TOBA YA RABBI

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

Mikono ninainuwa

Ilahi Rabbinnasi

 

Huku nikiomba duwa

Ewe Maliki Mkwasi

 

Pekeyo Mwenye uluwa

Kwa mwengine haipasi

 

Rabbi tutakabalie

Ya Samiu ya Alimu

 

 

 

 

Niruzuku ghufurani

Niepushe na maasi

 

Nakuomba ya Manani

Dhamiri inanighasi

 

Naungua kifuani

Kama moto wa nuhasi

 

Rabbi tutakabalie

Ya Samiu ya Alimu

 

 

 

 

Kheri ukinishushia

Nasahau kwa wepesi

 

Mitihani yanijia

Mimi nazidisha kasi

 

Wewe wanichukulia

Miye nazidi kuasi

 

Rabbi tutakabalie

Ya Samiu ya Alimu

 

 

 

 

Ujalie ucha Mungu

Uwe kwangu ni libasi

 

Adui wako na wangu

Wasiwasi lkhannasi

 

Mfunge mtie pingu

Asiipate nafasi

 

Rabbi tutakabalie

Ya Samiu ya Alimu

 

 

 

 

Twa'a iwe ni sibugha

Nipambe kwa ikhlasi

 

Nikutii kwa faragha

pia mbele ya unasi

 

Uniepushe na zagha

Unitowe wasiwasi

 

Rabbi tutakabalie

Ya Samiu ya Alimu

 

 

 

 

Rabbi siku ya Miadi

Ninywe ndani ya gilasi

 

Aninywishe Muhamadi

Kiu kwangu iwe basi

 

Unirehemu Wadudi

Unipe Firidausi

 

Rabbi tutakabalie

Ya Samiu ya Alimu

 

 

 

 

 

Tafsiri: ya baadhi ya maneno:

1- Sibugha = 'Pambo'

Mwenyezi Mungu anasema: "Sibughatullah = Pambo la Mwenyezi Mungu."  Al Baqarah -138

2- Zagha = 'Kupotoka'

Mwenyezi Mungu anasema: "Falamma zaaghu azaagha Llahu qulubahum = Walipo potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke." Saff -5