SOKO LA RAMADHAAN HILOO LINAFUNGULIWA

 

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY

 

 

Ndugu zangu Waislamu

Soko la Ramadhaan ndiyo kwanza linafunguliwa na hiloo linakaribia kufungwa.

 

Ndugu zangu Waislamu

Ramadhaan ni Soko linalofunguliwa kila mwaka kisha likafungwa, hupata faida ndani yake mwenye kutaka kupata faida na hula hasara mwenye kutaka kula hasara.

Ramadhaan ni soko tulilowekewa na Mola wetu Mtukufu (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa ajili ya kuchuma ndani yake thawabu nyingi kiasi cha uwezo wa mtu. Soko liko wazi na milango yake iko wazi na idadi yake ni ishirini na tisa au thelathini tu haizidi, na kila siku mlango mmoja unafungwa. Kwa hivyo anayetaka kuwahi na awahi.

 

Ndugu zangu Waislamu

Inatupasa kuukaribisha mwezi huu kwa furaha na tabasamu na kwa moyo mkunjufu, kwani ndani yake mna kheri nyingi sana, na baina yake na baina ya Ramadhaan nyingine Mwenyezi Mungu husamehe madhambi mengi sana yakiepukwa yale makubwa.

 

Ndugu zangu Waislam

Kutokana na manufaa mengi yaliyomo ndani ya mwezi huu, Mtume wetu mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiusubiri kwa hamu kubwa sana.

 

Huyu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyekwisha samehewa madhambi yake yaliyotangulia na yale yanayofuatilia, Mtume aliyekabidhiwa funguo zote za hazina za ardhini. Alikuwa mara unapoingia mwezi huu akiikaza barabara nguo yake ya chini (saruni) na nyakati za usiku akiwaamsha watu wake ili wajishughulishe na ibada ndani yake, na hii ni kwa sababu alikuwa akiujua vizuri utukufu wa Mola wake na alikuwa akiitambua vizuri zawadi aliyowatayarishia waja Wake wanaoshindana katika kufanya mema ndani ya mwezi huu.

 

Imepokelewa pia katika athar kuwa Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) walikuwa wakimuomba Mola wao kabla ya Ramadhaan kwa miezi sita ili awafikishe mwezi huu, na baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhaan walikuwa wakiendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kwa muda wa miezi sita mingine ili azikubali ‘amali zao njema walizofanya ndani yake na ili awaghufirie madhambi yao.

 

 

STAREHE YA DUNIA

Walikuwa wakifanya yote hayo kwa sababu walikuwa wakitambua vizuri kuwa starehe za dunia ni haba sana.

Mwenyezi Mungu Anasema:

“Sema starehe ya dunia ni kidogo” [An-Nisaa: 77]

 

Starehe za dunia hakika ni ndogo sana, kwani tukichukulia mfano wa mwezi huu wa Ramadhaan ambao ndani ya mchana wake utamuona mtu aliyefunga, akijishughulisha kukusanya kila aina ya vyakula. Sambusa, mikate ya chila maandazi n.k. Lakini magharibi inapoingia akishakula tende na kunywa gilasi ya maji, na baada ya kuswali Magharibi akarudi nyumbani na kunywa bakuli lake la uji, ile hamu ya kula vile alivyojikusanyia wakati wa mchana ishaondoka. Hana hamu tena ya kula hata kama chakula hicho ni kizuri namna gani, na iwapo atajilazimisha kula basi atakuwa anajitafutia mwenyewe matatizo katika tumbo lake.

Kwa ajili hii Mwenyezi Mungu Akatujulisha kuwa starehe za dunia ni haba sana.

Ama starehe za huko Peponi ni kubwa, nyingi na hazichoshi.

Mwenyezi Mungu Anasema:

“Hawatataka kuondoka humo”

Kwani huko hakuna kushiba wala kukinai, isipokuwa ni kufaidika na kutaladhadh kusikokuwa na mwisho.

Ladha ya chakula, ladha ya mandhari nzuri nzuri, ladha zote za huko hazikatiki wala hazichoshi.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anasema:

“Al-Firdaws ni sehemu ya juu huko Peponi, ipo kati kati, na hiyo ndiyo sehemu iliyo bora kupita zote”.

Na katika Al-Bukhaariy na Muslim, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Mnapomuomba Mwenyezi Mungu, basi muombeni Al-Firdaws, kwani hiyo ipo sehemu ya juu kabisa na kati kati ya Pepo, na hapo ndipo chemchem za mito ya Peponi inapoanzia”.

“Kwa ajili hiyo” anasema Ibn Kathiyr:

“Mwenyezi Mungu Anaposema:

“Hawatataka kuondoka humo”, maana yake ni kuwa hawatachoka kutizama mandhari zake na hawatopenda kuchagua mahali pengine badala yake, na hawatopenda kuhamishwa kutoka hapo”.

 

 

VYAKULA VYA PEPONI

Ama starehe ya vyakula vya huko inakhitalifiana na starehe ya vyakula vya hapa duniani, kwani huko hakuna kushiba wala kukinai, bali ni kustarehe na kutaladhadh tu.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anasema;

“Watu wa Peponi wanakula na kunywa, hakuna kwenda haja ndogo huko wala haja kubwa wala kutema mate.”

Wakamuuliza;

“Vipi chakula (kitatokaje tumboni)?”

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Kinatoka kwa njia ya jasho lenye harufu ya Miski. Aliye katika daraja la chini kabisa Peponi, anahudumiwa na watumishi elfu kumi, kila mmoja kati yao anabeba sinia mbili (za vyakula), moja ya dhahabu na moja ya fedha zenye rangi tofauti, ladha anayoipata katika chakula alichokula ndani ya sinia ya mwanzo ni ile ile anayoipata katika sinia ya mwisho.”

[Ibn Abi Duniya, At-Twabaraaniy na ameisahihisha Al-Mundhiry katika kitabu chake cha At-Targhiyb wat-Tarhiyb].

 

Na Mwenyezi Mungu Anasema:

“Na utakapoyaona huko utaona neema na ufalme mkubwa” [Ad-Dahr: 20]

 

 

QIYAAMU RAMADHAAN (TAARAWIYH)

UMUHIMU WA SWALAH

Tukiwa bado tumo ndani ya soko la Ramadhaan leo tutalitembelea angalau kwa ziara fupi soko la Swalah, soko ambalo ndani yake mna faida nyingi zaidi kupita biashara zote nyingine.

