WALIOJIFICHA NYUMA YA PAZIA LA KARBALA

 

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa ta’ala), kutujaalia uhai na fursa hii ya kuweza kuandika tukio hili ambalo limekuwa likisimuliwa kwa mtazamo wa uadui na chuki.

 

Kuzungumzia kisa cha Karbala kumekuwa ni mila na msingi mkubwa katika imani ya Kishia. Michezo ya kuigiza, makala na mashairi yanayoandikwa kuhusu Kifo cha Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), ni matukio ya kusikitisha kwani wafuasi hulazimika kujipiga na hatimaye kujijeruhi kwa mantiki hasa ya kuomboleza msiba huo. Matukio haya yote ya kujitoa muhanga yametawala katika mwezi wa Muharram kiasi kwamba inaonesha umuhimu wa tukio hili na nadhani Aashuraa ndio siku muhimu sana katika Kalenda ya Kishia katika mwaka mzima.

 

Inasikitisha kuona kwamba mazingatio makubwa kuhusu somo hili la Karbala yamepotoshwa na kuonekana kwamba ni vita vya pande mbili, Al-Husayn dhidi ya Yazid, haki dhidi ya batil, kiu ya kutaka kusimamisha haki dhidi ya utawala wa kidhalimu, na hata baadhi ya wababaishaji wamefikia kusema kwamba ilikuwa ni vita vya Shia dhidi ya Ahlus Sunnah.

 

Katika kukieleza kisa hiki, tutazingatia matukio halisi yaliyotokea Karbala kwa kuwaangalia wahusika wote katika tukio hilo la Aashuraa na tutaona kuna msiba mwingine uliojificha kwani wanapoadhimisha kifo cha Sayyidna Al-Husayn kwa kuwatambua wauaji wake na kuwalaani, lakini hakuna aliyebakiza hasira zake hata kidogo kwa wale waliomkimbia katika wasaa muhimu. Kwani ni watu hawa waliofichwa ambao wanastahili kuitwa Wasaliti na Wauaji wa Karbala, ambao ndiwo tutawazungumzia katika makala hii.

 

Ilikuwa ni Mwezi wa Ramadhani, Mwaka wa 60H wakati barua kutoka Kufah zilianza kumiminika katika nyumba ya ‘Abbaas ibn ‘Abd al-Muttalib mjini Makka, ambapo Al-Husayn ibn ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa akiishi baada ya kuhama kutoka Madina, barua zilizokuwa zikimtaka kuwaongoza watu wa mji wa Kufah katika mapindunzi dhidi ya Yazid ibn Mu’awiyah (Radhiya Llaahu ‘anhu), na kumuhakikishia ushirikiano na bay’aha. Tukio hili lilitokea miaka miwili baada ya kifo cha Mu’awiyah (Radhiya Llaahu ‘anhu). Watu wa Kufah walikuwa wanamuona Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), kama kiongozi wao na licha ya kumuandikia barua za kumtaka yeye kuhamia Kufah pia walituma ujumbe maalum uliokwenda kumuona mara nyingi, kwa siku moja alikuwa anapelekewa mpaka barua 600 ambazo zilikuwa zinaelezea msaada na ushirikiano watakaompa.

 

Kufah ulikuwa ni mji wa kipekee, na watu wake pia walikuwa wakipekee. Mwaka wa 37H, Sayyidna ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), alihamisha makao yake makuu kutoka Madina hadi Kufah na kuanzia wakati huo mji huo ukawa ndio maskani kwa wale waliojiita wapenzi wa Ah al-bayt. Baada ya muafaka kati ya Sayyidna Al-Hasan (Radhiya Llaahu ‘anhu) na Mu’awiyah (Radhiya Llaahu ‘anhu) katika mwaka wa 41H, wengi wa wale waliokuwa upande wa jeshi la Sayyidna Al-Hasan (Radhiya Llaahu ‘anhu) walihamia na kuishi Kufah na wakati wa kifo cha Mu’awiyah (Radhiya Llaahu ‘anhu), mwaka wa 60H wakazi wengi wa Kufah walikuwa ni wapenzi wa Sayyidna ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu), na ndiyo maana nafasi ilipotokea, watu wa Kufah amabao waliokuwa wakijiita Shi’a (Wafuasi) wa Ahl al-bayt, walitaka Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) awaongoze dhidi ya Yazid.

