NINI BAADA YA RAMADHANI?

 

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY

 

Ndugu zangu Waislam,

Assalaam aleikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tumekwishauaga, zile siku njema na nyakati za usiku zilizojaa baraka ndani yake tulokuwa tukiamka na kusoma Qurani na kujitahidi katika kufanya kila amali za kumridhisha Mola wetu, ndiyo zishatutoka.

Lile kumi la mwanzo la mwezi mtukufu wa Ramadhani, kumi la Rahmah, na kumi la pili la Maghfirah, na la tatu kumi la Kuepushwa na Moto, yoote hayo tumekwishayamaliza.

Tumekiaga chuo cha Subira na ucha Mungu. Tumejisubirisha kutokana na matamanio ya nafsi zetu mbali na ushawishi wa shetani. Misikiti ilijaa waumini, misahafu iligawiwa na kusomwa kwa wingi, maji, tende, na vyakula vya aina mbali mbali viligawiwa bure kwa nia ya kutaraji malipo mema kutoka kwa Mlipaji bila ya hesabu.

Bila shaka yoyote tumeuaga mwezi huu Mtukufu baada ya kufaidika nao kutokana na mafunzo yake mbali mbali pamoja na kufanya biashara na Mola wetu, biashara isiyododa.

Mwenyezi Mungu anasema;

Kwa yakini wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Sala, na katika yale Tuliyowapa wakatoa kwa siri na kwa dhahiri, hao wanatumai(faida ya) bishara isiyododa (isiyobwaga).

[Fatir - 29]

Bila shaka tunategemea thawabu nyingi sana kutoka kwa Mola wetu Mkarimu, kwa ajili ya kuupokea vizuri mwezi Wake Mkarimu.

Kwa ajili ya yote hayo inatupasa tumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa neema zake hizo na Ukarimu Wake huo.

Na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala akasema;

“Na pia mtimize hisabu hiyo, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongozeni ili mpate kumshukuru”.

[Al Baqarah - 185]

 

VIPI TUTAMSHUKURU MWENYEZI MUNGU?

Je! Tutamshukuru kwa kurudi kama tulivyokuwa kabla ya Mwezi wa Ramadhani au tutamuonyesha Mola wetu matunda mema ya neema zake alizotuneemesha nazo katika mwezi wake?

Maulamaa wanasema kuwa; Ukitaka kujuwa kiasi gani Ibada zako za Ramadhani zimekubaliwa, basi itizame hali yako ilivyokuwa baada ya kumalizika mwezi huu mtukufu, kisha uilinganishe na ilivyokuwa kabla yake. Ukiona kuwa imekuwa bora kuliko pale ilivyokuwa kabla ya kuanza mwezi wa Ramadhani, basi mshukuru Mola wako. Ama ukiona kinyume cha hivyo, basi usiilaumu isipokuwa nafsi yako.

 

IFICHE AKIBA YAKO KIBINDONI

Ikiwa umejitahidi kuzichuma thawabu zako ukaweza kujipatia akiba itakayotufaa siku ambayo hazitofaa ndani yake mali wala watoto, basi ifiche akiba hiyo kibindoni wala usianze kuwagawia watu na kuitupa huku na kule kisha ukaondoka patupu ukiwa umefilisika.

Mtume(Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliwauliza Masahaba wake  (Radhiya Llahu anhum):

“Mnamjuwa yupi aliyefilisika?”

Masahaba (Radhiya Llahu anhum) wakasema;

“Aliyefilisika tunayemjuwa sisi ni yule asiyekuwa na pesa wala kitu chochote”.

Mtume(Swalla Llahu alayhi wa sallam) akasema;

“Aliyefilisika katika umati wangu ni yule atakayekuja Siku ya Kiama akiwa na Sala zake, Funga zake, Zaka zake, anakuja (na vyote hivyo), akiwa amemtukana huyu, amemsingizia uwongo huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu, kisha zinachukuliwa thawabu zake na kupewa huyu na yule, na zikeshamalizika thawabu zake kabla ya kumaliza madeni ya watu, zinachukuliwa dhambi zao, na kutwishwa nazo yeye, kisha akaingizwa Motoni”

(Huyo ndiye aliyefilisika).

 

Ndugu zangu Waislam, Siku ya Kiama hakuna kitakachokufaa isipokuwa thawabu zako ulizojikusanyia hapa, na hakuna huko mahali pengine isipokuwa Peponi au Motoni. Basi zizuwie vizuri thawabu zako na usiwagawie watu na kuzipoteza bure kutokana na kuwasengenya watu, kuwatukana, kuzungumza juu ya mabaya yao, kuwadhulumu, nk.