Swalah ni nguzo ya pili ya Kiislamu baada ya Shahada mbili, na Swalah ni ibada anayoipenda sana Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), na daraja yake ni kubwa kupita ibada zote zilizobaki, nayo ni nguzo ambayo kwayo Dini inasimama juu yake.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Kichwa cha jambo ni Uislamu na nguzo yake ni Swalah na kilele chake ni Jihaad”.

Na Swalah ni ‘amali ya mwanzo atakayoulizwa mja siku ya Qiyaamah. Ikikubaliwa, basi ‘amali zote zilizobaki zitakubaliwa, ama ikikataliwa basi zilizobaki nazo pia zitakataliwa, kwani tofauti iliyopo baina yetu na baina ya makafiri ni Swalah.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliendelea kuusia juu ya Swalah katika maisha yake yote na hata pale alipokuwa akivuta pumzi zake za mwisho alikuwa akiusia huku akisema:

“Swalah Swalah na kilichomilikiwa na kuume kwenu”.

 

 

SWALAH ZA SUNNAH

Mwenyezi Mungu Ametuwekea shari’ah ya kuswali Swalah za Sunnah ili zipate kutusaidia katika kuinyanyua Swalah ya Fardhi kutokana na makosa au upungufu wowote unaopatikana ndani yake kutoka kwetu.

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“La mwanzo atakaloulizwa mja siku ya Qiyaamah katika ‘amali zake ni Swalah. Mwenyezi Mungu Atawaambia Malaika wake akiwa Yeye ni mwenye kujua zaidi:

“Tizameni katika Swalah ya mja Wangu. Ameitimiza au hakuitimiza”.

Ikiwa ameitimiza, basi ataandikiwa thawabu za Swalah iliyotimia, ama ikiwa imepungua chochote ndani yake, basi Mwenyezi Mungu Atasema;

“Tizameni ikiwa mja Wangu ameswali Swalah za Sunnah”.

Ikiwa anazo Swalah za Sunnah, atasema:

“Mtimizieni mja Wangu fardhi yake kutoka katika Sunnah zake.” Kisha ‘amali zilizobaki zitakubaliwa kwa njia hiyo.” [Abu Daawuud]

 

Kutokana na Hadiyth zilizotangulia Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akatuwekea shari’ah ya kuswali Swalah za Sunnah, na akaitilia nguvu sana katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhaan kwa kutuwekea shari’ah ya kuswali Swalah ya Qiyaam Ramadhaan (Taarawiyh).

Qiyaam Ramadhaan pia inajulikana kwa jina la ‘Taarawiyh’ (mapumziko), kwa sababu Maswahaba wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) walikuwa wanaposwali Swalah hii wakipumzika baada kila rakaa nne, na Swalah hii ni Sunnah kwa wanawake na wanaume.

Anasema Irfijah (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa:

“Sayiduna ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akiamrisha watu kuiswali Jamaa’ah Swalah ya Qiyaam Ramadhaan (Taarawiyh), na alikuwa akimweka Imaam mwanamume upande wa wanaume na Imaam mwanamke upande wa wanawake na mimi nilikuwa Imaam wa wanawake”. [Al-Bayhaqiy na Fiqhus Sunnah, Sayyid Saabiq]

 

Swalah hii huswaliwa baada ya Swalah ya ‘Ishaa na kabla ya Swalah ya witri na huswaliwa rakaa mbili mbili, na inaweza pia kucheleweshwa mpaka wakati wowote katika nyakati za usiku.

Imepokelewa na Maimaam wa Hadiyth wa Ahlus Sunnah kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa amesema:

“Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akipendekeza watu waiswali Swalah hii lakini bila kulazimisha. Alikuwa akisema:

“Atakayeswali Qiyaam Ramadhaan kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia”.

Hii ni neema kubwa sana ambayo hatoiacha isipokuwa yule ambaye hana madhambi aliyotanguliza.

Na imepokelewa na Maimaam wote wa Ahlus Sunah isipokuwa At-Tirmidhiy kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) kuwa amesema:

“Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliswali Msikitini, na watu wengi wakaswali pamoja naye, kisha akaswali tena siku ya pili yake na watu wakaongezeka, kisha wakakusanyika usiku wa tatu, lakini Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwatokea. Ulipoingia wakati wa asubuhi akasema;

“Nilikuoneni mlichofanya (kuningoja kwenu), na hakuna kilichonizuwia nisitoke nikasali pamoja nanyi isipokuwa nilihofia isije ikafaridhishwa juu yenu”. Na hii ilikuwa katika mwezi wa Ramadhaan.

 

 

IDADI YA RAKAA ZAKE

Imepokelewa kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hajapata kuswali zaidi ya rakaa kumi na moja, iwe katika mwezi wa Ramadhaan au mwezi mwingine wowote ule, ingawaje zipo baadhi ya riwaya ambazo Shaykh Al-Albaaniy anasema kuwa zina udhaifu ndani yake zinazosema kuwa Maswahaba wengine (Radhiya Llaahu ‘anhum) walikuwa wakisali rakaa ishirini.

 

 

KUISWALI JAMAA’AH

Taarawiyh inaweza kuswaliwa Jamaa’ah na pia anaweza mtu kuiswali peke yake, isipokuwa Ma’ulamaa wengi wanaona kuwa kuiswali Jama’ah Msikitini ni bora zaidi, ingawaje wapo wanaoona kuwa kuiswali nyumbani ni bora zaidi na kila mmoja anazo hoja zake.

Tulitangulia kueleza kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliiswali Jama’ah Swalah hii na akasema kuwa hakuna kilichomzuia kuendelea kufanya hivyo isipokuwa kwa ajili ya kuwahofia ummati wake isije ikateremshwa amri ya kufaridhishwa, kisha ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakati wa ukhalifa wake akawakusanya watu wawe wanaiswali Jamaa’ah nyuma ya Imaam mmoja.