 

Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliamua kumtuma binamu yake aitwae Muslim ibn ‘‘Aqil kwenda Kufah kuchunguza kuhusiana na maombi yaliyokuwa yakimininika kila siku na akipata ukweli wa madai hayo amuandikie Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), ili ahame Makka pamoja na Familia yake na kuungana nae katika mji wa Kufah.

 

Muslim alifikia katika nyumba ya Muslim ibn ‘Awsajah al-Asadi katika mwezi wa Dhul Qa’dah na pindi watu wa Kufah walipofahamu kuwasili kwa Muslim ibn ‘‘Aqil walijitokeza kwa wingi sana na kwa kipindi kifupi walifikia 12,000 ambao wote walijitolea kwa hali na mali kumsaidia na kumlinda Sayyidina Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), afikapo Mji wa Kufah. Idadi ilipozidi na kutimia 18,000,

 

Muslim alipata matumaini makubwa na hatimae kumtuma mjumbe ampelekee habari Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) kwamba watu wa Kufah wamempa Bay’ah (kiapo cha utii) na kumtaka aondoke Makka na kumfuata katika mji wa Kufah.

 

Habari zilipomfikia Yazid (Radhiya Llaahu ‘anhu), ambae alikuwa Damascus, kuhusu yaliyokuwa yakitokea katika mji wa Kufah, aliamua kumbadilisha Gavana wa Kufah, Nu’ma’n ibn Bashir na kumpeleka Ubaydullah ibn Ziyad huko kwa amri ya kumsaka Muslim ibn ‘‘Aqil na kumuua. Ibn Ziyad alifika Kufah mwazoni mwa mwezi wa Dhul Hijja akifuatana na askari 17 waliopanda Farasi, akiwa amejifunika uso wake kwa kilemba alichovaa. Watu hawakuweza kumtambua vizuri na kwa sababu hiyo watu wa Kufah walidhani yeye ndio Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) waliyekuwa wanamtegemea. Walimsalimu “ Amani na iwe kwako, Ewe Mtoto wa Rasulullah”. Kwa maantiki hiyo Ibn Ziyad alifahamu ukweli wa uvumi ulioenea, na waligundua kosa lao pale mmoja wa askari wa ibn Ziyad alipowaeleza kwamba huyo alikuwa ni Gavana mpya wa Kufah, Ubaydullah ibn Ziyad.

 

Baada ya kufika katika makao yake ya Gavana wa Mji wa Kufah, Ubaydullah alimtuma mjumbe, akimpa kitita cha Dirham 3000, akatafute mahali alipofikia Muslim akijifanya kama msafiri aliyetoka katika mji wa Hims ulioko Syria kwa lengo la kutaka kuungana nao katika mapinduzi. Alimpata Muslim ibn ‘Aqil katika nyumba ya Hani ibn Urwah nae pia akatoa bay’ah kwake na kumpa Dirham alizokuwa nazo Abu Thumamah al-Amiri ambaye alipewa jukumu la Mweka Hazina  wa Muslim. Baada ya kukaa nao kwa muda mfupi na kugundua mipango ya mapinduzi alirejea kwa ibn Ziyad na kumueleza alichogundua. Hani ibn Urwah baada ya kukamatwa alikataa kwamba anajua lolote kuhusu Muslim lakini alipoletwa yule msafiri wa kutoka Hims alikubali ingawa alikataa kutaja alipo Muslim.

 

Muslim ibn ‘Aqil alipofahamu kukamatwa kwa Hani ibn Urwah, aligundua kuwa wakati wa mapambano umewadia akapiga mbiu ya vita “Yah Mansur” na kwa muda mfupi walikusanyika watu 4,000 waliotoa Bay’ah na uaminifu kwa Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), na kuelekea katika nyumba ya Gavana. ‘Ubaydullah ibn Ziyad, alipomuona Muslim ibn ‘Aqil na watu wa Kufah aliwatuma viongozi wa koo kwenda kuzungumza na hao waliojikusanya kuondoka na kumuacha Muslim peke yake na pia kuwatahadharisha kuhusu maafa yatakayowafika pindi jeshi kutoka Damascus litakapofika.  Maswali na majuto yaliaanza miongoni mwa waliojiita Mashia:

(a)   Kwani ni sisi peke yetu tutakaopigana?

