RAMADHANI HUFUTA MADHAMBI YALIYOTANGULIA

Suleyman Mohammad Said

 

Amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam);

“Mwenye kufungaRamadhani kwa imani na kwa kutaraji kupata thawabu, husamehewa madhambi yake yaliyotangulia”.            

 

Pia amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam);

“ Mwenye kusimama ramadhani (kwa kusali ) kwa imani na kwa kutaraji kupata thawabu husamehewa madhambi yake yaliyotangulia”.     

 

Na amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam);

“ Mwenye kusimama (kwa kusali ) usiku wa Laylatul Qadri kwa imaani na kutaraji kupata thawabu basi atasamehewa madhambi yaliyotangulia”.              

 

Pia amesema Mtume  (Swallah Llahu alayhi wa sallam) katika hadithi tofauti kuwa mwezi huu wa Ramadhani ni mwezi ambao hufunguliwa milango ya pepo na hufungwa milango ya moto na mashetani hufungwa, pia hufunguliwa milango ya rehma na milango ya msamaha.           

 

 Hizi ni baadhi ya fadhila za mwezi huu na kila muislam anatakiwa ajihimu katika msimu huu wa kheri ili aingie katika wale watakaopata rehma na kusamehewa madhimbi yao yaliyotangulia. Ni jambo lisilofichika kuwa kila mmoja ana madhambi yanayomshinda mwenzake na kila mtu anahitaji kufutiwa dhambi zake hizo ili daftari lake liwe tupu, kwa hivyo inatakiwa watu wajipinde kwa kufanya ibada na kuomba msamaha kwa Mola wao ili wapate kusamehewa.

 

Na sababu za kusamehewa kama tulivyo elezwa katika hadithi za Bwana Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam), kwa mwenye kufunga na kusali usiku, na sala inayokusudiwa hasa ni sala ya Tarawehe, hivyo watu wajihimu kusali sala hii adhimu ambayo ni zawadi kwetu na haipatikani fursa ya kuisali sala hii isipokuwa katika Ramadhani na rakaa zake kwa ukamilifu ni ishirini na kadri mtu anapoozisali sala za usiku nyingi iwe tarawehe kisha akasali tahajudi na witri basi fadhila za mtu huyo huzidi na mtu huyo huhesabika ameifahamu maana ya Ramadhani.

Ama yule anayelala tu baada ya futari na sala zote za usiku kumpita, basi ni mwenye kupata khasara kubwa, kwani amejiharamishia mwenyewe fadhila za mwezi huu.       

 

Jambo la mazingatio zaidi ni kuhusu nia ya huyo anayefanya ibada hizi kwani katika hadithi tulizokwisha zizungumza zimeweka bayana juu ya atakayepata atayetimiza suna mbali mbali na kumwekwa sifa za huyo anayefanya ibada hizi kisha akasemehewa madhamb iyake, na sifa zenyewe ni :

Kuamini Mwenye kufanya hayo kwa kumuamnini Mola wake nayo ni kuzifanya amali hizo kwa ajili ya Allah tu si kwa sababu watu wamuone na kumzungumza kuwa fulani nimcha Mungu basi atakapoepukana na riya ndipo ataingia katika wale watakaosamehewa. Zaidi ya hayo ni kule kujiepusha na maasi, kwa sababu kadri mja anapomuasi Mola wake ndipo anapokuwa mbali nae katika kukubaliwa maombi yake

 

 

 

Kutaraji kulipwa thawabu.         

Muumini wa kweli ni yule anayefanya ibada hali ya kuwa moyo wake umetulizana  na kuwa na yakini kuwa  ile ibada aifanyayo atalipwa na Mola wake thawabu wala kutokuwa na shaka atapata malipo ama hapati? Hivyo mja anatakiwa ataraji kupata malipo kutokana na ibada azifanyazo hata  zikiwa ni ndogo na khasa katika mwezi kama huu wa Ramadhani ambao umesifiwa kuwa ni mwezi wa kusamehewa madhambi.

 

Mja vile vile atatakiwa afuate shuruti za toba nazo ziko nyingi, na kwa ufupi asifanye tena madhambi yake na anuwie kuacha kabisa, vile vile awe na unyenyekevu na kuonyesha kujuta kwake mbele ya Mola wake juu ya yale madhambi aliyoyafanya na kama kamdhulumu mtu afanye kila aliwezalo kumrejeshea mwenyewe haki yake. Kama kaiba basi arejeshe mali ya watu. Hizi  ni miongoni mwa sifa ambazo anatakaiwa mja ajivishe nazo, ili apate kusamehewa madhambi yake katika mwezi huu mtukufu.

 

Ewe Mola tusamehe madhambi yetu na turehemu kwa hakika wewe ni mwenye kurehemu waja wako. “Amin”