KISA CHA THAALABA NA KUKATAA KWAKE KUTOA ZAKA

Imeafsiriwa na Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

 

Wengi miongoni mwa makhatibu wa misikitini wanainasibisha na Sahaba Thaalaba bin Hatib  (Radhiya Llahu anhum) aya ya 75 ya Surat At Tawba.

Katika aya hiyo Mwenyezi Mungu anasema:

"Na miongoni mwao hao (wanafiki) wako waliomuahidi Mwenyezi Mungu kuwa ; "Akitupa katika fadhila Zake tutaoa sadaka na tutakuwa miongini mwa wanaotenda mema. Lakini alipowapa hizo fadhila Zake walizifanyia ubakhili na wakakengeuka. Nao (mpaka hivi sasa ) wanakengeuka. Kwa hivyo (Mwenyezi Mungu) Akawalipa unafiki (kuutia) nyoyoni mwao mpaka siku ya kukutana naye kwa sababu ya kuhalifu kwao waliomuahidi Mwenyezi Mungu na kwa sababu ya kusema kwao uwongo."

Attawba  - 75-77

Kimetungwa kisa kirefu kinachonasema kuwa Thaalaba  (Radhiya Llahu anhum) ndiye aliyekusudiwa katika aya hii kuwa alikataa kutoa zaka kumpa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Kisa kinasema kuwa Thaalaba alikuwa masikini sana na kwamba alikuwa mwingi wa kwenda msikitini mpaka akapewa jina la kubandika akaitwa 'Njiwa wa msikiti'.

Kisa kinaendela kusema kuwa; Siku moja Thaalaba alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

"Niombee dua ili Mwenyezi Mungu aniruzuku wanyama wengi sana." na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamuombea dua na idadi ya kondoo wake ikaongezeka ikambidi atafute nyumba nje ya mji wa Madina. Akawa hasali isipokuwa baadhi tu ya sala za fardhi.

Idadi ya kondoo ikazidi kuongezeka na safari hii ikabidi asogee nje zaidi ya mji wa Madina, na akawa hana tena wakati wa kusali isipokuwa siku ya Ijumaa tu.

Idadi ya kondoo ikaongezeka tena akaacha kusali hata hiyo Ijumaa, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipompeleka mjumbe wake kwa ajili ya kukusanya pesa za Zaka, Thaalaba akakataa, akasema: "Hakuna Zaka yenu katika mali yangu, mali hii ni yangu mwenyewe nimeirithi kwa babu zangu."

Kisa kinaendelea kusema kuwa; Thaalaba alihisi vibaya akachukua mali ya Zaka na kuipeleka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyeikataa mali hiyo. Na alipofariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), Thaalaba alichukua mali ya Zaka akamuendea Abubakar, akamuambia:  "Chukua", lakini Abubakar akaikataa akamwambia: "Siwezi kukubali alichokikataa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)."

Akaipeleka kwa Omar naye pia akasema: "Wallahi siwezi kukubali alichokikataa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)."

 

Kisa hiki si cha kweli na isnadi yake ni ya kupangwa, juu ya kuwa kimesimuliwa na maulamaa wakubwa kama vile Ibni Kathiyr na Ibni Jariyr na Ibni Athiyr, na hii ni kwa sababu zifuatazo:

 

1- Mwenyezi Mungu hakatai toba ya mja wake.

Mwenyezi Mungu anasema

"Wakitubu wakasimamisha Sala na wakatoa Zaka basi iacheni njia yao (waacheni)."

Al Tawba – 5

Na akasema:

"Sema: "Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Bila shaka Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika yeye ni Mwingi wa kusaheme dhambi (na) Mwingi wa kurehemu."

Azzumar 53

Aya zilizotangulia zinatujulisha kuwa hata mshirikina akitubu basi Mwenyezi Mungu ataikubali toba yake, itakuwaje basi aikatae toba ya Muislamu aliyeacha kutoa Zaka?

 

2- Anasema Imam Al Qurtuby katka Jamia al Ahkam:

“Thaalaba alipigana vita vya Badr, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alishuhudia kuwa ni Muislamu wa kweli, kwa  hivyo kisa hiki anachonasibishwa nacho si cha kweli.

Jamea al Ahkam

 

3- Anasema Al Hafidh al Iraqi katika tahakiki ya hadith za kitabu cha al Ahyaa:

“Hadithi hii imetolewa na Al Tabarani na isnadi yake ni dhaifu”

 

4- Anasema Ibni Hajar katika Al Isaba:

“Kisa hiki sidhani kama ni sahihi kwa sababu Thaalaba huyu amepigana vita vya Badr, na hadithi sahihi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu inasema kuwa; Waliopigana vita vya Badr hawaingii motoni, na kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwaambia; “Fanyeni mtakacho, mumekwisha ghufuriwa madhambi yenu.

Aliyefikia daraja hii itakuwaje awe mnafiki kama inavyeleza aya?”

 

 

____________________________________

(kisa hiki nimekifasiri kutoka katika site ifuatayo:

http://audio.islamweb.net/islamweb/index.cfm?fuseaction=ReadContent&AudioID=22183#14913