KUVAA CHUMA AU SHABA KUNABATILISHA SALA:?

Suali
Assalaam Aleykum Warahmatullah,

Kuuliza si ujinga na njia mojawapo ya kupata kujua.

Ni hadith gani ya Mtume inayokataza kuvaa chuma au shaba kwenye swala
? Je impeokewa na nani hadith hiyo ? Tunaomba kujua kwani tunaona
masheikh wengi wanaswali wamevaa saa.


Jawabu
Kutoka kwa Abu Obeida kutoka kwa Jabir bin Zaid kutoka kwa Ibn
Abass kasema, amekataza Mtume wa Mwenyezi Mungu kusali na "Al Anuk

wa Shabah",Na Al Anuk tafsiri yake ni madini ya tin, na Shabah
tafsiri yake ni shaba nyekundu. Na madini yaliyobakia yameingizwa
hapa kwa njia ya kiasi (analogy), Na kiasi ni msingi katika misingi
ya sharia.
Hadith kaipokea Al Imam Rabii al jameh al sahih hadithi namba 294.

Juma Al Mazrui

----------------------------------------------------------------------------

 Majibu:

Sheikh, wa'alaykum salaam warahmatullah,

Suala la kukatazwa kuvaa saa katika Swala halijasemwa wazi pahala popote kwa upekuzi wangu.

Inavyoonyesha kuwa makatazo hayo yametukia kwa kufasiriwa na kufahamika maana ya pamoja ya maelezo yanayosemekana kuwa ni ya hadithi ambayo imesimuliwa na Rabii Ibn Habiib, katika wasimulizi wanaotegemewa na Maibadhi, kuwa Mtume (rahma na amani za Allah zimwelee yeye) alikataza kuswali na madini ya risasi (au chuma) na shaba.  Kama alivyofasiri Rabii katika kitabu chake. Na katika kufafanua hayo mmoja wa Masheikh wa Kiibadhi As Ssalimy akasema kukatazwa huko ni kwa sababu hayo ni mavazi ya watu wa motoni. Akiegemeza maelezo yake hayo kutokana na hadithi kuwa mtu alimwendea Mtume rahma na amani za Allah ziwe naye. akiwa amevaa pete ya shaba, Mtume akamwambia kuwa anasikia harufu ya Masanamu kutoka kwake, yule mt! u akaitupa pete ile. Na mara nyingine akavaa pete ya dhahabu na Mtume rahma na amani za Allah ziwe naye akamwambia kuwa naona kwako pambo la watu wa motoni, yule mtu kusikia hivyo akaitupa vilevile…

Inaonyesha kutokana na haya maelezo yanayohusiana na Mtume rahma na amani za Allah ziwe naye ambayo yametajwa  hapo juu, ndipo baadhi ya wanachuoni wa Kiibadhi wakapatia hoja ya kukatazika kuvaa saa au kitu chenye madini katika swala. Na wakasema baadhi yao kuwa ni haramu na wengine kuwa ni makruhu.

Hata hivyo, hadithi hiyo imedhoofishwa na baadhi ya wanachuoni katika kitabu cha Fat-hul Baari, sasa tuangalie je, saa kukatazwa kwake kuvaliwa katika Swala ni nini mantiki yake? Inavyoelekea waliokataza ni kwa sababu kuna aina ya chuma katika saa, na chuma imekatazwa kwa mujibu wa hadithi hiyo iliyotajwa huko juu.

Sasa kitu cha kuzingatia ni kuwa chuma kwa sababu ni katika vitu au mapambo ya motoni, ndiyo maana ikakatazwa kwa mtu kutumia katika Swala. Lakini je, hiyo chuma yenyewe ni kitu najisi? Na je, hukumu ya kidunia inalingana na hukumu za akhera? Tutazame maelezo yafuatayo;

Ingawa chuma imetajwa kuwa ni katika mambo ya motoni, kwa mujibu wa hadithi juu, lakini tunaona katika sehemu tofauti katika Qur’an Mwenyeezi Mungu anatuonyesha manufaa ya matumizi ya vyuma hapa duniani. Mifano ni kama aya zifuatazo:nataja baadhi tu;

1   1-    {{ (Tukamwambia Daud) “Tengeneza (nguo za chuma) pana, na upime vizuri katika kuunganisha; na fanyeni vitendo vizuri; bila shaka Nayaona (yote) mnayoyatenda}} Suratu Saba’, 11

2   2-    {{ Na Tukamfundisha (Daud) matengenezo ya mavazi kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika mapigano yenu. Je, mtakuwa katika wanaoshukuru?}} Suratul Anbiyaa, 80

3   3-    {{ Kwa hakika Tuliwapeleka Mitume Wetu kwa dalili waziwazi na Tukaviteremsha Vitabu na uadilifu pamoja nao, ili watu wasimamie uadilifu. Na Tumekiteremsha (Tumekiumba) chuma, chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu; na ili Mwenyeezi Mungu ajulishe anayemnusuru na Mitume wake, na hali ya kuwa hawamuoni Mwenyeezi Mungu. Kwa yakini Mwenyeezi Mungu  ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.}} Suratul Hadiyd, 25

Shahidi hizo ni kuthibitisha kuwa hizo ni hukmu za kidunia ambazo Mwenyeezi Mungu katoa ruhsa na kuelekeza kuwa mna manufaa katika vyuma kwa wanaadam.

Suala laja kuhusu unajisi au ubaya wa chuma katika Swala. Iko wazi kuwa chuma na shaba si vitu najisi na haviwezi kuharibu Swala ya mtu, na kuhusu vitu vilivyokatazwa na Mtume rahma na amani za Allah katika Swala vimetajwa waziwazi na sababu zake ziko wazi kuhusiana na ibada hiyo. Mfano makatazo ya kuswali kwenye kaburi; Hekima ni makatazo ya kufanya ibada katika sehemu isiyo safi au kwa kutaka msaada kwa asiye Mwenyeezi Mungu.  Na makatazo ya kuswali katika nyakati zilizokatazwa kama wakati wa kuchomoza jua na kushuka maana pamoja na makatazo hayo, pia baadhi ya riwaya zinasema hu! enda zikafananisha ibada zetu na ibada za wale waliokuwa wakiabudu vingine asiye Allah. Au makatazo ya kuswali na hali umebanwa na haja ndogo/kubwa; kwani hali hiyo itashughulisha moyo wa mtu katika Swala yake na kumuondolea utulivu kwenye Swala. Vilevile makatazo ya kuswali sehemu zenye vinyago, picha n.k. kwani kutaondosha  kumakinika kwa mtu kwenye Swala yake.

Kisha baada ya kuona makatazo hayo yaliyotajwa katika hadithi mbalimbali, tunapata uchambuzi ufuatao ambao tunaugawa katika mafungu yafuatayo:

  1-    Kutoshughulika au kushughulishwa na kitu katika swala.

  2-    Kutoswali sehemu yenye uchafu/najisi.

  3-    Kutoswali katika maeneo ambayo hupelekea ile swala kuwa ni kwa ajili ya kuomba au kutaka msaada kingine kisicho Mwenyeezi Mungu.

Kutokana na hayo tuliyotaja, tunaona kwamba hiyo hadithi ya makatazo ya kuswali na chuma au shaba:

  a-    Haiwezi kuchukuliwa kuwa vitu hivyo ni mapambo watu wa motoni moja kwa moja.

  b-    Haiwezi kuchukuliwa kuwa chuma au shaba ni vitu vilivyo najisi au uchafu na kutoweza kutumika wakati wa Swala.

3   c-    Haiyumkiniki kuwa kuvaa chenye chuma au shaba kwenye Swala au penginepo kutasababisha kumpelekea mtu kuhisi awe anaabudu asiye Allah.

   d-    Haiwezi kusemwa hapa kuwa makatazo hayo yaliyotajwa ni ya kiibada katu (ambayo hayahitaji rai wala muono) kwani kwa ujumla wa maelezo yaliyokuja ni yale yenye kupimika kiakili na kuweza kuyalinganisha na shahidi zingine. Ama hayo masuala ya kiabada katu yasiyohitaji uchambuzi wala kupimwa kiakili ni kama masuala ya kutayamamu, kuoga janaba au idadi ya rakaa za swala na mfano wa hivyo ambavyo vimekuja katika maandiko yaliyothibiti tena kwa mitiririko mingi tofauti na maelezo kama hayo tuliyoyaona yenye kukataza kuvaa chuma au shaba ambayo yamekuja katika simulizi moja lisilo na mitiririko mingi na lisilowafikiana na maandiko sahihi yaliyothibiti kwenye Kitabu na Sunnah.!

Ama inavyoonesha katika mtazamo unaostahiki wa kisheria na makusudio sahihi yaliyomo katika  makatazo  katika hadithi hiyo ambayo kama ni sahihi, huenda yakawa kwa makusudio ya kumkataza mtu kutopatikana mishughuliko katika Swala.

Na hivyo, hukumu kama hiyo ya kukataza mtu kuvaa saa katika Swala, hakutolazimu hali ya aina moja kwa watu wote, kuna wanaovaa na haiwashughulishi hata chembe wala hata kuihisi chochote, na kuna watakaohisi na ikawashulisha kiasi, na kuna wanaovaa na ikawashughulisha sana kwa kuitizama; ima kujua wakati au kuistaajabia uzuri au vilivyomo ndani yake.

Na kutokana na hali hizo basi, na hukumu pia hutofautiana baina ya hali za hao wavaaji, kuna itakayokuwa kuvaa kwao ni sawa hakuna ubaya, kuna ambao itakuwa ni makruhu na kuna itakayokuwa haifai. Na kila mmoja anaijua nafsi yake zaidi.

Pia kwa nini ikatazwe saa tu kwa sababu inadaiwa ina chuma, na isikatazwe mikanda ya suruali ambayo ina chuma tena kikubwa kuliko cha saa? Na nguo ngapi zenye vifungo vya chuma na havijapewa  hukumu kama hiyo ya saa? Na kama suala hapa ni uharamu wa chuma, basi tumeona katika aya mbalimbali kuwa hakupatikani uharamu huo. Ama ikiwa ni kwa sababu ya kumshughulisha mvaaji katika Swala, basi ijulikane si chuma tu au saa bali ni kitu chochote kile kinachomshughulisha mtu katika Swala yake na kumuondoshea utulivu na mawazo yake, moja kwa moja kitakuwa hakifai na bora kiepukwe.

WA ALLAHU A’ALAM