hapana sababu yoyote
ya mtu kutumia hoja kama hizo katika kuithibitisha
Ibada ya aina yoyote ile. Isitoshe zipo hoja zenye nguvu kuliko hizo
zinazotegemea Hadiyth zilizo sahihi zinazotilia nguvu ziara ya mji huu mtukufu wa Madiynah.
Ziara Ya Msikiti
Kwanza
kabisa itabidi tusahihishe itikadi yetu kuhusu ziara ya mji huu mtukufu katika
kutia niyyah ya Ziara.
Nia ya ziara ya Mji wa Madiynah, inatakiwa iwe ni kuuzuru Msikiti wa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na isiwe kulizuru kaburi
lake, kama wanavyotia nia hiyo baadhi ya watu. Ingawaje kuzuru makaburi kwa niyyah ya kuwaombea maiti na kujikumbusha Akhera ni
jambo jema, lakini kufunga safari ndefu kwa ajili hiyo haijuzu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
amesema:
((Isifungwe safari
ndefu (kwa
ajili ya ibada) isipokuwa kwenda katika Misikiti mitatu; Al-Masjidul
Haraam (Makkah), na Msikiti wangu huu (Madiynah), na Msikiti wa Ilyaa (Baytul
Maqdis).)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na wengineo]
Na akasema:
((Swalah katika Msikiti
wangu ni bora kuliko Swalah elfu katika Misikiti
mingine, na Swalah katika Msikiti wa Makkah (Masjidul Haraam) ni bora mara elfu
mia kuliko Misikiti mingine.)) [Imam
Ahmad bin Hanbal]
Mwenyezi Mungu huumba na kuchagua atakavyo. Ametuchagulia sayari ya ardhi miongoni
mwa sayari zote kuwa ni mahali petu pa kuishi, na Akamchagua mwanadamu miongoni
mwa viumbe vyote Akamtukuza, kisha Akawachagua Mitume (‘Alayhimus Salaam)
miongoni mwa binadamu wote na kuwatukuza, na Akamchagua Muhammad (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ni Imaam wa Mitume yote, na Akaichagua Misikiti
katika ardhi kuwa ni mahali patukufu kupita sehemu zote, kisha Akaichagua
Misikiti hii mitatu kuwa ni mitukufu zaidi miongoni mwa Misikiti yote, na Yeye
ndiye Anayeumba na kuchagua na sisi jukumu letu ni kufuata tu. Kwa sababu
Anayeumba ndiye Mwenye kujua na si aliyeumbwa.
Mwenyezi Mungu
Anasema:
{{Na Mola wako huumba
atakavyo na huchagua (atakavyo); Hawana (viumbe)
hiari; Mwenyezi Mungu Ameepukana na upungufu, na Ametakasika na hao
wamshirikishao (naye).}} [Al-Qasas: 68]
Bustani Katika Bustani
Za Peponi
Hapana Hadiyth sahihi
isemayo; "Baina ya Kaburi langu na mimbari
yangu bustani katika bustani za Peponi." Bali Hadiyth iliyo
sahihi ni ile iliyopokelewa na Imam Al-Bukhaariy na Muslim na At-Tirmidhiy na
An-Nasaiy na Imaam Ahmad inayosema kuwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu)
amesema, kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Baina ya NYUMBA yangu na Mimbari yangu, bustani katika bustani za Peponi”
(Bayna BAYTY wa mimbariy, na sio Bayna Qabriy wa Mimbary).
Kwa hivyo itikadi
iliyo sahihi ni kutia niyyah ya kuuzuru Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa sallam) na sio kaburi lake, na hii ni kwa sababu unapofika pale
kaburini na kumswalia na kumsalimia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam),
wewe na aliyepo popote duniani thawabu zenu ni sawa sawa, maana aliye mbali pia
Swalah na Salaam zake zinafikishwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam). Lakini ulichofaidika wewe ni kule kusali
kwako ndani ya Msikiti wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na hasa katika
Ar-Rawdhah Ash-Shariyf, na pia unafaidika na ziara yako katika sehemu nyingine
takatifu za Madiynah.
Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa sallam) amesema:
((Niswalieni,
kwani popote mlipo Swalah zenu ninafikishiwa.)) [Imepokewa na Abu Daawud, Imam Ahmad na At-Tabarani]
Na akasema:
((Mwenyezi Mungu Ana
Malaika wanaotembea ardhini, wananifikishia salaam kutoka kwa
ummah wangu.)) [Imepokewa na An-Nasai,
Ad-Daramiy na Ibni Habban]
Ziara Ya Msikiti
Inapendeza mtu aoge na kuvaa nguo nadhifu, kisha aende Msikitini na kuingia kwa
mguu wa kulia kwa utulivu na unyenyekevu na kusema pale anapoingia:
“A’udhu biLlaahi mina Shaytwaani rajiym, BismiLlaahir Rahmanir
Rahiym Allaahumma Swaliy ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa sallim Allaahumma
gh-firliy dhunuubiy wa ftah liy abwaaba rahmatik.”
Na maana yake ni: Baada ya kusema
A’udhu biLlaah na BismilLaah, kisha unamswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam) na ‘Aali zake na unamuomba Mwenyezi Mungu maghfirah na akufungulie
milango yake ya Rahma.
Ni vizuri unapoingia
Msikitini kwanza uelekee Ar-Rawdhah (sehemu iliyopo baina ya nyumba yake na
mimbari yake ndani ya Msikiti), na kuswali hapo Tahiyyatul Masjid raka’ah
mbili, ukishindwa kwa sababu ya zahma, basi swali sehemu yoyote ile ndani ya
Msikiti, na ukishaswali elekea penye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam) kwa utulivu na kwa moyo mkunjufu, na unapofika penye kaburi lake sema;
“Assalamu ‘Alayka ya RasuulaLlaah wa
RahmatuLlaah wa Barakaatuh!
Na anaweza kuzidisha kwa kusema:
“Swalla Allaahu wa sallam ‘alayka wa
‘alaa asw-haabika, wa jazaaka Allaahu ‘an ummatika khayra, Allaahumma Aatihi
al-wasiylata wal fadhwiylata wa b’ath-hul maqaamal mahmuudal lladhiy wa’adtah”
Na maana yake ni:
“Amani iwe juu yako
ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na rahma za Allaah na
barakah zake.”
“Rahma za Allaah na amani ziwe juu yako na juu ya Maswahaba zako, na akulipe
Allaah kheri wewe na ummah wako, Ee Allaah mpe wasiylah na fadhila na mnyanyue
katika makazi matukufu ambayo umemuahidi”
Kisha unasogea mbele
kidogo na unamsalimia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), aliyezikwa umbali wa
dhiraa moja na kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kisha hatua
moja nyingine unamsalimia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Kwa sababu Maswahaba
wawili hawa (Radhiya Allaahu ‘anhuma) wamezikwa karibu na
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Kisha unaelekea Qiblah
na kujiombea mwenyewe Du’aa na kila unayempenda na
unawaombea ndugu zako Waislamu, kisha unaondoka.
Si vizuri kunyanyua
sauti na kuomba kwa sauti kubwa, unatakiwa uombe kwa
sauti ndogo na kwa moyo mkunjufu, kiasi cha kuweza kujisikia mwenyewe tu. Iwapo
utasoma juu ya ukuta wa nyumba yake (Swalla Allaahu
‘alayhi wa sallam), ambayo sasa ni kaburi lake, utaona kuwa imeandikwa Aayah
isemayo;
{{Ya ayyuha lladhiyna aamanuw Laa tarfa’uw
aswaatakum fawqa swawti Nnabiy.}}
Na maana yake ni:
{{Enyi
mulioamini msipaze sauti zenu kuliko sauti ya Mtume.}} [Suratul-Hujurat:
2]
Sayyiduna
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwahi kuwasikia watu wawili wakipaza sauti zao
mahali hapo, akawaambia:
“Mungelikuwa
nyinyi ni watu wa hapa hapa Madiynah, basi ningelikupigeni bakora.”
