LAYLATUL QADR
Sameer Zulfikar
Shukrani zote zinamstahikia Mola aliyeturuzuku kuudiriki mwezi mtukufu wa Raamadhani na kwa rehma zake tunamuomba atujumuishe katika wal watakaopata baraka za usiku mtukufu uitwao Laylatul Qadri katika mwezi huu.
Huu ni usiku mmoja katika kila mwezi wa Ramadhani, na usiku huu una fadhila nyingi ambazo zinamfanya muislam ajihimu kuudiriki kwa kufanya ibada ili apate yale yaliyoahidiwa kwa anayeudiriki.
Katika usiku huu ndio imeteremshwa Qur-ani kutoka katika Lauhil Mahfudh hadi mbingu ya dunia kama ilivyopokewa kutoka kwa sahaba Ibnu Abbas (Radhiya Llahu anhu). Na Qur-an inaatuthibitishia kuwa uteremsho wa Qur-ani ulikuwa katika usiku huu. Amesema Allah katika suratul Qadar aya ya kwanza;
“Hakika tumeiteremsha Qur-ani katika usiku mtukufu (Laylatul Qadri )", basi na itoshe utukufu wa usiku huu kwa kuteremshwa kitabu kitukufu ambacho ni uongofu kwa waumini wa kiislam.
Pia amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) katika kuufadhilisha usiku huu kuliko mengineyo;
“Mwenye kusimama (kwa kusali) katika usiku mtukufu wa Laylatul Qadri kwa imani na kutaraji kulipwa thawabu, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”
Imepokewa na Imam Bukhari na Imam Muslim.
Na fadhila zaidi ya usiku huu zimeelezwa katika Qurani. Mwenyezi Mungu anasema;
“Huo usiku wa heshima (huo) ni bora kuliko miezi elfu.”
(Qadr 97:3)
Kwa kweli mwenye kuzingatia aya hii hatakubali umpite usiku huu akiwa amelala au akiwa anafanya maasi au mambo ya kipuuzi kama kucheza karata, bao, kupiga soga mabarazani, kuangalia TV nakadhalika. Kwani hii miezi elfu moja ni sawa na miaka thamanini na tatu na miezi mine. Ni umri wa mwanadamu na ni wachache wanaovuka umri huo, hivyo kuudiriki usiku mmoja tu kwa kufanya ibada, fadhila zake ni kuliko miaka hiyo, hivyo si jambo la kudharauliwa na kila muislam anatakiwa autilia shime.
Wanavyuoni wanasema; "Mtu atalipwa kwa lile alifanyalo. Akiwa anafanya maasi katika usiku huu basi itakuwa maasi yake ni mabaya kuliko miezi elfu moja, kama ilivyokuwa mwenye kufanya mema katika usiku huu huwa ni bora kuliko miezi elfu".
Na wala sio maana yake kuwa ukiudiriki usiku huu kwa mema usifanye tena ibada katika miaka 83, bali lilokusudiwa ni fadhila zake zilivyokuwa nyingi, na sio unatosheleza kwa kutofanya ibada miezi elfu, kwani kila siku madhali mwanadamu yupo hai basi anatakiwa atekeleze amri za Allah Subhanahu wa Taala na kujikurubisha kwake kwa kufanya ibada.
Isitoshe, hakuna mwenye uhakika kuwa ibada zake zimepokelewa mia juu ya mia hata ikabidi asifanye ibada tena.
Usiku huu tumetunukiwa si kwa kujibweteka baada ya Ramadhani bali huu usiku ni zawadi tu, ni sawa na mfanyakazi akapewa zawadi siku moja katika mwaka kwa utendaji wake mzuri, hii haimanishi kuwa mishahara yake hatapata tena katika miezi iliyobaki au maana yake asiwe na jitihada tena, bali maana ya zawadi hii ni kutunukiwa na kupongezwa kwa bidii yake na huwa ni changamoto katika kuongeza bidii hiyo ili na mwaka unaofuata apate tena zawadi na ndivyo ilivyo katika usiku huu kadri ya jitihada ya mtu, katu kufanya ibada ndio kuudiriki kwake huwa kwepesi.
