Kwa nini Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu)?

 

 

LOGO-Ysmall.jpg

Kwa nini Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu)?

 

Haider:          Katika mazungumzo yaliyopita ulitaka tuzungumze juu ya uadilifu wa Masahaba, ukasema kuwa watu hawa hawasemi uongo. Utasemaji nikikuuliza juu ya Sahaba ambaye zimepokelewa kutoka kwake hadithi nyingi kupita kiasi. Kupita hata uwezo wake?

Khalid:          Kama kwamba unataka tuzungumze juu ya hadithi za Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) zilizopokelewa kutoka kwa baadhi ya Masahaba (Radhiya Lllahu anhu)?

Haider:          Ndiyo, tuzungumze juu ya Masahaba wanaohusika na elimu ya hadithi.

Khalid:          Si bora tuzungumze juu ya aalim wa hadithi mashuhuri kupita wote katika Masahaba?

Haider:          Nani unayemkusudia ?

Khalid:          Namkusudia Abdul Rahman bin Sakhar al Dousiy, yule Sahaba aliyejitolea kuifanya kazi ya elimu hii ya hadithi.

Haider:          Mara ya mwanzo leo nalisikia jina hili.

Khalid:          Hulaumiki, kwa sababu Sahaba huyu anajulikana zaidi kwa umaarufu wake kuliko kwa jina lake. Nakusudia Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu).

Haider:          Nishamkumbuka! mwanachuoni wetu maarufu aitwae Hussein Sharafuddin Al Mousawiy alizungumza juu yake katika kitabu kizuri sana kiitwacho ‘Abu Hurairah’, na akabainisha ndani yake udhaifu wa riwaya zake mtu huyu.

Khalid:          Kabla sijasema lolote kuhusu kauli yako hii, ningependa kukuuliza suali moja. Umewahi kusoma chochote juu ya Sahaba huyu mtukufu (Radhiya Lllahu anhu) katika vitabu vya Masunni?

Haider:          Kusema kweli sijapata kusoma chochote, isipokuwa nimekwishasikia mengi sana juu yake mtu huyu kutoka kwa wanavyuoni wetu, na wote wanasema kuwa hadithi zilizopokelewa kutoka kwake zote si sahihi. Hata hivyo na tuzungumze juu yake, lakini kwa utulivu, na suali langu la mwanzo nataka kujua ; mtu huyu amesilimu mwaka gani?

Khalid:          Inajulikana kuwa Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) amesilimu mwaka wa saba baada ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuhajiri kwenda Madina na umri wake wakati ule ulikuwa miaka thelathini, na alikuwa akiishi al Suffah (mtaa ulioshikamana na nyumba ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) mahali walipokuwa wakiishi masikini na wacha Mungu, na alikuwa daima pamoja na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), hambanduki, kila anapokwenda alikuwa naye mpaka siku ile Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipofariki dunia.

Haider:           Lakini kinachostaabisha ni ule uwezo wake wa kuhifadhi hadithi hata akaweza kuhifadhi hadithi nyingi kuwapita Masahaba wote.

Khalid:          Hii inatokana na dua aliyoombewa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pale Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) alipomuendea Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kumshitakia udhaifu wake wa kuhifadhi, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia; ‘‘Itandaze nguo yako’’, na alipoitandaza (Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamuombea dua) kisha akamwambia; ‘Sasa jifunike nayo kifuani pako’, akajifunika na tokea siku hiyo hakusahau tena hadithi.

Haider:          Hadithi hii ngeni kwangu, je umewahi kuifanyia tahakiki ewe ndugu Khalid ?

Khalid:          Hadithi hii imesimuliwa na Bukhari na wengineo kwa hivyo ni sahihi Alhamdulillah, na hadithi hii haimo ndani ya vitabu vya maulamaa wa Kisunni peke yao, bali imo hata ndani ya vitabu vya hadithi vya Kishia.

Imeandikwa katika kitabu cha ‘Al Kharaij’ (1/75) na katika ‘Bihar al Anwar’ (18/913) mlango wa ‘Miujiza ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kukubaliwa kwa dua zake’ kuwa; Abu Hurairah alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam); ‘Mimi nasikia kutoka kwako hadithi nyingi kisha nazisahau’ Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia; ‘Tandaza guo lako lote’, akatandaza kisha Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akauweka mkono wake ndani yake kisha akamwambia; ‘Jifunike nalo’, ‘nikajifunika’ anasema Abu Hurairah; ‘na tokea siku hiyo sijasahau tena hadithi’.