Anasema ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Abdil-Qaariy:

“Nilitoka usiku mmoja katika mwezi wa Ramadhaan mimi na ‘Umar bin Al-Khattwaab kuelekea Msikitini, tukawaona watu wamegawanyika na kufarikiana, kila mmoja anaswali peke yake. Mtu anakuwa anaswali peke yake kisha kundi lingine (linakuja na) linaswali nyuma yake. ‘Umar akasema:

Mimi naona ikiwa tutawakusanya wote wasali nyuma ya imamu mmoja itakuwa bora. Kisha akafanya hivyo na akamweka Ubay bin Ka’ab awasalishe watu. Kisha nikatoka naye usiku uliofuata na tukawaona watu wote wanasali nyuma ya imamu mmoja akasema;

‘Ni’mal bid’at haadhihi’ “Jitihada jema sana hii na ile wanayolala ikawapita ni bora zaidi kuliko wanayoiswali”, akikusudia kuwa kuiswali nyakati za mwisho za usiku ni bora zaidi.

Neno Bid’ah alotumia ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) katika riwaya hii halina maana ya ‘Uzushi’, kwani ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) hawezi kuwa mzushi, bali Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha kuwa atakalotufundisha ‘Umar au yeyote kati ya Makhalifa walioongoka (Radhiya Llaahu ‘anhum) (Khulafaa Raashidiyn) ni katika Sunnah.

Kutoka kwa Al-Irbaadh bin Saariyah (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha yaliyoingiza hofu nyoyoni na kututoa machozi machoni. Tukamuuliza; ‘Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu kama kwamba mawaidha (haya ni) ya kutuaga?’

Akatuusia, akasema:

“Nakuusieni kumcha Mungu na kusikia na kutii hata akiwa amri wenu mtumwa, kwani atakayeishi kati yenu ataona khitilafu nyingi, kwa hivyo ni juu yenu kufuata Sunnah yangu na Sunnah za Makhalifa waadilifu walioongoka (katika riwaya nyingine amesema; “watakaokuja baada yangu) muzibane Sunnah zao kwa magego…” [Imepokelewa na At-Tirmidhiy na Abu Daawuud na Ibn Maajah na wengineo].

 

Hii ni sawa na muadhini wa pili aloongeza ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) wakati wa ukhalifa wake, muadhini ambao wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) haukuwepo, lakini ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyetawala ukhalifa baada yake aliuendeleza na wala hakuusimamisha, na hii ni kutokana na fahamu yao Makhalifa hawa juu ya Hadiyth iliyotangulia iliyosimuliwa na Al-Irbaadh bin Saariyah (Radhiya Llaahu ‘anhu).

 

Kwa ajili hiyo neno Bid’ah, alokusudia ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) hakukusudia Bid’ah ya upotofu (kullu bid’atin dhwalaalah), bali alikusudia Bid’ah ya kilugha na si ya kidini na maana yake ni ‘jitihada jema’ (Mubdi’u), kwani ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni mcha Mungu kuliko hao wanaojaribu kumkosoa na ni mtu wa mwisho kabisa kutegemewa kuleta uzushi katika Dini.

 

Na ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) asingeruhusu watu waiswali Jamaa’ah Swalah hiyo angekuwa hakumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiiswali Swalah hii Jamaa’ah pamoja na Maswahaba wake (Radhiya Llaahu ‘anhum), yeye mwenyewe (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa Imaam wao, na akaacha kuendelea kufanya hivyo kwa kuhofia wasije wakafaridhishiwa. Ama baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ile hofu ya kufaridhishiwa ikaondoka kwa kukatika kwa Wahyi, na Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) walikuwa wakiiswali Jamaa’ah Swalah hiyo, isipokwa walikuwa wakisali kila kundi nyuma ya Imaam yeyote yule, na Jamaa’ah zikawa nyingi Msikitini wakati mmoja, na kwa ajili hiyo ‘Umar akawakusanya ili waiswali nyuma ya Imaam mmoja.

 

Udhuru aloutoa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pale alipoacha kutoka na kuswali nao ulikuwa:

“HAKUNA KILICHONIZUWIA NISITOKE NIKASWALI PAMOJA NANYI ISIPOKUWA….”,  hii ikimaanisha kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akitamani kutoka na kuswali pamoja nao, isipokuwa hofu yake ilikuwa ni moja tu, nayo ni kuwa Isije Ikafaridhishwa juu yao.

Anasema Imaam Maalik katika Muwattwaa kuwa:

Swalaatut-Taarawiyh ni Sunnah iliyotiliwa nguvu, na kwa ajili hiyo Makhalifa wote waongofu (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliitilia mkazo Swalah hii wakiwemo ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhum) na wakawa wanaipendekeza kuswaliwa Jamaa’ah wanaume na wanawake pia.

“Ama kauli yake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:

“Nilihofia isije ikafaridhishwa juu yenu”, anaendela kusema Imaam Maalik:

“Anasema Al-Qaadhiy Abu Bakr kuwa huenda ikawa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alifunuliwa kuwa akiendelea kuiswali pamoja nao itakuja faridhishwa, au labda alidhania tu kuwa huenda ikafaridhishwa, au huenda akawa anahofia asije mmoja katika umati wake atakaposikia kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiiswali siku zote Swalah hiyo katika Jamaa’ah akadhania kuwa ni fardhi kisha akawajulisha watu hiyvo kisha watu wakaionea uvivu” [Mwisho wa maneno ya Imaam Maalik].

 

Imepokelwa pia kutoka kwa Abu Daawuud na An-Nasaaiy na Ibn Maajah na Al-Haakim na At-Tirmidhy, na lafdhi ya Hadiyth hii ni ya Imaam At-Tirmidhiy kama ilivyoandikwa katika sharh ya Tuhfatul-Ahwadhiy anasema:

“Kutoka kwa Abu Dharr amesema: ‘Tulifunga pamoja na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na hakuswali pamoja na sisi (Swalah ya Taarawiyh) mpaka zilipobaki siku saba kabla kumalizika mwezi (wa Ramadhaan), akatuswalisha Taarawiyh mpaka ilipomalizika thuluthi ya mwisho. Kisha usiku wa sita (kabla ya kumalizika kwa Ramadhaan) hakutuswalisha, akatuswalisha usiku wa tano (kabla ya kumalizika Ramadhaan) mpaka ulipomalizika nusu ya usiku.