(b)  Wako wapi wengine?

(c)  Kutatokea nini Jeshi kutoka Damascus likiwasili?

(d)  Tutafanyaje?  Itakuwaje? 

 

Msimamo wa watu waliokula kiapo cha kumsaidia na kumhami Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) na Ahl al-bayt dhidi ya Yazid na majeshi kutoka Syria, watu ambao nguvu na umoja wa viapo vyao walivyovitoa kwamba wanampenda, kumuamini na watamlinda Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), vilimsababisha mjukuu huyu wa Mtume akawa anajiandaa kwenda Kufah akiambatana na watu wake wakaribu na wapenzi wake, msimamo wa watu hawa vigeugeu ulishindwa kuhimili vitisho.

 

Mmoja baada ya mwengine waliaanza kuondoka kutoka katika jumba la Gavana na kufikia jioni Muslim ibn ‘Aqil alikuwa amebaki na watu 30 tu, aliwasalisha Maghrib na kuongozana nao hadi nje ya mlango wa jumba la Gavana na cha kusikitisha alitoka nje na watu wasiopungua kumi (10) na kabla hajagundua kinachoendela alijikuta peke yake katika bara bara za mji wa Kufah. Ajabu iliyoje kwa wale waliomwandikia Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), kwa hiari na mapenzi yao wenyewe ili aje kuwaongoza dhidi ya Yazid, na kutoka idadi ya watu 18,000 waliotoa Bay’ah, waliomwitia mjukuu wa Rasulullah sallallahu alayhi wasallam, kwa malengo, hakubaki hata mmoja  na Muslim ibn ‘Aqil kumsaidia na hata kumpatia mahala pa kulala usiku ule.

 

Hatimaye, akiwa amechoka kwa kiu aligonga mlango, na mwenyeji wake, mama mmoja baada ya kumtambua kwamba ni Muslim ibn ‘Aqil alimkaribisha ndani, lakini kijana wake ambae aliapa kutotoa siri alisubiri na kulipokucha tu alipeleka habari kwa Gavana. Kilichofuata Muslim alishtukia nyumba ya yule mama imezingirwa. Mara tatu alifanikiwa kuwarudisha waliotaka kumshika lakini nyumba ilipoanza kuchomwa moto alitoka nje na kuaanza kukabiliana nao. Ilikuwa ni mpaka ‘Abdur-Rahman ibn Muhammad ibn al-Ash-ath ambae ndie aliyetumwa  kumkamata, kumhakishishia usalama wake hatimae aliuweka upanga chini, na hilo lilikuwa ni kosa kwani walimchukua hadi kwa ibn Ziyad. (Historia hii ni kwa mujibu ya wanazuoni wa Kishia).

Muslim alijua kifo chake kimewadia na machozi yalianza kumtoka lakini si kwa ajili yake isipokuwa ni kwa sababu alifahamu Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), alikuwa jangwani kwenye jua kali njiani akija Kufah ambapo atakutana na ghadhabu za adui aliyejitayarisha na licha ya yote adhabu kali ya watu waliomwalika ambao walimsusa yeye wakati wa mwisho na hatimae kumfikisha hapo alipo. Alimuomba ibn al-Ash’ath amtumie Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), ujumbe ufuatao “Ibn ‘Aqil amenituma kwako, anasema URUDI NA FAMILIA YAKO. USIDANGANYWE NA WATU WA KUFAH, NI WALE WALE AMBAO BABAKO ALIWAPENDA SANA NA HATA ALIKUWA TAYARI  KUFA KWA AJILI YAO. WATU WA KUFAH WAMENIDANGANYA MIMI NA PIA WAMEKUDANGANYA WEWE, NA KWA KWELI MUONGO HANA AKILI/HAYA.”

