TUKAE KIMYA KWA NINI?

 

Swaleh Suheil Abeid

Natoa nyingi shukuri

Haji Udii mwandani

 

Shairi lako ni zuri

ulosema ni yakini

 

Mavazi yalodhihiri

yanachangiya kuzini

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Zindukani tushauri

tukae kimya kwa nini?

 

Ni wajibu tuhubiri

tutangaze mitaani

 

Libasi za kikafiri

zikomeshwe majumbani

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Wake hawajisitiri

hata haya hawaoni

 

Ziwazi zao swadiri

na rangi za midomoni

 

Umbo lote ladhihiri

utosi hadi nyayoni

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Abaya wazikasiri 

zawabana badanini

 

Kamwe haziwasitiri

zawaonya viungoni

 

Nyuso ziwazi dhahiri

nyele kupakwa launi

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Wamo katika ghururi

dada zetu majumbani

 

Vipindi vya kikafiri

katika telivisheni

 

Sana vimewaathiri

wazitamani fesheni

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Kasumba imewaghuri

kuiga ya Uzunguni

 

Marinda yalo kaswiri 

yawafika mapajani

 

Nguo ziso desituri

waume waigizani?

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Na ya rijali kathiri 

nao wamo hatiyani

 

Libasi zawaaziri

kuiga wamerikani

 

Wajiona ni wazuri

kumbe kama hayawani

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Suruale zilo kaswiri

na rangi za nyweleni

 

Wazivaa za hariri

nguo zabana mwilini

 

Na kipuli hunawiri

kimevawa shikioni

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Libasi za kikafiri

watisha hawajioni

 

Waenda tupu dhahiri

kwa kuigiza fesheni

 

Hata hawatahayari

zimewatoka imani

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Waume mwajiaziri

dhahabu mwavaliyani?

 

Vidoleni idhahiri

shingoni na kifuani

 

Wengine wajifakhiri

kwa bangili mikononi

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Libasi ziso za kheri

waja mwazitakiani?

 

Mwangiya kwenye kufuri

kinyume cha yetu dini

 

Mukiiga makafiri

mutaingiya motoni

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?

 

 

 

 

Kaditamati shairi

nimefika kikomoni

 

Natumuombe Qahari

atupe nyingi imani

 

Atuepushie shari

akhera na duniyani

 

Tumo katika hatari

tukae kimya kwa nini?