Haider:          Lakini kinachoshangaza ni kuwa Abu Hurairah huyu amesimuliwa hadithi nyingi zisizoweza kulingana na muda wake mfupi tokea aliposilimu.

Khalid:          Kwa kuanzia ndugu Haider, ningependa kukuuliza iwapo unazijuwa idadi ya hadithi alizozisimuliwa Abu Hurairah?

Haider:          Maelfu kwa maelfu ya hadithi.

Khalid:          Jaribu kunipa idadi sahihi, kwani katika vitabu sita maarufu vya Masunni na katika Muwata-a cha Imam Malik hadithi za Abu Hurairah zilizopokelewa ndani yake idadi yake ni 2218 zilizokubaliwa na katika vitabu vya Sahih Bukhari na Sahih Muslim mna hadithi 609 tu za Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) na walizokubaliana juu yake Bukhari na Muslim ni 326, ziko wapi sasa hizo hadithi maelfu kwa maelfu?

Haider:          Si mimi ninayesema hivyo, haya ni maneno ninayowasikia maulamaa wetu wengi wanapozungumza juu ya mtu huyu.

Khalid:          Masahaba wengi na maulamaa wengi pia wamemsifia sana Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) na wameisifia elimu yake pia, mfano wa Abu Saeed al Khudary (Radhiya Lllahu anhu) aliposema;

                        ‘Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema kuwa ‘Abu Hurairah ni chombo cha elimu.’

                        Imam Shafi naye alisema; “Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) hodari wa kuhifadhi kupita wote wenye kuhifadhi hadithi katika wakati wake”.

                        Ama Imam Bukhari yeye amesema yafuatayo juu ya Abu Hurairah; “Maulamaa wapatao mia nane wamepokea hadithi kutoka kwake, na alikuwa hodari wa kuhifadhi kupita watu wote wa elimu ya hadithi wa zama zake.”

Haider:          Lakini anacholaumiwa Abu Hurairah ni kuwa hapana mtu yeyote duniani aliyewahi kusimulia hadithi nyingi kuliko yeye. Hapana mwanadamu yeyote anayeweza kuhifadhi hadithi nyingi kama hizo.

Khalid:          Kwanza kabisa uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi unatokana na baraka za ile dua aliyoombewa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

                        Pili Mtu aliyekiwishajitolea kutafuta elimu na kusikiliza hadithi za Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ataweza kweli kushindwa kukusanya idadi hiyo ya hadithi?

                        Tatu Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) alikuwa na wanafunzi wengi waliopokea kutoka kwake hadithi hizo.

                        Nne Hadithi alizozisimuliwa Abu Hurairah zimo ndani yake maneno ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na zingine ni juu ya matendo ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na nyingine ni juu ya matendo ya baadhi ya Masahaba yaliyokubaliwa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Tano Zipo hadithi ambazo Abu Hurairah amesimulia juu ya aliyoyasikia kutoka kwa Masahaba (Radhiya Lllahu anhu) yale ambayo Masahaba hao waliyasikia kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Sita zipo hadithi nyingi pia zisizosihi isnadi, yaani hadithi alosingiziwa tu Abu Hurairah kuwa amesimulia wakati yeye hakuzisimulia hadithi hizo.

Saba kupania kwake Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) kwa ajili ya kuifanya kazi hii tu. Yaani kuzikusanya hadithi za Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Nane Ulizungumza juu ya uwezo wake wa kuhifadhi hadithi ukasema kuwa hapana mwanadamu anayeweza kuhifadhi namna hiyo. Sasa mimi nitakuuliza suali; Uwezo upi unaoshangaza zaidi, ule wa Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) kuhifadhi hadithi elfu chache alizozisikia kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa muda wa miaka mitano au ule wa yule aliyehadithia maelfu kwa maelfu ya hadithi?

Haider:          Pengine unawakusudia Maimamu wetu!

Khalid:          Wala si katika Maimamu, bali hawa ni watu wa kawaida tu na hawaifikii hata chembe daraja ya Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu), na mmoja wao ni Aban Bin Taghalab ambaye Jaafar Al Sadeq amesema juu yake; “Hakika Aban Bin Taghalab amesimulia hadithi zangu 30,000, kwa hivyo na nyinyi zisimulieni”.

