SALA YA IJUMAA
Fadhila za Siku ya Ijumaa
Zimepokelewa hadithi nyingi zinazotujulisha kuwa Siku ya Ijumaa ni siku tukufu kupita siku zote.
Mtume (SAW) amesema;
"Siku tukufu kupita zote ni Siku ya Ijumaa, hiyo ndiyo siku aliyoumbwa Adam (AS) na siku hiyo aliingizwa Peponi, na siku hiyo ndiyo aliyotolewa humo, na Kiama hakitosimama katika siku nyingine isipokuwa siku (hii) ya Ijumaa".
Muslim
Dua ndani yake
Zimepokelewa hadithi nyingi pia kuwa katika Siku ya Ijumaa upo wakati maalum ambao dua ndani yake inakubaliwa.
Kutoka kwa Abu Saeed na Abu Huraira (Radhiyallahu anhum) wamesema;
"Mtume (SAW) amesema;
"Siku ya Ijumaa ina masaa kumi na mawili. Ndani yake mna saa maalum ambayo mja yeyote Muislam ikimkuta saa hiyo akiwa anaomba dua ya kheri basi inakubaliwa - na itafuteni zaidi (saa hiyo) katika nyakati za mwisho wa mchana".
Annasai - Abu Daud - Al Hakim - na akasema kuwa hadithi hii ni sahihi kufuatana na masharti yaliyowekwa na Imam Muslim
Kukithiri kumsalia Mtume (SAW) ndani yake
Kutoka kwa Aus bin Aus (RA) amesema kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Siku tukufu kupita zote ni Siku ya Ijumaa, ndani yake ameumbwa Adam na siku hiyo ndiyo siku litakapopulizwa (baragumu) na siku hiyo ndiyo watu wote watakapokufa. Kwa hivyo nisalieni sana siku hiyo (ya Ijumaa) kwani ninafikishiwa Sala zenu".
Imeotelwa na maimam wote watano (wa hadithi) isipokuwa Attirmidhiy
Kusoma Suratul Kahaf
Zimepokelewa hadithi nyingi pia zinazopendekeza mtu kusoma Suratul Kahaf Siku ya Ijumaa.
Kutoka kwa Abu Saeed Al Khodary (RA) amesema kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Atakayesoma Suratul Kahaf siku ya Ijumaa Mwenyezi Mungu atamuangazia nuru baina ya Ijumaa mbili".
Annasaiy - Al Baihaqiy - Al Hakim
Kuoga na kuvaa nguo nzuri na kujipaka mafuta mazuri na kujipamba
Zimepokelewa hadithi nyingi pia zinazohimiza watu kuvaa nguo nzuri, kujipaka mafuta mazuri na kujipamba Siku ya Ijumaa.
Kutoka kwa Abu Saeed (RA), kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Kila Muislam anatakiwa aoge kwa ajili ya Siku ya Ijumaa na avae nguo zake nzuri, na kama anayo mafuta mazuri, basi ajipake".
Bukhari-Muslim na Imam Ahmed
Imepokelewa pia kuwa Mtume (SAW) alikuwa akisema juu ya membari huku akiwahutubia watu siku ya Ijumaa;
"Mtu atapungua nini ikiwa atajinunulia nguo mbili akawa anazivaa Siku ya Ijumaa badala ya kuvaa nguo zake anazozifanyia kazi?".
Abu Daud na Ibni Majah
Kwenda mapema msikitini
Zimepokelewa hadithi nyingi zinazohimiza kwenda mapema msikitini Siku ya Ijumaa, igawaje zipo khitilafu baina ya maulamaa juu ya wakati wake.
Imepokelewa kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Mtu anapokoga Siku ya Ijumaa kama anavyokoga kwa ajili ya janaba, kisha akenda (msikitini) katika saa ya mwanzo, anakuwa mfano wa mtu aliyejikurubisha kwa kutoa ngamia, na atakayekwenda katika saa ya pili anakuwa mfano wa aliyejikurubisha kwa kutoa ng'ombe, na atakayekwenda katika saa ya tatu anakuwa mfano wa aliyetowa mbuzi mwenye mapembe, na atakayekwenda katika saa ya nne anakuwa mfano wa aliyejikurubisha kwa kutoa jogoo, na atakayekwenda katika saa ya tano anakuwa mfano wa aliyejikurubisha kwa kutoa yai, na Imam akishaingia msikitini (akapanda juu ya membari) malaika (nao) wanahudhuria kusikiliza mawaidha".