Laylatul Qadri huteremka Malaika pamoja na Jibril kwa amri ya Allah huja kushuhudia waja wa Mola wao wakiwa kwenye ibada na kuwaombea dua,amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) “ Huteremka Malaika na roho (za viumbe watakatifu) katika (usiku) huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo (Qadr 97:4)
Inaeleweka kuawa Malaika Jibril kazi yake kuu imekwisha nayo ilikuwa kuteremsha wahyi kwa Mitume naye ni mkuu wa malaika wote, na hateremki Jibril (‘Alayhis Salaam) isipokuwa katika usiku huu kutokana na utukufu wake.
Pia usiku huu hubainishwa kila jambo litakalotokea kwa mwaka unaofwatia wanapewa Malaika hao kuja kuwafikishia Malaika wa duniani kwa kila mwenye majukumu yake, na hayo yamesemwaa katika Suratul Dukhan.
Mwenyezi Mungu anasema;
“Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima."
(Dukhan 44:4) .”
Vile vile Allah ameusifu usiku huu kwa kuuita usiku wa amani, amesema katika suratul Qadri aya ya mwisho;
“Ni amani (usiku) huo mpaka mapambazuko ya alfajiri.”
(Qadri 97:5).
Aya hii inafahamisha kuwa amani inapatikana na utulivu unakuweko katika usiku huu ili wale wanaotaka kujikurubisha kwa Mola wao wapate wepesi bila ya usumbufu. Pia zimepokewa baadhi ya hadithi kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
“Mashetani hawana nafasi ya kuwapotoa watu katika usiku huo.”
Usiku wa Laylatul Qadr huu haukuwepo katika umma zilizotangulia, usiku huu ni kwa umma huu wa Nabi Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na hikma ya kupewa uma huu wa Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) neema hii ni kama ilivyopokewa kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alionyeshwa amali za watu waliopita pamoja na umri wao kuwa mkubwa kama inavyoelezwa kuwa Nabii Nuh (‘Alayhis Salaam) alilingania watu wake muda wa mika mia tisa na hamsini, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaingiwa na wivu kwa umma wake kwamba umri wao ni mdogo ukiwa ni baina ya miaka 60 na 70 kwa hivyo amali zao zitapitwa na watu waliotutangulia, ndipo Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) akaamtunuku usiku huu iwe ni sababu ya kuweza kuwapita waumini wa umma zilizopita katika amali zao nayo ni kuthibitisha utukufu wa Umma huu wa Mtume Muhammad kuliko Uma zote zilizotangulia, lakini yule atakayokithirisha kufanya ibada katika masiku ya kumi la mwisho ndio awe na matarajio hayo, sio kuchapa usinginzi na kujishughulisha na michezo uwe na matarajio ya kuupata usiku huu mtukufu wa Laylatul Qadr.
Ramadhani ya ngapi inapatikana Laylatul Qadri?
Wametafautiana waanavyuoni wa kiislam juu ya tarehe maalumu ya Laylatul Qadr nayo inatokana na mapokezi ya hadithi mbali mbali yaliyopokewa kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), yakiwemo yaliyo sahihi na dhaifu ndani yake.
Kauli yenye nguvu na ndiyo iliyosemwa na wanavyuoni wengi ni kwamba Laylatul Qadr ni usiku unaopatikana ndani ya mwezi wa Ramadhan tena katika kumi la mwisho usiku wa kuamkia tarehe za witri za kumi la mwisho (odd numbers), yaani usiku wa kumkia tarehe ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano, au ishirini na saba, au ishirini na tisa.
Kwa maana nyengine ni kwamba usiku huu haujulikani, bali muislam anatakiwa ajitahidi kufanya ibada katika kumi la mwisho.
Kauli hii inatokana na maneno ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) yaliyopokewa na Imam Bukhari kutoka kwa bibi Aisha (Radhiya Llahu anhaa).a) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
“Jitahidini kuutafuta Laylatul Qadr katika siku za witri la kumi la mwisho la Ramadhani.”.Na vile vile imepokewa hadithi nyengine na Imam Bukhari kutoka kwa saahabaa Ubaada bin Samit (Radhiya Llahu anhu).a) amesema : “Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) siku moja alitaka kutujulisha tarehe ya Laylatul Qadr ikawa kuna watu wawili wanagombana ,akasema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) nimetaka kukujuulisheni Laylatul Qadr lakini nimeshasahaulishwa na Mola wangu, lakini jitahidini katika usiku wa kuamkia ishirini na moja, na ishirini na tatu na ishirini na tano .”
Kutokana na dalili hizo na nyenginezo tunafahamu ya kuwa usiku huu haujulikani kwa tarehe maalumu bali ni kujitahidi katika siku kadhaa, pengine itaangukia katika moja ya hizo.
