Kisa cha Msikiti wenye jina la ajabu
kupita yote Ulimwenguni
Kifuatacho ni kisa kilichoandikwa ndani ya kitabu kiitwacho
'Maajabu katika historia ya utawala
wa Al-Uthmania (Ottoman
empire)'.
Mwandishi wa kitabu
hicho Ustadh Arukhan Muhammad Ali ameandika yafuatayo:-
"Yupo kati yenu
aliyewahi kusikia juu ya msikiti
wenye jina la ajabu kama
hili? Jina la msikti ni
(Nishakula mimi).
Basi hili ni jina
la msikiti uliopo katika eneo la Fateh katika mji
wa Istanbul, na jina lake kwa lugha
ya Kituruki ni 'Sanikiy Yadam',
na maana yake (Nishakula mimi!), na sababu ya kupewa
jina hili la ajabu ni kisa
kizuri cha ajabu chenye ibra ndani
yake kwa mwenye kuzingatia."
Anaendelea kusema Ustadh Arukhan;
"Katika kijiji hiki alikuwa akiishi
mcha Mungu mmoja fakiri jina
lake Khayruddin Kajji Afandi. Na sahibu yetu huyu alikuwa kila
anapokwenda sokoni akatamani kununua tunda au nyama au haluwa, alikuwa akisema nafsini mwake; "Sanikiy Yadam', (Nishakula mimi!), kisha
hanunui tena tunda lile au nyama
ile au haluwa ile na badala
yake hurudi nyumbani na kuziingiza
pesa zenye thamani ya kununulia
vitu hivyo ndani ya kisanduku
chake na kuzidunduliza kidogo kidogo.
Na baada ya miaka
mingi kupita huku akijinyima vyakula vya anasa
visivyo vya lazima na
kula vyakula vya dharura tu,
pesa zile zikaongezeka akaweza kupata thamani ya kujenga msikiti
mdogo kijijini pake.
Na kwa vile watu
wa kijiji chake wanakijua kisa chake mcha
Mungu huyu fakiri na namna
alivyoweza kuujenga, wakaupa msikiti wake huo jina la; "Sanikiy Yadam', na maana yake;
(Nishakula mimi!)."
Ibra tunayopata katika kisa hiki;
Kiasi gani cha pesa tungeweza
kukusanya kwa
ajili ya masikini na wenye
kuhitaji misaada, na qasri ngapi
tugeweza kujijengea huko Peponi Inshaallah,
lau kama kila mmoja wetu
baada ya kwisha kula, ataweza kujinyima kununua kile kisicho
cha dharura, ambavyo ni vingi mno
na kutenga thamani ya vitu
hivyo kwa ajili ya kuwasaidia
ndugu zake?
Ndugu yangu Muislamu! Mtume wetu mtukufu
(Swalla Llahu alayhi wa
sallam) alikuwa mkarimu sana, na
katika mwezi huu mtukufu alikuwa
mkarimu kupita kiasi. Imepokelewa katika hadithi sahihi kuwa; 'Alikuwa
mkarimu kupita upepo uliopelekwa (kwa ajili ya
kueneza rehma na baraka kila
mahala).'
Jaribu kuifanyia kazi hadithi hii kwa kutenga kila siku kiasi
kidogo tu cha pesa baada ya
kuacha kununua baadhi tu ya
vile visivyo vya lazima, tena baada
ya kwisha kula, kisha kwa pesa hizo
uingize furaha ndani ya nyoyo
za ndugu zako wenye dhiki
na shida ambao ni wengi
sana! Na kwa
njia hii utaweza kujijengea qasri nyingi huko
Peponi – Inshaallah