SIFA ZA MUISLAMU
Na Omar Rijal
Kujiepusha
na chuki
Chuki na uadui ni kazi ya shetani. Penye
chuki na uadui hapana jema lolote linalofanyika na
ni furaha kwa shetani. Chuki inayoruhusiwa kwa
Waislamu ni ile ya kuchukia uovu na maadui wa Allah (s.w.) - maadui wa Uislamu
na Waislamu.
Waislamu wanakatazwa kuwa na urafiki na maadui wa
Allah.
Enyi mlioamini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu
kuwa marafiki, mnaowapelekea (habari zenu) kwa ajili ya urafiki hali yakuwa
wameishaikanusha haki iliyokujieni..." (60:1).
Enyi mloamoni! Msifanye urafiki na watu ambao
Mwenyezi Mungu amewakasirikia; na wamekata tamaa ya kupata malipo ya Akhera
kama
walivyokata tamaa makafiri walio makaburini... (60:13).
Enyi mloamoni! Msifanye urafiki na wale
walioifanyia mzaha na mchezo dini yenu miongoni mwa wale waliopewa kitabu
kabla yenu na miongoni mwa makafiri. Na mcheni Mwenyezi Mungu
kama
nyinyi na wenye kuamini. (5:57).
Pamoja na hivyo haina maana Waislamu wasiwafanyie
uadilifu hawa maadui wa Allah na maadui wa Uislamu, bali Waislamu wataendelea
kuwatendea wema na kuishi nao kwa wema iwapo watataka amani.
Kuwa mwenye Kusamehe
Muislamu anatakiwa ajenge tabia ya kuwavumilia wengine. Awe
na tabia ya kujihesabu. Ajione kuwa naye
kama
binaadamu wenzake ni mkosaji na angependa asamehewe na wale aliowakosea kwa
makusudi au kwa bahati mbaya. Kitendo cha kuwasemehe wale waliokukosea
ni kitendo cha uchaji Mungu chenye malipo makubwa
mbele ya Allah (s.w.)
Kama inavyobainishwa
katika aya zifuatazo:
Na yaendeeni upesi upesi maghufira ya Mola wenu na Pepo (yake) ambaye upana
wake (tu) ni (sawa na) mbingu na ardhi. (Pepo) iliyowekewa
wamchao Mungu. Ambao hutoa katika (hali ya) wasaa
na katika (hali ya) dhiki, na wazuiyao ghadhabu na wanasamehe watu (na
wawafanyiao ihsani); na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao ihsani.
(3:133-134).
Basi vyote hivi mlivyopewa ni starehe ya maisha ya
dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na cha kudumu (milele).
Watakistahiki wale walioamini na wakawa
wanamtegemea Mola wao. Na wale wanaojiepusha na
madhambi makubwa na mambo mabaya, na wale ambao wanapokasirika husamehe.
(42:36-37).
Mwenye kuwasamehe wengine husamehewa makosa yake na
Allah (s.w.):
Na wasiape wale wenye mwendo mzuri (wa dini) na wenye wasaa (katika maisha
yao)
miongoni mwenu (wasiape kujizuia) kuwapa walio jamaa na maskini na waliohama
kwa njia ya Mwenyezi Mungu; na waachilie mbali, (wapuuze yaliyopita.
Linalopita hupishwa); Je, nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu
akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
msamaha (na) mwingi wa rehema. (Basi nyinyi sifikeni kwa
sifa hizi). (24:22).
Naye Mtume (s.a.w.) Anatufahamisha ubora wa
kusamehe katika hadithi zifuatazo:
U'qbah bin Amir (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Ee U'qbah! Je,
nikufahamishe juu ya watu wema kuliko wote katika dunia hii
na akhera?" Alijibu Ndio, Akasema (Mtume): "Utaendeleza
uhusiano mwema na mtu aliyevunja uhusiano kati yako
na yeye; utampa yule aliyekunyima; na utamsamehe yule aliyekudhulumu".
(Baihaqi).
Abu Hurairah (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume waallah
amesema kuwa Musa (a.s.), mwana wa Imran, aliuliza: Ee Mola wangu!
Nani, katika waja wako anayeheshimika (Mwenye hadhi) zaidi
mbele yako? (Allah) alimjibu: Yule anayesamehe japo ana nguvu au uwezo
(wa kutosamehe) (Baihaqi).
Hivyo Allah (s.w.) Anatuusia:
"Shikamana na kusamehe na amrisha mema na wapuuze majahili:.
(7:199).
Kukataa kusamehe baada ya kuombwa msamaha na yule
aliyekukosea ni jambo ovu. Allah (s.w.) Hamsamehe
yule asiyesamehe wanaadamu wenzake. Ukweli ni
kwamba wanayotukosea wanaadam wenzetu hata tuyaone ni makubwa vipi, ni madogo
sana
ukilinganisha na makosa yetu kwa Allah (s.w.). Inakuaje sasa tushindwe
kusamehe haya makosa madogo madogo na wakati huo
tunatamani kusamehewa milima na milima ya makosa yetu?
Hivyo, yule anayetaka kusamehewa na Allah, basi awe
mwepesi wa kuwasamehe wanaadamu wenzake. Kuhusu uovu wa
kukataa kuwasamehe wale waliokiri makosa
yao
na kuomba msamaha, anasema Mtume (s.a.w.):
"Kama
mtu, anakiri makosa yake kwa mwingine na kutaka msamaha, na yule akatakaa
kutoa msamaha, basi hatanyweshwa maji ya kawthar (huyo aliyekataa, kusamehe).
(Tabrani).
Kujizuia na Hasira
Kujizujia na hasira ni tabia njema inayoambatana na tabia ya kusamehe.
