Hija
ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa
sallam)
(Kama ilivyohadithiwa na Jabir bin Abdillah (Radhiya Llahu anhu)
Muhammad Faraj Salem Al saiy
Anasema Imam Muslim:
"Nimehadithiwa na Abubakar bin Abi Shaibah na Ishaq bin Ibrahim, wote
pamoja. Na kutoka kwa Hatim amesema kuwa Abubakar
amesema;
'Nimehadithiwa na
Hatim bin Ismail Al Madani, kutoka kwa Jaafar bin Muhammad, kutoka kwa baba yake
(Radhiya Llahu anhum) kuwa alisema:
"Tulimwendea Jabir bin Abdillah (Radhiya
Llahu anhu), akaanza kutuuliza majina yetu mmoja mmoja mpaka akaishia kwangu.
Nikamwambia:
'Mimi ni Muhammad bin Aliy bin
Hussain". Akakivamia kichwa changu, kisha akanifungua kifungo changu cha
juu kisha cha chini yake, kisha akauweka mkono wake kifuani pangu, na wakati huo nilikuwa bado kijana. Akaniambia;
"Marhaban
(karibu) ewe mwana wa ndugu yangu. Uliza unalotaka kuuliza".
Nikamuuliza, na
wakati ule alikuwa kipofu, na wakati wa Swala ulipowadia aliinuka huku akiikusanyakusanya
nguo yake, kila akijifunika nayo upande mmoja wa bega lake, upande wa pili
inaanguka kwa sababu ya udogo wake.
Akatuswalisha, kisha nikamwambia:
"Tuhadithie juu ya Hija ya Mtume
(Swallah Llahu alayhi wa sallam)".
Jabir (Radhiya Llahu anhu) akasema:
"Watu walipoarifiwa kuwa Mtume (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) atahiji mwaka huu, walianza
kumiminka mjini Madina kwa wingi sana, kila mmoja akitamani aongozwe na Mtume (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) na afanye kama atakavyofanya.
(Ilipowadia siku ya safari)
Tukaondoka naye mpaka tulipowasili Dhul Hulaifa (Abaar Ali - mikati ya watu wa Madina), Asmaa binti Umays akamzaa Muhammed bin Abubakar
Al Siddique (Radhiya Llahu anhu), akamtuma mtu kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi
wa sallam) kumuuliza nini afanye. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
"Oga, kisha weka kitambaa na utie nia ya Ihram (nia ya kuhiji)".
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa
sallam) akaswali msikitini kisha akampanda ngamia wake anayejulikana kwa jina
la Al Qaswaa, na alipokuwa katikati ya jangwa nikainua kichwa changu
kutizama waliokuwa mbele ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), nikaona
watu wengi sana, upeo wa macho yangu wakiwemo waliopanda wanyama na wanaokwenda
kwa miguu, kisha nikatizama kuliani kwake, nikaona hivyo hivyo, kisha upande
wake wa kushoto nikaona hivyo hivyo, na nyuma yake hivyo hivyo, na Mtume (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) akiwa pamoja nasi huku wahyi ukimteremkia, huku
akituhadithia, na kila anachokifanya, sisi tulikuwa tukimfuata.
Kisha akaanza kusema;
"Labbayka llahumma labbayka,
labbayka laa shariyka laka labbayka. Innal hamda wa neamata
laka wal mulk, laa shariyka laka".
Na watu wakawa wanasema kama anavyosema".
Jabir bin Abdillah (Radhiya Llahu
anhu) akaendelea kusema:
"Hatukuwa tukitia
nia nyingine isipokuwa nia ya Hija, (hatukuwa tukijuwa aina nyingine za Hija),
hatukuwa tukijuwa juu ya Umra. Tukaendelea na safari mpaka
tulipoifikia Al Kaaba tukiwa pamoja naye, akaligusa jiwe jeusi kisha akaanza
kutufu. Katika mizunguko mitatu ya mwanzo alikuwa akenda kwa
kukazana, na katika minne iliyobaki akenda mwendo wa kawaida. Alipomaliza
akenda penye Maqamu Ibrahim Alayhi ssalaam, akasoma:
"Wattakhidhu min maqami Ibrahima
musalla"
Al Baqarah - 125
Na maana yake (Na mahali alipokuwa akisimama Ibrahim
pafanyeni pawe pa kuswalia).
Akaelekea kibla na
kuswali rakaa mbili mahali hapo, akasoma katika rakaa ya mwanzo (alhamdu pamoja
na) Qul ya ayuha l kafirun na katika rakaa ya pili akasoma (alhamdu pamoja na)
Qul huwa llahu ahad, kisha akarudi penye jiwe jeusi, akaligusa kisha akatokea
mlangoni kuelekea Safa.
Alipokaribia Safa akasoma:
"Inna Safaa wal Marwata min shaairi
llahi - abdau bimaa badaa
llahu bihi"
Na maana yake ni:
(Hakika Safa na
Marwa (Majabali mawili yanayofanyiwa ibada ya Saa'yi huko Makka) ni katika
alama za kuadhimisha dini ya Mwenyezi Mungu -
naanzia pale alipoanzia Mwenyezi Mungu).