                        Na mwengine Muhammad bin Muslim bin Rabah, huyu amesema juu yake An Najashi katika kitabu chake kiitwacho Al Rijal ukurasa wa 163 kuwa; ‘Muhammad amepokea kutoka kwa Al Baqer hadithi 30,000 na amepokea kutoka kwa Al Sadiq hadithi 16,000.’

                        Na mwengine Jaber bin Yazid al Juafiy aliyesimulia hadithi nyingi sana za watu wa Nyumba ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ambaye Al Koshy katika tarjima yake uk.194 akimnukuu mtu huyu ameandika yafuatayo; “Nimehadithiwa hadithi 50,000 hajapata kuzisikia mwengine isipokuwa mimi”.

Na Al Hurr al Amiliy ameandika katika hitimisho la kitabu chake kiitwacho ‘Wasael’ (20/151) kutoka kwa Jabir yafuatayo; “Kuwa yeye amehadithiwa hadithi 70,000 kutoka kwa Al Baqer na amehadithia hadithi zipatazo140,000.

Sasa tukirudia suali lako; Je hadithi alizozisimulia Abu Hurairah zinaweza hata kukaribia idadi ya hadithi alosimulia mtu huyu? Kwa kukupa habari tu, Abul Hussein huyu ameandika kitabu kiitwacho ‘Al Muraja-at’ ambacho ndani yake amewasifia sana na kuwatetea watu hawa waliohadithia maelfu kwa maelfu ya hadithi, kwa nini basi asingefanya uadilifu angalau kidogo akamtetea na Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) pia?

Haider:          Lakini wapokeaji wa hadithi wa madhehebu ya Kishia Mwenyezi Mungu awarehemu wanajulikana kuwa ni watu wema na waadilifu na wanajulikana pia kwa uwezo wao mkubwa wa kuhifadhi. Tafadhali usizikanushe fadhila hizi ewe Khalid.

Khalid:          Ama kuhusu uwezo wa kuhifadhi, jambo hili halina haja hata kuzungumza juu yake, kwani hadithi zilizoandikwa ndani ya vitabu vyenu vya asili zinagongana na kupingana. Ama kuhusu wema wao lau kama ungesoma kidogo tu katika vitabu vya kishia mfano kitabu kiitwacho ‘Rijal al Koshy’, nk. ungeujuwa vizuri wema wao watu hawa waliohadithia hadithi kwa maelfu. Na  hapa nakunukulia riwaya iliyoandikwa katika kitabu hiki cha ‘Rijal al Koshy’ uk. 95 inayomzungumzia juu ya mmoja wa watu hao aitwae al Uqaili. Anasema Al Koshy: “Al Uqaili alikuwa miongoni mwa masahaba wa Amiri l Muuminin, na alikuwa mlevi wa kutupwa lakini alikuwa akihadithia hadithi kama alivyokuwa akizipokea.”

                        Na Abu Hamza al Thamali Thabit bin Dinar naye pia alikuwa mlevi kama ilivyoandikwa katika kitabu hicho cha Al Koshy uk. wa 76.

                        Ali bin Hamza al Batainiy alikuwa akiiba pesa za Al Maasum na khums wanazolipa maimamu wa kishia, na hata amefikia kulaaniwa na kuambiwa kuwa ni muongo. Yote haya yanapatikana katika kitabu kiitwacho ‘Al Waqifiyah dirasah tahaliyliyah (1/418)’. Na wengi wengineo. Kwa hivyo katika vitabu vya Mashia si muhimu kwao uadilifu wa msimuliaji wa hadithi, inatosha tu msimuliaji huo awe ni mtu anayewapenda Ahli l Bayt basi hadithi zake zitakubalika na si muhimu hata kama atakuwa muongo au mlevi au mwizi au awe fasiqi namna gani.

Haider:          Juu ya yote uliyosema ewe ndugu Khalid, lakini hizi riwaya za Abu Hurairah hazikubaliwi na maulamaa wetu na hii ndiyo sababu huwezi kuziona ndani ya vitabu vyetu.riwaya za mtu huyu.