 

Baadae siku hiyo, Siku ya Arafa, mwezi 9 Dhul Hijja, Muslim ibn ‘Aqil alichukuliwa sehemu ya juu kabisa ya jumba la Gavana na wakati akichukuliwa alikuwa akisoma Tahlil, Tasbih, Takbir na akifanya Istighfar. Maneno yake ya mwisho haya yafuatao yalionyesha chuki na kukasirishwa na watu wa Kufah, “EWE ALLAH, KUWA HAKIMU KATI YETU NA WATU WETU, WALITUHADAA NA HATIMAE KUTUKIMBIA.” Kutoka juu kichwa chake kilianguka chini katika vumbi mbele ya macho ya watu waliomwalika na kula kiapo mbele yake ambao walimpa matumaini lakini kwa uoga na hila zao walimtelekeza. Na kwa wakati huo Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), alikuwa njiani.

 

‘Ubaydullah ibn Ziyad aliingia Kufah na watu 17 tu, kwa kila mtu aliyekuja naye kulikuwa na na watu Elfu(1/1000) waliochukua Bay’ah kwa Muslim ibn ‘Aqil, lakini cha kusikitisha hakuna hata mmoja wao alieinua upanga kumhami. Hakuna hata sauti ya kishujaa iliyotoka kupinga kuuliwa kwa Muslim, na cha kushangaza ni kwamba hawa ndio wale wale waliokuwa wanamwambia Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), “ NJOO, TUKO PAMOJA NAWE”

 

Baada ya kupokea barua ya Muslim ibn ‘Aqil, Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliaanza matayarisho ya safari ya Kufah. Alimtuma Mjumbe aitwae Qays ibn Mus-hir kuwajulisha watu wa kufah kwamba alikuwa wamtarajie. Lakini mjumbe huyu alikamatwa na Gavana wa Kufah pindi tu alipofika na kulazimishwa kupanda kwenye kinara na kuwatukana Husayn na Babake (Radhiya Llaahu ‘anhuma) lakini alipanda juu ya kinara na kuwasifia Sayyidna ‘Aliy na Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhuma) huku akiwaeleza kwamba Sayyidna Al-Husayn alikuwa njiani anakuja na akawaomba wamsaidie kama walivyoahidi. Alimalizia hotuba yake kwa kumlaani ibn Ziyad na kwa amri ya ibn Ziyad alifurumushwa kutoka huko na kuuwawa, cha kusikitisha ni kwamba licha ya maombi na kilio cha Qays, watu wa Kufah hawakutikisika hata kidogo.

 

Mjini Makka idadi kubwa ya masahaba na watoto wa masahaba walimsihi Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) asiende Kufah kwa kumkumbushia vitimbwi vya watu wa Kufah dhidi ya babake na kakake. ‘Abdullah ibn ‘Abbas, ‘Abdullah ibn ‘Umar, Jabir ibn ‘Abdillah, Abu Sa’id Al-Khudri, ndugu yake Muhammad na shemejiye ambae pia ni binamu yake ‘Abdullah ibn Ja’far, hawa wote hawakukubaliana na walijaribu kumshawishi Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) kutokwenda Iraq. Lakini Sayyidna Al-Husayn alikuwa ameshaamua  na aliaanza safari yake kutoka Makka mnamo mwezi 8 wa Dhul Hijja, ilhali hajui yaliyomsibu Muslim ibn ‘Aqil.

 

Baada ya safari ngumu na taabu ya takriban mwezi mmoja, walifika Iraq, ndipo walipopata habari kwa mara ya kwanza kuhusu usaliti wa watu wa Kufah na kifo cha Muslim ibn ‘Aqil na baadaye pia  alifahamu kuhusu kifo cha Qays ibn Mus-hir. Idadi kubwa ya waarabu wa jagwani walikuwa wamejiunga na kundi la Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), wakidhani kwamba tayari Kufah ilikuwa katika himaya yake. Al-Husayn aliwahutubia kwa kusema, “Watu wetu wametuasi,, kwa hivyo yoyote anaetaka kuondoka na afanye hivyo” na baada ya muda mfupi walibaki wale waliotoka Makka tu na ndio alioendelea nao na safari ya Kufah.

