Pamoja Na Bwana Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
Katika Ramadhaan

 

Imetayarishwa Na Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

Shukrani zote ni zake Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote. Tunamshukuru, tunamtegemea na tunajilinda kwake kutokana na shari za nafsi zetu na amali zetu zilizo ovu. Atakayeongozwa na Mwenyezi Mungu hapana wa kumpotosha na atakayeachwa, hatopata wa kumuongoza.

Ninashuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja wake na Mtume wake na kipenzi chake. Ameutimiza Ujumbe, ameifikisha Amana, amewanasihi Ummah na amepigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kama inavyopaswa. Mola wetu zifikishe swala na salaam zetu kwa kipenzi chako huyu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mola wetu, warehemu wazee wetu na walimu wetu na kila aliyekuwa sababu katika malezi na elimu yetu. Walio hai na waliokwishatutangulia.

Mola wetu, zijaze nyoyo zetu imani na utuingizie matumaini na utulivu ndani ya nafsi zetu. Tuenezee kheri na baraka na masikilizano majumbani mwetu. Wahifadhi watoto wetu, tujaalie wake zetu na watoto wetu wawe pambo la macho yetu.

Mola wetu, tutunukie ucha Mungu ili tuweze kuepukana na kukuasi. Tujaalie tuwe watiifu wa amri zako ili tustahiki kuingia ndani ya Pepo yako. Tumiminie matumaini ndani ya nyoyo zetu ili tuwe na nguvu za kuyapuuza masaibu ya dunia.

Mola wetu, zipe nguvu nyoyo za wapiganao Jihadi dhidi ya adui wako kote ulimwenguni. Ziongoze risasi zao, zielekeze shabaha zao, zithibitishe hatua zao na uwape nusura iliyo karibu Yaa rabbil ‘aalamiyn – Aamiyn.

Mwenyezi Mungu Anasema:

ÔóåúÑõ ÑóãóÖóÇäó ÇáøóÐöíó ÃõäÒöáó Ýöíåö ÇáúÞõÑúÂäõ åõÏðì áøöáäøóÇÓö æóÈóíøöäóÇÊò ãøöäó ÇáúåõÏóì æóÇáúÝõÑúÞóÇäö Ýóãóä ÔóåöÏó ãöäßõãõ ÇáÔøóåúÑó ÝóáúíóÕõãúåõ æóãóä ßóÇäó ãóÑöíÖðÇ Ãóæú Úóáóì ÓóÝóÑò ÝóÚöÏøóÉñ ãøöäú ÃóíøóÇãò ÃõÎóÑó íõÑöíÏõ Çááøåõ Èößõãõ ÇáúíõÓúÑó æóáÇó íõÑöíÏõ Èößõãõ ÇáúÚõÓúÑó æóáöÊõßúãöáõæÇú ÇáúÚöÏøóÉó æóáöÊõßóÈøöÑõæÇú Çááøåó Úóáóì ãóÇ åóÏóÇßõãú æóáóÚóáøóßõãú ÊóÔúßõÑõæäó.

{{Ni mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qur-aan ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uwongozi na upambanuzi. Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhaan) afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini basi (atimize) hesabu (ya siku alizowacha kufunga) katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.}} [Al-Baqarah: 185]

 

Mwezi wa Ramadhaan ndio huo ushaingia. Mwezi wa Rahmah, mwezi wa Barkah, mwezi wa Maghfirah, mwezi wa kuepushwa na moto wa Jahannam.

Mwenyezi Mungu ametutunukia mwezi huu kama ni zawadi kutoka Kwake kwa ajili ya kututakasa, kuturehemu, kutughufuria madhambi yetu, kuzinyanyua darja zetu na kuzilainisha nyoyo zetu.

Kwa ajili hii, inatupasa kuukabili ukarimu huu utokao kwa Mola wetu Mkarimu (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kujitakasa na kutubu kutokana na madhambi tuliyoyachuma miezi kumi na moja iliyopita, huku tukimuomba atughufurie na huku tukimuahidi kutoyarudia tena madhambi hayo.

