KUITANGULIZA
KABLA YA WAKATI WAKE
Kila aliyefunga Mwezi wa Ramadhaan na akawa anamiliki
chakula cha kumtosha kwa muda wa siku moja, inamwajibikia kutoa Zakaatul Fitri,
nayo ni pishi ya tende au pishi ya ngano au pishi ya shaiyri. Anatakiwa atoe
kwa ajili yake na kwa ajili ya kila anayemtegemea kama vile wanawe, wakeze nk.
na kuwapa masikini ili nao wapate kufurahi katika Siku ya Sikukuu.
Kwa vipimo vya kisasa, pishi moja ya mbao iliyokuwa ikitumika
wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni kiasi cha kilo 2.
Zakaa hii ni wajibu kwa kila Muislam mdogo na mkubwa,
mwanamume au mwanamke.
Ibn ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) amefaridhisha kwa kila mtu kutoa Zakaatul Fitri katika mwezi wa Ramadhaan,
pishi ya tende (au) pishi ya shaiyri, ikiwa yeye ni mtumwa au mtu aliye huru,
mwanamume au mwanamke, mdogo au mkubwa miongoni mwa Waislam".
[Al-Bukhaariy na Muslim]
Zakaatul Fitri ilifaridhishwa katika mwezi wa Sha’abaan
mwaka wa pili baada ya Hijra kwa ajili ya kumtwaharisha aliyefunga kutokana na
makosa yoyote yale aliyotenda katika mwezi wa Ramadhaan pale alipokuwa
amefunga, kutokana na mazungumzo ya upuuzi au madhambi, na wakati huo huo Zakaah
hiyo itawafaa masikini na wahitaji ili nao wapate kufurahi pamoja na Waislam
wenzao katika Sikukuu.
Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:
"Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
amefaridhisha Zakaatul Fitri kwa ajili ya kumtwaharisha aliyefunga kutokana na
maneno ya upuuzi au madhambi madogo madogo na ili masikini nao wapate chakula.
Atakayeitoa (Zakaah hiyo) kabla ya Swalah (ya ‘Iyd) inakubaliwa Zakaah yake,
ama atakayeitoa baada ya Swalah (ya ‘Iyd), itahesabiwa kama ni Swadaqah ya
kawaida tu".
Abu Daawuud na Ibn Maajah na Ad-Daaraqutniy
Anayeitoa Zakaah hiyo ni mtu aliyefunga. Anajitolea
yeye mwenyewe, mkewe na watoto wake wanaomtegemea na anawatolea pia wote wale
wanaomtegemea wakiwemo watumishi wake.
Iliyowajibishwa katika Zakaatul Fitri ni pishi ya ngano
au ya shaiyri au ya tende au ya zabibu au ya mchele au ya mahindi na vinginevyo
vilivyo na mfano huo katika vyakula.
Imaam Abu Haniyfah peke yake amejuzisha kutoa pesa
zenye thamani hiyo badala ya kutoa nafaka panapo udhuru.
Ma’ulamaa wengi wamekubaliana kuwa Zakaatul Fitri
itolewe katika Ramadhaan ya mwisho, lakini wamekhitalifiana juu ya wakati
maalum unaowajibika kuitoa.
Wapo waliosema kuwa wakati unaowajibika kuitoa ni pale
jua la Ramadhaan ya mwisho linapozama, na wengine wakasema kuwa wakati wake ni
kuanzia baada ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu.
Kutokana na hitilafu hii tunapata faida ya kuwajibika
kumtolea Zakaah hiyo mtoto aliyezaliwa kabla ya kuingia alfajiri ya siku ya
Sikukuu na baada ya jua kuzama, je mtoto huyo anatolewa Zakaah?
Kwa wale wenye kufuata rai kuwa wakati wa kuitoa Zakaah
hiyo ni pale jua la siku ya Ramadhaan ya mwisho kuzama, mtoto huyo hatolewi
Zakaah kwa sababu amezaliwa baada ya kumalizika wakati wa kuwajibika, na kwa
wenye kufuata rai ya pili, kwa sababu amezaliwa kabla ya wakati unaomwajibika.
KUITANGULIZA KABLA YA WAKATI WAKE
Ma’ulamaa wengi wanakubali kuwa Zakaatul Fitri inaweza
kutangulizwa na kutolewa kabla ya wakati wake kwa siku moja au mbili.
Hadiyth iliyopokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar
(Radhiya Llaahu ‘anhu) inasema;
"Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
ametuamrisha kuitoa Zakaatul Fitri kabla ya watu kutoka Msikitini (katika Swalah
ya ‘Iyd)".
Anasema Nafi’ (Radhiya Llaahu ‘anhu):
"Ibn ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa
akiitoa kwa siku moja au siku mbili kabla ya Siku ya Sikukuu".
Ama zaidi ya hapo, Ma’ulamaa wamekhitalifiana.
Imaam Abu Haniyfah amesema:
"Inaweza kutolewa wakati wowote ule katika mwezi
wa Ramadhaan".
Imaam Ash-Shaafi’iy amesema:
"Inajuzu kuitoa (hata) katika siku za mwanzo za
mwezi wa Ramadhaan".
Imaam Maalik amesema:
"Inajuzu kutanguliza kwa siku moja au mbili kabla
ya Sikukuu."
Lakini Ma’ulamaa wote wamekubalina kuwa haijuzu
kuiahirisha na kuitoa baada ya ‘Iyd.