Tukamwambia; ‘Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, si bora ungeendelea kutuswalisha sehemu ya usiku iliyobaki?’

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Atakayeswali na Imaam mpaka atakapomaliza (Imaam) Swalah, ataandikiwa thawabu ya aliyeswali usiku wote”.

Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakutuswalisha mpaka zilipobaki siku tatu kabla ya kumalizika mwezi, akatuswalisha na akawaita Jamaa’ah zake na wake zake na akatuswalisha mpaka wakati wa kula daku ulipoingia.

 

Hadiyth hii ina faida nyingi sana ndani yake, lakini ili nisiwachoshe wasomaji nitaelezea faida mbili tu nazo ni kuwa:

1- Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwaswalisha Swahaba zake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) Swalah ya Taarawiyh yeye akiwa Imaam wao na akawaita watu wa nyumba yake pia.

2- Katika Soko hili la Taarawiyh, atakayeswali nyuma ya Imaam mpaka mwisho ataandikiwa thawabu ya aliyeswali usiku kucha.

 

 

KHITILAFU YA UBORA

Hata hivyo ipo khitilafu baina ya Ma’ulamaa kuhusu namna bora wa kuiswali Swalah ya Taarawiyh.

Anasema Imaam Ash-Shaafi’iy na wengi katika wanafunzi wake, na pia Imam Abu Haniyfah na Ahmad na baadhi ya Wanavyuoni wa madhehebu ya Imaam Maalik na wengineo kuwa ni bora kuiswali Jamaa’ah kama alivyofanya ‘Umar na kama walivyofanya Makhalifa waongofu waliokuja baada yake na pia Maswahaba na waliokuja baada yao, na ikaendelea katika hali hiyo mpaka wakati wetu huu sasa.

Ama Imaam Maalik na Abu Yuusuf na baadhi ya wafuasi wa Imaam Ash-Shaafi’iy wao ingawaje wanaona kuwa ni vizuri kuiswali Jamaa’ah, lakini wanasema kuwa ni bora zaidi kuiswali nyumbani mtu peke yake.

 

 

QUR-AAN TUKUFU

Ndugu zangu Waislam

Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Ramadhaan inaendelea kututoka na milango inaendelea kufungika, na biashara inaendelea kuchangamka. Kwani kila siku zinapokaribia kumalizika Mtume wenu Mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akizidi kuikaza shuka yake na kukesha usiku wake na kuamsha watu wake.

Ndugu zangu Waislam

Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema;

“Hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu (mnayoinunua) ni yenye thamani sana, hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni Pepo”. [At-Tirmidhiy, Al-Haakim, Al-Bayhaqiy na wengineo].

 

Anasema Ibnul Qayyim:

“Ajabu mtu baada ya kutambua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye bidhaa bora, kisha anakwenda kufanya biashara na mwengine mwenye bidhaa duni, na ajabu kubwa zaidi ni pale mtu anapotambua kuwa hana budi Naye Mola wake na kwamba hapana awezae kuondoa shida zake isipokuwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), kisha anajiweka mbali naye”.

Kwa ajili hiyo ndugu zangu Waislam, tuzidishe kufanya biashara na Mola wetu mtukufu katika mwezi huu wa Ramadhaan huku tukitarajia bidhaa yake tukufu, bidhaa ghali kupita zote, Jannatul Firdaws.

 

 

BIASHARA YA KUSOMA QUR-AAN

Mwenyezi Mungu Anasema;

“Kwa yakini wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Sala, na katika yale Tuliyowapa wakatoa, kwa siri na kwa dhahiri, hao wanatumai (faida ya) BIASHARA isiyododa (isiyobwaga)” [Fwaatir: 29]

Na Akasema:

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qur-aan ili iwe uongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi (baina ya haki na batili)” [Al-Baqarah: 185]

Katika Aayah hii Mwenyezi Mungu Anausifia Mwezi huu mtukufu wa Ramadhaan kuwa ni bora kuliko miezi yote kutokana na kuuchagua kwa kuiteremsha Qur-aan tukufu ndani yake, kitabu chenye uongofu, kilichopambanua baina ya haki na batili, ili kiwe hoja zilio wazi kwa kila mwenye kukisoma.

 

Ma’ulamaa wanasema kuwa ili kufaidika na mafundisho yake, lazima kusoma huko kuwe kwa kutafakari na kuzingatia. Kwani yeyote anayetaka kufaidika na Kitabu hiki kitukufu lazima awe anakisoma kwa moyo mkunjufu ulio hadhir na kwa kuzingatia aya zake huku akitambua kuwa yaliyomo ndani yake ni maneno anayohutubiwa yeye.

Mwenyezi Mungu Anasema:

“Kwa yakini katika jambo hili mna ukumbusho kwa mwenye moyo au kwa ategaye sikio, naye mwenyewe awe hadhiri” [Qaaf: 37]

Anasema Ibni Qutaybah katika kitabu chake kiitwacho ‘Tafsiyr Ghariyb Al-Qur-aan’:

“Aya hii inatufundisha kuwa ili mtu afaidike na mafundisho yaliyomo ndani ya Qur-aan tukufu lazima moyo wake uwe hadhiri pale anapiosoma au anapoisikiliza”.

 

Imetolewa na Ad-Daylamiy kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) katika Hadiyth aloinyanyua moja kwa moja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa:

“Mnapoisoma Qur-aan muisome vilivyo na muibainishe kwa ubainifu, muwe mnasimama (na kutafakiri) penye maajabu yake, na muusitue na kuuamsha moyo (muuharikishe) kwa hiyo Qur-aan, na isiwe hamu ya mtu ni kuimaliza sura tu.”

 

Ndugu zangu Waislam

Mwenyezi Mungu hutukuza na kuadhimisha anachotaka. Kama alivyowachagua baadhi ya Malaika wake akawafanya kuwa wajumbe, na kuwachagua miongoni mwa wanaadamu na kuwafanya kuwa Mitume, akauchagua mwezi wa Ramadhaan na miezi mitukufu kwa kuiadhimisha kuliko miezi mingine, Mwenyezi Mungu Ameichagua pia Qur-aan tukufu ambayo ni maneno yake akayaadhimisha juu ya maneno yote mengine, kwa hivyo kuweni wenye kufahamu na wenye kutukuza yale Aloyatukuza Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), kwa sababu hatukuzi yale Aloyatukuza Mwenyezi Mungu isipokuwa mwenye kufahamu na mwenye akili.