 

Ziyad alikuwa ameuweka mji wa Kufah katika hali ya tahadhari, na pindi habari zilipomfikia kuhusu kukaribia kwa msafara wa Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), alitoa kikosi cha askari 4,000 ambao walikuwa wanakwenda kupigana vita na Daylamites, waende kumzuia Al-Husayn. Kikosi hiki kilikuwa chini ya ‘Umar ibn Sa’d.  Nadhani bila shaka watu wa Kufah walishuhudia kwa macho yao kuondoka kwa kikosi hicho,  hii ingekuwa ni nafasi yao ya mwisho ya kutekeleza Bay’ah kwa Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), waliyoitoa  kupitia Muslim ibn ‘Aqil. Hii ilikuwa ni fursa adhimu ya kukimbilia upande wa mjukuu wa Rasullullah sallallahu alayhi wa-alihi wasallam, kwani baada ya mwaliko na uthibitisho wa kushirikiana na kumlinda aliwacha amani ya Makka na kuja kwenye uwanja wa vita nchini Iraq. Lakini uaminifu huo, ushujaa na kujituma hakukuonekana kutoka kwa watu wa Kufah. Ni wachache tu miongoni mwao waliojitokeza kumsaidia Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) hapo Karbala.

 

Na Jua lilipokuchwa mwezi 10 Muharram, Mashia wa Kufah walikuwa wameshachelewa kurekebisha makosa yao kwani mchanga wa Karbala ulitapakaa damu ya Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) na wafuasi wake 71 au 72 na watoto 2.

 

Miaka mine (4) baadaye Mashia wa Kufah walijaribu kurekebisha makosa yao ya kuwatelekeza familia ya Rasulullah sallallahu ‘alayhi wa-alihi wasallam. Kulijitokeza kikundi kilichojiita TAWWAABUN, ambao walifanya ni jukumu lao kuwataja na kuwalani waliomuua Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu). Walipokuwa wanaelekea Syria baada ya kutoka kumuona ibn Ziyad, walipitia Karbala katika eneo la kaburi la Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), ambapo walikesha usiku mzima wakijipiga, wakilia na wakisimulia kisa hicho ambacho walikiruhusu kutokea miaka mine iliyopita. Kama wangeonesha msimamo na mapenzi hayo kwa Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), wakati alipokuwa akiwahitajia sana, nadhani historia ya Uislamu ingechukuwa mkondo mwengine.

 

Mashia walipomtelekeza Zayd ibn ‘Aliy, walimtegemea Ja’far as-Sadiq kama kiongozi wa kweli, ilikuwaje basi kama Imam Ja’far as-Sadiq alikuwa na wafuasi wengi kwanini basi alishindwa kusimamisha jeshi la kupigana dhidi ya utawala wa Ummaya na ‘Abbaas? Jibu linapatikana katika mapokezi ya Abu Ja’far al-Kulayni katika kitabu chake al-Kafi, ambacho ni kitabu cha Hadith kinachohishimika sana na Mashia:

 

Sudayr as-Sayrafi amesema: Niliingia kumuona Abu ‘Abdillah alayhis salam na nikamuuliza “kwa Jina La Mwenyezi Mungu, hutasita kuchukua silaha” akauliza “kwanini nichukue”  nikajibu “kwa sababu una wapenzi na wafuasi wengi (Mashia) kuliko aliokuwa nao,”  “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, kama Amir al-Mu’minin (Sayyidna ‘Aliy), angekuwa na Mashia wengi kama ulivyonao, Taym (kabila la Abu Bakr) na Adi (kabila la ‘Umar) wasingekuwa na uwezo wowote dhidi yake”  akaniuliza “Na unadhani kuna Mashia wangapi, Sudayr”