Khalid:          Ndugu Haider naona bora nimalize mazungumzo haya mazuri baina yetu kwa kukujulisha kuwa Mashia waliotangulia walikuwa wakiziandika na kuzifanyia kazi hadithi za Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu), na pia maneno yake na fatwa zake zote hizo zilikuwa zikiandikwa na maulamaa wengi wa mwanzo wa Kishia na walikuwa wakizifanyia kazi pia na utazikuta kwa mfano katika kitabu cha Mirza Hussein Nuri al Tubrusi katika kitabu chake kiitwacho Mustadrak al Wasael. Ndani ya kitabu hicho ameandika hadithi nyingi za Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) katika mlango wa ‘Al Ijarah’ (14/28), bali Sheikh al Mufiyd pia ameandika hadithi nyingi za Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) katika kitabu chake kiitwacho Al Amaliy na utazikuta katika ukurasa 111-112-113.

                        Na Sheikh Al Saduq naye pia katika kitabu cha ‘Maaniy al akhbar’ ukurasa wa 80-90 ameandika hadithi zake, na pia katika kitabu ‘Ikmal al din’, ukurasa wa 136, na katika kitabu cha Al Khiswal wa thawab al aamal pia na katika vitabu vingi vinginevyo. Kwa nini basi unakanusha tu kabla ya hata kuangalia kwanza ndani ya vitabu? Daima mimi husema kuwa tatizo la vijana wa Kishia wenye kupenda kheri huwa hawapendi kusoma vile vitabu vya asili vya Kishia na pia hawaulizi dalili kutoka kwa mashekhe wao, bali wao wanasema tu kila wanachoambiwa na wale mashekhe wanaopenda kuzungumza bila dalili.

Haider:          Unataka kuniambia kuwa yote wanayosema wanavyuoni wetu juu ya mtu huyu si ya kweli?

Khalid:          Ndiyo ewe ndugu Haider, kwani maulamaa wote wa Ahlu Sunnah wamekubaliana juu ya ukweli wa riwaya zake Sahaba huyu mtukufu (Radhiya Lllahu anhu), na pia maulamaa wa Kishia waliotangulia nao pia wamezikubali riwaya zake, na kama utasoma vitabu vyenu vilivyoandikwa na maulamaa wa zamani basi hutamuona yeyote kati ya maulamaa wenu mwenye kumchukia au mwenye kuzikataa riwaya zake isipokuwa mtu mjinga ambaye Mwenyezi Mungu hakumfungua kifua chake apate kunufaika na elimu iliyo sahihi. Na lau kama utamuuliza yeyote anayemtukana au anayejaribu kumuondolea hadhi yake Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) ‘Kwa nini unamchukia Sahaba huyu namna hii? Umesoma nini juu sira ya Sahaba huyu? Ameukosea nini Uislamu? Hutoweza kupata jawabu yoyote itakayokukinaisha, kwani tuhuma zote hizo zinatokana na ujinga wa watu wachache wasiosoma chochote katika vitabu vya Kisunni wala vya Kishia.

Haider:          Lakini anayezitoa makosa hadithi za Abu Hurairah hufanya hivyo kwa ajili ya kuitakia kheri elimu hii ya hadithi isije ikaingia ndani yake hadithi zisizo sahihi.

Khalid:          Wanaojaribu kumtia ila Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) kusudi lao hasa ni moja tu; nalo ni kuitia ila Sunnah iliyotahirika ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Na kwa vile hawakupata njia nyingine ya kuitia ila, wakaona bora wawatie ila waliotunukulia Sunnah hiyo, na kwa vile Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) ndiye mashuhuri kupita wote na ndiye aliyesimulia riwaya nyingi zaidi kupita wote ndiyo sababu wakawa wanajaribu kumtia ila.

                        Ijulikane kuwa watu kama Abu Hurairah (Radhiya Lllahu anhu) na walio mfano wake katika Masahaba watukufu (Radhiya Lllahu anhu), Mwenyezi Mungu ndiye aliyewajaalia kuifanya kazi hii ya kutufikishia Sunnah hii tukufu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Sunnah ambayo ndani yake yamo mafundisho na sheria anayoipenda Mwenyezi Mungu na kuridhika nayo. Na sisi tunawapenda kwa ajili hiyo na kwa ajili ya mengi mema waliyo nayo.