Assalaam Alaykum,

Shairi lifuatalo linaloitwa TUJITAHIDI NA SUNNA ni katika jumla ya mashairi yaliyotungwa na Sh. Khamis bin Nassor Al-Nabhany, Mola amrehemu.Shairi hili alilitunga baada ya kuona kijijini kwao vijana wengi wameshiriki ulevi

TUJITAHIDI NA SUNNA

Wazee na as-habu, Akh-wa na ukhtina

Nimeandika kitabu, Kiasi kukumbushana

Kidogo nimekutubu, Si ila kuambizana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Faradhi iwe kamili, Tujitahidi na sunna

Tufunge tena tusali, Kwa usiku na mchana

Na tukimiliki mali, Twende Maka na Madina

Tujitahidi na sunna, Tukamilisha faradhi

Aidha zaka tutowe, Kwa amri ya Rabbana,

Walokhusika wapewe, Bila ya kupendeleana

Kwa kipimo wagawiwe, Pasi kudhulumiana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Tukae tukikumbuka, Kua uhai hapana

Wengi waliotutoka, Wala hawarudi tena

Jambo jema la kushika, Ni kumtii Rabbana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Tunyanyueni mikono, Tukisikia adhana

Tusali na sala tano, Na dua kuombeana

Tuombe masikizano, Jamii muuminina

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Tujitahidi na dini, Ndio jambo la maana

Na sadaka tutoweni, Ina ubaya khiyana

Tumlaani shetani, Laanahul mal-una

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Tuitambuwe dunia, Kua si kubwa ni duna

Hii dunia ni njia, Twapita si maskana

Dunia yatuzomea, Na huku yatutafuna

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Pana safari lazima, Kubwa mfano haina

Sote inatuandama, Aasi na msalihina 

Habakii mtu nyuma, Babu na baba na mwana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Soteni lazima kwenda, Mbele yake Subhana

Kila tuliyoyatenda, Wenyewe tutayaona

Mwenye lake talipanda, Sayyia au hasana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Dhalimu na madhulumu, Walo wakikopeshana

Wakae wakifahamu, Siku ya kwenda kutana

Wanaekewa zakumu, Chakula cha kulishana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Wako wapi watukufu, Walokuwa na majina

Ambao ni maarufu, Na sote tukiwaona

La mwisho ni udhaifu, Hali zao hairana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Waliokuwa na raha, Wanangiwa na mahana

Wote wapiga siyaha, Kina wakiambiana

Hayupo mwenye furaha, Jamii wanadangana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Tuwatazame wazuri, Walio wakijivuna

Maringo na ujeuri, Fedhuli na kujiona

Unakwisha uhodari, La kulifanya hawana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Wako wapi maridadi, Wa vikoi na fulana

Kwenda huku wakirudi, Na kujiona wapana

Sasa hawajisafidi, Unawapata mdhana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Iwapi ile suhuba, Watu kutemebleana

Kila wendapo washiba, Karamu kupikiana

Jamii wapiga toba, Na wote ni mahuzuna

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Tuwatazame walevi, Waliowakilevyana

Na ukali kama uvi, Na watu kuwatukana

Unawishia ujuvi, Khatima wachukiana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Ndugu zangu nawambia, Kama kunabihishana

Ni kali mno dunia, Yauma tena yabana

Atakaeichezea, Ajuwe watapambana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Kuna adhabu akhera, Ya namna kwa namna

Toba ya Rabbi sitara, Allahu mustaana

Tuombeni maghfira, Kwa Rabbil-aalamina

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Niliyowahadithiya, Ni ya kweli si ya dhanna

Kwa maneno yangu haya, Ni kama kuzinduana

Na iwapo ni mabaya, Nawaomba samahana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Tammati sina la kwamba, Ni bora tatulizana

Lakini radhi naomba, Kwa wazee na vijana

Musije mukanigomba, Ikawa kununiana

Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

.