HUKUMU
ZA MSIKITI
Sameer kutoka Yemen
Shukurani njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu aliyeujaalia Msikiti kuwa
ni nyumba tukufu hapa ulimwenguni,na sala na amani
zimfikie Mtume wetu Muhammad pamoja na jamaa zake na masahaba zake na kila
mwenye kushikamana na misikiti.
Ninachukuwa fursa hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kujaribu kuelezea
hukumu za Msikiti ambazo tunahitajika waislam kuzifahamu ,na hii inatokana kuwa
nafasi ya Msikiti kwetu ni kubwa mno tofauti na wanavyofahamu baadhi ya watu
kuwa Msikiti ni kama sehemu ya kukusanyika waislam kwa ajili ya kutekeleza
ibada ya sala tu.
Msikiti ni kituo kamili cha kuwakusanya waislam katika kufanikisha mambo
yao yote ya kilimwengu na tukiangalia historia ya Uislam tutakuta kuwa
Msikiti, Mtume (S.A.W) ulikuwa ni
makutano ya waislam kila penye haja ya kufanya hivyo,bali ilifikia hadi Msikiti
kuwa ni sehemu pia ya kupanga na kupangua namna ya kukabiliana na Makafiri
wakati wa vita .
Hivyo kutokana na umuhimu huo tumeonelea ni busara kuziangalia hukumu
zinazoambatana na misikiti ili tuweze kufaidika na nyumba hii tukufu ,na tuweze kujiepusha na makatazo kwayo.
Maana
ya msikiti
Maana ya Msikiti kilugha ni kila sehemu inayosujudiwa, ama katika sheria
Msikiti ni sehemu yoyote ya ardhi iliyokusudiwa na mwenyewe kwa ajili ya kuwa
Msikiti (kusaliwa)pamoja na kuiweka wakfu sehemu hiyo,
yaani ili sehemu ya ardhi iitwe Msikiti na kuchukuwa hukumu za Msikiti basi ni
lazima mmiliki wa ardhi hiyo atamke kuwa sehemu hiyo ni wakfu kwa ajili ya
msikti na lengo ni kuweza kuutumia kila muumini kwa kusali na kuweza kusaliwa
sala za Jamaa.
Hii ndio maana ambayo huzungumzwa katika
vitabu vyetu, pia kuna hali nyengine ambazo ardhi huwa ni
Msikiti lakini.
Zimekuja hadithi za Mtume zinazotufahamisha kuwa kila sehemu ya ardhi
inafaa kuwa Msikiti, imepokelewa na sahaba Jabir (RA)
kuwa, amesema Mtume (S.A.W) " Imejaaliwa sehemu ya ardhi ni Msikiti kwangu
(na kwa umma wangu), na kuwa ni
Yaani sehemu yoyote katika ardhi basi inaweza ikawa ni Msikiti bali
muislam akiwa safirini na akataka kusali ,basi anaweza
akasali popote pale, muhimu pawe ni pasafi kutokana na najisi, ama katika
baadhi ya umma zilizotangulia wao walikuwa hawawezi kutekeleza ibada zao
isipokuwa wakiwepo katika sehemu maalumu, pia imejaaliwa sehemu yote ya ardhi
kuwa ni safi kwa anayetaka kutayammam akiwa amekosa maji ya kutawadha.
Hadithi hii ina mafunzo mengi ,na moja kati ya
hayo ni kuwa Muislam hatakiwi kuacha sala kwa hali yoyote ile, wala hana
kisingizio kwa kusema hana maji ya kujitoharisha au hawezi kusali mpaka afike
Msikitini ,hata hivyo nafasi ya Msikiti itabakia kuwepo na ni bora kwa
anayeweza kufika Msikitini akafanya ibada zake humo kuliko kusali popote tu, na
bila ya shaka atakayekuwa na ufahamu huu wa kukataa kwenda Msikitini basi
amekwenda kombo wala hajafahamu hasa lengo la Mtume (S.A.W).
Msikiti
wa mwanzo kujengwa duniani.
Msikiti wa mwanzo kujengwa duniani ni Msikiti wa Makka (Al-Qaba) kama
alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qura-an "Hakika Msikiti wa kwanza kuwekwa
kwa watu (duniani ) ni Msikiti wa Makka " (Al-Imran 3: 96)
Na imepokewa hadithi kutoka kwa sahaba Abi Dharri radhi za Mwenyezi
Mungu ziwe juu yake amesema: "Nilimuuliza Mtume (S.A.W) ni Msikiti gani wa
mwanzo uliojengwa duniani ? ,akanijibu ni Msikiti wa Makka, nikamuuliza kisha
upi ,akasema kisha ukajengwa Msikiti wa Aksa (uliopo Palestina )…."Hadithi
imepokewa na Imam Bukhari na Muslim.
Kutokana na mapokezi hayo inatubainikia kuwa Msikiti wa Makka (Al-Qaba tukufu)
ndio Msikiti wa mwanzo kujengwa duniani, na aliyeujenga Msikiti huo ni Nabii
Ibrahim rehema na amani juu yake, kisha ukajengwa Msikiti wa Al-Aqsa na mjukuu wake Nabii Yaakub bin Is-hak bin
Ibrahim, ama Nabii Suleiman yeye hakuujenga kwa maana ya kuasisi bali yeye aliufanyia matengenezo upya.