Hasira humpata mtu anapooudhiwa. Wakati mwingine
huja ghafla na kumnyima mtu wakati wa kufikiri.
Hasira zinaongozwa na shetani, hivyo humnyima mtu
nafasi ya kutumia akili, hekima na busara. Hivyo
humpelekea mtu kufanya matendo ambayo hugeuka kuwa majuto baadaye.
Hasira hasara.
Kujizuilia na hasira ni kitendo cha ucha Mungu
chenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.). Rejea Qur'an (3:133-134)
na (42:36-37).
Pia ubora wa kujizuilia na hasira unadhihirika katika Hadithi zifuatazo:
Abu Hurairah amesimulia kuwa mtu mmoja alimuomba Mtume(s.a.w.):"Niwaidhi'.Mtumeakasema:
"Usighadhibike". Kisha akarudia mara nyingi akisema"
Usighadhibike. (Bukhari).
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema:
"Mtu mwenye nguvu si bingwa wa mieleka bali mtu mwenye nguvu ni yule
anayejizuilia na hasira". (Bukhari na Muslim).
Ibn Umar amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: "Hapana
mja aliyemeza kidonge kichungu mbele ya Allah (s.w.) Kuliko kidonge cha hasira
alichokimeza, huku akitaraji radhi ya Allah (s.w.)." (Ahmad).
Mbinu za kujizuia na hasira zimebainishwa katika
Qur'an
kama
ifuatavyo:
Shikamana na kusamehe na amrisha mema na wapuuze majahili (wajinga). Na
kama
wasi wasi wa shetani ukikusumbua basi (sema:Audhubillah)
jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Bila shaka yeye ndiye asikiaye
na ajuaye. (7:199-201).
Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa mbinu za
kujizuilia na hasira ni hizi zifuatazo:
(i) Kushikamana na kusamehe.
(ii) Kushikamana na kuamrisha mema.
(iii) Kuwapuuza majahili.
(iv) Kujikinga kwa Allah (s.w.) na uovu wa shetani.
Pia Mtume (s.a.w.) Anatupa mbinu nyingine za kupambana na
hasira katika hadithi zifuatazo:
Atiyyah bin Urwah Ba'id ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Hakika hasira
zinatoka kwa Shetani, na Shetani ameumbwa kutokana na moto na hakika moto
huzimishwa na maji. Kwa hiyo yoyote miongoni mwenu
atakayepandwa na hasira, na atawadhe". (Abu Daud).
Abu Zarr (r.a.) Ameeelza kuwa Mtume wa Allah
amesema: "Wakati wowote mmoja wenu atakapopandwa na hasira akiwa amesimama, na
akae chini.
Kama
(kwa kufanya hivyo) hasira itamtoka ni vyema;
lakini
kama
haitatoka, na alale chini." (Ahmad, Tirmidh).
Kutokana na Hadithi hizi Mtume (s.a.w.)
anatuelekeza tupunguze hasira zetu kwa:
(i) Kutia udhu
(ii) Kukaa chini iwapo tumesimama.
(iii) Kulala chini.
Kuwa na subira na Uvumilivu
Subira ni kitendo cha kuwa na uvumilivu na utulivu baada ya kupatwa na
matatizo au misuko suko mbali mbali katika maisha ya kila siku. Muislamu
anatakiwa awe ni mwenye kusubiri baada ya kupata
shida au matatizo
kama
tunavyoamrishwa katika Qur'an.
"Enyi mlioamini! Jisaidieni (katika mambo yenu)
kwa kusubiri na kuswali. Bila
shaka Allah yupo pamoja na wanaosubiri." (2:153).
"Enyi mlioamini! Subirini na washindeni wengine
wote kwa kusubiri na kuweni imara na mcheni allah mpate kufaulu".
(3:200).
Suala la kupatwa na matatizo, misiba na misukosuko
mbali mbali ni jambo la kawaida katika maisha ya hapa duniani. Hatuna budi
kufahamu kuwa ulimwengu huu haukusudiwa na Mola
Muumba uwe pepo.
Bali
umekusudiwa uwe uwanja wa kumtahini mwanaadamu.
Hivyo viumbe vyote vilivyomzingira pamoja na
matukio na miondoko yote ya maisha viko pale
kama
vifaa vya kumtahini mwanaadamu. Suala la kutahiniwa mwanaadamu limewekwa
bayana katika Qur'an:
Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai
iliyochanganyika: (ya mwanamume na mwanamke), ili tumfanyie mtihani (kwa amri
zetu na makatazo yetu) kwa hivyo tukamfanya ni Mwenye kusikia (na) mwenye
kuona. Hakika sisi tumemuongoa, (tumembainishia) njia (zote mbili hizi; kuwa
hii ndiyo ya kheri na hii ndiyo ya shari). Basi (mwenyewe
tena) atakuwa mwenye shukurani au awe mwenye kukufuru, (kukanusha). (76:2-3).
Ametukuka yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme (wote); naye
ni mwenye uwezo juu ya kila kitu. Ambaye ameumba
mauti na uhai ili kukujaribuni (kukufanyieni
mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye
ni Mwenye Nguvu na Mwenye Msamaha. (67:1-2).
Na tutakufanyieni mitihani mpaka tuwadhihirishe (wajulikane) wale wanaopigania
dini miongoni mwenu na wanaosubiri; nasi
tutadhihirisha habari zenu. (47:31).
Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, na hali hamjajiwa na
mfano wa (yale yaliyowajia) wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka
na madhara na wakatetemeshwa
sana
hata Mitime na walioamini pamoja nao wakasema: "Nusura ya Mwenyezi Mungu
itafika lini?" Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu iko
karibu. (2:214).
