RAMADHANI NI MWEZI WA QURANI

Suleyman Mohammad Said.

       

Mwezi  wa Ramadhani ni mwezi bora kuliko miezi yote, na moja kati ya sababu ya ubora wake ni kule kuteremshwa katika mwezi huu Qurani tukufu.

Hakika Qurani ni uongofu na nuru na ndio kinachowaongoza waislam, na tangu kuteremka kwake hadi dunia itapomalizika Qurani itabakia kama alivyoshushiwa Bwana wetu Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Katika makala hii nitaizungumzia Ramadhan ukiwa ni mwezi wa Qurani na namna gani Qurani imeteremshwa na fadhila za mwenye kuisoma. 

 

Uteremsho wa Qurani

Hakika Qurani imeteremshwa katika hatua tatu kutoka kwa Allah hadi kutufikia sisi duniani.

 

Hatua ya kwanza

Kushushwa Qurani kutoka kwa Allah  hadi kwenye Lawhil Mahfudh.

Amesema Allah katika suratul Buruj;

Bali hiyo ni Qurani tukufu, Iliyotolewa katika huo ubao uliohifadhiwa (wa Mwenye enzi Mungu)."

(Al-Buruj  85:21-22).

 

Hatua ya pili

Kutoka katika Lawhil Mahfudh hadi wingu wa dunia.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Hakika Tumeiteremsha Qurani katika Laylatul-Qadr (usiku wa mwezi wa Ramadhan)."

(Qadr 97:1)

Na usiku huu unapatikana ndani ya mwezi wa Ramadhani tu.

 

Hatua ya tatu

Uteremsho wa mwisho ambao ulikuwa kutoka katika wingu wa dunia na kushuka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kupitia kwa malaika Jibril (‘Alayhis Salaam), na uteremsho huu ulitofautiana na iliyotangulia kwani huu ulikuwa ni wa muda hadi muda, yaani tokea Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kupewa utume hadi kukutana na Mola wake, ilikuwa ikiteremshwa kidogo kidogo, na wamesema wanavyuoni wetu kwamba Qurani imeteremshwa duniani hadi mwisho wake kwa kipindi cha muda wa miaka ishirini na tatu  tokea kupewa Utume Bwana Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hadi kufariki kwake.

 

Fadhiza za kusoma Qurani ndani ya Ramadhani.

Imepokewa katika hadithi kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa anasoma Qurani pamoja na malaika Jibril (‘Alayhis Salaam) kila siku katika mwezi wa Ramadhani, tena ikawa  Jibril (‘Alayhis Salaam)  anamsomesha Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) yale aliyoteremshiwa. Huko ni kudurusu, kisha ikawa kila mwaka wakitalii kwa pamoja baina ya Jibril na Bwna Mtume na kuumaliza msahafu mzima mara moja, ama mwaka aliofariki Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) walidurusu Qurani mara mbili baina ya Mtume na Jibril.       

 

Kutokana na mapokezi haya nikielelezo kuwa tunatakiwa tuisome Qurani zaidi katika mwezi wa Ramadhani kuliko miezi mengine, na itoshe kumfuata kiongozi wetu Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hata kama hatutazijuwa fadhila zake.

Lakini Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hakutuacha patupu bila  bila ya kutueleza fadhila za kusoma Qurani kwa ujumla kwani kuna mapokezi mengi yaamepokewa na baadhi ya mapokezi hayo ni:

 

v                 Kutoka kwa sahaba Abdallah  bin Omar amesema kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema; “Ataambiwa mwenye kuisoma Qurani (siku ya kiyama); 'soma na upande daraja na soma kama ulivyokuwa ukisoma duniani, kwani hakika makazi yako peponi kidaraja ni aya ya mwisho utakayoisoma”.

Imam Ahmad na Imam Tirmidhy

Yaani kadri mja atakaposoma aya nyingi ndipo daraja yake huwa ya juu zaidi.

 

v                 Pia amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam);

"Mwenye kusoma herufi moja ya Qurani atalipwa thawabu kumi, na wala sisemi kuwa Alif Lam Mim ni herufi moja bali Alif ni herufi, Laam ni herufi na mim ni herufi.”

Hizo ni thawabu za herufi moja tu seuze mwenye kusoma sura nzima au juzuu nzima atapata thawabu ngapi ?

 

v                 Na kama ilivyothibiti kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa Sheitani anaikimbia nyumba inayosomwa Suratul Al- Baqarah. Inaposomwa Suratul Baqarah shetani huwa, haisogelei nyumba hiyo ili  kuingiza shari zake.

Qurani ni  kinga.

 

Hizi ni miongoni mwa hadithi chache zinazotufahamisha umuhimu wa kusoma Qurani.