Hassan al Basry  (Radhiya Llahu anhu), alipoambiwa kuwa pana mtu anayependa kumsema vibaya mbele ya watu, alimwambia mkewe apike chakula kizuri, kisha akampa chakula hicho mtumishi wake na kumtaka ampelekee mtu huyo anayemsema vibaya.

Alipoulizwa kwa nini umetenda hivyo, akajibu;

Mimi nina madhambi mengi, na mtu huyu kila anaponisema vibaya kwa watu, huwa ananipunguzia madhambi yangu. Kwa ajili hiyo, nikaona ni bora nimpe tunza nzuri ninayoweza kumpa”.

Maulamaa wanasema;

“Mfano wa mtu aliyehangaika kuchuma thawabu nyingi kisha akawagawia watu kutokana na kuwasengenya na kuwatukana na kuwadhulumu, ni mfano wa mtu aliyeshona nguo nzuri, kisha baada ya kuimaliza na kuipamba, akachukua mkasi na kuanza kuikata kata nguo hiyo”.

 

SALA

Ndugu zangu Waislam, kama tulivyokuwa tukiijaza misikiti katika mwezi wa Ramadhan, basi tuendelee hivyo hivyo katika miezi yote, kwani Mungu wa Ramadhani ni Yule Yule Mungu wa miezi iliyobaki. Na Mtume wenu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) hakupata kuacha kusali jamaa isipokuwa penye udhuru mkubwa kabisa usioweza kuepukwa. Hata wakati wa vita alikuwa akisali jamaa, wakati wa vita, vichwa vinakatwa katwa kwa mapanga, mikuki inazama ndani ya miili ya watu huku farasi wakipiga kelele na vumbi likitimka, yeye (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akiisimamisha Sala ya jamaa.

Huu ndio mwenendo wake, na anayekwenda kinyume na mwenendo wake, basi aipime tena imani yake.

Hebu tumsikilize Abdillahi bin Masaood (Radhiya Llahu anhu) akituelezea mambo yalivyokuwa wakati wa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam);

Abdillahi bin Masaood anasema;

Anayetaka kuonana na Mola wake kesho akiwa na furaha, basi azitunze Sala hizi kila zinaponadiwa (anapoadhini), kwani Mola wenu amemwekea Mtume wenu mwenendo wa uongofu, na hizi (Sala) ni katika mwenedo wa uongofu. Na kama nanyi pia mtasali majumbani mwenu kama anavyosali mtu huyu aliyechelewa (anavyosali) nyumbani kwake, mtakuwa mumeuacha mwenendo wa Mtume wenu, na mkiuacha mwenendo wa Mtume wenu, basi mtapotoka. Tulikuwa wakati wa Mtume(Swalla Llahu alayhi wa sallam), hakuna anayeacha kusali (jamaa) isipokuwa mnafiki anayejulikana (na kila mtu) kwa unafiki wake. Alikuwa mtu analetwa (msikitini akiwa anaumwa) akishikwa mikono na kuongozwa mpaka anasimamishwa katika safu

Muslim

Hadithi katika mlango huu ziko nyingi sana.

 

KUTOWA

Ndugu zangu Waislam, tuendelee kutowa kama tulivyokuwa tukitowa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwani mali tuliyokuwa nayo na uwezo tuliokuwa nao ni mtihani tuliopewa na Mola wetu, na Siku ya Kiama tutaulizwa juu ya kila senti, vipi tumeichuma na katika nini tumeitumia.

Mwenyezi Mungu anawajulisha na kuwasahihisha wale wanaodhania kuwa hiyo mali waliyopewa, walipewa kwa ajili kukirimiwa au kwa ajili ya ubora wao.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Lakini mwanadamu, Mola wake anapomfanyia MTIHANI Akamtukuza na kumneemesha, basi husema; “Mola wangu amenitukuza”

Na Anapomfanyia MTIHANI Akampunguzia riziki yake, husema; “Mola Wangu Amenidhalilisha”.

Sivyo hivyo (mnavyodhania)! Bali nyinyi (matajiri) hamuwatazami mayatima kwa jicho la huruma.

Wala hamujihimizi kulisha masikini

Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa

Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi.”

[Suratul Fajr – 15 – 20]

Na Mtume wetu(Swalla Llahu alayhi wa sallam) anasema;

"Kuna kingine unachofaidika nacho katika mali yako isipokuwa kile unachokula kikaoza, na  unachokivaa kikachakaa na unachotoa sadaka KIKABAKI?"

Masahaba (Radhiya Llahu anhum) wanasema;

“Mtume wetu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akitowa utowaji wa asiyeogopa kufilisika”.

