Huu ni utenzi maarufu uliokuwa ukisomwa na Sheikh Said bin Ahmed katika miaka ya sitini baada ya kila akimaliza mawaidha yake katika kipindi chake cha dini katika Idhaa ya wilaya ya pwani ya Kenya Broadcasting Service - Mombasa siku hizo.

 

DUA

Twakuomba mtukufu - Aso kijana na kufu

Mola wetu maarufu - Allahu ulo Karima

 

Mikono tumeinuwa - Mola wetu watujuwa

Taqabali zetu dua - Utupe lilo na wema

 

Mola matozi yatoka - Hakika yabubujika

Tumetubu kwa hakika - Waja wako tumekoma

 

Ya Rabbi tupe elimu - Utupe njema fahamu

Ya kutambua vigumu - Vya dini yako Karima

 

Utupe matunda yake - Tuisome tusichoke

Mola elimu iweke - Moyoni mahala pema

 

Rabbi ijapo hukumu - Isiwe kwetu ni ngumu

Tusiweze kudhulumu - Tukuche wewe Karima

 

Utupe na kupendana - Sisi na wetu vijana

Mapenzi yaso khiana - Yalo mazuri daima

 

Tutuze mijini mwetu - Tuqidhie deni zetu

Kabila ya kuja kwetu - Mjumbe wa mauti mwema

 

Kula ajae na shari - Waijua yake siri

Ivunde yake dhamiri - Asiweze kusimama

 

Rabbi sala na salamu - Zimfikie hashimu

Na swahabaze kiramu - Na aali na kila mwema

 

Amina Rabbi amina - Amina Rabbi amina

Amina Rabbi amina - Ya Rabbi watusikia