Mwenyezi Mungu Anasema:

æóÇáøóÐöíäó ÅöÐóÇ ÝóÚóáõæÇú ÝóÇÍöÔóÉð Ãóæú ÙóáóãõæÇú ÃóäúÝõÓóåõãú ÐóßóÑõæÇú Çááøåó ÝóÇÓúÊóÛúÝóÑõæÇú áöÐõäõæÈöåöãú æóãóä íóÛúÝöÑõ ÇáÐøõäõæÈó ÅöáÇøó Çááøåõ æóáóãú íõÕöÑøõæÇú Úóáóì ãóÇ ÝóÚóáõæÇú æóåõãú íóÚúáóãõæäó

{{Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua.}} [Aali ‘Imraan: 135]

Sayidul-Istighfaar

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mwenyezi Mungu huifurahia toba ya mja wake kuliko mmoja wenu anapokuwa juu ya mnyama wake jangwani akamuangusha na kumkimbia.)) [Imepokewa na Bukhaariy]

Na katika riwaya ya Muslim na wengine:

((Mwenyezi Mungu huifurahia toba ya mja wake kuliko mmoja wenu anapokuwa juu ya mnyama wake jangwani akamuangusha na kumkimbia, akiwa amebeba chakula na maji yake (mtu huyo), kisha mtu huyo akakata tamaa, akauendea mti na kuegemea chini ya kivuli chake akiwa keshakata tamaa ya kumuona tena mnyama wake. Na anapokuwa katika hali hiyo, ghafla anamuona mnyama wake mbele yake. Akazishika hatamu zake, kisha akasema kwa furaha: "Mola wangu Wewe ni mja wangu na mimi ni mola wako". “Alikosea kwa wingi wa furaha.”)) [Imepokewa na Muslim na wengine.]

Na sababu ya Mwenyezi Mungu kuifurahia toba hiyo ni kuwa anaridhika na nia ya mja wake juu ya kuwa alikosea kutamka.

Ndugu zangu Waislamu, huu ndio wakati wa kuomba maghfirah. Jitaabishe ndani ya mwezi huu upate kupumzika siku ile watu watakapotaabika. Mche Mungu zaidi upate kuwa mwenye matumaini siku ile watu watakapokata tamaa. Lia sana upate kucheka siku ile watu watakapokuwa na khofu.

Jisogeze kwa Mola wako kwa kustaghfiru, kwani Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba maghfira kwa Mola wake kila siku mara mia moja.

Miongoni mwa dua za kuomba maghfirah ni hii inayoitwa 'Sayyid al Istighfaar' (Dua bora ya kuomba Maghfirah kupita zote) aliyotuusia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Imepokelewa kutoka Shaddaad bin ‘Aus (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Bwana wa kuomba maghfira ni kusema:

Çááøóåõãøó ÃóäúÊó ÑóÈøöí áÇ Åöáóåó ÅáÇ ÃóäúÊó ÎóáóÞúÊóäöí æóÃóäóÇ ÚóÈúÏõßó æóÃóäóÇ Úóáóì ÚóåúÏößó æóæóÚúÏößó ãóÇ ÇÓúÊóØóÚúÊõ ÃóÚõæÐõ Èößó ãöäú ÔóÑøö ãóÇ ÕóäóÚúÊõ ÃóÈõæÁõ áóßó ÈöäöÚúãóÊößó Úóáóíøó æóÃóÈõæÁõ áóßó ÈöÐóäúÈöí ÝóÇÛúÝöÑú áöí ÝóÅöäøóåõ áÇ íóÛúÝöÑõ ÇáÐøõäõæÈó ÅöáÇ ÃóäúÊó.

((Allahumma anta Rabbiy laa ilaaha illa anta, khalaqtaniy wa ana ‘abduka, wa ana ‘alaa ‘a-hdika wa wa’adika ma statwa’atu. A’udhu bika min sharri ma sana’atu, abuu laka bini’imatika ‘alayya wa abu'u laka bidhanbiy, faghfirliy, fainnahu laa yaghfiru dhunuuba illa anta.))

