SALATUL GHAIB

Inajuzu mtu kumsalia maiti asiyekuwepo, yote sawa ikiwa aliyekufa yupo nchi ya karibu au nchi ya mbali.

Mpaka lini maiti asiyekuwepo anaweza kusaliwa?

Mtume (SAW) alimsalia Al Najashi aliyefariki katika nchi ya uhabeshi (Ethiopia), na bila shaka alijulishwa juu ya kifo chake kwa wahyi, kwa hivyo huenda ikawa aliarifiwa siku ile ile aliyomsalia.

Ama yule bibi aliyefariki na kuzikwa bila Mtume (SAW) kuarifiwa, kisha Mtume (SAW) alipokwenda makaburini akalikuta kaburi lake likiwa bado jipya, kisha akauliza;

"Kaburi la nani hili?"

Akajibiwa kuwa ni kaburi la Bi Fulani, akatajiwa jina lake, kisha akasema;

"Kwa nini msinijulishe?"

Akajibiwa;

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu siku hiyo ulikuwa umefunga tena umelala, tukaona haina haja ya kukuhangaisha".

Kisha akawaambia;

"Msifanye hivyo. Mara nyingine mtu yoyote akifa miongoni mwenu lazima muniarifu nipate kumsalia, kwani Sala yangu juu yake ni rahma".

Kisha akaliendea kaburi hilo na kumsalia.

Imam Ahmed - Annasai - Al Hakim na Ibni Habban

Hapa pia hapakutajwa muda gani ulipita tokea alipozikwa Bibi huyo mpaka pale aliposaliwa.

Katika kitabu cha Sahih al Bukhari ipo hadithi inayosema kuwa Mtume (SAW) aliwasalia mashahidi waliokufa katika vita vya Uhud baada ya kupita miaka minane tokea wazikwe.

 

VIPI INASALIWA?

Sala ya maiti asiyekuwepo inasaliwa kama Sala ya maiti ya kawaida (maiti aliyekuwepo).

SHURUTI ZAKE

Shuruti zake pia ni sawa na shuruti za Sala yoyote ya kawaida kama vile mtu kuwa na tohara pamoja na udhu, (ametahirika katika hadathi ndogo na kubwa), kuelekea kibla, na awe amevaa nguo za kujisitiri.

Inakhitalifiana na Sala ya kawaida katika wakati, kwa sababu Sala ya maiti inaweza kusaliwa wakati wowote ule maiti atakapoletwa, hata ikiwa katika zile nyakati zinazokatazwa kusali ndani yake, ingawaje baadhi ya maulamaa kama vile Imam Ahmed na Ibn Al Mubarak wanaona kuwa haijuzu kusaliwa pale juwa linachomoza na pale linapozama.

NGUZO ZAKE

1.     Kutia nia - Nia ni kitendo cha moyoni na haina uhusiano wowote ule na ulimi.

2.     Kusali kwa kusimama kwa mwenye uwezo - Haijuzu mtu kumsalia maiti akiwa amepanda mnyama au akiwa amekaa, ila kama hana uwezo wa kusimama.

3.     Takbira nne - Imepokelewa kutoka kwa Bukhari na Muslim kuwa Mtume (SAW) alipomsalia Al Najashi alisoma takbira mara nne. Anasema Sayed Sabeq katika Fiqhil Sunnah kuwa ni vizuri mtu kutonyanyua mikono katika Sala ya maiti isipokuwa katika takbira ya mwanzo. - (Ipo khitilafu baina ya maulamaa juu ya kunyanyua mikono katika takbira zilizobaki).

4.     Na 5- Kusoma Alhamdu kimya kimya baada ya takbira ya mwanzo na kumsalia Mtume (SAW) baada ya takbira ya pili. Imepokelewa kutoka kwa Imam Shafi katika Musand yake na kutoka kwa Bukhari na Attirmidhiy kuwa kusoma Alhamdu baada ya takbira ya mwanzo na kumsalia Mtume (SAW) baada ya takbira ya pili ni katika nguzo za Sala ya maiti.

Sala ya Mtume (SAW) inaweza kusomwa kwa sigha yoyote ile kama vile kusema (AllAhumma salliy alaa Muhammad wa alaa aali Muhammad) au kama mtu ataisoma kwa ukamilifu;

(Allhumma salliy alaa Muhammad wa alaa aali Muhammad kama sallayta alaa Ibrahima wa ala aali Ibrahima wa barik ala Muhammad wa alaa aali Muhammad kama barakta ala Ibrahima wa alaa aali Ibrahima fil aalamiyna innaka hamiydun majiyd).