 

Ndugu zangu Waislam

Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa Qur-aan, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiisoma na kuiadhimisha Qur-aan tukufu zaidi katika mwezi huu kupita miezi mingine yote. Kwa hivyo na sisi tujitahidi kuuhitimisha msahafu ndani ya mwezi huu angalau mara moja, hii ni kwa uhaba kabisa, kwani mwezi huu ni mwezi wake, na ndani yake mna thawabu nyingi sana na manufaa mengi sana kwa ajili yetu.

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayesoma herufi moja (tu) katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu atalipwa thawabu. Na kwa kila thawabu moja atalipwa kumi (nyingine). Si semi kuwa alif laam miym ni herufi moja, bali ‘alif’ ni herufi (moja), ‘laam’ ni herufi (moja) na ‘miym’ ni herufi (moja)”.

Yaani mtu anapotamka; ‘Alif laam miym’, anakuwa keshajipatia thawabu thelathini, na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakae.

Huyu ndiye Mola wetu mkarimu, na bila shaka katika mwezi Wake huu wenye baraka malipo yake huongezeka maradufu.

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa mkarimu kupita wote katika mambo ya kheri, na alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi wa Ramadhaan wakati anapokutana na Jibriyl (‘Alayhis Salaam), na alikuwa akikutana naye kila Ramadhaan mpaka mwezi unapomalizika, na alikuwa akimsikiliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) Qur-aan yote, na kila anapokutana na Jibriyl, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa mwingi wa kheri mfano wa upepo uliopelekwa (kwa ajili ya kueneza kheri)” [Al-Bukhaariy na wengine]

 

Ndugu zangu Waislam

Kila kitu kwa hesabu yake. Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Ataambiwa msomaji wa Qur-aan; ‘Soma upande daraja (za juu Peponi). Isome vilivyo kama ulivyokuwa ukiisoma duniani na daraja yako inaishia mwisho wa aya utakayoisoma” [Abu Daawuud na At-Tirmidhiy na wengineo]

Kwa hivyo ukisoma juzuu moja tu, basi daraja yako itaishia hapo, na hivi ndivyo ilivyo kila unapoisoma zaidi utapandishwa zaidi katika daraja za juu kabisa za huko Peponi

 

 

BAADHI YA HADIYTH JUU YA FADHILA ZA QUR-AAN TUKUFU

Kutoka kwa Abu Umaamah (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Someni Qur-aan, kwa sababu itakuja siku ya Qiyaamah kuwaombea shafa’ah wasomaji wake” [Muslim]

 

Kutoka kwa An-Nawwaas bin Sam’aan (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Italetwa Qur-aan siku ya Qiyaamah pamoja na wasomaji wake waliokuwa wakiifanyia kazi duniani ikitanguliwa na Suratul Baqarah na Aali ‘Imraan zikiwatetea wasomaji wake” [Muslim]

 

Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Mbora wenu ni yule atakayejifunza Qur-aan kisha akafundisha” [Al-Bukhaariy]

 

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) amesema:

“Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):

“Mwenye kuisoma Qur-aan akiwa mahiri katika kuisoma, atakuwa pamoja na Malaika watiifu. Na mwenye kuisoma Qur-aan huku akihangaika katika kuyatamka maneno yake atalipwa ujira mara mbili” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenyezi Mungu kwa Kitabu hiki Atayanyanua makundi ya watu na Atayaacha (makundi) mengine” [Muslim]

 

 

KUMI LA MWISHO

Hii ni tafsiri ya makala yaliyoandikwa na Al-Haafidh Ibn Rajab Al-Hanbaliy niliyobahatika kuyasoma na kufaidika nayo sana, nikaona bora kuyatafsiri katika lugha ya Kiswahili ili na wenzangu wafaidike pia:

BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym,

Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu peke Yake na swalah na salaam zimfikie yule ambaye hapana Mtume baada yake, Amma ba’ad:

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) amesema:

“Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) linapoingia kumi la mwisho akiikaza vizuri shuka yake, akikesha usiku wake na akiamsha watu wa nyumba yake” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

‘AMALI ZA KUFANYA KATIKA KUMI LA MWISHO LA RAMADHAAN

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akilihusisha kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhaan kwa ‘amali zifuatazo ambazo hakuwa akizifanya katika siku nyingine zisizokuwa hizo:

 

·        AKIKESHA

Na maana ya kukesha inaweza kuwa alikuwa akifanya ibada usiku kucha, na hii inatokana na Hadiyth ya Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) aliposema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa katika siku ishirini za mwanzo za Ramadhaan akichanganya baina ya Swalah na kulala, lakini zinapobaki siku kumi (yaani za mwisho), alikuwa akipania na kuikaza barabara shuka yake” [Ahmad bin Hanbal]

Huenda pia ikawa na maana kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akikesha sehemu kubwa ya usiku na si usiku wote, na hii inatokana na Hadiyth nyingine ya Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) katika Swahiyh Muslim isemayo:

“Sikumbuki kama aliwahi kuswali usiku woote mpaka asubuhi”

 

·        AKIAMSHA WATU WAKE

Alikuwa akiamsha watu wake kwa ajili ya kuswali katika usiku wa kumi la mwisho tofauti na usiku wa siku nyingine.

Anasema Sufyaan At-Thawriy:

“Napenda linapoingia kumi la mwisho mtu awe anaswali nyakati za usiku na ajitahidi sana ndani yake, na awaamshe watu wa nyumba yake pamoja na wanawe ikiwa wataweza kustahamili, kwani imesihi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akimgongea mlango Bibi Faatwimah na ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhum) huku akiwaambia;

“Hamuamki mkaswali?”

Na imesihi pia kuwa akishamaliza kuswali Tahajjud katika nyakati za usiku na kabla ya kusali Witri alikuwa akimuamsha Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa), na imepokelewa pia kupendeza kwa mtu na mkewe kuamshana kwa ajili ya kusali tahajjud hata ikibidi kummichia maji mwenzake usoni.