Akasema: ((Atakayesema hayo wakati wa mchana akiwa na yakini juu yake, kisha akafa siku hiyo kabla ya usiku kuingia, huyo ni katika watu wa Peponi. Na atakayesema hayo wakati wa usiku akiwa na yakini juu yake, akafa kabla ya asubuhi kuingia, huyo ni katika watu wa Peponi.))

[Imepokewa na Bukhaariy, Attirmidhy, Annasai na wengine]

Maana yake (Dua ya Sayidul-Istighfaar)                   

Ewe Allaah. Wewe ni Mola wangu mlezi hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Wewe

Çááøóåõãøó ÃóäúÊó ÑóÈøöí áÇ Åöáóåó ÅáÇ ÃóäúÊó

Umeniumba na mimi ni mja Wako

ÎóáóÞúÊóäöí æóÃóäóÇ ÚóÈúÏõßó

Na mimi nimo katika kutekeleza maamrisho Yako na wa’adi Wako niwezavyo

æóÃóäóÇ Úóáóì ÚóåúÏößó æóæóÚúÏößó ãóÇ ÇÓúÊóØóÚúÊõ

Ninajikinga Kwako na kila shari niliyoitenda

ÃóÚõæÐõ Èößó ãöäú ÔóÑøö ãóÇ ÕóäóÚúÊõ

Ninakiri Kwako kwa neema Zako juu yangu

ÃóÈõæÁõ áóßó ÈöäöÚúãóÊößó Úóáóíøó

Na ninakiri Kwako juu ya dhambi zangu

æóÃóÈõæÁõ áóßó ÈöÐóäúÈöí

Kwa hivyo unisamehe kwa sababu hapana mwenye kusamehe madhambi isipokuwa Wewe

ÝóÇÛúÝöÑú áöí ÝóÅöäøóåõ áÇ íóÛúÝöÑõ ÇáÐøõäõæÈó ÅöáÇ ÃóäúÊó.

Namtakia kila Muislamu Ramadhaan njema ya mwaka huu na kila mwaka, huku nikimuomba Mwenyezi Mungu Atujaalie tufaidike na Ramadhaan hii na nyingi zijazo, miaka baada ya miaka  - Aamiyn.

Kutoka kwa Ka’ab bin Ujarah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema kuwa siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda juu ya membari yake na alipoikanyaga ngazi ya mwanzo alisema 'Aamiyn', kisha akapanda ngazi ya pili akasema tena 'Aamiyn' na juu ya ngazi ya tatu pia alisema 'Aamiyn'. Alipoteremka tulimuuliza: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tumekusikia leo ukitamka maneno si kawaida yako?" Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema:

((Alinijia Jibriyl nilipokuwa juu ya ngazi ya mwanzo akaniambia: 'Ametengwa mbali mtu aliyeiwahi Ramadhaan kisha asighufuriwe madhambi yake, sema 'Aamiyn', nikasema: 'Aamiyn'. Nilipopanda ngazi ya pili akaniambia: ‘Ametengwa mbali yule ambaye umetajwa mbele yake kisha asikuswalie, sema 'Aamiyn', nikasema; 'Aamiyn'. Nilipokuwa juu ya ngazi ya tatu akaniambia: 'Ametengwa mbali aliyeishi na wazazi wake wawili wakiwa katika umri mkubwa au mmoja kati yao kisha wasimuingize Peponi (wasiwe sababu ya kumuingiza Peponi)' sema; 'Aamiyn'. Nikasema: ‘Aamiyn.’))

Maana ya Hadiyth:

Ramadhaan ni mwezi mtukufu tuliotunukiwa na Mola wetu (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa ajili ya kutumiminia Rahmah na Maghfirah na kutuepusha na Moto. Muislamu wa kweli haiachi fursa kama hii ndani ya mwezi kama huu uliojaa khayr nyingi ndani yake na Barkah. Bali huongeza jitihada katika kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu na kujiepusha na kumuasi. Mwenye kuipuuza neema kama hii, huyo anastahiki kutengwa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa kumswalia ni katika matendo adhimu na yenye kusababisha kupata Rahmah za Mwenyezi Mungu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

((Atakayeniswalia mara moja, Mwenyezi Mungu atamswalia (atamtakia rahmah) mara kumi.)) [Imepokewa na Muslim]

Na akasema:

((Wenye kustahiki zaidi kuwa nami siku ya Qiyaamah ni wale wenye kuniswalia kwa wingi.)) [Imepokwa na Attirmidhy]

Na akasema:

((Isugulike juu ya mchanga pua ya yule niliyetajwa mbele yake kisha asiniswalie.)) [Imepokewa na Attirmidhy]

Kuwatendea mema wazazi ni katika matendo anayoyapenda Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).