 

FUNGA

Katika mafundisho ya mwezi wa Ramadhani, tumejifunza pia ustahamilivu wa Funga. Kama tulivyoweza kustahamili kuufunga mwezi mzima, basi tujaribu katika meizi isiyokuwa Ramadhani kustahamili kufunga angalau siku tatu katika kila mwezi. Na mtu akifunga siku tatu katika kila mwezi, basi thawabu zake ni sawa na yule aliyefunga mwaka mzima. Na hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu hulipa kwa kila jema moja mara kumi, kwa hivyo funga ya siku moja, mtu hulipwa kwa amali ya siku kumi, na amali ya siku tatu malipo yake huwa ya siku thelathini.

Ama ikiwa siku tatu kwa mwezi ni nzito, basi tujaribu kujizowesha kwa kufunga angalau siku moja kila mwezi, hii ni kwa kujizowesha tu.

Mtume(Swalla Llahu alayhi wa sallam) anasema;

Mtu anapofunga siku moja kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu humbaidishia moto umbali wa miaka sabini”.

Imesimuliwa na Maimamu wote wa hadithi isipokuwa Abu Daud.

 

QURANI

Mwenyezi Mungu anasema;

“Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa (kwa kuteremsha) kitabu chenye maneno yanayowafikiana, yanayokaririwa (bila kuchosha); husisimka kwayo ngozi za wale wanaomwogopa Mola wao. Kisha ngozi zao na nyoyo zao huwa laini kwa kumkumbuka Mola wao. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, kwa huo humwongoa amtakaye. Na anayeachiwa na Mwenyezi Mungu kuwa amepotea , basi hakuna wa kumuongoa.”

[Azzumar -23]

 

Maulamaa wanasema;

“Mtu anapotamani kuzungumza na Mola wake, basi ende kusali, (kwa sababu ndani ya Sala, yanapita mazungumzo baina ya mja na Mola wake), na mtu anapotamani Mola wake azungumze naye, basi aisome Qurani, kwani Qurani ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyowateremshia waja wake akitujulisha nini anachotutaka kutoka kwetu, na maamrisho na makatazo Yake Subhaanahu wa Taala juu yetu.

Qurani ni kiungo baina yetu na Mola wetu, Qurani ni katiba yetu Waislam na ndani yake mna pumzi ya Mola wetu Subhanahau wa Taala.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Na namna hivi tumekufunulia Wahyi kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini wala imani. Lakini tumefanya kitabu hiki (Qurani) ni nuru…”

[Ash Shuura – 52]

Na akasema;

“(Na hiki) Kitabu; tumekiteremsha kwako chenye baraka nyingi; ili wapate kuzifikiri Aya zake, na wenye akili wawaidhike”.

[Sad - 29]

Kwa hivyo tusiihame Qurani na kuiacha, tusije tukaingia katika wale watakaoshitakiwa na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kwa Mola wake, pale Mwenyezi Mungu aliposema;

“Na Mtume alikuwa akisema; “Ee, Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya Qurani hii kuwa kitu kilichoachwa (kilichohujuriwa)”.

[Al Furqan – 30]

Katika kuisherehesha aya hii anasema Ibni Kathir;

“Kutokuisoma Qurani na kushughulikia mengine ni katika kuihama. Kutokutafakari juu ya Aya zake ni katika kuihama.

Kutoifanyia kazi Qurani ni katika kuihama.

Kupenda kusikiliza nyimbo na maneno mengine yasiyokuwa na maana huku ukiisukuma upande Qurani, ni katika kuihama”.

Mtume(Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema;

“Isomeni Qurani, kwa sababu Siku ya Kiama itakuja kuwaombea shifaa wanaoisoma”.

Muslim

Na akasema;

“Mfano wa Mwislamu anayesoma Qurani ni mfano wa Balungi, harufu yake nzuri na ladha yake nzuri, na mfano wa Mwislamu asiyesoma Qurani ni mfano wa Tende, haina harufu yoyote lakini ladha yake nzuri, na mfano wa Mnafiki anayesoma Qurani, ni mfano wa mrehani, harufu yake nzuri lakini ladha yake chungu, na mfano wa Mnafiki asiyesoma Qurani, ni mfano wa Handhalah (tunda chungu sana lililofanana na tango), halina harufu yoyote, na ladha yake chungu”.

Bukhari na Muslim

Allah Allah ndugu zangu Qurani musiiweke nyuma, kwani atakayeiweka nyuma, basi itamsukumiza Motoni – Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na Moto wake.

Na atakayeiweka mbele Qurani, basi itamuongoza na kumuingiza katika Bustani za Al Rahmani.

 

Tunamuomba Mwenyezi Mungu azikubali amali zetu zote njema tulizotenda katika mwezi huu Mtukufu, atusamehe katika yale tuliyopunguza, na atujaalie tuufikie mwezi wa Ramadhani ujao na mingi mingine tukiwa katika hali iliyo bora kuliko hii, tukiwa sote tumerudi kwa Mola wetu kurudi kwa haki,  na Umma wetu urudishe heshima na utukufu wake. Aaamin

 

Wasslaam aleikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh