Makosa ndani ya Swala

HUKMU YA KUVAA CHUMA NDANI YA SALA

 

ELIMU YA FIQHI

 

Fiqhi - ni elimu inayohusiana na hukmu za Kiislamu katika matendo yote ya kimaisha, yakijumuisha ibada, uhusiano wa aila, uhusiano wa kijamii, uhusiano wa jirani, mambo ya jinai, uhusiano baina ya Muislamu na Muislamu mwenzake, uhusiano baina ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu, katika siku za amani na katika siku za vita na pia katika siku nyingine zisizokuwa hizo.

Fiqhi inatufundisha hukmu za namna hiyo na kutujulisha kipi kinachowajibika kufanya na kipi kisichowajibika. Inatufundisha pia yale ya haramu na ya halali, Sunnah na yale yanayochukiza, 'Makruh', na inatufundisha pia yanayofaa na yasiyofaa pamoja na hukmu nyingine kama hizo.

Kwa hivyo elimu ya Fiqhi ni elimu inayotubainishia kwa mfano; kuwajibika kwa Sala tano, na kwamba katika shuruti za kumwajibikia mtu ni kuwa na uwezo na pia kuingia kwa wakati wa Sala, na kwamba kusema ndani yake kunaiharibu Sala na namna ya kujitia tohara na vipi tohara au udhu unatenguka nk.

Elimu hiyo pia inatufundisha juu ya vyakula vilivyoharamishwa kama vile nyama ya nguruwe nk.

Kwa ajili hiyo, tunaelewa kuwa amri yoyote aliyotuteremshia Mwenyezi Mungu Subhanahu wa taala ni katika fiqhi, yote sawa ikiwa amri hiyo ni ya kuamrisha juu ya jambo au kukataza lisifanywe.