ADABU ZA
MSALANI
[Na Adam. Yemen]
Muislamu anatakiwa afuate mafunzo ya dini
yake katika harakati zake zote,hata anapotaka kwenda haja basi atambue adabu na
mafunzo ya Uiislamu kisha afuate.
Nijambo la msingi kufahamu kuwa sehemu za
kufanya haja (choo) ni moja kati ya makaazi makuu ya Sheitani, hivyo muislamu anatakiwa
achukue kila tahadhari na kufuata miongozo ya Uislamu ili asidhurike na viumbe
hivi vibaya. Kuna adabu nyingi za kwenda haja, ambazo Uislamu umetufunza katika
hali tofauti,miongoni mwa hizo nikama zifuatazo :
1).Kuhakikisha kuwa upo mbali na watu
ikiwa unataka kufanya haja sehemu ya wazi, pia jiepushe na sehemu zifuatazo:
sehemu yenye kivuli wanachotumia watu kwa mapumziko.
Amesema mtume (s.a.w);
"Jiepusheni na laana tatu (nazo ni)
kufanya haja katika vianzio vya maji, njiani na kwenye kivuli.".
Pia chini ya mti wenye matunda, kwenye
maji kidogo yaliyotuama.
Amesema mtume(s.a.w);
"Asifanye mmoja wenu haja ndogo
katika maji yaliyotwama kisha akakoga ndani yake."
2) Wakati wa kuingia sehemu ya
haja.Unapotaka kuingia tanguliza mguu wa kushoto huku ukisema maneno haya;
"Allahumma inniy audhu bika minal
khubuthi wal khabaith."
Na maana yake ni; "Mola wangu,
najilinda kwako na shari ya majini wa kiume na majini wa kike."
3) Baada ya kuingia chooni. Kabla ya
kuanza kufanya haja ni vizuri kuhakikisha kuwa maji au mawe ya kujitoharisha
yapo kwani alikuwa Mtume (SAW) akiandaa maji katika chombo kabla yakufanya
haja. pia inakatazwa mtu kuzungumza au kuimba au hata kufanya zogo hadi kusikia
walio nje.
4) Wakati wa kufanya haja. Utaegemea mguu
wako wa kushoto wakati wa kufanya haja hali ya kuwa umechuchumaa kwani
inasaidia kutoka uchafu kwa wepesi, na kwa hali yoyote ile jiepushe na kufanya
haja ukiwa umesimama. Usiangalie utupu, wala kile kinachotoka, na asikichezee,
pia usiangalie mbinguni au kugeuka kulia na kushoto, usielekee kibla wala
usikipe mgongo ikiwa unakwenda haja sehemu ya wazi.
Amesema Mtume ( SA W);
"Anapotaka kufanya haja mmoja wenu
asielekee kibla wala asikipe mgongo."
Na wala usilielekee jua pale linapozama
au linapochomoza. Jihadhari na cheche za kile kinachotoka, kwani Mtume (SA W)
amesema;
"Ataadhibikiwa ndani ya kaburi yule
asiyejiepusha na cheche (za haja ndogo na kubwa)".
5) Baada ya kumaliza kufanya haja zako
unatakiwa uhakikishe kuwa hakuna kitu kinachobaki, hivyo unatakiwa ufanye kila
njia ili kuhakikisha kuwa uchafu umekwisha, kisha anza kujisafisha kwa kutumia
mawe masafi kisha malizia kwa maji, na inatosha kutumia maji matupu bila ya
mawe, na pindi ukikosa maji basi mawe yanatosha lakini kwa kutimiza shuruti
zake ambazo zimetajwa kwenye vitabu vya fiqhi, pia jiepushe kujisafisha kwa
kutumia mifupa au chakula kwani ni miongoni mwa kukufuru neema ya Mola wako,
jisafishe kwa kutumia mkono wako wa kushoto na kuanzia sehemu inayotoka haja
ndogo.
6) Baada ya kujitoharisha.Usikae kwa muda
mrefu pale ulipofanyia haja kwani inasababisha ugonjwa wa ini kama ilivyopokewa
kutoka kwa Lukman. Baada ya hapo vaa nguo zako kisha utawadhe kama udhu wa sala
7) Wakati wa kutoka. Unapotaka kutoka tanguliza mguu wako wa kulia huku unasema;
"Ghufraanaka - Ewe Mola nakuomba
unisamehe, namshukuru Allah aliyeniondoshea yanayoniudhi na kunibakishia
yanayoninufaisha"