Assalaam Alaykum,

 

Ufuatao ni utenzi unaoeleza kisa cha mtume wa Mwenyezi Mungu, Seyyidna Ayyub ALAYHIS SALAAM. Utenzi huu umetungwa na:

Mwinyi Muhammad Abdulla Shatry wa Lamu.

 

 

                    UTENZI WA KISA CHA NABII AYYUB (A.S.)

 

    1.    Bismillahi Qadimu, Arrahmani Rahimu, Mwenye enzi ya kudumu, Muumba ndiwe Jalia

 

    2.    Uloumba ulimwengu, Arshi juu ya mbingu, Ukapanga na mafungu, Waja kuwamiminia

 

    3.    Aridhi ukatandika, Ziumbe ukawaweka, Hukuwa na mshirika, Ni kazi yako Moliwa

 

    4.    Ukanyesha na mivua, Ukalitowa na jua, Miti nayo ikamea, Ikanawiri dunia

 

    5.    Hakuna mtenda kazi, Ila ni wewe muyuzi, Mwenye mkubwa uyuzi, Ndiwe wa kutegemewa

 

    6.    Ukaumba majabali, Makubwa yaso mithali, Ndani yake muna mali, Na aridhi kuziwiya

 

    7.    Ukakusnaya milima, Ya mitanga ilokwima, Meupe ukiiona, Na raha kuyangalia

 

    8.    Yote ni kazi ya Mola, Asokula asolala, Na kwake huna muhula, Popote utarejea

 

    9.    Katengeza kwa udongo, Na tope zenye mavundo, Mwanadamu lake umbo, Quruani yatwambia

 

    10.    Ukayaweka mauti, Kwetu sisi ni sharuti, Huja pasi na wakati, Siku zikisikilia

 

    11.    Tahadhari mwanadamu, Yataka ujifahamu, Siku zikishakutimu, Budi huna nakwambia

 

    12.    Ewe mja usojali, Kumbuka huna mahali, Mauti hayako mbali, Popote hukungilia

 

    13.    Ghafula hukukabili, Mauti hayako mbali, Na jina likabadili, Wendo wakakulilia

 

    14.    Nakuomba ndugu yangu, Tafadhali nisikia, Roho si ya ulimwengu, Hakuna cha kubakia

 

    15.    Wawapi wanazuoni, Matajiri masikini, Na wenye nguvu wendani, Kama hawakuzaliwa

 

    16.    Wako wapi wenye nguvu, Akili na uwerevu, Hawakuwa watukivu, Leo wameshika ndia

 

    17.    Mamako alihajali, Mimba yako kahimili, Uzito kama jabali, Hakushindwa katukuwa

 

    18.    Kwa kite kaitukuwa, Henenda akijishuwa, Na mangi akiongowa, Kwa kazi yake Karima

 

    19.    Ukazawa mwanadama, Huna mbele wala nyuma, Kakuyeya wako mama, Kwa uwezo wa Karima

 

    20.    Ulimwengu si makazi, Kwa kila alomuyuzi, Ni mapito ya wemuzi, Ya kwenenda mui mwema

 

    21.    Baada haya kunena, Nina kiswa waungwana, Cha Ayubu tumwa mwema, Nimependa kukitowa

 

    22.    Nimependa kufasiri, Niwape zake khabari, Nimeona ni uzuri, Mupate kumuelewa

 

    23.    Babake alitajiri, Alina mali kathiri, Alihai kadhukuri, Mali nda mwane nabiya

 

    24.    Alipokufa babake, Kayashika mali yake, Ayyubu ndie pweke, Mali kaikusanyia

 

    25.    Alitajiri ajabu, Wa majumba na dhahabu, Na wana wenye adabu, Mola memruzukia,

 

    26.    Alikuwa na hekima, Za fahamu ya ilima, Na akili zilo tama, Yote kampa Jalia

 

    27.    Alikuwa mahabubu, Kwa watu na maswahibu, Akipendeza Ayubu, Kwa watu ni maridhia

 