Je, watu wanadhani wataachwa (wasitiwe katika misukosuko)
kwa kuwa wanasema, "Tumeamini?" Basi ndio
wasijaribiwe (wasipate mitihani)? Hapana; bila shaka tuliwatia katika
taabu wale waliokuwa kabla
yao,
na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale walio wa kweli na
kuwatambulisha (wale walio) waongo. (29:2-3).
Ili
kukamilisha kusudio hili la kumjaribu (kumtahini) mwanaadamu Mwenyezi Mungu (s.w.)
Ameupamba huu ulimwengu kwa machungu na matamu yaliyochanganyika. Uzuri au
mazuri hayapatikani kwa urahisi ila mpaka kuvuka
vikwazo vingi vya matatizo na misukosuko ya namna kadhaa wa kadhaa. Na uzuri
au mazuri yanapopatikana hayabakii milele bali huwa
ni ya muda mfupi kwani nayo yamezingirwa na matatizo na mikasa elfu moja na
moja. Hii ndio sura halisi ya maisha ya huu ulimwengu.
Kwa hiyo wale wanaodhania ulimwengu huu ni mahali
pa starehe - kufurahia maisha tu bila ya kuonja machungu yake watakuwa
wamejidanganya mno na badala yake wataishi maisha ya huzuni, wasiwasi na
kukata tamaa. Kinyume chake, Waislamu wanatakiwa wawe na
uhakika juu ya maisha ya huu ulimwengu kuwa ni ya majaribio na mafanikio
yatapatikana kwa kutenda wema kwa ajili ya Allah (s.w.) Na kusubiri au
kustahamili mazito, matatizo na misukosuko yote ya maisha itakayowakabili.
Kufanya subira si jambo jepesi bali ni jambo
linalohitaji jitihada na uzima kubwa
kama Qur'an
inavyoatuusia:
Ewe Mwanangu! Simamisha swala, na uamrishe mema, na
ukataze mabaya, na usubiri juu ya yale yatakayokusibu (kwani mwenye kuamrisha
mema na kukataza mabaya lazima zitamfika tu taabu); Hakika hayo ni katika
mambo yanayostahiki kuazimiwa (na kila mtu). (31:17).
Na anayesubiri na kusamehe (atalipwa wema wake).
Bila shaka
hilo
ni katika mambo makubwa ya kuazimiwa kufanywa (na kila Muislamu). (42:43).
Kufanya subira ni kitendo cha hali ya juu cha Ucha
Mungu na Mwenyezi Mungu (s.w.) Ameahidi malipo makubwa kwa yule
atakayejitahidi kusubiri
kama
tunavyojifunza katika aya zifuatazo:
Sema: "Enyi waja wangu mlioamini! Mcheni Mola wenu.
Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema; na
ardhi ya Mungu ina wasaa. Na bila shaka wafanyao subira (wakajizuilia
na maasia na wakaendelea watapewa ujira wao pasipo hisabu". (39:10).
Na tutakutieni katika msukosuko wa (baadhi ya mambo haya); hofu na njaa na
upungufu wa mali na wa watu na wa matunda. Na wapashe
habari njema wanaosubiri. Ambao uwapatapo msiba husema:"Hakika sisi ni
wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye tutarejea (atatupa jaza (yake)"
. Hao juu
yao
zitakuwa baraka baraka zitokazo kwa Mola wao na rehema; na ndio wenye kuongoka.
(2:155-157).
Pia Mtume (s.a.w.) Anatufahamisha kuwa malipo ya subira ni
Pepo na kusamehewa madhambi
kama
tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo:
(i) Abu Hurairah (r.a.) Amehadithia kuwa Mtume wa Allah amesema, Mwenyezi
Mungu (s.w.) Amesema, "Sina malipo mengine ila pepo kwa mja wangu aliyeamini
ambaye anasubiri wakati ninapomchukulia kipenzi chake kutoka miongoni mwa
wakazi wa ulimwengu." (Bukhari).
(ii) Anas (r.a.) Amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa
Mwenyezi Mungu akisema kuwa allah (s.w.) Amesema, "Ninapomtia msuko suko mja
wangu katika vitu vyake viwili vipenzi (macho yake) na akatulia kwa subira,
nitamlipa macho yake kwa Pepo." (Bukhari).
(iii) Abu Said na Abu Hurairah wameeleza kuwa
wamemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Aslani Muumini hafikwi na makero (matatizo),
magumu au ugonjwa, huzuni au hata wasi wasi moyoni, iwe hakusamehewa dhambi
zake. (Bukhari na Muslim).
(iv) Imesimuliwa katika mamlaka ya Abu Hurairah kuwa Mtume
wa Mwenyezi Mungu amesema Muislamu mwanamume au Muislamu mwanamke
ataendelea kuwa katika majaribu juu ya maisha yake,
mali
yake na watoto wake mpaka amkabili Mwenyezi Mungu (s.w.) Katika hali ambayo
dhambi zake zote zimesamehewa. (Tirmidh).
Hivyo kila Muislamu wa kweli hanabudi kujitahidi
kusubiri kwa lolote zito litakalomfika na ajiliwaze kwa maliwazo aliyofunza
Mwenyezi Mungu (s.w.) Kwa kusema:
"Innalillaahi Wainnailayhir-Raji'uun".
Tafsiri:
"Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake yeye
tutarejea".
Muislamu hatakiwi achoke kusubiri wala asitamani kufa au kuomba kifo kutokana
na mazito yaliyomfikia:
Anas (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Pasiwe na yoyote
miongoni mwenu anayetamani kufa (au anayeomba kifo) kwa sababu ya tatizo
lolote lililomfikia.