Kutoka kwa Abdullahi bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: "Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu; matendo yepi yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu?” Akasema: ((Swala katika wakati wake.)) Nikamuuliza: "Kisha ipi?" Akaniambia: ((Kisha kuwatendea mema wazazi wawili.)) Nikamuuliza: “Kisha ipi?” Akaniambia: ((Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Na kinyume cha hayo ni kutowatendea mema wazee wawili. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Watatu hawafaidiki na amali zao (hawazipatii thawabu amali zao). Mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, asiyewatendea wema wazazi wake wawili, na mwenye kukimbia akawaacha wenzake uwanjani siku ya vita.)) [Imepokewa na Attabarani]

Ndani ya mwezi huu


Ndani ya mwezi huu mna Maghfirah na kunyanyuliwa Darjah na thawabu nyingi. Na ndani ya kila usiku wa mwezi huu Mwenyezi Mungu, huwaepusha na Moto wengi miongoni mwa waja wake.

Ndani ya mwezi huu du’ah zinatakabaliwa wakati wa kula futari, nyakati za usiku, tunaposoma Qur-aan, ndani ya Swalah na wakati wowote mtu anapoamua kunyanyua mikono yake na kumuomba Mola wake.

Usiku mmoja peke yake wa 'Lailatul Qadar' ni bora kuliko miezi elfu.

Milango ya Moto inafungwa na ya Pepo inafunguliwa, na mashetani wanakomelewa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Atakayefunga Ramadhaan kwa imani na kwa kutarajia, hufutiwa dhambi zake zilizotangulia.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Na akasema:

((Mwenyezi Mungu anao anaowaepusha (na Moto) kila mchana na usiku.)) [Sahih At-Targhiib-988]

 

Kwa hivyo Mola wetu Mkarimu tutakabalie na sisi du’aah zetu, tujaalie tuwe katika watakaohitimisha Qur-aan mara nyingi ndani ya mwezi huu na miezi mingine. Tufutie dhambi zetu na utujaalie tuwe miongoni mwa hao utakaowaepusha na Moto – Aamiyn.

Sharti Za Kukubaliwa Amali

Sharti la mwanzo la kukubaliwa kwa amali, ni kuihusisha amali hiyo iwe halisi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), na sharti la pili ni amali hiyo ikubaliane na mafundisho aliyokuja nayo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Hapana amali inayokubaliana na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupita ile aliyokuwa akiitenda mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Yafuatayo ni baadhi ya matendo aliyokuwa akiyatenda ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhaan. Nakuleteeni ili yawe dira itakayotumulikia na kutuongoza njia, huku tukifunga kama alivyokuwa akifunga, na kufanya ibada nyingine kama alivyokuwa akizifanya.

Vipi Alikuwa Akiukaribisha Mwezi?

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haanzi kufunga mpaka ahakikishe kuwa mwezi umeonekana. Alikuwa akiutafuta na akiwaamrisha wengine wautafute, na anapojuulishwa na yeyote kati ya Swahaabah zake (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ameuona mwezi, na yeye huamrisha umati wake kufunga.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Fungeni mnapouona na fungueni mnapouona, na mnaposhindwa kuuona kwa ajili ya mawingu basi kamilisheni mwezi wa Shaaban siku thelathini.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Alikuwa akiwakataza watu wake kufunga siku moja au mbili kabla ya kuandama mwezi, na aliwahi kusema:

((Msiutangulie mwezi wa Ramadhaan kwa kufunga kabla yake siku moja au siku mbili isipokuwa kama mtu anayo kawaida ya kufunga (ndani ya siku hizo) basi na afunge.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Kutia Nia

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika saumu za fardhi akitia nia tokea usiku kabla ya kuingia alfajiri na alikuwa akisema:

((Asiyetia nia tokea usiku hana swaum.)) [Imepokewa na Annasai kutoka kwa Bibi Hafsah (Radhiya Allaahu ‘Anha), Sahiih-al-Jami’i 6535.]