    28.    Uli na nguvu muili, Na sura zake jamali, Na biashara amali, Ndio alokifanyia

 

    29.    Kamuoa mwana mwema, Rahama binti Fartima, Babu yake nitasema, Ndie Yusufu nabiya

 

    30.    Ayyubu alioa, Wake watatu sikia, Wawili wakakimbia, Rahama akabakia

 

    31.    Riwaya ilopokewa, Watoto walozaliwa, Ni kumi kuongezewa, na wanane kutimia

 

    32.    Kawaeya wake zake, Pamoja na wana wake, Hawakumuata pweke, Kwa raha na mazowea

 

    33.    Mkubwa mtoto wake, Kawalika ndugu zake, Harimala jina lake, Kwake akawatukua

 

    34.    Kawapikia chakula, Ndugu yao Harimala, Haukupita muhula, Balaa zikawangia

 

    35.    Balaa zikawafika, Kwa msiba ulotuka, Ya ukuta kuanguka, Wanawe wakajifia

 

    36.    Mali yakataharika, Mno akafilisika, Yali yakipuputuka, Kila siku kupungua

 

    37.    Ali na mengi majumba, bustani na mashamba, Na wanyama wa kutunga, Wote hawakubakia

 

    38.    Maradhi yalimshika, Siku nyingi na miaka, Hakuwa akipunguka. Ila kuzidi nabiya

 

    39.    Maradhi ya kiajabu, Yalompata Ayubu, Hakusaza matibabu, Na wanaojua dawa

 

    40.    Mabombwe yalikitoka, Na ngozi ikatanika, Mkewe akashutuka, Kamba unani nabiya

 

    41.    Muili hukushanuka, Na mabombwe hukutoka, Nawe umebadilika, Na wazidi kwendelea

 

    42.    Hata naona ajabu, Yalonipata muhibu, Ni kazi yake Wahabu, Ilahi yamueleya

 

    43.    Kamba wewe hufahama, Yalonipata Rahama, Mitihani ya Karima, Nami taisubiria

 

    44.    Maradhi ya miujiza, Ya ngozi yake kuoza, Wadudu wakitapuza, Muilini kwa nabiya

 

    45.    Hakuona la sahali, Ugonjwa kauhimili, Mkubwa ulo thaqili, Mola aloqadiria

 

    46.    Rahama kamuhimili, Kenda nae huko mbali, Nti yenye majabali, Kibanda kamjengea

 

    47.    Kenda nae taratibu, Kamueka kwa adabu, Hakusikia dharubu, Za mikukuto ya ndia

 

    48.    Kali chakula hakuna, Wala maji ya kunwa, Ndaa ilipowabana, Rahama hakungojea

 

    49.    Kateremka mjini, Rahama katumaini, Tapata mwema mwendani, Riziki kumpatia

 

    50.    Watu walipomuona, Kwa umoya wakanena, Ndoo kwetu wata bwana, Shere wakimtezea

 

    51.    Rahama hakukubali, Waloyasema rijali, Kaomba Mola Jalali, Amlinde na mabaya

 

    52.    Ayyubu akamwita, Kamba wewe huniata, Ni gani wenda tafuta, Nambiya nipate juwa

 

    53.    Kamba wewe mume wangu, Nakuapia kwa Mungu, Sitakutupa bwanangu, Wala sibadili nia

 

    54.    Kanena na moyo wake, Ni wapi mimi nifike, Kakumbuka mwanamke, Upesi akamwendea

 

    55.    Mlango akaubisha, Akataka kukopesha, Nikipata tarejesha, Kanena wangu nabiya

 

    56.    Mwanamke kwa umbeja, Kishipa kikampija, Akanena kwani ngoja, Lilokueta nambiya

 

    57.    Hukuya nyumbani kwangu, Ila kunipa matungu, Akuone mume wangu, Apate kukuridhia

 

    58.    Rahama akamjibu, Mwanamke kwa ghadhabu, Nina wangu Ayyubu, Nilopewa na Jaliya

 

    59.    Mimi sitokukiridhi, Kwani mimi meniudhi, Una kitu chenye hadhi, Ukitaka niatia

 