Kama
amefika mwisho wa kuvumilia na aseme: "Ee Allah
nibakishe hai iwapo kuishi ni bora zaidi kwangu na nifishe
kama
kufa ndio bora kwangu". (Bukhari na Muslim).
Maeneo ya Subira:
Katika Uislamu subira inatakiwa ihudhurishwe katika maeneo yafuatayo:
Kwanza:
kusubiri unapofikwa na misukosuko au matatizo mbali
mbali ya kimaisha miongoni mwa khofu, kufiwa, kuugua, kuuguliwa, kukosa
maslahi ya kimaisha na matatizo mengine mbali mbali yanayowafika wanaadamu
katika maisha ya kila siku.
Pili: kusubiri au kuwa wastahimilivu katika kutekeleza maamrisho ya Allah (s.w.)
katika maisha yetu yote. Maamrisho kama kusimamisha
swala tano, kufunga Ramadhan, kuwatendea wema wazi, mayatima, maskini,
majirani na wanaadam wengine, kuchunga haki za wengine, (n.k.) ni matendo mja
anayotakiwa aendelee kuyafanya mpaka mwisho wa maisha yake. Juu ya kusimamisha
swala, tunaamrishwa katika Qur'an:
"Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kufanya hivyo..."
(20:132).
Tatu: kusubiri au kuwa wavumilivu katika kumtii allah
(s.w.) Kwa kuacha yale aliyotuharamisha. Movu mengi yaliyoharamishwa
na Allah (s.w.), machoni mwa mwanaadamu yanaonekana
kuwa mazuri na starehe yenye mvuto mkubwa. Kwa mfano nami asiyeona jinsi ule,
uzinifu, muziki, kamari, riba, hongo, nyama ya nguruwe, n.k. vinavyowavutia
walimwengu na kuwazamisha humo mamilioni. Mtume (s.a.w.)
Amesema:
Pepo imezungukwa na yasiyopendeka (vikwazo) na Moto
umezungukwa na vitu vya anasa (carnal desires), Muslim).
Nne: ni kusubiri au kustahimili maudhi kutoka kwa
wanadamu wenzetu. Misukosuko na matatizo mengi
yanayomkabili mwanadamu ni yale yanayosababishwa na wanaadamu wenzake.
Muislamu wa kweli hatalipiza kisasi kwa maovu
aliyofanyiwa na mwingine, wala hatamuapiza na kumlaani aliyemfanyia maovu hayo
bali atastahimili kwa matarajio ya kupata malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu (s.w.).
Waislamu tunatakiwa mara kwa mara tumuombe Allah (s.w.)
Atumiminie subira
kama
yeye mwenyewe anavyotuelekeza kuomba:
"... Mola wetu! Tumiminie subira na tufishe hali ya
kuwa Waislamu". (7:126).
"Mola wetu! Tumiminie subira na uithibitishe
miguu yetu, na utusaidie juu ya watu hawa makafiri". (2:250).
Kuwa Mkarimu
Ukarimu ni miongoni mwa tabia njema anayotakiwa
ajipambe nayo Muislamu. Muislamu anatakiwa awe mwepesi wa
kuwakirimu wengine kwa kuwasaidia wakati wanapokuwa katika hali ya kuhitajia
msaada bila ya kutarajia malipo yoyote kutoka kwao. Sifa ya wakarimu
inabainishwa katika aya zifuatazo:
Na huwalisha chakula maskini na mayatima na
wafungwa, na hali yakuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho). (Husema wenyewe
katika nyoyo zao wanapowapa chakula hicho): "Tunakulisheni
kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu (tu) hatutaki kwenu malipo
wala shukrani". "Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo
siku yenye shida na taabu". (76:8-10).
Pia kumfanyia mgeni takrima ni jambo lililowajibishwa kwa Waislamu, Waislamu
kama tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo:
(i) Abu Hurairah (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema,"Yule
anayemuamini Allah na siku ya mwisho hatamdhuru jirani yake, na yule
anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho atamkirimu mgeni wake na yule
anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ataongea mazuri au atakaa kimya".
(Bukhari na Muslim).
(ii) Abu Shuraikh Ka'ab (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume (s.a.w.) Amesema, "Yoyote
anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho hanabudi kumkirimu mgeni wake,
na jukumu lake (la kumhangaikia sana) ni mchana mmoja na ukarimu (kumfurahisha
mgeni) ni siku tatu na zaidi ya hapo ni sadaqa. Si vyema
kwa mgeni kuendelea kubaikia baada ya siku tatu na kuendelea kumuweka
mwenyeji wake katika hali ya uzito". (Bukhari na
Muslim).
Kiigizo chetu cha ukarimu ni Mitume wa Allah (s.w.).
Tunafahamishwa katika Qur'an juu ya ukarimu wa
Nabii Ibrahim:
Je! Imekujia hadithi ya wageni wahishimiwao wa (Nabii)
Ibrahimu? Walipoingia kwake wakasema: "Salaam (Alaykum);" Na (yeye Ibrahimu)
akasema: "(Alaykumus) Salaam". (Na katika moyo wake anasema): "Ninyi watu
nisiokujueni". Mara akaenda kwa ahali yake na
akaleta ndama aliyenona. Akampeleka karibu yao. (Walipokuwa
hawajanyosha mikono kula alisema: "Mbona hamuli!" (51:24-27).
Katika hadithi, amesimulia Ibn Abbas (r.a.) Kuwa:
Mtume (s.a.w.) Alikuwa mkarimu sana kuliko watu wote na alikuwa akizisha
ukarimu katika mwezi wa Ramadhan..." (Bukhari).
