KUTHIBITISHA MWEZI WA RAMADHAN NA TAREHE NYENGINE ZA KIISLAMU

 

Qur'an wa Sunnah Society
Imefasiriwa Na Abufarida Muhammad A. Basawad

 

 

Al-hamdu lillah. Sifa zote njema na shukrani ni zenye kumthubutukia Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu. Tunamuhimidi na kumshukuru Yeye na kumtaka msaada na msamaha. Kwake Yeye tunajilinda na ushawishi wa nafsi zetu na makosa yetu. Yeyote ambae alieongozwa na Mwenyezi Mungu (kwa Rehma Zake hawezi kupotolewa na yeyote. Na aliepotolewa na Mwenyezi Mungu (kwa Hikma Zake) hawezi kuongozwa na yeyote.

Nashuhudia yakwamba hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki illa Allah, peke yake, Asokuwa na mshirika na Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni mtume Wake.

MWEZI KONGO (CRESCENT) HUTHIBITISHA TAREHE ZA KIISLAMU:

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametubainishia ya kwamba kuandama kwa mwezi ndio njia ya pekee ya kuthibiti kwa tarehe na matukio ya kiislamu kama vile 'Idd na Hija. Na akasema

Wanakuuliza juu ya miezi.
Sema: "Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili (ya mambo) ya watu (mengine) na ya Hija (zao)." [Al-Baqarah (2):189]

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ametilia mkazo sana jambo la kuuona mwezi kongo, haswa katika kutambua mwanzo na mwisho wa mwezi wa Ramadhani. Imepokewa kutoka kwa idadi kubwa ya maswahaba (Radhiya Llahu anhum) kuwa mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Fungeni (waislamu) mukiuona mwezi kongo. Ukifichikana, basi kamilisheni siku thalathini katika hisabu ya Sha'baan. Na mufungue muuonapo mwezi kongo. Ukifichikana, basi kamilisheni siku thalathini."[1]

Alikuwa mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akishughulika zaidi katika kuhakikisha kuandama kwa mwezi wa Sha'baan, kwa sababu ifikapo siku ya ishirini na tisa huutafuta mwezi wa Ramadhani au hukamilisha siku thalathini kabla ya kuanza kufunga. Ikapokewa kutoka kwa 'Aisha (Radhiya Llahu anhaa):

"Alikuwa mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akishughulika sana kuhusu (kujuwa mwanzo wa) Sha'baan kuliko miezi mingine. Kisha alikuwa akifunga baada ya kuonekana (mwezi kongo wa) Ramadhani. Ukifichikana (mwezi) basi yeye huhesabu siku thalathini (za Sha'baan) kisha baadae akafunga."[2]

MASHAHIDI WANAOHITAJIKA:

Wanavyuoni wa kiislamu wamekubaliana ya kuwa mashahidi wawili wa kiislamu wanatosheleza ushahidi wao kuhusu kuandama kwa mwezi. Ushahidi wao umetokamana na riwaya kutoka kwa baadhi ya maswahaba (Radhiya Llahu anhum) ya kwamba, amesema mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

"Waislamu wawili waadilifu wakiapa (wameuona mwezi) basi fungeni au fungueni saumu zenu."[3]

Wakakubaliana wanavyuoni wengi zaidi kuwa ushuhuda wa Muislamu mmoja utatosheleza kuhusu kuandama kwa mwezi. Dalili yao ni kwamba Ibn 'Umar (Radhiya Llahu anhu) amesema:

"Watu walikuwa, wakiutafuta mwezi kongo (wa Ramadhani). Mimi nikampasha habari mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) yakuwa nimeuona mwezi. Kwa hivyo akafunga (siku iliyofuata) na akawaamrisha watu wafunge."[4]

USHAHIDI WA UTAALAMU WA NYOTA:

Hupatikana miongoni mwa watu ambao wanapendekeza kuhisabu masiku kulingana na ilimu ya nyota katika kuukadiria mwezi kongo. Hilo si jambo geni kwani lilizushwa jambo kama hilo katika nyakati za mwanzoni mwa uislamu na mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akalipinga. Ikapokewa kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Llahu anhu), mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Sisi ni taifa lisilojuwa kusoma wala kuandika. Hatutumii maandishi wala hesabu za ilimu ya utaalamu wa nyota (katika kufunga). Mwezi ni kadha na kadha (akaashiria kwa mikono yake mara tatu, akakunja kidole cha gumba mara ya tatu, kumaanisha siku ishirini na tisa) au ni kadha na kadha na kadha (akaashiria kwa mikono yake mara tatu, kumaanisha siku thalathini)."[5]

Riwaya ya Abu-Dawud, ikaendelea zaidi: "Kwa hivyo Ibn 'Umar alikuwa akimaliza kufunga na watu pamoja bila ya kuzitegemea hisabu za wataalamu wa nyota."

Hii inaonyesha vipi mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alitaka kuifanya ibada hii iwe rahisi na pia iwe katika daraja ya watu wa kawaida. Ikaepushwa ibada kama hii na ilimu maalumu za ki-sayansi (iwapo ni za kweli au za shaka). Kwa sababu hii, ndipo akasema Ibn Taymiyyah (rahimahullah):

"Hali ya taifa hili ya kutojuwa kusoma na kuandika ni sifa, kwani lajitosheleza na kila matatizo katika utekelezaji wa misingi ya ibada."

Basi yoyote atakaepinga jambo hilo, huyo atakuwa amekwenda kinyume na 'ijma ya wanavyuoni wanaothaminika; atakuwa yuwajaribu kuchafua pambo na mipangilio ya dini hii, na hatari zaidi atakuwa ni mwenye kumuasi mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

 

KUTOELEWEKA I: UHAKIKA WA MWANZO WA MWEZI

Jambo la kawaida lisiloeleweka na lenye umuhimu kwa watu wengi ni iwapo hatufanyi jitihada katika kukubali ushuhuda wa wale waliodai kuuona mwezi (kwa ushahidi wa wataalamu wa nyota na njia nyenginezo) basi huenda tukahatarisha kuzibatilisha baadhi ya ibada zetu kwa kufunga katika siku zisizostahiki. Mwenendo kama huu umekataliwa katika uislamu juu ya matukio mengi:

a. Jambo hili lahusiana na kutia shaka kuhusu ukweli (ushuhuda) wa waislamu waadilifu (udul). Tumekatazwa kutokamana na (Nas ya) Qur'an na Sunnah.

b. Jambo hilo ni kwenda kinyume na mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ambae aliekubali ushuhuda wa watu bila ya kukawiya na vile vile bila ya kuulinganisha ushuhuda huo na ushahidi wa utaalamu wa ilimu ya nyota.

c. Jambo hilo linafanana na tabia ya mayahudi ambao waliojikalifisha na sharia juu ya nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa kuzifanya hizo sheria ngumu zaidi. Akasema mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

"Jihadharini na (kuvuka mipaka) kuongeza mambo kwenye dini; kwa hakika waliokuwa kabla yenu waliangamizwa kwa kuongeza mambo katika dini."[6]

d. Jambo hilo laonyesha ujinga wa kutojua ni lini mwezi wa kiislamu huanza. Nukta hii, imeelezwa na Ibn Taymiyyah (rahimahullah):

"Watu wengi wanadhania ya kuwa mwezi mpya ukijitokeza mawinguni basi huo ndio usiku wa kwanza wa mwezi, bila ya kujali iwapo watu wameuona mwezi au la. Hayo ni makosa. Ni sharti mwezi huo ujitokeze kwa watu na watu wauone ili kuuanza mwezi. Ndio sababu ya mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema: '(Uhakika wa) Saumu huanza ile siku muanzapo kufunga.'[7] Ikamaanisha ya kwamba: hii ndio siku ambayo munayoitambua kama ndiwo wakati wa kufunga n.k. kwahivyo ikiwa nyinyi hamukuitambua siku hiyo basi hamutofaidika nayo."[8]