Nikajibu “ kama laki moja”  akauliza “ Laki Moja”   “nikajibu ndyio na labda laki mbili”  akauliza tena “ laki mbili” nikajibu “Ndiyo na labda nusu ya dunia” akanyamaza. Halafu akaniambia “Unaweza kunisindikiza hadi Yanbu” nikakubali. Akaamrisha Farasi na Punda watayarishwe, kwa haraka nikapanda Punda, lakini akaniambia “Sudayr, unaweza kuniachia mimi nikapanda Punda?”  nikamjibu “Farasi ni mzuri na ana hadhi pia”  lakini akanijibu “Ninaridhika kwa kupanda Punda” nilishuka, akapanda Punda nikapanda Farasi na alau tukaanza safari yetu. Wakati wa sala ulipofika akaniambia: “Shuka, Sudayr na tusali”  lakini akabadilisha mawazo kwa kusema  “eno hili majani yamekuwa makubwa na hatuwezi kusali hapa” tuliendelea na safari yetu hadi tulipofika katika eno tambarare lenye udongo mwekundu. Alimwangalia Kijana mmoja ambae alikuwa akichunga kondoo wake, halafu akaniambia “Sudayr, kwa jina la Mwenyezi Mungu, kama ningekuwa na Mashia kiasi cha kondoo walioko hapa, isingekubalika mimi kuepuka kunyanyua silaha . Tulishuka na Kusali na tulipomaliza niligeuka na kuaanza kuwahisabu wale Kondoo, na walikuwa 17 tu.

 

Inaonesha kisa cha Karbala kilimfundisha Imam Ja’far As-Swaadiq kuhusu tabia ya wanaojiita Mashia, kitu ambacho hawa wa leo wanakataa kuelewa: kwamba katika matatizo na maafa yaliyowakuta watu wa nyumba ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam), Mashia walichangia kwa kiasi kikubwa, tena mchango wa Mashia ulikuwa ni mkubwa sana kuliko ule wa maadui zao halisi. 

Kwa maana hiyo haishangazi kuona kwamba hakuna Imam yeyote baada ya Al-Husayn, aliyejaribu mapinduzi dhidi ya utawala wa wakati huo. Karbala iliwafundisha vile watu wa kufah, ambao walijiita Mashia, jinsi walivyokuwa vigeugeu na wasaliti. Ni kutokana na hawa Mashia ndio Imam Ja’far amesema;

 

“Hakuna anaetuchukia zaidi kuliko wale wanaojifanya wanatupenda” 

 

Pia Imam Ja’far amesema

 

“Hakuna Ayah ambayo Mwenyezi Mungu amewazungumzia wanafiki, isipokuwa sifa hizo zinapatikana kwa wale wanaojita Mashia”

 

Kabla ya Sayyidna Al-Husayn, kakake Sayyidna Al-Hasan alitolewa kafara na wasaliti wa Kufah. Katika kitabu chake al-Ihtijaj, mwanazuoni na mwandishi maarufu wa kishia, Abu Mansur at-Tabarsi ameyahifahi maneno ya Sayyidna Al-Hasan katika kitabu chake hicho:

 

“Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, nadhani Mu’awiyah alikuwa na afadhali sana kwangu kuliko wale waliodai kwamba ni katika kundi langu (Mashia)”.

 

Ndugu zangu Waislam, yaliyotokea Nchini Afaghanistan wakati wa uvamizi wa Amerika na tukio la uvamizi uliomalizika hivi karibuni nchini Iraq, na majuma mawili tu yaliyopita, Mashia kwa ushirikiano na serikali ya Amerika waliandaa uchaguzi ambao makusudio na hatimae matokeo ya uchaguzi wote mnayafahamu, nadhani hili si jambo linalohitajia kuliandikia makala lakini wote tunafahamu hila, njama na usaliti uliofanyika dhidi ya Uislam.

 

Tunapenda kuwakumbusha kuhusu wale wanaodai kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisulubiwa kinyume kabisa na kauli ya Muumba wa mbingu na Ardhi illilyopo katika kitabu chake kisichokuwa na shaka ndani yake:

 

. . . Hali hawakumuua wala Hawakumsulubu, bali walifananishiwa Mtu mwingine . . . 

                          (An-Nisaa:157)                      

 

Kitu cha kushangaza, hawa jamaa kwa kuonesha majonzi na mapenzi yao wakaufanya msalaba kuwa ni alama ya ibada yao, alaa jamani tusemaje. Hali kadhalika kama kweli Mashia wanampenda na wanahuzunika kwa kifo cha Sayyidna Al-Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), huko Karbala, itakuwaje basi wauone na kuufanya udongo wa eneo hilo kuwa mtukufu kwa kutengeneza TURBA ambazo ni lazima kusujudu juu yake?  Si vizuri kutosheleza kwa maoni yetu pekee, lakini hata wewe mwenyewe jaribu kufumbua kitandawili hiki.