Imetolewa na Imaam Maalik katika Muwattwaa kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akishaswali kiasi cha kuswali katika nyakati za usiku, na inapoingia nusu ya pili ya usiku akiwaamsha watu wa nyumba yake kwa ajili ya kuswali huku akiwasomea Aayah ifuatayo:

“Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo” [Twaahaa: 132]

 

·        AKIIKAZA VIZURI SHUKA YAKE

Ama kuhusu ‘kuikaza vizuri shuka yake’, Ma’ulamaa wamekhitalifiana juu ya tafsiri yake. Wapo wanaosema kuwa hii ni kutujulisha juu ya jitahada kubwa anayofanya katika ibada ndani ya kumi la mwisho. Na wengine wakasema kuwa maana yake ni kuwa alikuwa akijiepusha kulala na wake zake, na zipo riwaya zinazotilia nguvu maana hii zinazoeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa hapandi kitandani mpaka imalizike Ramadhaan. Na katika Hadiyth iliyosimuliwa na Anas (Radhiya Llaahu ‘anhu) anasema;

“Alikuwa akilikunja tandiko lake na kuwaepuka wake zake”.

 

·        KUAKHIRISHA FUTARI MPAKA WAKATI WA DAKU

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) na pia kutoka kwa Anas (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiichelewesha futari yake na kuila wakati wa daku. Na Hadiyth yenyewe kama ilivyoelezwa na Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) inasema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa inapoingia Ramadhaan akiswali nyakati za usiku na akilala (pia), na linapoingia kumi la mwisho akiikaza shuka yake vizuri, na akijiepusha na wake zake (kulala nao), na alikuwa akikoga baina ya adhana mbili na alikuwa akiila futari yake wakati wa daku” [Ibni Abi ‘Aaswim]

 

Na kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:

“Msiiendeleze (Swawm yenu), (lazima mule futari) na kama yeyote kati yenu anataka kuendelea na Swawm (bila kula futari yake), basi aendelee mpaka wakati wa daku (tu)”.

Wakasema;

“Lakini wewe unaendeleza ee Mtume wa Mwenyezi Mungu”.

Akasema;

“Mimi nakhitilafiana na nyinyi, mimi nina mlishaji anayenilisha na mnywishaji anayeninywisha” [Al-Bukhaariy]

Kutokana na haya, inaonesha kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa anaendela na Swawm yake usiku wote, na huenda ikawa alikuwa akifanya hivyo kwa sababu alikuwa akiona kuwa anakuwa mwepesi zaidi katika jitihada zake za kufanya ibada nyakati za usiku ndani ya kumi la mwisho la Ramadhaan, na hakuwa akipata udhaifu wowote kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa akimlisha na kumnywesha.

 

·        KUOGA BAINA YA ADHANA MBILI

Tulitangulia kueleza katika Hadiyth ya Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) kuwa (Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ‘alikuwa akikoga baina ya adhana mbili’, na kusudi lake ni kuwa alikuwa akioga baina ya adhana ya Magharibi na adhana ya ‘Ishaa.

Anasema Ibn Jariyr:

“Walikuwa wakipendelea kuoga kila usiku katika kumi la mwisho. Na Al-Nakha’iy alikuwa akikoga katika kumi la mwisho kila usiku, na walikuwepo miongoni mwao waliokuwa wakipenda kuoga na kujipaka mafuta mazuri kila usiku wanaoutegemea kuwa Laylatul Qadr itakuwa ndani yake.

Kutokana na haya inatubainikia kuwa kila usiku unaotegemewa kuwa Laylatul Qadr utakuwa ndani yake inapendeza mtu kuoga na kuvaa nguo nzuri na kujipaka mafuta mazuri, na pia inapendeza kufanya hivyo kila Ijumaa na katika Sikukuu na inapendeza mtu kuvaa vizuri katika kila Swalah.

Na kujipamba sehemu za nje ya mwili hakukamiliki pambo lake mpaka mtu ajipambe ndani ya nafsi yake pia kwa kujitakasa kutokana na madhambi yake kwa njia ya kutubu na kurudi kwa Mola wake. Kwani kujipamba mtu mwili wake wakati ndani yake kumeharibika hakutomsaidia kitu. Na haijuzu kumkabili Mfalme wa wafalme Mwenye kujuwa yaliyo dhahir na yaliyo siri na yaliyofichikana zaidi kuliko siri, ambaye hatizami nyuso zenu, bali anazitizama nyoyo zenu na matendo yenu bila ya mtu kujitakasa nje na ndani yake.

Kwa hivyo atakayesimama mbele Yake inampasa ajipambe nje yake kwa nguo safi na ndani yake kwa moyo msafi wenye kumcha Mungu.

 

 

ITIKAFU

Katika Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu anhaa) amesema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akifanya itikafu katika kila kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhaan mpaka alipofariki dunia.”

Na katika Swahiyh Al-Bukhaariy, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akifanya itikafu katika kila Ramadhaan siku kumi, ama katika mwaka alofariki ndani yake alifanya itikafu siku ishirini”.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akifanya itikafu katika siku kumi zile ambazo ndani yake unatarajiwa usiku wa Laylatul Qadr ili asijishughulishe na jingine ghayri ya kumuomba na kumdhukuru Mola wake.

Hujitenga na kuacha shughuli zake zote kwa ajili ya kufanya itikafu kwa moyo wake wote ili apate kumtii Mola wake na kujikurubisha Kwake.

Kwa hivyo mwenye kufanya itikafu anakuwa amejitenga na kuacha shughuli zake zote kwa ajili ya kumtii Mola wake kwa moyo wake wote, na kwa ajili hiyo hapana kinachomshughulisha isipokuwa twa’aa ya Mola wake na kufanya yale yanayomridhisha tu.

Na kila mja anapomjua zaidi Mola wake akampenda, basi huwa hastarehe isipokuwa pale anapoacha shughuli zake zote kwa ajili ya kumuabudu.

 

 

LAYLATUL QADR

·        Mwenyezi Mungu Anasema:

“Hakika Tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatul Qadr (usiku wenye heshima kubwa).

Na jambo gani litakalokujulisha (hata ukajua) ni nini huo usiku wa Laylatul Qadr?