Rai hii imetiliwa mkazo na riwaya ifuatayo akasema Abu Al-Bakhturi, "Tulikwenda kufanya umra na tukaushuhudia (kuuona) mwezi kongo wa Ramadhani, tulipokuwa mahali paitwapo Dhatu 'Irq, ingawa mwezi wenyewe ulikuwa ni wa siku mbili au tatu. Kisha baadae tulipomuona Ibn 'Abbas (Radhiya Llahu anhu) tukamueleza kuhusu jambo hilo nae Ibn Abbas (Radhiya Llahu anhu) akatuambia, "amesema mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): Mwenyezi Mungu amelifanya jambo la kuutazama mwezi kongo liwe ni alama ya Ramadhani. Kwa hivyo Ramadhani huanzia ule usiku muuonapo. Iwapo umefichamana nanyi basi kamilisheni hisabu."[9]

Jee, ikiwa wanaodai yakuwa wameuona mwezi walisema uwongo au walipitikiwa? Maadam uislamu wao ni wenye kudhihirika na ni waaminifu basi ni sharti kukubali ushuhuda wao na kuanza kufunga (au kufungua). Hatuna haki yoyote kukataa bila ya kuwa na ushahidi ulio wazi (unaoafikiana na sunnah kama ilivyoelezwa mbeleni). Iwapo walikuwa kweli wamekusudia kusema uwongo basi wao watastahiki madhambi peke yao, nasi tutakuwa (Insha-Allah) ni wenye kulipwa kheri zetu kwa kushikamana na sunnah.

MUUNGANO WA MIPAKA: (MATLA')

Kutokamana na hadithi zilizopita, inampasa kila muislamu afuate amri kuhusu kuonekana kwa mwezi. Kwa kulikariri jambo hilo, ikapokewa kutoka kwa Abu Huraira, 'Aisha na wengineo (Radhiya Llahu anhum), mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"(Uhakika wa) Saum huanza ile siku muanzapo kufunga; (Uhakika wa) Fitr ('Idd) huwa ni ile siku mumalizapo kufunga; (Uhakika wa) Adh-ha ('Idd) huwa ni ile siku munapochinja."[10]

Kwa hivyo uonekanapo mwezi popote ulimwenguni na angalau muislamu mmoja muaminifu, hii yamaanisha ya kwamba umma mzima umeuona. Kutokamana na hayo, kama hadithi iliyopita inavyotuashiria juu ya kila muislamu kuwajibika kuupokea mwezi huo mpya, maadamu habari zitamfikia na wakati utamruhusu kuyatekeleza yanayompasa.

KUTOELEWEKA II: MATLA' TAFAUTI

Idadi kubwa ya watu wameipotoa riwaya ifuatayo ya Kurayb. Akatuhadithia Kurayb yakwamba Umm ul-Fadhl Bint ul-Harith alimtuma kwenda kwa Mu'awiyah (Radhiya Llahu anhu) huko Damascus. Baada ya kuutekeleza utumishi huo akiweko Sham, mwezi wa Ramadhani ukaandama usiku wa Ijumaa jioni nae kurayb akauona. Kisha akarudi Madina na akawasili katika siku za mwisho mwisho wa mwezi. Akaonana na Ibn 'Abbas ambae akamuuliza ni lini mwezi wa Ramadhani ulipoandama huko Ash-Sham. Kurayb akasema "Tumeuona usiku wa Ijumaa" Ibn 'Abbas akamuuliza "Je wewe mwenyewe uliuona?" akajibu Kurayb, "Ndio, nimeuona pamoja na watu wengine, na kwa ajili hiyo watu wakafunga pamoja na Mu'awiyah." Hapo tena Ibn 'Abbas akasema, "Lakini sisi tumeuona usiku wa Ijumamosi, kwa hivyo sisi tutaendelea kufunga mpaka tukamilishe siku thalathini au tuuone (mwezi kongo wa shawwal)." Kurayb akamuuliza, "Kwani wewe hukubali kuuona na kufunga kwa Ma'awiya?" Akajibu Ibn 'Abbas: "Laa! Hivi ndivyo tulivyoamrishwa na mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)."[11]