Na katika riwaya nyingine alisema:

((Asiyetia nia kabla ya kuingia alfajiri hana swaum.)) [Imepokewa Al Bayhaqi na Addaraqutni Sahiih-al-Jami’i, 6534]

Na alisema:

((Asiyetia nia ya kufunga kabla ya kuingia alfajiri, huyo hana funga.)) [Imaam Ahmad na watatu wengine, Sahiih-al-Jami’i, 6538]

Hizi zote zinahusiana na swaum za fardhi, kwa sababu katika swaum zisizokuwa za fardhi mtu halazimiki kutia nia tokea usiku.

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika baadhi ya siku zisizokuwa Ramadhaani anapokwenda kwa wake zake asipate chakula huuliza: ((“Kipo chakula chochote?" na anapojibiwa: "Hapana", yeye husema: "Basi mimi nimefunga.”)) [Imepokewa na Muslim]

Kula Futari (Kuftari)

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiharakisha kula futari na akilichelewesha daku. Alikuwa akisema: ((Umati wangu utakuwa katika khayr kama utaendelea kuharakisha (kula) futari na kuchelewesha (kula) daku.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Na katika Hadiyth nyingine alisema:

((Usiku ukianza kuingia upande huu na mchana kutoweka upande huu na jua kuzama, basi aliyefunga (awe) kesha kula futari.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Na kutoka kwa Abud-Dar-daa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

((Matatu ni katika matendo ya Mitume - Kuharakisha futari (kifungua kinywa), kuchelewesha daku, na kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto ndani ya Swalah.)) [Imepokewa na Attabaraniy]

Na futari ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa hafifu sana tofauti na yetu siku hizi. Alikuwa akila tende chembe 3 au 5 au 7 na kunywa maji. Anapokosa tende, hunywa maji kisha hukimbilia kuswali katika wakati wake wa mwanzo. [Imepokewa na Ahmad na Abu Daawud na Attirmidhy]

Na katika riwaya nyingine Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

((Atakayepata tende afungulie kinywa, na asiyepata tende afungue kinywa kwa (kunywa) maji.)) [Angalia Sahiih at-Targhiib, 1064]

Kuomba Du’aah

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisisitiza watu waombe du’aah wakati wa kula futari, kwa sababu du’aah ya wakati huo hairudi patupu, na akipendekeza hivyo sana. Katika du’aah alizokuwa akiomba ilikuwa:

"ÐåÈ ÇáÙãà æÇÈÊáÊ ÇáÚÑæÞ æËÈÊ ÇáÃÌÑ Åä ÔÇÁ Çááå"

Na maana yake: ((Kiu imekatika na mishipa imerutubika na ujira (thawabu) umepatikana kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.)) [Imepokewa na Abu Daawuud – Addaraqutni na Al Hakim]

Na alikuwa akipendekeza kuwalisha futari waliofunga. Alikuwa akisema: ((Atakayemfutarisha aliyefunga anapata thawabu sawa na zake, na thawabu za yule aliyefunga hazipungui kitu ndani yake.)) [Angalia Sahiih at-Targhiib, 1072]

Kula Daku

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hajawahi hata siku moja kuacha kula daku. Jambo lililowafanya baadhi ya wanavyuoni kutamka kuwa kula daku ni kitendo cha wajibu.

Alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Kuleni daku kwa sababu katika kula daku mna barka.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Na akasema:

((Daku lote lina barka, kwa hivyo msiache kula hata ikibidi kunywa fundo ya maji, kwa sababu Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanawatakia rahmah wanaokula daku.)) [Angalia Sahiih at-Targhiib, 1062 na Sahih al Jam Sahiih-al-Jami’i, 3577]

Katika barka za kula daku ni kupata thawabu kwa ajili ya kufuata mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na pia linakupa nguvu za kufanya ‘ibaadah wakati wa mchana na katika kufanya shughuli za kawaida.