Malipo haya kuwakirimu watu ni kupata takrima ya allah (s.w.) Huko Peponi kama
inavyobainishwa katika aya zifuatazo:
"Basi Mwenyezi Mungu atawalinda (wakarimu) na shari ya siku hiyo na
kuwakutanisha na neema na furaha. Na atawajaza Mabustani (ya Peponi)
na maguo ya hariri, kwa sababu ya kusubiri (kwao).
Humo wataegemea viti vya enzi, hawataona humo jua (kali)
wala baridi (kali). Na vivuli vyake vitakuwa karibu
yao, na mashada ya matunda yake yataning'inia mpaka chini. Na
watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae.
Vigae vya fedha; wamevijaza kwa vipimo.Na humo
watanyweshwa kinywaji kilichochanganyika na tangawizi. Huo
ni mto ulio humo (Peponi) unaitwa Salsabili. Na watawazungukia (kuwatumikia),
wavulana wasiochakaa, ukiwaona utawafikiri ni lulu
zilizotawanywa. Na utakapoyaona (yaliyoko) huko utaona neema (zisizo kuwa
na mfano) na kijani kibichi na ufalme mkubwa. Juu
yao wana nguo za hariri laini, za kijani kibichi na
za hariri nzito. Na watavikwa vikuku vya fedha, na
Mola wao atawanywesha kinywaji safi kabisa (Awaambie):"Hakika haya ni malipo
yenu; na amali zenu zimekubaliwa". (76!
:11
-22).
Kujiepusha na uchoyo na ubahili
Uchoyo na ubahili ni kinyume cha ukarimu. Mtu mchoyo ana
kasoro katika imani yake. Anaona kuwa chochote alichonacho amekipata
kwa jitihada na akili yake tu.
Pia anahofu kuwa akitoa kumpa mwingine atapungukiwa au atafilisika.
Mtume (s.a.w.) Ametunabahisha hilo katika hadithi
zifuatazo:
Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Mtu anasema: "Hiki changu!
Hiki changu! Lakini ukweli ulivyo ni kwamba,
vilivyo vyake katika mali yake ni vitu vitatu: "Kile alichokula au kile
alichokitoa sadaqa (hakika) amekiweka akiba, na kingine chochote zaidi ya hivi,
hakika si vyake (si vyenye kumfaa) na ataondoka awaachie watu".
(Muslim).
Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema:
"Chakula cha watu wawili kina watosha watu watatu, na chakula cha watu watatu
kinawatosha watu wanne". (Bukhari na Muslim).
Jabir bin Abdullah (r.a.) Ameeleza: Mtume wa Allah
amesema: "Chakula cha mtu mmoja kinawatosha watu wawili na chakula cha watu
wawili kinawatosha watu wawili na chakula cha watu wawili kinawatosha watu
wanne na chakula cha watu wanne kinawashibisha watu wanane".
(Muslim).
Hivyo ukizingatia hadithi hizi, utaona kuwa hapana sababu
ya Muislamu kuwa mchoyo au bahili.
Uchoyo na ubahili ni tabia mbaya na malipo yake ni
kwenda Motoni kama inavyobainishwa katika Qur'an:
Yule anayetoa (zaka, sadaka na vingnevyo) na kumcha Mwenyezi Mungu.
Na kusadiki jambo jema (akalifuata).
Tutamsahilishia njia ya kwenda Peponi. Na afanyae
ubakhili, asiwe na haja ya viumbe wenzake.
Na akakadhibisha mambo mema (asiyafanye).
Tutamsahilishia njia ya kwendea Motoni.
Na amali zake hayatamfaa atakapokuwa anadidimmia (Motoni
humo). (92:5-11).
Kuwa Mwenye Kutosheka
Kutosheka ni kuridhika na neema uliyonayo.
Kutosheka ni utajiri kuliko utajiri wote uliopo
ulimwenguni.
Abu Hurairah (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah
amesema, utajiri si kuwa na mali nyingi lakini utajiri ni kutosheka". (Bukhari
na Muslim).
Muislamu anatakiwa awe ni mwenye kutosheka na kile
alichoruzukiwa na Mola wake. Kila mtu amekadiriwa riziki yake
na Allah (s.w.). Hakuna mwenye uwezo
wa kumpunguzia au kumzidishia mtu riziki. Hili
linabainishwa katika Qur'an katika usia wa Mzee
Luqman kwa wanawe:
Ewe mwanangu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na
uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi,
Mwenyezi Mungu analileta (amlipe aliyefanya); bila shaka Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi wa mambo yaliyofichikana, (na) Mjuzi wa mambo yaliyo dhahiri. (31:16).
Pia Allah (s.w.) Anatuhakikishia:
"Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Allah..."
(11:6).
Juu ya moyo wa kutosheka Mtume (s.a.w.) Anatuwaidhi
katika Hadithi ifuatayo:
Imesimuliwa katika mamlaka ya Abdullah Bin Amr bin Al-'As (r.a.) Kuwa Mtume wa
Allah amesema: "Yule aliyeingia Uislamu na akajaaliwa kupata riziki
inayotosheleza mahitaji yake muhimu na Mwenyezi Mungu akamfanya kuwa mwenye
kutosheka na kila alichotunukiwa, hakika amefuzu kikweli".
(Muslim).
Kujiepusha na tamaa na kuomba-omba
Kinyumke cha kutosheka ni kuwa na tamaa au kutotosheka. Kutotosheka
ni ufakiri wa moyo. Moyo wa
kutotosheka huzaa tabia nyingi mbaya ikiwa ni pamoja na upupiaji
mali,
uchoyo, na kuomba omba. Muislamu anatakiwa ajitahidi kutosheka
na alichonacho na hata
kama
anahisi yuko katika dhiki ajitahidi kujizuilia kunyoosha mkono wa kuomba
chochote kwa yoyote kwa kadiri iwezekanavyo.