Haijuzu mtu kupangusa
mikono yake kwenye kuta za kaburi kisha akajipangusia mwilini pake au kubusu yale mapambo ya kaburi, kama wanavyofanya baadhi ya watu kwa
kutegemea eti wanapata baraka za mahali hapo.
Haya ni katika mambo aliyokataza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
sallam) aliposema:
((Musigeuze kaburi
langu kuwa mahala pa Ibada, na mniswalie popote mlipo,
kwa sababu Swalah zenu ninafikishiwa.))
Kumbuka - Tulivyoamrishwa
ni kumswalia na kumsalimia Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa sallam), na sio kumuomba yeye akuondolee shida zako. Du’aa ni Ibada, na ibada zote zinaelekezwa kwa Mwenyezi Mungu peke
Yake.
Unapomaliza kulizuru
kaburi, omba Du’aa ukiwa umeelekea
Qiblah na umelipa mgongo kaburi la Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa sallam) - Usielekee
kaburini huku ukiomba Du’aa.
Makaburi Ya Baqiy’i
Hakuna ulazima ila
akipenda mtu vizuri kwa wanaume tu, kuyazuru makaburi ya Baqiy’i, mahala
walipozikwa Maswahaba wengi sana (Radhiya Allaahu ‘anhu), pamoja na wake za
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wajukuu zake (Radhiya Allaahu ‘anhu),
na wengi katika waliofuata baada yao, kama vile Imaam Malik na Naafiy’ na wengi
wengineo (Mwenyezi Mungu Awarehemu).
Kumbuka kuwa waliozikwa
hapo wote ni ndugu zako Waislam, kwa ajili hiyo unatakiwa unapoyafikia makaburi
hayo, ufanye kama alivyokuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam),
kwani Mtume wenu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa mara
anapoyafikia makaburi hayo akiwasalimia na kuwaombea Du’aa wote waliozikwa humo
bila ya kubagua. Alikuwa akisema:
“Assalaamu ‘Alaykum ahl ddiyaari minal
muuminin wal muslimiyn, wainnaa in shaa Allaahu bikum laahiquwn. Yarhamu Allaahul mustaqdimina minna wa min-kum wal-muta-akhiriyn. Nas-alu
Allaaha lanaa walakum al ‘aafiyah. Allaahumma laa tuh-rimnaa ajrahum
walaa tuftinnaa ba’adahum, waghfir lanaa walahum”
Ziara Ya Msikiti Wa Qubaa
Unapokuwa Madiynah
unaweza kwenda Msikiti wa Qubaa (Masjid Qubaa) ingawa
si jambo la lazima, Msikiti wa mwanzo ulojengwa na Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa sallam), ambao Mwenyezi Mungu Amesema juu yake:
{{Msikiti uliojengwa juu
ya msingi wa kumcha Mungu tangu siku ya kwanza (ya
kufika kwa Mtume Madiynah) unastahiki zaidi wewe usimame humo. Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa. Na
Mwenyezi mungu Anawapenda wajitakasao.}} [At-Tawbah: 108]
Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kwenda hapo kila Jumamosi, akiwa amepanda
mnyama, na kuswali raka’a mbili. Na alikuwa akisema:
((Mtu akijitahirisha
nyumbani kwake, kisha akaenda Msikiti Qubaa na
akaswali hapo raka’a mbili, huandikiwa thawabu za aliyefanya ‘Umrah.)) [Imepokewa
na Imam Ahmad, An-Nasai, Ibni Maajah na Al-Haakim[
Mashahidi Wa Uhud
Unaweza kuzuru
mashahidi wa Uhud na kuwaombea, na hapo lipo kaburi la ‘ammi yake Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa sallam) Sayyiduna Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ‘Sayyidu
Shuhadaa’, pamoja na Maswahaba wengine (Radhiya Allaahu ‘anhum) waliokufa
mashahidi. ‘Ammi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliuliwa hapo
alipopigwa mkuki katika vita vya Uhud na kuzikwa pale pale alipouliwa.
Kwa vile mahali hapo
pana makaburi mengine, kwa hivyo ni vizuri mtu
kuwatolea salaam waliozikwa hapo kwa kutamka yale yale uliyotamka pale
ulipoyazuru makaburi ya Baqi’i.