
LAYLATUL QADR
Muhammad Faraj Salem Al Saiy
Hizi ni siku za kumi la mwisho la Mwezi mtukufu wa Ramadhani, siku ambazo ndani yake umo usiku mtukufu wa Laylatul Qadr.
Katika mwaka mzima hapana usiku mtukufu kuliko usiku huu wa Laylatul Qadr.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Hakika Tumeiteremsha (Qurani) katika Laylatul Qadr (usiku wenye
hishima kubwa) (usiku wa
mwezi wa Ramadhani).
Na jambo gani litakalokujulisha
(hata ukajua) ni nini huo usiku wa
Layaltul Qadr?
Huo usiku
wa hishima
ni bora kuliko
miezi elfu.
Huteremka Malaika na
roho (za viumbe watukufu) katika (usiku) huo kwa idhini
ya Mola wao
kwa kila jambo.
Ni amani (usiku) huo mpaka mapambazuko ya alfajiri."
[SURATUL QADR: 97]
Na maana yake sura hii ni kuwa mtu anapofanya amali njema kama vile kusali, kusoma Qurani kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndani ya usiku huo mmoja tu, basi thawabu zake ni sawa na kuzifanya amali hizo kwa muda wa miezi elfu.
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa linapoingia kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani akiwaamsha wake zake pamoja na wanawe kwa ajili ya kukithiri katika kufanya ibada hizo pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu aupate usiku huo.
NI USIKU UPI HUO?
Wapo maulamaa wanaosema kuwa Layaltul Qadr inakuwa katika usiku wa ishirini na moja, na wengine wanasema kuwa ni usiku wa ishirini na tatu na wengine ishirini na tano na wapo baadhi wanaosema kuwa unapatikana katika usiku wa ishirini na tisa, na wapo wengine wanaosema kuwa usiku huo unaweza kupatikana katika usiku wowote ule baina ya tarehe hizo.
Hata hivyo wengi miongoni mwa maulamaa wanasema kuwa Layaltul Qadr inapatikana katika usiku wa ishirini na saba, na hii inatokana na hadithi sahihi zikiwemo mbili zifuatazo;.
Ya kwanza iliyopokelewa na Imam Ahmed, kutoka kwa Ibni Umar (Radhiya Llahu anhu) kuwa alisema;
"Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema;
"Anayetaka kuutafuta (usiku huo wa Laylatul Qadr), basi na autafute katika usiku wa ishrini na saba".
Na hadithi iliyosimuliwa na Muslim na Imam Ahmed na Abu Daud na Attirmidhiy kuwa Ubay bin Kaab (Radhiya Llahu anhu) amesema;
"Wallahi naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye hapana mwengine isipokuwa Yeye, umo (usiku huo) ndani ya mwezi wa Ramadhani, wallahi naujua ni usiku gani huo. Huo ni usiku ambao ndani yake Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alituhimiza sana kusali. Huo ni usiku wa ishirini na saba, na dalili yake ni jua linatoka asubuhi yake jeupee bila miale".
KUSALI USIKU WAKE NA KUKITHIRI KATIKA KUOMBA DUA
Kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema;
"Atakayesali usiku wa Lailatul Qadr kwa imani huku akitaraji kutoka kwa Mola wake, anasamehewa madhambi yake yote yaliyopita".
[Bukhari na Muslim]
Imepokelewa kuwa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) alimuuliza Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam);
"Niwe nikisema nini nikiujuwa ni usiku upi huo?"
Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia;
"Sema;'Allahumma innaka afuwun tuhibbu l afuwa ffaafu anna".
[Ahmed - Ibni Majah – Attirmidhiy]