Huo usiku wa hishima ni bora kuliko miezi elfu” [Al-Qadr: 1-3]

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema juu ya mwezi wa Ramadhaan;

“Ndani yake mna usiku ulio bora kuliko miezi elfu, na alonyimwa kheri zake, basi amenyimwa (amekula khasara)” [Ahmad na An-Nasaaiy]

 

Ama kuhusu ‘amali za mtu kufanya katika usiku wa Laylatul Qadr, imepokelewa Hadiyth sahihi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa amesema;

“Atakayesimama usiku wa Laylatul Qadr kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa alotanguliza katika madhambi yake”.

Na maana ya neno ‘kusimama usiku wake’, ni kuuhuisha usiku huo kwa kuswali Tahajjud, na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimtaka Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anhaa) awe anaomba du’aa ndani yake.

 

Sufyaan Ath-Thawriy amesema;

“Du’aa ndani yake usiku huo kwangu mimi ni bora kuliko Swalah”.

Na kusudi lake ni kuwa kuomba du’aa kwa wingi ndani ya Swalah katika usiku huo ni bora kuliko Swalah isiyokuwa na du’aa ndani yake, na kama mtu atasoma Qur-aan na kuomba du’aa, hii itakuwa bora zaidi.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiswali ndani ya usiku wa Laylatul Qadr huku akisoma Qur-aan kwa utulivu, na kila anapoifikia Aayah inayozungumzia Rehma, alikuwa akimuomba Mwenyezi Mungu Amrehemu, na anapoifikia Aayah inayozungumzia adhabu alikuwa akimuomba Amuepushe nayo. Kwa hivyo katika Swalah yake yalikuwa yakijumuika mambo manne; Swalah, kusoma Qur-aan, kuomba du’aa na kutafakari, na hii ndiyo ‘amali bora iliyokamilika kupita zote katika usiku wa kumi la mwisho na katika usiku mwengine pia.

 

Bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anhaa) alisema kumuuliza Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):

“Unaonaje ninapofanya ibada katika usiku wa Laylatul Qadr niwe nikisema nini?”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia;

“Sema; “Allaahumma innaka ‘afuwun tuhibbul ‘afwa, faafu ‘anniy.”

Na maana yake ni:

“Mola wangu wewe ni Mwingi wa kusamehe, unapenda kusamehe, kwa hivyo nisamehe”.

Na ‘Al-‘Afuwwu’, ni katika majina ya Mwenyezi Mungu, na Yeye ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya waja Wake, Mwenye kuyafuta na kuyaondoa na Mwenye kuacha kumtia adabu anayestahiki.

Na kwa vile Yeye Anapenda kusamehe, kwa hivyo bila shaka Anapenda pia waja Wake wawe wanasameheana wao kwa wao, na wakishasameheana wao kwa wao, na Yeye Anawapitishia ‘afwa Yake. Na Mwenyezi Mungu Anapenda kusamehe kuliko kuadhibu. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akisema;

“Najikinga kwa radhi Zako kutokana na ghadhabu Zako, na najikinga kwa kusamehe Kwako kutokana na adhabu Yako” [Muslim]

 

Na tumeamrishwa kuomba maghfira katika usiku wa Laylatul Qadr baada ya kujitahidi katika kufanya ‘amali njema nyakati za usiku katika kumi la mwisho, na hii ni kwa sababu ‘wanaojua’, wanajitahidi katika kufanya ‘amali njema huku wakiona kama kwamba hawakufanya lolote, kisha wanamuomba Mola wao awasamehe kama kwamba wamefanya madhambi au wamepunguza katika haki za Mola wao.

 

 

SABABU ZA MAGHFIRAH KATIKA MWEZI WA RAMADHAAN

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefunga Ramadhaan kwa imani na kutaraji thawabu, atasamehewa yaliyotangulia katika madhambi yake, na atakayesimama (akaswali) usiku wa Laylatul Qadr kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa yaliyotangulia katika madhambi yake”.

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu ‘anhu) pia kuwa amesema; ‘Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema;

“Atakayeswali usiku wa Ramadhaan kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa madhambi aliyotanguliza” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

·        Hadiyth hizi zilizosimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu ‘anhu) zinatufundisha kuwa kila moja katika sababu tatu hizi zinasababisha kusamehewa mtu madhambi yake aliyotanguliza.

Na mambo yenyewe ni Swawm ya mwezi wa Ramadhaan, kuswali katika usiku wake (Taaraawiyh), na kuswali katika usiku wa Laylatul Qadr (Tahajjud).

Kuswali katika usiku wa Laylatul Qadr peke yake kunatosheleza mtu kufutiwa madhambi yake, yote sawa ikiwa katika siku ya mwanzo ya kumi la mwisho au kati yake au mwisho wake, na yote sawa pia ikiwa ameihisi Laylatul Qadr au hakuihisi, na kufutiwa madhambi kunaendelea mpaka mwezi unapomalizika.

 

Ama katika kufunga mwezi wa Ramadhaan na kuswali usiku wake (Taarawiyh), ili mtu asamehewe madhambi yake, sharti awe amefunga na kusali mwezi mzima.

Akishaukamilisha mwezi, Muislamu anakuwa keshatimiza kufunga Ramadhaan na kuswali ndani ya usiku wake, na kwa ajili hiyo anastahiki kughufiriwa madhambi yake baada ya kutimiza masharti mawili hayo ya kufunga na kuswali.

 

·        Kwa hivyo atakayeukamilisha mwezi wa Ramadhaan kwa kufunga na kuswali atakuwa keshakamilisha sharti alopewa, na kitakachobaki ni kupokea ujira wake kutoka kwa Mola wake na ujira huo ni kughufiriwa madhambi yake. Na Waislamu wanapotoka kwenda kuswali siku ya ‘Iyd wanagawiwa ujira wao huo na kwa ajili hiyo wanarudi majumbani mwao wakiwa washalipwa ujira wao kwa ukamilifu. Na atakayepunguza katika ‘amali zake, na ujira wake pia utapunguzwa. Kila kitu kwa hesabu yake, na kwa ajili hiyo mtu asiilaumu isipokuwa nafsi yake.