Imepokelewa na maimam wote wa hadithi isipokuwa Ibni Majah
Kusali Sunnah kabla ya Sala ya Ijumaa
Inaruhusiwa mtu kusali Sala za Sunnah azitakazo Siku ya Ijumaa mpaka pale Imam anapoingia msikititni na kupanda juu ya membari, hapo hairuhusiwi tena kusali Sala za Sunnah isipokuwa kama ndiyo kwanza mtu anaingia msikitini, anaruhusiwa kusali Sunnah ya Tahiyyatul Masjid, kisha akae kusikiliza hotuba ya Ijumaa.
Imepokelewa kuwa mtu mmoja aliingia msikitini Siku ya Ijumaa wakati Mtume (SAW) anahutubu, akamuuliza;
"Umesali?"
Akasema;
"La - sikusali".
Mtume (SAW) akamwambia;
"Sali rakaa mbili".
Imepokelewa na Maimam wote wa hadithi
Na katika riwaya nyingine imepokelewa kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Mmoja wenu akiingia msikitini Siku ya Ijumaa na imam anahutubia, asali rakaa mbili na asizifanye zikawa refu".
Ahmed na Muslim na Abu Daud
Kuwajibika kwake
Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Sala ya Ijumaa ni Fardhi kwa kila Mwislam aliyebalegh, aliyeko ndani ya mji, mwenye uwezo wa kwenda msikitini, asiyekuwa na udhuru wowote ule unaokubaliwa kisheria wa kumzuwia asende msikitini.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Enyi mlioamini! Kukiadhiniwa kwa ajili ya Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kumtaja Mwenyezi Mungu na acheni biashara. Kufanya hivi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua (hivi basi fanyeni).
Na itapokwisha Sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mweneyzi Mungu na Mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu".
Al Jumua - 9-10
Mtume (SAW) aliwahi kusema juu ya watu wasiokwenda kusali Ijumaa;
"Ilinipitikia niamrishe mtu asalishe watu, kisha (niondoke nende) nikazichome moto nyumba za watu wasiohudhuria Sala ya Ijumaa".
Ahmed na Muslim
Na akasema;
"Baadhi ya watu lazima waache kuzikimbia Sala za Ijumaa, ama sivyo Mwenyezi Mungu atazipiga muhuri nyoyo zao kisha watakuwa miongoni mwa walioghafilika".
Muslim - Ahmed - Annasaiy
Wasiolazimika kusali Sala ya Ijumaa
Kutoka kwa Ibni Abbas (RA) amesema kuwa alimsikia Mtume (SAW) akisema;
"Atakayeusikia muadhini na asiuitikie basi Sala yake haikubaliwi ila kama anao udhuru".
Wakamuuliza;
"Udhuru upi huo?"
Akasema;
"Hofu au maradhi".
Abu Daud
Impokelewa kutoka kwa Ibni Abbas na kutoka kwa Ibni Maliyh (RA) kuwa wakati fulani ilinyesha mvua kali na walimsikia Mtume (SAW) akiamrisha watu wasali majumbani mwao.
Abu Daud na Ibni Majah
Wote hawa hawalazimiki (si wajibu kwao) kusali Sala ya Ijumaa, lakini wanatakiwa wasali badala yake Sala ya Adhuhuri rakaa nne. Ikiwa watajikalifisha wenyewe na kwenda kusali Sala ya Ijumaa, basi Sala yao ni sahihi na hawatosali Sala ya Adhuhuri
Wakati wake
Wakati wa Sala ya Ijumaa ni wakati ule ule wa Sala ya Adhuhuri
Idadi ya watu wanaotakiwa ili waweze kuisali Sala hiyo
Hapana hitilafu baina ya maulamaa kuwa Sala ya Ijumaa lazima isaliwe jamaa, isipokuwa wamekhitalifiana juu ya idadi ya watu wanaotakiwa ili Sala hiyo iweze kusaliwa.
Wapo wanaosema kuwa wawili wanatosha na wengine wakasema watatu na wengine wakasema sharti watimie watu arubaini nk.
Katika tahakiki yake ndani ya kitabu chake kiitwacho 'Niylul awtaar' Imam Al Shaukani amesema;
"Mtume (SAW) amesema;
"Watu wawili na kwenda juu ni jamaa".
Na watu wote wanasali jamaa wakiwa wawili kwenda juu, na Sala ya Ijumaa ni Sala kama sala nyingine yoyote, hapana tofauti baina yao, na hapana dalili yoyote ile inayoihusisha sala hii kwa idadi maalum ya watu, tofauti na sala nyingine".
Sunnah baada ya Sala ya Ijumaa - rakaa nne au mbili
Zimepokelewa hadithi zinazosema kuwa Mtume (SAW) alikuwa baada ya Sala ya Ijumaa akisali rakaa nne za Sunnah pale pale msikitini, na akizisali rakaa mbili mbili.
Imepokelewa pia kuwa anapozisali Sunnah hizo nyumbani kwake alikuwa akisali rakaa mbili tu.
Muslim na Abu Daud na Attirmidhiy
MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY