UZAZI WA MPANGILIO NA KUZUWIA UZAZI

Sheria ya Kiislamu inatilia nguvu kuongezeka kwa vizazi na inahesabu kuongezeka huko kuwa ni neema itokayo kwa Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu watoto wa na wajukuu."

An Nahl – 72

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Oweni wenye kupendeza, wenye kuzaa, kwa sababu mimi nitajifaharisha kupitia kwenu (kwa kuwa na watu wengi) kupita uma zote."

Ahmed na Abu Daud na Annasai

Ipo tofauti baina ya 'uzazi wa mpangilio' na 'kuzuwia uzazi'.

Uzazi wa mpango ni halali iwapo utatumika kwa njia za kisheria, ama kuzuwia uzazi ni haramu isipokuwa kwa udhuru unaokubalika.

Inapohitajika kuzaa kwa mpangilio kutokana tabu anayopata mzazi anayezaa mfululizo, inaruhusiwa kutumia njia walizokuwa wakitumia Masahaba (RA) kama vile kuyatupa nje maji ya uzazi, na pia inajuzu kutumia dawa zisizoleta madhara.

Imepokelewa katika Bukhari na Muslim kutoka kwa Jabir (RA) kuwa amesema;

"Tulikuwa tukimwagia nje (maji ya uzazi) wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na qurani ilikuwa ikiteremka."

Akimaanisha kuwa ingelikuwa ni haramu, basi ingeteremshwa aya ya kukataza au kuharamisha kufanya hivyo.

Na inajuzu pia kutumia njia nyingine kama vile kumeza vidonge au kuiginza loop nk. ikiwa zitatumiwa kisheria tena kwa ajili ya kupangilia tu na si kwa ajili ya kuzuwia, na fatwa zilizotolewa na maulamaa wengi zinaruhusu kuzuwia kwa muda wa kiasi cha miaka mitatu. (kupumzika miaka mitatu baada ya kila uzazi).

Ama kuzuwia uzazi moja kwa moja kwa kisingizio cha kuogopa umasikini au kutoweza kulea vizuri, hiyo ni haramu.

Ifuatayo ni Fatwa iliyotolewa na kamati ya kudumu ya maulamaa katika mkutano wake wa nane wa kamati ya maulamaa wakubwa uliofanyika katika mwezi wa Shaaban mwaka 1396H;

"Shukrani ni za Mwenyezi Mungu peke Yake, na sala na salamu zimfikia yule ambaye hapana Mtume baada yake.

Kwa vile sheria ya Kiislamu inatilia nguvu kuongezeka kwa vizazi, kwa hivyo tunaona kuwa vizazi ni neema kubwa katika neema za Mwenyezi Mungu alizowapa waja wake, na dalili nyingi zilizomo ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu na ndani ya mafunzo ya Mtume wake (SAW) zimepitiwa na kamati ya kudumu. Na kwa vile kuzuwia uzazi kunapingana na maumbile ya kibinadamu ambayo Mwenyezi Mungu amewaumba kwayo, na kwa vile ni kinyume cha sheria ya Kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu amewaridhia nayo waja wake, na kwa vile wanaolingania watu katika kuzuwia uzazi lengo lao kubwa ni kupunguza idadi na kuudhoofisha umma wa Kiislamu ili wawe na uwezo wa kuzitawala nchi zao na kuwatawala watu wake.

Na kwa vile kuyakubali hayo ni katika matendo ya wakati wa ujahilia, na katika kuwa na dhanna mbaya juu ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, na katika kuudhoofisha uhuru wa Waislamu. Kwa ajili ya yote hayo, kamati imeamua kuwa haijuzu kabisa kufunga uzazi wala kuzuwia uzazi ikiwa kusudi lake ni kuogopa umasikini, kwa sababu Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kutoa riziki na Ndiye Mwenye nguvu.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na hakuna nyama yoyote (yaani kiumbe chochote) katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Mwenyezi Mungu."

Surat Hud – 6

Ama ikiwa kuzuwia huko ni kwa dharura isiyoepukika kama vile mwanamke hawezi kuzaa isipokuwa kwa njia ya opreshen (operation), au kuchelewesha uzazi kwa ajili ya sababu maalum (zenye kukubalika kisheria)walizoziona wazazi, hapo hapana ubaya kuzuwia au kuchelewesha uzazi, na hii inatokana na hadithi mbali mbali zilizopokelewa kutoka kwa Masahaba (RA) kuwa walikuwa wakiyatupa nje maji ya uzazi, na kama walivyoeleza maulamaa mbali mbali katika kuruhusu kutumia dawa za kuzuwia uzazi au kuitowa mimba kabla ya kutimia siku arubaini, bali kuzuwia uzazi wakati mwingine huwa lazima inapothibiti kuwa mzazi atadhurika."

Wallahu taala aalam