Amesema Sulaymaan:

“Swalah ni mezani, atakayekamilisha na Mwenyezi Mungu Atamkamilishia, ama atakayepunguza, basi wenyewe mnajuwa nini Mwenyezi Mungu Amesema juu ya wapunjao”

((Waylun lilmutwaffifiyn (maangamizo yatawathubutikia wapunjao))

Swalah na ibada zote hukmu zake ni kama hivyo, atakayekamilisha, huyo anakuwa kipenzi cha Mwenyezi Mungu, ama atakayepunja basi Waylun lilmutwaffifiyn.

Basi haoni hayaa mtu, katika matamanio ya nafsi yake anafanya kwa ukamilifu, kisha anakwenda kupunja katika Swawm na Swalah yake?

 

·        Watu wema waliotangulia walikuwa wakijitahidi kufanya amali zao kwa ukamilifu kisha wanajishughulisha kumuomba Mwenyezi Mungu Azikubali ‘amali zao hizo huku wakiogopa Mwenyezi Mungu Asije akazikataa.

Hawa ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Amesema juu yao;

“Na hao ambao wanatoa waliyopewa, na hali nyoyo zao zinaogopa” [Al-Muuminuun: 60]

Imepokelewa kuwa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akisema;

“Kuweni watu mnaojishughulisha sana na kukubaliwa kwa ‘amali zenu kuliko mnavyojishughulisha na amali zenyewe, hamkumsuikia Mwenyezi Mungu aliposema;

“Mwenyezi Mungu huwapokelea wamchao tu?” [Al-Maaidah: 27]

 

Na kutoka kwa Al-Hasan (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:

“Hakika Mwenyezi Mungu Ameujaalia Mwezi wa Ramadhaan kuwa ni uwanja wa waja Wake, wanashindana ndani yake katika kumtii na katika kutaka radhi Zake. Wengine wanashinda na kufuzu, na wengine wanabaki nyuma kisha wanajuta. Inastaajabisha kuona watu wanacheka na kucheza katika siku ambazo wafanyao mema wanafuzu na wafanyao maovu wanakula hasara”.

 

Na miongoni mwa sababu za mtu kusamehewa madhambi yake ni kumfuturisha aliyefunga, kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kuomba maghfirah. Du’aa ya aliyefunga inakubaliwa wakati anapokuwa amefunga na baada ya kufuturu, na pia Malaika wanawaombea maghfirah waliofunga mpaka pale wanapofuturu.

Kwa vile sababu za mtu kusamehewa madhambi ndani ya mwezi huu ni nyingi sana, basi mtu anayenyimwa maghfirah ndani yake huwa amekula hasara kikweli.

 

·        Basi lini anaweza kughufiriwa yule aliyekosa maghfirah katika mwezi huu? Lini anaweza kusamehewa yule aliyekataliwa ombi lake katika usiku wa Laylatul Qadr? Atatengenea lini yule asotengenea ndani ya mwezi huu? Lini ataamka yule asiyeujua utukufu kisha akaghafilika katika mwezi wa Ramadhaan? Kisichochumwa na kuvunwa kinapokuwa juu ya mti wakati wa mavuno, basi matokeo yake kitakatwa na kuchomwa moto, na atakayefanya mchezo asipande siku za kupanda, basi siku ya kuvuna hatovuna isipokuwa majuto na hasara.

 

 

RAMADHAAN MWEZI WA KUEPUSHWA NA MOTO

Kwa vile katika kumi la mwisho la Ramadhaan watu wengi wanaepushwa na Moto, na kwa vile kusamehewa kwa madhambi kunapatikana pia kwa njia ya kufunga na kusali, ndiyo maana Mwenyezi Mungu akatutaka pale mwezi unapomalizika tumtukuze na kumshukuru.

Mwenyezi Mungu Anasema:

“Mtimize hesabu hiyo na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwa Amekuongozeni, ili mpate kumshukuru” [Al Baqarah: 185]

Kwa hivyo shukrani zote ni Zake yule aliyewaneemesha waja Wake kwa kuwawezesha kufunga na kwa kuwaghufuria madhambi yao na kuwaepusha na Moto.

Ewe ambaye Mola wake amemuacha huru na Moto, usije ukarudia tena baada ya kuepushwa nao. Mola wako anakuepusha nao na wewe bado tu unendelea kuusogelea? Mola wako anakuepusha nao na wewe hutaki kuukimbia?

 

·        Kwa hivyo anayetaka kunusurika na Moto katika mwezi wa Ramadhaan azitafute sababu zitakazomwezesha aachwe huru nao, na Mwenyezi Mungu Amezieneza sababu hizo ndani ya mwezi huu.

Katika Swahiyh ya Ibn Khuzaymah imeandikwa:

“Zidisheni ndani yake mambo manne. Mambo mawili kwa ajili ya kumridhisha Mola wenu na mambo mawili hamwezi kuepukana nayo;

Ama mambo mawili mtakayomridhisha kwayo Mola wenu ni kutamka ‘Laa ilaaha illa Allaah’, na kusema ‘Astaghfirullaah’.

Ama mawili msiyoweza kuepukana nayo; Mumuombe Mola wenu akuingizeni Peponi na akuepusheni na Moto.”

 

Sababu zote nne zilizotajwa katika Hadiyth hii zinamwezesha mtu aachwe huru na Moto na kupata maghfirah, na hii ni kwa sababu tamko la ‘Tawhiyd’; ‘Laa ilaaha illa Allaah’, linaondoa madhambi na kuyafutilia mbali, na neno hili ni sawa na mtu kumuacha huru Mtumwa.

Ama neno ‘Astaghfirullaah’, litasababisha kusamehewa mtu madhambi yake, na du’aa ya aliyefunga inakubaliwa pale anapokuwa amefunga na hata anapofuturu. Na Ishtighfaar bora ni ile inayoambatanishwa na tawbah. Kwani anayeomba maghfirah kwa ulimi wake wakati moyo wake umeazimia baada ya kumalizika mwezi kurudi tena katika maasi, huyo Swawm yake inakataliwa na mlango wa tawbah anafungiwa.

Katika du’aa muhimu pia ni kumuomba Mwenyezi Mungu Akuingize Peponi na akuepusha na Moto, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kusema juu yake;

“Hayo ndiyo lengo letu” [Abu Daawuud na Ibn Maajah]