Thawabu za kula daku zinapatikana kwa kula chakula chochote kabla ya muadhini wa Alfajiri, hata kama ni tende au maji. Bali Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kusema:

((Daku bora kwa Muislamu ni tende.)) [Imepokewa na Abu Daawuud na Ibni Hibban na Al Baihaqy]

Alikuwa akiendelea kula na kunywa mpaka alfajiri inapoingia na hii inatokana na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

æóßõáõæÇú æóÇÔúÑóÈõæÇú ÍóÊøóì íóÊóÈóíøóäó áóßõãõ ÇáúÎóíúØõ ÇáÃóÈúíóÖõ ãöäó ÇáúÎóíúØö ÇáÃóÓúæóÏö

((Na kuleni na kunyweni mpaka ukubainikieni weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku.)) [Al-Baqarah: 187]

Na aliwahi kumruhusu Sayyidna ‘Umar aendelee kula daku na kunywa maji yake huku akiusikia muadhini. Pia imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Mtu anapomsikia muadhini na chakula kimo mikononi, asikirudishe mpaka amalize haja yake.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad, Abu Daawuud na Al-Hakim. Imesahihishwa na Al-Albaaniy katika Sahiih-al-Jami’i, 1394]

‘Ibaadah Zake

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijitahidi zaidi kufanya ‘ibaadah ndani ya mwezi wa Ramadhaan kupita miezi mingine. Na katika mwezi huu Jibril (‘Alayhis Salaam) alikuwa akimsomesha Qur-aan. Kwa ajili hii watu wema waliotangulia walikuwa wakishindana katika kusoma na kuhitimisha Qur-aan ndani ya mwezi wa Ramadhaan.

Maulamaa wakubwa kama vile Imaam Az-Zuhri na Imaam Maalik na wengine wengi (Rahimahumu Allaah) walikuwa wakiacha kufanya darsi zao na pia wakisimamisha shughuli za kutoa fatwa katika mwezi huu kwa ajili ya kujishughulisha na kusoma Qur-aan na kuihitimisha mara nyingi.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa linapoingia kumi la mwisho akiukaza vizuri mkanda wake na akiwaamsha wake zake na kukesha nyakati za usiku. Alikuwa akifanya Itikafu ndani ya kumi la mwisho huku akiusubiri usiku wa Laylatul-Qadar, na alikuwa akiwahimiza watu kukithirisha ‘ibaadah ndani ya usiku huo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Atakayesimama (kwa kuswali na kuomba dua usiku wa) Laylatul-Qadar kwa imani na kwa kutarajia, amesamehewa dhambi zake zilizotangulia.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Ndugu zangu Waislam! Kumi la mwanzo limekwishamalizika, na la pili ndiyo hilo linaanza kutupa mgongo. Kwa hivyo panieni vizuri, kwa sababu siku zinakwenda haraka sana na wakati uliobaki ni mchache, na bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni ghali sana. Bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni Pepo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuogopa huianza mapema safari yake, na mwenye kuianza safari mapema atawasili mapema. Hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni ghali sana. Hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni Pepo.)) [Imepokewa na Attirmidhy na Al-Haakim katika Al-Mustadrak kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu)]

 Ukarimu Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

Alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mkarimu sana katika mwezi huu wa Ramadhaan. Imepokelewa kuwa; ((Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mkarimu sana, na ukarimu wake ulizidi kupita kiasi ndani ya mwezi wa Ramadhaan.)) [Imepokewa na Bukhaariy]

Na kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

((Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mkarimu sana, na alikuwa mkarimu zaidi ndani ya mwezi wa Ramadhaan wakati anapoonana na Jibriyl (‘Alayhis Salaam). Na alikuwa akionana na Jibriyl ndani ya kila usiku wa Ramadhaani anamsomesha Qur-aan. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapoonana na Jibriyl huwa mkarimu kuliko upepo uliotumwa (kueneza khayr kila mahali).)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Kusimama Nyakati Za Usiku (Qiyaam)

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwahimiza Swahaabah zake (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuswali nyakati za usiku katika mwezi wa Ramadhaan bila kuwalazimisha. Alikuwa akisema:

((Atakayeswali (Qiyaam) usiku katika mwezi wa Ramadhaan kwa imani na kwa kutarajia, amesamehewa dhambi zake zilizotangulia.)) [Imepokewa na Muslim, 759]

[Pia imepokewa kwamba] atakayeswali Taraawiyh, basi anahesabiwa kuwa ameswali Qiyaam.

