HUKUMU YA KUFUGA MBWA

 

Na Shamim Khamis

Dini ya kiislam imeweka misingi maalumu kwa kila jambo na kuliwekea jambo hilo vidhibiti na mipaka, kwani kila kitu kitakuwa na faida zake na madhara yake iwapo hakikuchungiwa sheria na desturi zake.

Katika ufugaji wa mbwa nako pia kumewekwa sheria zake na taratibu maalumu. Jambo hili la ufugaji mbwa hivi sasa limeenea sana katika jamii za kiislam kwa kuwaiga watu wa magharibi na wale wasiokuwa waislam katika tabia zao mbaya na ulazima wa kuwa na mbwa ndani ya nyumba au familia.

Kwa hakika watu hao hugharamika sana kwa kuwatunza mbwa wao hata kuwanyima wanaadamu wenziwao, kiasi ambacho mbwa amepewa sehemu maalumu ya huduma na matumizi pamoja na heshima yake na nafasi yake katika familia.

Dini ya kiislam kupitia kwa Mtume wake Muhammad (SAW), kufuga mbwa majumbani bila ya haja yoyote na vile vile kuwepo mbwa katika nyumba za waislam bila ya haja ni kupelekea kunajisika vyombo na vitu vyengine kama vile viti, makochi, meza na hata nguo kwa sababu ya miguso ya mbwa na kuramba kwake sehemu hizo, kwani mbwa mara nyingi ana tabia ya kuramba ramba na kujiegemeza na vitu kama hivyo vilivyomo majumbani.

Wakati mwengine hufika kuramba sahani na vyombo vya matumizi ya jikoni na hapo husambaza najisi na virusi vyengine vibaya sana na hatari sana kwa afya za binaadamu.

Lengo la hadithi hii ni kubaianisha ubaya wa najisi ya mbwa na hatari zake, kwani najisi nyingi huondolewa mara moja tu kwa maji, baada ya kuhakikisha imeondoka. Lakini, najisi hii ya mbwa kwa ukali wake huondolewa mara saba kwa maji ikiwemo mara moja kwa mchanga.

Wamesema baadhi ya maulamaa kuhusu hekima ya kuzuia ufugaji mbwa bila ya haja, ni kwamba mbwa huwakera wageni wanaotembelea majumbani kwa kuwabwekea ovyo ovyo na kuwatisha wenye kuuliza na kuomba msaada majumbani pamoja na kuwakera na kuwaudhi wapita njia.

Muislam duniani anatakiwa asiwakere na kuwaudhi watu wala kusababisha maudhi kwa wenzake kwa kero na chagizo za mbwa wake. Mbali na kero hilo na maudhi hayo yanayosababishwa na ufugaji mbwa kiholela, pia kuna madhara mengine makubwa yanayotokana na jambo hilo ikiwemo kutokuingia Malaika wa Rehma katika nyumba inayofugwa mbwa.

Ushahidi wa hayo ni kauli ya Mtume (SAW) aliposema: "Alinijia Jibril (AS) akaniambia nilikuja kwako jana na hakukuwa na kitu kilichonizuia kuingia nyumbani mwako ila kulikuwa na mbwa ndani…..". Hadithi inaonesha kuwa Malaika Jibril hakuingia nyumbani kwa Mtume (SAW) kwa sababu ya kuwepo mbwa ndani yake, hapo Mtume (SAW) akaamrisha atolewe yule mbwa.

Katazo la kufuga mbwa majumbani bila ya haja yoyote haina maana ya ruhusa ya kuwatesa mbwa na kuwapiga na kuwaua, bali mbwa wamestahiki kuangaliwa kama wanyama wengine, kwani wao ni viumbe kama walivyo viumbe wengine wote, Mtume (SAW) amesema: "Lau kama mbwa si viumbe kama viumbe wengine, basi ningeamrisha wauliwe".

Mtume (SAW) anatueleza katika hadithi ya mtu aliyempa msaada mbwa na kumuondoshea kiu iliyomshika sana hata kukurubia kufa. Mwenyezi Mungu akamshukuru mtu huyo na kumghufiria madhambi yake. Hii ni kuonesha jinsi uislam unavyojali wanyama wakiwemo mbwa pamoja na viumbe hai vyengine. Mtume (SAW) amesema;

‘Asie na huruma harehemewi – Mrehemu aliye ardhini atakurehemu aliye mbinguni’.

Uislam umejenga nidhamu ya kuwatendea wema viumbe hai bila ya kujali hali zao na kufanya hivyo ni sawa na kutoa sadaka. Mtume (SAW) amesema: "Na katika kila moyo wa kiumbe hai ni sadaka".

Inafaa tuelewe kwamba pamoja na kuwa uislam haupendelei watu kufuga mbwa na kufuga kiholela, lakini pia umeruhusu watu kufuga mbwa kwa malengo maalum na kwa dharura khasa. Kwa hivyo mbwa wanaofugwa kwa haja maalum, kama vile mbwa wa kuwinda au wa kulindia mazao au wa kufugia wanyama au wa haja nyengine yoyote ile, basi hao wametolewa katika katazo la kutofugwa.

Mbwa hawa walioruhusiwa kufugwa ni lazima wawe wameelimishwa na kufunzwa vizuri sana, kiasi ambacho wataweza kupokea amri na kuitekeleza ipasavyo na vile vile ni lazima kwa muislam anaefuga mbwa wa namna hiyo, achunge sana najis na uchafu unaotokana na mbwa. Hivyo asiwaruhusu kuingia nyumbani na kuharibu vyombo.

Tabia ya kuweka maduka maalum ya kuuza na kununua mbwa haifai katika jamii ya kiislam, kwani jambo hilo litapelekea biashara hiyo ihalalike na kugeuka kuwa ni kitega uchumi na hasa ukiangalia kuwa baadhi ya Maulamaa wa kiislam wamesema kuwa mbwa yeye mwenyewe ni najis, kwa hivyo hatofaa kuuzwa kwa hali yoyote ile, kwani najis haiuzwi.

Ingawa wako Maulamaa wengine wanaoruhusu biashara ya mbwa wa kulindia na kufugia, lakini biashara ya mbwa haiko katika sura hiyo, bali ni mtindo tu wa mazoea ya kuiga watu wa magharibi juu ya kuwa na mbwa majumbani mwao.

Waislam tunatakiwa daima tuwe tunaangalia jambo lenye mas-lahi kwetu kidunia na kidini. Tukiangalia suala la kufuga mbwa kiholela tutakuta ni kupoteza wakati bure na kuharibu mali zetu kwa kuwashughulikia mbwa pamoja na kuwahudumikia. Kwa hivyo, suala hili halifai katika jamii ya kiislam.