Bismillahir Rahmanir Rahim
 
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Nimegundua kwamba mashairi yanayohusiana na utukufu wa
 Allah na udhaifu mkubwa wa mja mbele ya Dhati hiyo Tukufu ni machache Alhaswil ni kuwa nimeona nitoe
 changamoto kwa watunzi kuhusiana na mashairi ya aina hiyo. Kwa hakika udhaifu wetu waja mbele ya Muumba wetu
 ni mkubwa sana, na hakuna maneno yanayoweza kuubainisha inavyopasa.
 Zifuatazo ni beti chache za kukiri udhaifu wa mja mbele ya Mola.
Ulimwengu wetu umejaa ibra. Muumini anaposali, anapomuona mgonjwa, anapoona kitu cha kustaajabisha, alimradi
anapokiona kiumbe chochote kile, hukiri moyoni uadhama wa Allah na udhaifu wa mja mbele ya Mungu. 
Anuani ya shairi nimeona iwe: "Ninani (nina nini) Dhaifu Miye" nikikusudia kuwa mimi niliye dhaifu 
hivi ninamiliki kitu gani cha kunifanya niasi? Je, nina chochote nikimilikicho?
 Je, hata nafsi yangu ni mali yangu au ni mali ya Allah? Basi, NINANI DHAIFU MIYE? 
Shairi hili niliwahi kulituma pia wavuni, huko nyuma. Amma shairi la YA RABBI MOLA nimeshalipanga tayari 
ikiwa ni pamoja na ubeti wa Bw. Amur Nasser (Abuyousuf) ambao nimeuweka mwishoni kabisa kwani mshororo
wake wa awali haukuanza katika mpangilio niliokusudiwa wa maneno yaYa Rabbi Mola. Ubeti wenyewe
 lakini naona ni mzuri tu. Naanza na shairi la NINANI DHAIFU MIYE?
 
                  (1)
Bismillahi Wadudi, Allahu Rabbi Khaliki
Kwa haki nakuhimidi, Allahu hugawanyiki
Umpweke u Wahidi, huna haja huna dhiki
Ewe Mola Mutaali, pokea ungamo hili.
 
                  (2)
Ninani dhaifu miye, sijiwezi sijishiki
Ninani hakiri miye, sitoi na similiki
Ninani fakiri miye, sina kile sina hiki
Ewe Mola Mutaali, sikiza ungamo hili.
 
                  (3)
Sikiza ungamo hili, kama ni yangu laiki
Hizingatia mawili, ya mimi nawe Khaliki
Nakiri huna wa pili, U Pweke Mola Maliki
Ewe Mola wa Ukwasi, pokea ungamo hili.
 
                 (4)
Naungama takiraba, haja kwangu imesaki
Rabbi Bwana wa Qaaba, mja nimejaa dhiki
Bila Wewe sina heba, maadumu makhuluki
Ewe Jallahu Jalali, sikiza ungamo hili.
 
                 (5)
Nimedhoofu nafusi, inanichoma mikuki
Vipi mja nakuasi, kwendekeza uzandiki
Kama si Kwako Quddusi, kwa nani kuso mfaki?
Ewe Rabbana Rahimu, pokea ungamo hili.
 
                 (6)
Najidhalilisha Kwako, Ya Rabbi Mstahiki
Ninanyenyekea Kwako, Ya Rabbi Dhati ya Haki
Kila kiumbe ni Chako, Ya rabbi unomiliki
Ewe Qadiru Qahari, sikiza ungamo hili.
 
                 (7)
Mja kamwe hafanani, hata hafananishiki
Na dhati yako Manani, hata halinganishiki
Hutaniacha njiani, si kufu yako Razzaki
Ewe Mola wa Ukwasi, pokea ungamo hili.
 
******      *******            *******
 
             YA RABBI MOLA
 

                                   (1)

Ya Rabbi Mola Faridi    nakujia ni dhalili

Ya Rabbi Mola Wahidi    nimejaa ujahili

Ya Rabbi Mola Wadudi    wanitesa ubakhili

      Kwa nini sikudhukuri    mimi ni mali ya nani?

 

                                   (2)

Ya Rabbi Mola Jalali    unitoe ujingani

Ya Rabbi Mola Kamali    nimeshindwa mtihani

Ya Rabbi Mola Zamili    nimepotea jangwani

      Hutanitupa njiani    kwani mimi ni wa nani?

 

                                   (3)

Ya Rabbi Mola Karimu    sili sinywi cha haramu

Ya Rabbi Mola Rahimu    kamwe siishi dawamu

Ya Rabbi Mola Adhimu    sina kitu mahamumu

      Nileje kitu si changu    nami ni mja wa Mungu?

 

                                   (4)

Ya Rabbi Mola Alimu     sitiri madhambi yangu

Ya Rabbi Mola Qayyumu    unilinde na machungu

Ya Rabbi Mola Hakimu    nayaogopa marungu

      Nitatendaje ithimu     na siku kiko qiyamu?

 

                                   (5)

Ya Rabbi Mola Razzaki    nipe mja nitosheke

Ya Rabbi Mola Maliki    Kwako peke nijiweke

Ya Rabbi Mola Khaliki   shetani nipige teke

      Nitakuwaje kiburi    sina lile sina hili?

 

                                   (6)

Ya Rabbi Mola Ghafuru    naasi wanisamehe

Ya Rabbi Mola Qadiru    nilinde nisiwe penhe   

Ya Rabbi Mola Nadhiru    mja mimi hohe hahe

      Yawaje sikudhukuri    Rabbana ya Rahmani?

 

                                   (7)

Ya Rabbi Mola Raufu    mja nimejaa hofu

Ya Rabbi Mola Latifu    ninashindwa na siafu

Ya Rabbi Mola Atifu    naja Kwako uniafu

      Ni vipi sikudhukuri    Nawe U  pamoja nami?

 

                                   (8)

Ya Rabbi Mola Majidu    ni Zako zote heshima   

Ya Rabbi Mola Mujidu    nakuabudu kwa hima

Ya Rabbi Mola  Muridu    kuwa nami kwa daima

      Nitachezaje na zama    kumbe kesho ni qiyama?

 

Ndugu yenu,

Ahmed. Rashid

 

Huu hapa chini ni mchango wa Bw. Amur Nasser (Abouyousuf):

 

Ya Rabbi ya Rahmani     nirehemu mja Wako
Ya Rabbi Mola Manani     ninaomba toba Yako
Ya Rabbi Mola Amini     ghufrani  sifa Zako
Kwa nini sikudhukuri     ewe wangu Mwenye enzi?


Wenu Abuyousuf