Watoto wangu vipenzi

 

 

Rabi Khaliqul Ibadi
Mikono nainyanyua
Mitupu isijerudi
Ipokee yangu dua
Nakuomba Ya Wadudi
Kwa moyo uliotuwa
Ya Ilahi Ya manani
Waepushe na balia
 
 

Watoto wangu vipenzi

Uwajaze na imani
Waongeze tarkizi
Waifuzu mitihani

Uwe kwao ni Mlinzi

Ya Rabi Ya Rahamani
Ya Ilahi Ya Manani
Waepushe na balia
 
 
Waepushe na shetani
na kila unochukia
Waongoze kwa amani
ya akhera na dunia
Wafwate watamakani
Sirati Ilo sawiya
Ya Ilahi Ya Manani
Waepushe na balia
 
 
Wahifadhi Qur’ani
na masomo yao pia
Wasali misikitini
ni sunnah yake Nabiya
Wasiache abadani
Kukutii ya Jaliya
Ya ilahi ya Manani
waepushe na balia
 
 
Waepushe na haramu
wao na wenzao pia
Wana wa kiislamu
kila pembe ya dunia
Wafunuwe wafahamu
wawe Kwako maridhia
Ya ilahi ya Manani
waepushe na balia
 
 
Muhammad Faraj Salem Al Saiy