Hikma ya kufichwa Laylatul Qadri
Usiku huu umefichwa usijulikane na kila mtu kwa hikma maalumu, nayo ni kwamba lau ungalijulikana kuwa ni taarehe gani pengine watu wangaliacha kufanya ibada siku zote na kuusubiri usiku huu, jambo ambalo lingeangusha makusudio ya kumuabudu Allah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwani tunatakiwa tumuabudu Allah kila wakati, na huku kuwekwa nyakati maalumu kwa kuzidi fadhila si jengine isipokuwa kuwashajiisha waumini katika kukimbilia mambo ya kheri, na miongoni mwa nyakati zenye fadhila kuliko nyengine ni siku ya Ijuma ambayo ndani yake kuna wakati hupokelewa dua ya mja hapo hapo, lakini haujulikani ni upi wakati wenyewe, muhimu ni kujitahidi mchana kutwa kuomba dua, pia jina tukufu la Allah hili hakuna alijualo na mwenye kulitaja kisha akaomba dua hupokelewa haraka, hivyo mja anatakiwa ayasome majina ya Allah kila atakapo omba dua.
Hivyo hikma ya kufichwa usiku huu ni mja kuongeza bidii katika ibada kwani mja hatokuwa na uhakika ni usiku upi unaokusudiwa, hivyo atakuwa makini kuhakikisha kuwa masiku yote afanye ibada ili usimpite hata usiku mmoja, na mwenye kumuabudu Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika kila siku ndani ya Ramadhani basi ni hakika ataudiriki tu usiku huu na hii ndio hikma na ndio njia peke ya kuudiriki Laylatul Qadri.
Na hili la kukesha mwezi mzima sio gumu ikiwa mtu anajuwa thamani ya usiku huu. Tutoe mfano ikiwa itatangaziwa na shirika fulani kuwa atakaekesha mwezi atapatiwa mamilioni ya fedha. Hakika kivumbi cha watu kutaka hizo fedha kitakuwa ni kikubwa mno na kila mmoja atakwenda kuulizia shuruti na kutaka kujuwa atapitiwa saa ngapi kuhakikisha kuwa yupo amekesha, lakini huku ambako Allah ametutaka tukeshe mwezi huu kwa kufanya ibada wala si kukesha usiku kucha bali ni sehemu tu ukiidumisha itakutosha, ikiwa utajitahidi masaa mawili kabla ya alfajiri ukawa macho ili saa moja ukasali na nyengine ukajiandaa na kula daku na kusubiri sala ya Alfajiri kwa kuomba dua, itatosha sana, na ukiweza zaidi ya hivyo ni bora zaidi.
Na tujitahidi tusije tukapuuza haya tukaja kuingizwa katika wale wenye udhaifu wa imani zao, na hili haliko mbali kwani asiyejihimu na ibada basi imani yake hupunguwa tu hadi kuwa mnafiki, tumuombe Allah atuepushe na sifa hiyo mbaya, “Amin”.
Ibada za kufanya katika usiku huu.
Katika Laylatul Qadri mtu anaweza kuomba dua aitakayo katika siku yoyote atakayokesha ,na iwe kwa lugha yoyote ile, bali kila akiomba dua akaifahamu maana yake ndipo hupokelewa zaidi, pia anaweza mtu akafanya ibada azitakazo ikiwa ni kusali, kusoma Qurani na kumtaja Allah kwa wingi pamoja na kumsalia Bwana Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Lakini kwa vile Mtume wetu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amtufundisha ibada maalumu pamoja na dua maalumu hivyo itapendeza kufuata mafunzo hayo.
Bibi Aisha (Radhiya Llahu anhaa).a) alimuuliza Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam);
"Ni dua gani tuombe katika usiku huu?', Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akajibu;
“Muombeni Mola wenu msamaha, nayo ni kusema: “Allahumma innaka Afuwun tuhibbul Afwa Faafu anni”, yaani “Ewe mola hakika wewe ni msamehevu unapenda kusamehe basi nisamehe”.
Pia Mja anatakiwa akeshe kwa kusali kwani Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
“Mwenye kusimama kwa kusali usiku wa Ramadhani kwa kuamini na kutaraji kulipwa thawabu basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”
Ya Allah, hakika wewe ni msamehevu unapenda kusamehe basi tusamehe maadhambi yetu. “Amin"