‘Umrah

Alikuwa akipendekeza watu wafanye ‘Umrah ndani ya mwezi wa Ramadhaan. Alikuwa akisema:

((‘Umrah ndani ya mwezi wa Ramadhaan (thawabu zake) ni sawa na Hijjah.)) Na katika riwaya nyingine: ((Sawa na Hijjah pamoja nami.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Tabia Njema

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mbora wa mwenendo na tabia njema kupita watu wote, na alikuwa akiwaamrisha umati wake kuwa hivyo. Kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Kufunga siyo kujizuwia kula na kunywa peke yake, bali kufunga ni kujizuwia na maneno pamoja na vitendo viovu. Na kama mtu atakutukana au atakudharau, wewe muambie: "Mimi nimefunga, mimi nimefunga.")) [Angalia Sahiih-al-Jami’i, 88/5]

Na akasema:

((Ikiwa mtu hatoacha kusema uongo na kuufanyia kazi uongo huo, basi Mwenyezi Mungu hana haja ya kuacha kwake kula na kunywa.)) [Imepokewa na Bukhaariy, Attirmidhy, Al-Baihaqiy na wengine]

Kuunganisha Nasaba

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika mwezi huu akikithirisha kuwatembelea ndugu na jamaa zake na kuzidisha katika kuwatendea mema kuliko ndani ya miezi mingine.

Alikuwa akizidisha katika kuwatendea wema hata wake zake. Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa usiku akiwaingilia wake zake na mara nyingine alfajiri huingia akiwa bado mwenye janaba, kisha hufunga na kuendelea na swaumu yake. [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

Alikuwa akiwabusu baadhi ya wake zake huku akiwa amefunga na alikuwa akiimiliki nafsi yake.

Mwenye Huruma Kwa umati Wake

Alikuwa mwingi wa huruma kwa umati wake, aliwaruhusu wanaokula kwa kusahau waendelee na swaumu zao.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Mmoja wenu anaposahau akala na kunywa basi akamilishe swaumu yake kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyemlisha na kumnywesha.)) [Imepokewa na Bukhaariy na Muslim]

 

Na akasema: ((Aliyetapika bila kukusudia aendelee na swaumu, lakini aliyejitapisha kusudi alipe.)) [Imepokewa na Abu Daawuud, Attirmidhiy, Ibni Maajah na Imaam Ahmad]

Zakaatul-Fitwr

Katika mwezi wa Shaaban mwaka wa pili baada ya Hijrah (baada ya kuhamia Madiynah), Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaradhisha Zakaatul-Fitwr ili iitakase swaumu kutokana na dhambi ndogo ndogo zilizopatikana ndani ya mazungumzo na matendo. Na wakati huo huo Zakah hiyo iwe msaada kwa mafakiri na wasiojiweza katika kuisherehekea Sikukuu.

Imepokelewa kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema: ((Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaridhisha Zakah ya Fitwr kwa ajili ya kumtakasa aliyefunga kutokana na dhambi ndogo ndogo za mazungumzo na matendo, na ili wafaidike masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalah (ya ‘Iyd) inakubaliwa kama Zakah ya Fitwr, na atakayeitoa baada ya Swalah inakubaliwa kama Swadaqah ya kawaida.)) [Imepokewa na Abu Daawuud, Ibni Maajah na Addaraqutniy]

Alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akitoa Zakah ya Fitwr siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhaan kabla ya Swalah ya ‘Iyd kuswaliwa. [Imepokewa na Abu Daawuud, Ibni Maajah na Al-Haakim]