Tumekatazwa katika Qur'an tuwe si wenye tamaa:
"Wala msitamani vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko
wengine. Wanaume wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma;
na wanawake nao wanayo sehemu (kamili) ya vile
walivyovichuma. Na mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu". (4:32).
Kuhusu suala la omba omba Mtume (s.a.w.) Ametuuusia katika hadithi zifuatazo:
Abu Hurairah (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Allah
amesema: "Yule aombaye ili aongezee
mali
yake, haombi lingine ila moto wa maisha. (Muslim).
Ibn Umar (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu amesema: "Kama
mmoja wenu ataomba bila ya sababu ya msingi atakutana na Allah na uso usiokuwa
na nyama." (Bukhari na Muslim).
Ibn Umar (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah
alipokuwa Mimbarini akitoa khutba juu ya kutoa sadaqa na kujizuia na kuomba
omba alisema: "Mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini. Mkono
wa juu ni ule unaotoa na wa chini ni ule unaoomba".
(Bukhari na Muslim).
Kuomba kunaruhisiwa kwa dharura zifuatazo:
(i) Mtu aliyesimama kumdhamini mtu mwingine ili kuleta suluhu kati ya wagomvi
wawili huyu anaruhusiwa kuomba hata akiwa tajiri. Kwa mnasaba huu, wadhamini
wa Misikiti, madrasa, na shughuli mbali mbali za
Kiislamu wanaruhusiwa kuomba michango ya Waislamu ili kufanikisha shughuli
hizo.
(ii) Mtu aliyepata ajali na kuharibikiwa kabisa
vitu vyote
kama
vile ajali ya moto, mafuriko, n.k.
(iii) Mtu ambaye amepigwa na ufukara na amekosa kabisa mahaitaji muhimu ya
maisha
kama
chakula, malazi na makazi. Lakini mtu akiwa kama na angalau chakula cha siku
moja na malazi na akawa na dirham 50 mkononi mwake haruhusiwi kuomba kama
tunavyofahamishwa katika hadithi zifuatazo:
Abdullah bin Mas'ud ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Anayeomba
omba watu na ilhali ana mahitaji muhimu ya maisha atakuja siku ya Kiyama na
kuomba omba kwake kama mikwaruzo, vidonda au majeraha usoni mwake. Iliulizwa:
Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni
kiasi gani kinachomtosha mtu? Akajibu: Dirham 50 au thamani yake ya
dhahabu. (Abu Daud, Tirmidih, Nasai na Ibn Majah).
Sahl ameeleza kuwa Mtume wa allah amesema: Yeyote
yule anayeomba na ilihali anajitosheleza kwa kwa mahitaji muhimu, anaomba moto
(Jahannam). Nufali ambaye ambaye ni miongoni mwa
wasimulizi wa hadithi hii katika sehemu nyingine aliuliza: Ni yupi mwenye
uwezo ambaye kuomba ni haram? Akijibu (Mtume (s.a.w.): Yule mwenye uwezo
wa kupata chakula cha asubuhi na usiku. Mahali
pengine amesema: Yule mwenye chakula cha siku moja (Usiku
na mchana). (Abu Daud).
Kujiepusha na Husuda
Husuda ni miongoni mwa magonjwa makubwa ya moyo. Mtu mwenye husuda anadonda la
chuki moyoni mwake, juu ya neema alizoneemeshwa mwingine
na Mwenyezi Mungu (s.w.). Kwa maana nyingine anachukia utaratibu
wa Mwenyezi Mungu (s.w.) aliouweka katika kugawanya
neema zake kwa waja wake. Hasidi kutokana na chuki
yake dhidi ya mja aliyeneemeshwa na Mwenyezi Mungu (s.w.), huwa tayari kwa
hali na
mali
kumdhuru mja huyo asiye na hatia yoyote. Ni kwa msingi huu Mwenyezi Mungu (s.w.)
Anatufundisha kujikinga kwake na shari za viumbe vyake, akiwepo hasidi kama
tunavyosoma katika Suratul-Falaq:
Sema: "Ninajikinga na Mola wa Ulimwengu wote na shari ya Alivyoviumba, na
shari ya giza la usiku liingiapo na shari ya wale wanaopulizia mafundoni na
shari ya hasidi anapohusudu:. (113:1-5).
Husuda husababishwa na kutotosheka na kutoridhika
na neema za Mwenyezi Mungu (s.w.). Hasidi anataka kila neema aliyotunukiwa
mwingine awe nayo yeye au mwingine abakie bila neema hiyo. Anataka awe juu ya
mwingine na aonekane wa maana pekee katika jamii.
Akihisi kuwa kuna yeyote aliyemzidi kwa cheo,
utajiri, elimu, watoto, umaarufu, (n.k.) hupandwa na moto wa chuki moyoni
mwake ambao humsukuma kufanya visa mbali mbali dhidi ya huyo anayemhisi kuwa
amemzidi au yuko sawa naye.
Muislamu anatakiwa ajitakase na uovu huu wa husuda kwa kutosheka na kile
alichonacho akijua kuwa kila neema aliyopewa mwanaadamu imekadiriwa na
Mwenyezi Mungu (s.w.) Na hapana yeyote mwenye uwezo wa kupunguza neema ya mtu
aliyekadiriwa na Mola wake hata kwa kiasi cha chembe ndogo iliyoje na hakuna
yeyote awezaye kumuongezea mtu neema kuliko vile alivyokadiriwa na Mwenyezi
Mungu (s.w.).
Pia Muislamu wa kweli anajitahidi kujiepusha na
husuda ili asije akaziunguza amali zake njema alizozitanguliza na akawa
miongoni mwa watakaohasirika katika maisha ya akhera.