 

Wakati huo huo kuna makemeo kwa yule ambaye hajuwi kabisa kuisoma Qurani  na wala hajifunzi, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amemfananisha mtu wa namna hiyo kuwa ni sawa na gofu kwa kusema;

“Yule ambae hana katika kifua chake chochote katika Qurani (yaani haijuwi wala hakuhifadhi hata kidogo) ni mfaano wa gofu (jumba tupu lilohamwa na kongwe).”

 

Adabu za kusoma Qurani

Adabu za kusoma Qurani ni nyingi mno, lakini hapa  tutazitaja baadhi ambazo wengi wa watu huzipuuza na kuona ni jambo la kawaida hivyo wafanyavyo.

v                 Inatakiwa mwenye kusoma Qurani aisome kwa ajili ya Mola wake na kwa kutaraji kupata thawabu sio mtu anaisoma kwa ajili watu wamuone kuwa anasoma sana au anajuwa kusoma, yote hayo hayatomsaidia kitu katika akhera yake.

 

v                 Kuhudhurisha utukufu wa Qurani, kwa kuwa makini kwa yale ayasomayo na kuyazingatia kimaana ikiwa anafahamu, na kama haelewi mana yake basi na itoshe awe mwenye kusoma kuwa na utulivu na huku anajitahidi kujifunza maana yake.

Ama mwenye kuisoma Qurani bila ya kuwa na mazingatio, basi mtu huyo ni dhalili kuliko Jabali, kwani Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  amesema;

“Lau kama tungaliiteremsha hii Qurani juu ya mlima, ungaliuona ukinyenyekea (na) kupasuka kwa sababu ya hofu ya Allah. Na hii ni mifano tunawapigia (tunawaeleza) watu ili wafikiri."

(Al-Hashri 59:21)

v                 Kuisoma  hali ya kuwa na tohara kamili, ama akiwa na Janaba au akiwa mwanamke katika siku zake, basi ni haramu kuisoma Qurani na akiwa si katika hao wenye hali hizo mbili tulokwisha zitaja na akawa hana udhu, basi ni haramu kuisoma, pamoja na kuushika msahafu.

Ni haramu kugusa msahafu yule asiyekuwa na udhu, ama akiisoma bila ya kutizama msahafu itafaa lakini ni makruhu (hipendezi). Kwa hali yoyote mjaa anatakiwa awe na tohara kamili ili aweze kuisoma Qurani.

v                 Kuisoma Qurani ili hali umeelekea Qibla hili limetupwa na wengi mtu utamsikia akikwambia; 'si lazima kufanya hivyo', ni kweli sio lazima lakini hii ni adabu ya kusoma Qurani inahitaji kuchungwa kwa kila iinavyowezekana.

 

v                 Kutafuta sehemu iliyo safi na sehemu nzuri zaidi ni Msikitini, kwani ni nyumba tukufu, lakini la msingi ni kutafuta sehemu iliyo safi na nzuri sio mtu anasoma Qurani hadi anapoingia kujisaidia, au anakoga na huku utamsikia anasoma Qurani huku ni kuidhalilisha Qurani wala sio kuitukuza.

 

v                 Kujisitiri utupu, ama  hili wengi hulipuuza si wanaume wala sio  wanawake, hili limepuzwa mno hakika mtu anatakiwa aisome hali ya kuwa amejisitiri kama anavyotaka kusali na hii ni kwa sababu wakati mtu anaposoma Qurani huteremka malaika wa rehema juu yake, lakini akiwa utupu basi malaika  hao wanazuilika kuwa pamoja naye hivyo mtu hujikosesha mwenyewe fadhila.

 

v                 Kusoma kwa hukumu na sauti nzuri bila ya kuwakera wenzako, ikiwa msikitini basi usiwakere wanaosali kwa sauti yako, na ni bora uisome kwa sauti ya wastani kuepukana na riya

v                 Kuaanza kwa kusoma; “Audhubillahi minaa shaaitani raajim”, na asikate kisomo kwa kusikiliza mambo ya kipuuzi na wengine husoma Qurani na huku anasikiliza wimbo au khabari, kwa kuwa hivyo navyo vinampa rubaa (company).

 

Hizi ni baadhi ya adabu za kusoma Qurani, hivyo msomaji achunge kwa kufwata yale yanayopendeza na kuepukana na kila ovu au lenye kuchukiza.

Baada ya kufahamu umuhimu wa Qurani katika mwezi wa Ramadhani, hatuna budi kuazimia kumaliza angalau khitma moja katika Ramadhani nzima hii, na iwe ni kiwango kidogo, bali kama mtu uwezo wake ni mzuri basi na asome zaidi kwa kutaka malipo zaidi kwani hapa duniani kila mmoja anafanya kazi ili apate malipo zaidi, kwenye haya maisha ya mpito, jee hutaki ziada katika maisha ya milele?