RIBA
Riba katika lugha ya kiarabu maana yake
ni ziada.
Ama katika lugha ya elimu ya fiq-hi maana
ya neno 'Riba', ni ile ziada anayolipwa mdai juu ya rasilamali yake.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Na mkiwa mmetubu, basi mtapata
rasilmali zenu ; msidhulumu wala msidhulumiwe.
Na kama mkopi ana dhiki, basi (mdai)
angoje mpaka afarijike".
Al Baqarah - 279 - 280
Riba imeharimishwa katika dini ya
Manasara na Mayahudi pia, isipokuwa Mayahudi wao wanaamini kuwa kuchukuwa riba
kwa asiyekuwa Myahudi mwenzao ni halali.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Na kwa (sababu ya) kula kwao riba,
na hali wamekatazwa wasiile".
Annisaa - 161
Katika dini ya Kiislam, hukmu ya
kuharamisha Riba iliteremshwa kwa ukamilifu wakati wa Madina pale ilipoteremka
kauli yake Subhanahu wa Taala aliposema;
"Enyi milioamini! Mcheni Mwenyezi
Mungu na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa mmeamini.
Na kama hamtafanya (hivyo) basi fahamuni
mtakuwa na vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkiwa mmetubu, basi (mdai)
angoje mpaka afarijike. Na kama nyinyi (mnaodai mkizisamehe deni zenu)
mkazifanya sadaka, basi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua haya (basi fanyeni)".
Al Baqarah - 278-279
Mtume (SAW) ameitaja Riba kuwa ni
miongoni mwa madhambi saba makubwa yanayoangamiza;
Mtume (SAW) amesema;
"Jiepusheni na mambo saba
yanayoangamiza".
Masahaba (RA) wakamuuliza;
"Ni yepi hayo ewe Mtume wa Mwenyezi
Mungu?"
Akasema;
"Kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na
Uchawi, na Kuiuwa nafsi iliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu isipokuwa ikiwa kwa
ajili ya haki (kwa aliyefanya makosa yanayostahiki kuhukumiwa auawe), na Kula
Riba, na Kula mali ya yatima, na Kurudi nyuma katika vita (ukawaacha wenzako
peke yao), na kuwasingizia uongo wanawake wema wasio na makosa walioamini (kuwa
eti wamezini)".
Bukhari na Muslim
Na Mtume (SAW) amewalaani wote
wanaoshiriki katika kitendo hicho cha kula Riba.
Mtume (SAW) amesema;
"Mwenyezi Mungu amemlaani anayekula
Riba na anayelisha na mashahidi wake".
Bukhari- Muslim na Imam Ahmed
Mwenyezi Mungu anatuhimiza kuwa ikiwa mtu
anataka kumkopesha mwenzake mwenye shida, basi amkopeshe mkopo mwema bila ya
kumuongezea mwenzake dhiki, na kwamba kufanya hivyo ndiyo mali yake mtu
inaongezeka baraka itokayo kwa Mola wake, ama unapomkopesha mwenye shida kisha
ukachukua faida ya Riba, basi huko ni kumzidishia dhiki mwenzio na pia ni
kuiangamiza mali yako na kuiondolea barka.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Na zile (pesa za kukopeshea) riba
mtoazo (katika kuwakopesha watu) ili zizidi katika mali ya watu, mbele ya
Mwenyezi Mungu hazizidi (pesa hizo; bali zinaingia nuhusi na shakawa); lakini
(mali) mnayoyatoa kwa ajili ya Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu , basi
hao (wenye kufanya haya) ndio wazidishao (mali zao)".
Ar Rum- 39
Riba ziko aina mbili;
Ya kwanza ni zile pesa zaidi anazolipa
mtu aliyekopeshwa kwa kuhsurutishwa na mdai.
Yaani kwa mfano mtu akitaka kukopa
shilingi elfu, anashurutishwa kulipa shilingi elfu na zaidi. Sasa zile zaidi
ndiyo Riba yenyewe.
Ya pili ni Riba ya kufadhilisha
Nayo ni ile ya kubadilishana pesa kwa
pesa au chakula kwa chakula na kuchukuwa zaidi.
Kwa mfano mtu anapokwenda kubadilisha
dhahabu yenye uzito wa gram kumi kwa ajili ya kupata dhahabu nyengine
iliyomvutia zaidi, akalipwa badala yake dhahabu yenye uzito wa gram saba. Hiyo
inahesabiwa ni Riba.
Inavyotakiwa kwanza mtu aiuze dhahabu ile
kwa thamani yake, kisha ainunue dhahabu anayoitaka.
Mtume (SAW) amesema;
"Msiuze Dirham moja kwa Dirham
mbili, kwani nakuogopeeni Riba".
Na akasema;
"Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa
fedha, ngano kwa ngano, chumvi kwa chumvi, mkono kwa mkono, atakayechukua zaidi
au kutaka zaidi, kesha kula Riba".
Ahmed na Bukhari
Mtu mmoja alikwenda kwa Mtume (SAW) akiwa
amebeba tende.
Mtume (SAW) akamwambia;
"Tende hii haipatikani kwetu
hapa?"
Mtu yule akasema;
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu,
tumebadilishana tende yetu pishi moja kwa pishi mbili za tende hizi".
Mtume (SAW) akamwambia;
"Hiyo ni Riba, zirudishe, kisha uza
tende yetu, halafu nunua tende hizi".
Muslim