    60.    Ali na nyele safira, Rahama zalikin'gara, Mwanamke kwa hasira, Makasi kamuetea

 

    61.    Kazikata nyee zake, Akampa mwanamke, Kabeba mikate yake, Mumewe kampekea

 

    62.    Rahama akadhahabu, Akafika kwa Ayubu, Mumewe kataghadhabu, Maneno kimwelezea

 

    63.    Mumewe likamkera, Kutoa nyee safira, Zilikua nyee bora, Ni ndefu zikin'garia

 

    64.    Akamwapia Jalali, Mbee za wake rasuli, Si haramu ni halali, Chakula nilokwetea

 

    65.    Mla wewe mume wangu, Nimeuza nyee zangu, Nimekwapia kwa Mungu, Maovu kukutendea

 

    66.    Kanena tahakikisha, Na hadi taipitisha, Mboko mia takutwesha, Ninapopata afiya

 

    67.    Kiwa na afiya yangu, Tachunguza mke wangu, Ili nilipe matungu, Na kufuata sharia

 

    68.    Rahama akamjibu, Kwa sitaha na adabu, Kwamba uovu Ayubu, Siwezi kukufanyia

 

    69.    Rahama ayatamke, Amwambie mume wake, Amuombe Mola wake, Mateso kumwondolea

 

    70.    Kamwambia mke wangu, Naona haya kwa Mungu, Mestarehe na wanangu, Ashara wa thamania

 

    71.    Tasubiri Mola wangu, Na balaa za matungu, Maadamu moyo wangu, Na ulimi mebakia

 

    72.    Na ulimi nibakishe, Ilahi nikukumbuke, Dudu usimuoneshe, Ulimini kuningia

 

    73.    Walitoka kwa muili, Wadudu wote wawili, Tiati wamekabili, Ayyubu changaliya

 

    74.    Wa kwanza katumbukia, Mtoni akaingia, Mai yakamtukua, Ayyubu kionea

 

    75.    Wa pili kapanda bara, Kwenye jangwa la sahara, Akawa mnyama bora, Asali yake ni dawa

 

    76.    Hapohapo Jibrili, Kwa Ayubu kawasili, Yali mikono miwili, Kudhumani metukua

 

    77.    Metukua kudhumani, Metoka nayo peponi, Amepewa na Manani, Ayyubu kumwetea

 

    78.    Ayubu katakauli, Kamwambia Jibirili, Menikumbuka Jalali, Kunipa yangu afiya

 

    79.    Jibirili kamjibu, Menipa Mola Wahabu, Dawa yako kukutibu, Matunda ya jannatia

 

    80.    Akamwambia simama, Ayyubu tumwa mwema, Kwa amri ya Karima, Inshalla utatulia

 

    81.    Mimi nimetumwa kwako, Nipoze ugonjwa wako, Piga tini guu lako, La upande wa kulia

 

    82.    Yakatoka maji moto, Meupe yalo mazito, Akapowa tumwa wetu, Maradhi yakapungua

 

    83.    Kamwambia Jibirili, Upige nao wa pili, Wa kushoto sikuvuli, Maji yakaitokea

 

    84.    Mabaridi ya kutosha, Jibrili kamnwesha, Mola akamrejesha, Kama zamani nabiya

 

    85.    Maradhi yake kapona,  Tumwa akawa mzima, Akarudi kama zama, Kwa uwezo wa Jaliya

 

    86.    Ayyubu akanawiri, Kan'gara kama qamari, Ukarudi utajiri, Wake na watoto pia

 

    87.    Riwa nyengine hunena, Alibaki na Rahima, Kazaa wangine wana, Na mali yakarejea

 

    88.    Haya yaliyomsibu, Kumpata Ayyubu, Mitihani ya Wahabu, Nae kaisubiria

 

    89.    Mola anatufundisha, Kutaka kutuonesha, Maana ukiondeshwa, Sibabaike sikia

 

    90.    Uyatie akilini, Usubiri kwa Manani, Ndake Mola mitihani, Quruani yatwambia