Abu Hurairah (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah
amesema:
"Kuweni waangalifu juu ya husuda, kwani husuda inaunguza
mali
njema za mtu
kama
moto unavyounguza kuni. (Abu Daud).
Husuda au wivu unaoruhusiwa ni ule unaofanywa kwa
ajili ya kushindana katika kufanya mema. Wivu wa
namna hii sio ule wa kuchukia kuwa kwa nini fulani ameneemeshwa bali ni ule
unaomfaya mja ajitahidi zaidi kufanya mema
kama
anavyofanya au kumzidi mwingine. Mtume (s.a.w.) Ametufahamisha ni husuda ya
namna gani inayoruhusiwa kwa Muislamu katika hadithi ifuatayo:
Ibn Mas'ud (r.a.) Amehadithia kuwa Mtume wa Mwenyezi mungu amesema: Hapana
husuda (inayoruhusiwa katika Uislamu) ila kwa watu wawili: "Mtu ambaye
Mwenyezi Mungu (s.w.) Amempa mali na akampa uwezo wa kuitumia katika njia ya
Mwenyezi Mungu na mtu ambaye Mwenyezi Mungu amempa elimu na hekima akawa
anafundisha wengine pamoja na yeye mwenye kuingiza elimu hiyo katika vitendo".
(Bukhari na Muslim).
Kumtegemea Mwenyezi mungu (s.w.) na kuwa Jasiri:
Muislamu wa kweli daima humtegemea Mwenyezi Mungu kwa kila kitu. Ana yakini
kuwa hapana lolote litakalomfikia, baya au zuri, ila
litakuwa linatoka kwa Mwenyezi Mungu ana yakini kuwa ulinzi wa maisha yake na
mahitajio yake yote ya kimaisha yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu (s.w.).
Mwenyezi Mungu (s.w.) Anatuamrisha tumtegemee Yeye
tu. Hebu turejee aya zifuatazo:
Na tegemea kwa Yule aliye na uhai wa milele ambaye
hatakufa. (25:58).
"... Na kwa Mwenyezi Mungu awategemee Waislamu. Na
tuna nini tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali
ametuonyesha njia zetu. Na tutayavumilia maudhi yenu.
Basi kwa Mwenyezi Mungu tu wategemee wategemeao". (14:11-12).
"... Na anayemuogopa Mwenyezi Mungu, (Allah) humtengenezea njia ya kuokoka (na
kila balaa); na humpa riziki kwa namna asiyoitazamia. Na
anayemtegemea Mwenyezi Mungu yeye humtoshea. Kwa yakini Mwenyezi Mungu
anatimiza kusudio lake, Hakika Mwenyezi Mungu amekwisha kiwekea kila kitu
kipimo chake".(65:2-3).
Kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa kila jambo na hasa
wakati wa dhiki na kuhitajia msaada, huzidisha imani na ujasiri kwa waumini.
Hebu turejee aya zifuatazo:
Wale ambao watu waliwaambia:"Watu wamekukusanyikieni. Kwa
hiyo waogopeni". Lakini (maneno hayo) yakawazidishia imani wakasema:
Mwenyezi Mungu anatutosha. Naye ni mlinzi bora
kabisa. Basi wakarudi (vitani (na neema za Mwenyezi
Mungu na fadhila (zake), hakuna ubaya uliowagusa; na wakafuata yanayomridhisha
Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu". (3:173-174).
Na Waislamu walipoyaona majeshi walisema, 'Haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyezi
Mungu na Mtume wake. Mwenyezi Mungu
na Mtume wake wamesema kweli, na (jambo hili)
halikuwazidishia ila imani na utii. (33:22).
Hakika waumini wa kweli ni wale ambao anapotajwa
Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu; na wanaposomewa aya zake huwazidishia
imani na wakamtegemea Mola wao tu basi. (8:2).
Hivyo Waislamu hatuna budi kumtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.)
Kwa kila hali. Tukifanya hivyo imani yetu itazidi na
tutakuwa na moyo wa ujasiri wa kutuwezesha kupambana na hali yoyote ngumu
itakayotukabili kwa sababu tunayakini
kama halitufikii
lolote, baya au zuri, ila liko katika makadirio ya Mwenyezi Mungu (s.w.). Ni
vyema hapa tukumbushe kuwa kumtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.)
Ni kutekeleza wajibu wetu kwa juhudi na maarifa katika jambo lolote
tunalolifanya, kisha matokeo ya jitihada zetu tumuachie Mwenyezi Mungu (s.w.).
Hii hasa ndio maana ya kumtegemea Allah (s.w.)
Tunayofundishwa katika Qur'an
kama
inavyodhihirika katika aya zifuatazo:
Naam, wanaoelekeza nyuso zao kwa Mwenyezi Mungu na wakawa ni watendaji mema,
basi wao watapata malipo
yao kwa
Mola wao, wala haitakuwa hofu juu
yao
wala hawatahuzunika. (2:112).
Na kwamba, mtu hatapata ila kwa yale anayoyafanya.
(53:39).
Kinapokosekana kipengele hiki cha "kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila hali"
katika tabia au mwendo wa mja, nafasi yake inajazwa
na kipengele cha "woga". Woga na khofu juu ya
matukio mbali mbali ya maisha ya hapa ulimwenguni husababishwa na uhaba wa
imani juu ya Allah (s.w.) Na sifa zake. Mtu asiyemtegemea mwenyezi Mungu
hudhania kuwa mafanikio yote ya kimaisha hupatikana na
uwezo wa mwanaadam na kuwa ni mwanadamu pekee mwenye uwezo wa kujikinga na
shari zote zinazomkabili. Dhana hii humtia mtu katika wasi wasi
na woga atakapohisi kuwa tatizo au dhana fulani
linalomkabili litamshinda nguvu kwa kuwa hana uwezo au msaada wa kibinaadam wa
kumuwezesha kupambana nalo.
Muislamu wa kweli hapaswi kuwa mwoga wa chochote
kwa sababu hapana chochote kinachoweza kumdhuru, ila awe amekadiria hivyo
Mwenyezi Mungu (s.w.) na hapana mja awezaye kuepa ajali yake aliyoandikiwa na
mwenyezi Mungu. Muislamu anatakiwa awe imara katika kusimamisha Dini ya
allah katika kila kipengele cha maisha yake, bila
ya kuhofu chochote kwani yeye dima yuko chini ya ulinzi na uangalizi wa
Mwenyezi mungu (s.w.) Na halitamsibu ila lile alilomuadikia Mwenyezi Mungu (s.w.).
Sema: 'Halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi mungu. Yeye ni Mola wetu:.
Basi Waislamu wamtegemee Mwenyezi Mungu tu. (9:51).
Kujiepusha na woga na kukata tamaa
Pia Muislamu hatakiwi kukata tamaa na rehema za Mwenyezi Mungu (s.w.). Hakuna
kinachoshindikana kwa Mwenyezi Mungu Muislamu hana
budi kufanya jitihada katika kufanikisha jambo muhimu la maisha kwa kufuata
njia za hali anazoziridhia Mwenyezi Mungu (s.w.).
Kama
jambo
hilo
lina kheri na Yeye, basi mwenyezi Mungu (s.w.) Atalifanikisha. Mzee Yaquub (a.s.)
Akiwausia wanawe wasichoke kumtafuta Yusuf na ndugu yake alipowaambia:
"Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na Nduguye,
wala msikate tamaa na Rehema ya Mwenyezi Mungu. Hawakati tamaa
na Rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri".
(12:87).
Pia iwapo baada ya Muislamu kufanya juhudi na kutumia uwezo wake wote,
hakupata mafanikio aliyokusudia, asikate tamaa bali aridhike kuwa matokeo hayo
ndiyo yenye kheri mwake kwa kuzingatia Qur'an:
".. Lakini huenda mkachukia kitu nacho
ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho
ni shari kwenu. Na Mwenyezi
mungu ndiyeanayejua, (lakini) nyinyi hamjui". (2:216).
Kuwa wenye msimamo thabiti (Istiqama)
Muumini wa kweli anayemtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.)
Kwa kila hali hana budi kuwa na msimamo thabiti katika kuusimamisha na
kuufuata uislamu. Si muumini wa kweli yule
anaeyumba yumba (mudhadhabina) kwa kuchanganya haki na batili au utiii na uasi
katika kuendesha maisha yake ya kila siku. Mwenyezi Mungu (s.w.)
Ametuamrisha wale tutoao shahada ya kweli tuingie Uislamu wote au tuwe
Waislamu katika kila kipengele na kila hatua yetu ya maisha na wala tusiingie
nusu nusu. Anatuamrisha:
Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu wote, wala msifuate nyayo za shetani,
kwa hakika yeye kwenu ni adui dhahiri. (2:208).
Hivyo, kutamka tu shahada au kusema: "Tunakiri kuwa hapana Mola ila Mwenyezi
mungu na Muhammad (s.a.w.) Ni Mtume wake" haitoshi kutufanya kuwa Waislamu
wale walioahidiwa malipo makubwa huko akhera; bali tutakuwa wa kweli katika
shahada zetu iwapo tutaendesha maisha yetu yote kama alivyotutaka tuishi
Mwenyezi Mungu (s.w.) na kama alivyotuelekeza Mtume wake (s.a.w.).Waislamu
watakaokuwa imara katika kuutekeleza Uislamu katika maisha yao ya kila siku,
ndio walioahidiwa malipo makubwa ya Peponi katika maisha ya Akhera.
Hebu turejee aya chache zifuatazo:
Wale waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu kisha
wakabakia imara (wakawa na msimamo), hao huwateremkia malaika (wakawaambia), "Msiogope
wala msihuzunike, na furahini kwa pepo mliyokuwa mkiahidiwa. Sisi
ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika
akhera, na humo mtapata vitu vinavyopendwa na nafsi zenu, na humo mtapata
mtakavyovitaka". (41:30 -31).
Hakika wale watasema: 'Mola wetu ni Mwenyezi Mungu'.
Kisha wakatengenea (wakawa na msimamo) hawatakuwa
na khofu (siku ya kufa kwao wala baadaye) wala hawatahuzunika. Hao ndio watu
wa Peponi, watakaa humo (milele); na malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda:.
(46:13-14).
Hebu pia tuone jinsi Mtume (s.a.w.) anavyotuwaidhi juu ya kuwa
na msimamo katika uislamu wetu:
Sufyaan bin Abdullah (r.a.) Amesimulia kuwa alisema: Ee! Mtume
wa Allah niambie neno juu ya Uislamu ambalo
sitakuwa tena na haja ya kumuuliza mtu mwingine baada ya hapa. Alisema Mtume;
'Sema:Ninamuamini Mwenyezi Mungu kisha ubakie
katika msimamo huo". (Muslim).
Abu Hurairah (r.a.) amesimulia kuwa Mtume wa
Mwenyezi mungu amesema: Fuata barabara njia sahihi ya imani na kuwa na msimamo
huo, na ujue kwamba hapana yeyote atakayeokoka kutokana na amali yake (nzuri).
Mmoja akauliza: Hata wewe Mtume wa Allah? Akajibu (Mtume)
Hata mimi, ila mpaka Allah anikunjulie rehema Zake
na fadhila Zake. (Muslim).