Baadhi ya maulamaa wamesema kuwa hii itakuwa bora zaidi na kwa ukamilifu zaidi ingawaje hapana dalili ya kulazimika kuisoma kwa ukamilifu huo.

5.     Dua - Mtume (SAW) amesema;

"Mnapomsalia maiti muombeeni dua kwa ikhlasi (kwa moyo wote)".

Zipo hadithi nyingi zinazoelezea juu ya dua mbali mbali alokuwa akiomba Mtume (SAW) anaposalia maiti, na hapa nitaitaja mojawapo;

(Allahumma ghfir lahu warham-hu wa afu anhu wa afihi wa akrim nuzulahu wa wassia madkhalahu wa aghsilhu bimaain wa thaljin wa barad, wa naqihiy minal khataya kama yunaqa thawbu l abyadh mina ddanas)

Ni vizuri pia kuomba dua baada ya takbira ya nne. Anasema Imam Shafi kuwa ni vizuri kuomba dua ifuatayo;

(Allahumma laa tahrimna ajrahu wala taftinna baadahu waghfir lana walahu).

KUTOA SALAM

Wamekhitalifiana maulamaa juu ya salam ngapi zinatolewa baada ya kusali Sala ya maiti.

Anasema Imam Ahmed kuwa salam moja tu ndiyo Sunnah. Amma Imam Shafi, yeye anasema kuwa zinatolewa salam mbili.

VIPI INASALIWA

Unasimama mbele ya maiti kisha unanyanyua mikono juu na kusema: "Allahu akbar", kisha unaweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto na kusoma suratul fatiha, kisha unasema tena;"Allahu Akbar", kisha unamsalia Mtume (SAW) kwa sigha iliyotangulia kutajwa, kisha unasema tena; "Allahu akbar", kisha unamuombea dua maiti, kisha unasema tena;"Allahu akbar", kisha unaomba tena, kisha unatoa salam.

VIPI IMAM ANASIMAMA MBELE YA MAITI MWANAMUME AU MWANAMKE?

Imam anasimama sawa na kichwa cha maiti mwanamume, ama akiwa maiti mwanamke, basi anasimama katikati yake.

BORA ZIWE SAFU TATU

Ni vizuri safu ziwe tatu au zaidi, Mtume (SAW) amesema;

"Muislam akifa,kisha akasaliwa na watu wanaofika safu tatu, basi anaghufiriwa (maiti huyo)".

 

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY

 

KUMSALIA MAITI BAADA YA KUZIKWA

Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Inajuzu kumsalia maiti hata baada ya kuzikwa, tena wakati wowote ule hata kama alikwishasaliwa.

Imepokelewa kuwa siku moja Mtume (SAW) aliuliza juu ya mwanamke mmoja aitwae Ummu Mahjan (RA) aliyekuwa akifagiafagia msikitini;

"Yuwapi bibi huyu mbona simuoni siku hizi?"

Wakamjibu;

"Keshafariki (na keshazikwa)".

Mtume (SAW) akasema;

"Kwa nini msinambie?"

Akenda mpaka penye kaburi lake akawapanga msitari Masahaba wake (RA) na kumsalia.

Hadithi hii imetolewa na Bukhari na Muslim na Ahmed na Al Hakim na wengineo kwa njia mbali mbali.

Anasema Ibni l Qayim kuwa;

"Baadhi ya watu wanaipinga Sunnah hii kutokana na hadithi za Mtume (SAW) inayosema;

"Msiyakalie makaburi wala msiyaelekee pale mnaposali".

Anaendela kusema Ibni l Qayim;

"Hadithi hii ni sahihi, na aliyetamka maneno haya ni yule yule aliyemsalia mwanamke yule na alikwishawahi kuwasalia wengine pia makaburini pao baada ya kuzikwa.

Hii ni kauli yake na kile ni kitendo chake, na wala hapana mgongano baina yao, kwa sababu Sala iliyokatazwa kusaliwa makaburini si Sala iliyosaliwa pale makaburini, kwani hii ni Sala ya maiti inayosaliwa mahali popote pale, bali kuisali Sala ya maiti nje ya msikiti ni bora kuliko kuisali ndani yake, na kumsalia maiti akiwa ndani ya jeneza lake ni sawa na kumsalia akiwa kaburini mwake"

Natumai itafahamika