Fadhila
za kujenga Msikiti
Kwa kuwa Msikiti ni nyumba ya Mwenyezi Mungu,
na kutokana na utukufu wake kwa waumini basi kuna fadhila kubwa kwa mwenye
kujenga msikiti. Kuna mapokezi mengi yamepokewa kutoka kwa
Mtume S.A.W kuelezea fadhila za mwenye kujenga Msikiti, na muhimu kati ya
hadithi hizo ni ile iliyopokewa kutoka kwa sahaba Syd Uthman bin Affan (RA) (khalifa
wa Tatu wa Mtume (S.A.W). Imepokewa kuwa wakati Sahaba Uthman alipotaka
kuutanua Msikiti wa Mtume (S.A.W) baadhi ya watu walikataa kuungana nae juu ya
fikra hii na kutaka
Msikiti wa Mtume uwachwe
Na imepokewa kutoka kwa sahaba Uthman tena kuwa amemsikia Mtume (S.A.W)
akisema "Mwenye kujenga Msikiti, MwenyeziMungu atamjengea mtu huyo nyumba
peponi mfano wake ( Msikiti alioujenga )". (Muslim).
Kutokana na hadithi hizi
inatosha kufahamu umuhimu wa kujenga Msikiti kwani kila mmoja wetu anahitaji
kuingia peponi ,na kila mmoja anajitahidi kufanya ibada ili aweze kuingia humo
,lakini kwa yule anayejenga Msikiti basi tayari ameshahadiwa kuwa atajengewa
nyumba yake peponi ,hivyo ni ishara tosha kuwa mtu huyo ataingia peponi.
Na wanavyuoni katika kufasiri hadithi hii ya pili pale Mtume (S.A.W) aliposema :atajengewa nyumba mfano wake, maana yake ni
kwamba atajengewa nyumba peponi ambayo utukufu wake humo peponi utakuwa ni sawa
na utukufu wa Msikiti huku duniani, na kama tulivyotanguliza kusema kuwa
Msikiti ni nyumba tukufu duniani kuliko nyumba nyengine yoyote ile na hili
halina shaka, na wako waliosema kuwa atajengewa kutokana na thawabu zake za
kujenga Msikiti jengo kubwa tukufu la kifakhari humo peponi.
Pia Mtume (SAW) hakuwahimza watu
wajenge misikiti tu, bali yeye ndiye wa mwanzo
kuonyesha mfano katika suala hili, na haya tunayapata pale Mtume (S.A.W)
alipowasili Madina kwa mara ya kwanza kutoka Makka (Hijra), na alipofika tu
jambo la kwanza aliamrisha ujengwe Msikiti, nae akawa ni mmoja kati ya hao
wajenzi alikuwa akibeba matofali
Lakini tunaona kutokana na maneno ya Mtume (S.A.W) kuwa ni lazima kwa anayetaka
fadhila hizi basi awe amekusudia kujenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ,sio anajenga ili watu waseme, au wamuone ni mtu mwema,
na hili suala la kufanya amali njema kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndio msingi wa
kukubaliwa amali zetu ,hivyo kila mmoja ajitahidi anapowafikishwa na Mola wake
kufanya jambo jema basi atakase nia yake.
Pia tunatakiwa tuimarishe misikiti kwa ibada mbali mbali, kwani Mtume
S.A.W amesema kuwa "Watu wa aina saba watapata kivuli siku ya kiama siku
isiyokuwa na kivuli isipokuwa hicho, na mmoja kati ya hao saba ni mtu ambaye
moyo wake umeshikamana na misikiti”, yaani anautukuza Msikiti na kufanya ibada
kwa wingi zikiwemo sala, itikafu na mengineyo kama kusoma Qur -an.
Na amesema Mtume (S.A.W) kutufahamisha utukufu wa Msikiti kuwa
"Sehemu iliyobora mbele ya Mwenyezi Mungu ni misikiti
,na sehemu zinazomchukiza Mwenyezi Mungu ni Masoko" (Muslim).
Misikiti
iliyobora zaidi
Baada ya kufahamu nafasi na utukufu wa misikiti hapa duniani na kwamba
ni nyumba tukufu kuliko nyumba nyengine ,pia hiyo misikiti imetofautiana kwa
utukufu ,kuna mingine inafadhila zaidi ,nayo ni misikiti mitatu , Mtikiti wa
Makka kisha Msikiti wa Mtume S.A.W Madina, kisha Msikiti wa Kudsi (iliopo
Palestina ).
Na utukufu huu ni kutokana na hadithi mbali mbali za Mtume (S.A.W) kama
alivyosema "Sala moja katika Msikiti wangu (Madina ) ni bora kuliko Msikiti mwengine kwa mara elfu isipokuwa
msikti wa Makka " imepokewa na Imamu Bukhari na Muslim.
Pia amesema " sala moja katika Msikiti wa Makka ni bora kuliko sala
mia moja katika Msikiti wangu ." imepokewa na
Imamu Ahmad bin Hanbal na Ibnu Hibbani.
Na amesema Mtume (SAW) katika hadithi nyengine kuwa "Sala moja
katika Msikiti wa Aksa ni bora kuliko sala mia tano
katika misikiti mengine " imepokewa na Imam Bazzar.
Kutokana na mapokezi hayo tunafahamu kuwa Sala moja katika Msikiti wa
Makka ni bora kuliko sala laki moja katika Msikiti mwengine ,na sala moja
katika Msikiti wa Mtume (S.A.W) ni bora kuliko sala elfu moja katika Msikiti
mwengine ,na sala moja katika Msikiti wa Aksa (Baytil Makdid ) ni bora kuliko
sala mia tano katika msikti mwengine.
Ama misikiti isiyokuwa hiyo mitatu basi yote ni sawa katika fadhila za sala ,wala hakuna ulio bora kuliko mwengine kwa dhati ya
Msikiti .
Wallahu aalam.