Baada ya majadiliano kuhusu riwaya hii, Shaykh-ul-Islam Ibn Taymiyyah (Rahimahullah) akamalizia:

"Kwa ufupi, yoyote itakaemfikia habari ya kuonekana kwa mwezi na akapata wasaa wa kufunga au kumaliza kufunga au kuchinja basi hana budi atekeleze. Ushahidi kamili na riwaya nyingi kutoka kwa Ma-Salaf unaunga mkono kikamilifu mas-ala hayo. Kuweka vipimo vya masafa au miji ni kukhalifu malengo na shar' (sheria ya uislamu)."[12]

Imam Ash-Shawkani (rahimahullah) akaigusia hii riwaya kutoka kwa Kurayb na akataja maoni mbali mbali ya wanavyuoni walivyozungumza. Kisha akaeleza kama ifuatavyo:

"Inakupasa kujua ya kwamba ushahidi unaokubalika ni kama alivyosema Ibn 'Abbas (Radhiya Llahu anhu) waziwazi kutoka kwa mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Na sio katika ijtihadi yake, kama wanavyofasiri baadhi ya watu, wakati aliposema, 'Hivi ndivyo tulivyoamrishwa na mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).' Maelezo yake aliyoyapokea kutoka kwa mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni yale yaliyonukuliwa na Al-Bukhari, Muslim na wengineo, walivyopokea ya kwamba:

'Musifunge mpaka muuone mwezi na musimalize saumu zenu mpaka muuone...'

Hii haihusiani na sehemu maalum bali hayo ni maelezo kwa waislamu wote kwa ujumla. Kwa hivyo huo ni ushahidi wa wazi ya kuwa kuonekana kwa mwezi katika sehemu moja kunawahusu watu wa sehemu yoyote nyingine. Sababu ni kwamba watu (waislamu) katika sehemu fulani wakiuona, hiyo yamaanisha kuwa waislamu wote wameuona; linalowahusu wao (waliouona) vile vile litawahusu wengine (katika sehemu nyingine.) Licha ya hayo, mji wa Ash-Sham haukuwa mbali mno kutoka Madina hata ipatikane matla' tafauti. Ibn 'Abbas alikataa kuwafuata waliouona. Hii yamaanisha tabia yake imetokamana na ijtihadi yake na kwa hivyo hauwezekani huo kuwa ni ushahidi (makhsusi)."[13]

Siddiq Hassan Khan (rahimaullah)[14] akasema:
"Mwezi kongo utakaposhuhudiwa na watu katika kitongoji chochote, basi itawapasa watu wote wakubaliane kuhusu kuonekana kwa mwezi huo. Ushahidi unatokamana na hadithi zinazoeleza kuhusu kuanza na kumaliza kufunga kwa kuuona mwezi kongo. Hadithi hizi zawaeleza Umma mzima wa waislamu: Muislamu yoyote akiushuhudia mwezi popote, ushuhuda wake utakuwa ni ushuhuda wa waislamu wote. Itakuwa ni makosa kwenda kinyume na hivi kwa kuitumia hadithi ya Kurayb (sahih Muslim) kwa sababu Ibn 'Abbas kwenye hadithi hiyo hakukatazwa na mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kufuata utazamaji wa sehemu nyingine za mji."[15]

Kuhusu mas-ala haya, akaeleza mwanachuoni wa karne hii, Muhammad Nasir Ud-Din Al-Albaani, (Rahimahullah):

"Matla' zinahusiana wala hazina mipaka maalum ambayo watu waweza kuyatafautisha ili wazitegemee... wanavyuoni wengi hawakuyapa uzito mas-ala hayo ya tafauti za matla'. Ushahidi ukapatikana kutokamana na hadithi iliyosahih, 'Fungeni kwa kuuona na fungueni kwa kuuona.'

Huu ndio ukweli uliothubutu, wala mtu asiupinge ukweli huu kwa kuitumia hadithi ya Ibn 'Abbas, huwenda ikawa ni bora kusema yakwamba hadithi ya Ibn 'Abbas inawahusu waliofunga kwa kuuona mwezi kwenye sehemu yao na baadae wakati wa Ramadhani wakajuwa ya kwamba mwezi kongo ulionekana mahali pengine siku moja kabla. Katika hali hiyo, watu hao wataendelea kufunga na wenzao kwenye sehemu yao mpaka wakamilishe siku thalathini au wauone mwezi wao. Jambo hilo litaondoa kutatizika na hadithi ifahamike kwa watu wote watakaofikiwa na habari za kuandama kwa mwezi kutoka sehemu yoyote. Ni wazi ya kwamba mas-ala haya ni rahisi kuyatekeleza siku hizi."[16]

 

KWA MUKHTASAR:

Ufuatao ni mukhtasar wa maelezo yaliopita:
a. Kuanza kwa mwezi wa ki-islamu hutegemea (kwa min-ajil ya kufunga, Hija na matukio mengine ya ki-islamu). Kuuona mwezi kongo kwa macho makavu.

b. Ushahidi wa utaalamu wa elimu ya nyota haufai kutumiwa katika kuthibitisha, kuhakikisha na wala kumkanusha muislamu muaminifu alieuona mwezi.

c. Pindi mwezi kongo uonekanapo popote ulimwenguni itawapasa watu wengine wote kufunga, maadamu habari zitawafikia ndani ya muda ambao watakuwa wepesi wa utekelezaji. Watu wasiowajibika kutekeleza amri hiyo ni waislamu wanaoishi chini ya mamlaka ya serikali inayokanusha (kwa masikitiko), kwa sababu mbalimbali, kufuata kuonekana kwa mwezi kutoka nchi nyengine.

d. Mwanzo wa mwezi ni kuonekana kwa mwezi kongo, bila ya kujali iwapo mwezi huo uliandama kabla, baada ama ndio umejitokeza wakati huo. Kwa hayo tunamuomba Allah (s.w.t.) atuongoze na atuwezeshe kuifuata Sunnah wakati wowote na mwito wetu wa mwisho uwe ni: AL-HAMDU LILLAHI RABBIL 'ALAMIN.




Nukta Ya Maelezo:

[1] Bukhari,Muslim na wengineo; imepokewa na Abu Hurayrah, 'Aisha, 'Adiyy Bin Hatim, Hudhayfah, Ibn 'Abbas, Ibn 'Umar, Jabir Bin 'Abdillah na maswahaba wengine.
[2] Abu Dawud, Ahmad na wengineo; imepewa hukmu ya usahihi na al-Haakim, Adh-Dhahabi na Al-Albaani.
[3] Ahmad, an-Nasa'i na ad-Daaraqut'ni; imehukumiwa usahihi wake na al-Albaani.
[4] Abu Dawud na wengineo; imehukumiwa kuwa sahih na adh-Dhahabi, Ibn Hajar na al-Albaani.
[5] Bukhari, Muslim, Abu Dawud na an-Nasa'i.
[6] An-Nasa'i, Ahmad na wengineo, imesahihishwa na Ibn Taymiyyah na wengineo.
[7] Abu Dawud, at-Tirmidhi na wengineo, imehukumiwa kuwa sahih na al-Albaani na wengineo.
[8] Al-Fatawi 5:203.
[9] Muslim na wengineo.
[10] Abu Dawud, at-Tirmidhi na wengineo, imehukumiwa kuwa sahih na al-Albaani na wengineo.
[11] Muslim.
[12] Al-Fatawi 5:111.
[13] Nayl ul-Awtar, 4:268.
[14] Akiwa ni miongoni mwa wanavyuoni wakubwa aliewhi kuishi katika bara hindi.
[15] Ar-Rawdhat un-Nadiyyah, 1:224.
[16] Tamam ul-Minnah, uk 398.