Akaanzia Safa, akaupanda mlima huo
mpaka alipoweza kuiona Al Kaaba akaelekea kibla akasema:
"Laa ilaha illa llahu - allahu akbar",
Kisha akasema:
"La Ilaha Illa Llahu Wahdahu
Lashariyka Lahu lahul mulku walahul hamdu Wahuwa Alaa Kulli Shay-In Qadiir. La
Ilaha Illa Llahu Wahdau, anjaza waadahu, wa nasara abdahu, wahazamal Ahzaaba
Wahdah”.
Kisha akaomba dua, kisha akarudia
kusema hivyo mara tatu, kisha akashuka kuelekea Marwa, alipofika katikati ya
bonde akawa anakwenda mwendo wa kukazana, na
alipolifikia jabali la Marwa akalipanda kwa mwendo wa kawaida, na alipolifika
juu yake akasoma na kufanya kama alivyofanya alipokuwa juu ya Safa.
Akaendelea hivyo mpaka tawafu yake ilipomalizikia
Marwa akasema:
"Lau kama
amri niliyopewa (hivi sasa) ningelipewa kabla, nisingechukuwa pamoja nami
mnyama na ningeijaalia (tawafu yangu na saayi yangu) kuwa Umra, na kama yupo
kati yenu asiyekuwa na mnyama basi avue nguo za Ihram na aijaalie iwe
Umra".
Akainuka Suraka bin Malik bin Jaathum (Radhiya
Llahu anhu) akasema:
"Ewe Mtume wa
Mwenyezi Mungu, (hukmu hii) ni kwa ajili ya mwaka huu tu au milele?"
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaviingiza vidole vyake vya mkono wa kulia ndani
ya vidole vya mkono wa kushoto na kusema:
"Umra na Hija
zishaingiliana" akasema hivyo mara mbili, kisha akasema; "La bali
milele".
Aliy (Radhiya Llahu anhu) akawasili
kutoka nchi ya Yemen akiwa na ngamia wa Mtume (Swallah
Llahu alayhi wa sallam), akamkuta Fatma (Radhiya Llahu anhu) amekwishavuwa nguo
za Ihram na kuvaa nguo za kawaida za rangi rangi na ametia wanja. Akamkataza, kwa ajili hiyo, lakini Fatma (Radhiya Llahu anhu) akamwambia:
"Baba yangu
ameniamrisha kufanya hivi".
Akaenda kwa
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kumshtaki Fatma kwa vile alivyofanya
(kuvua nguo za Ihram na kupaka wanja) na kwa kule kusema kwake kuwa Baba yake
ndiye aliyemuambia, akamjulisha kuwa yeye alimkataza kwa kufanya kwake vile.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamjibu:
"Ni kweli, (na)
wewe umetia nia gani ya kuhiji ulipokuwa unakuja?"
Akasema:
"Nilisema; 'Allahumma mimi natia nia ile ile aliotia Mtume wako".
Akamwambia:
"Basi mimi
ninaye mnyama, kwa hivyo tusivuwe (nguo za Ihram)".
Idadi ya wanyama aliokuja nao Aliy (Radhiya
Llahu anhu) kutoka Yemen ikichanganywa na idadi ya
wanyama aliokuja nao Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ikafikia ngamia mia
moja.
Watu wote wakavua Ihram zao na kukata nywele isipokuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa
sallam) na wachache waliokuja na wanyama wao.
Ilipofika siku ya Tarwiya - siku ya
tarehe 8 Dhul Hija, watu wakaondoka kuelekea Mina wakitia nia ya Hija, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akampanda mnyama
wake na kuelekea huko pamoja nao. (Walipowasili Mina), wakaswali Adhuhuri,
Alasiri, Magharibi, Isha na Alfajiri (Qasran, kila
Sala katika wakati wake).
(Baada ya kuswali alfajiri) Akasubiri
kidogo mpaka jua lilipochomoza akaamrisha lisimamishwe hema mahali paitwapo
Namira, - karibu na Arafat -. Mtume (Swallah Llahu
alayhi wa sallam) akaondoka kuelekea Namira na
akapitiliza Muzdalifa bila ya kusimama penye Mash-ari l haram, juu ya kuwa
Makureshi walidhania atasimama hapo kama walivyokuwa wakifanya wakati wa
Ujahilia.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa
sallam) hakusimama mpaka alipowasili Arafat, akaliona hema lishasimamishwa pale
Namira kama alivyoamrisha, akashuka na kupumzika hapo mpaka ulipoingia wakati
wa adhuhuri, akaamrisha aletwe ngamia wake Al Qaswaa, akampanda na
kwenda moja kwa moja mpaka alipofika katikati ya bonde la Arafat akasimama na
kuwahutubia watu akasema:
"Hakika ya damu zenu na mali zenu
(ni tukufu sana kwa hivyo) ni haramu baina yenu (kumwaga damu zenu na
kudhulumiana baina yenu) kama ulivyokuwa utukufu wa siku yenu hii, katika mwezi
wenu huu, katika mji wenu huu, visasi vyenu vyote vya wakati wa ujahilia viko
chini ya mguu wangu - nishavibatilisha - na kisasi cha mwanzo cha kumwaga damu
yetu ninachokibatilisha ni kisasi cha (kumwaga) damu ya Ibni Rabia bin Al
Harith - alikuwa na mtoto anayenyonyeshwa katika kabila la Bani Saad,akauliwa
na watu wa kabila la Hudhayl - Na riba iliyokuwa ikichukuliwa wakati wa
Ujahilia ishabatilika, na riba ya mwanzo ninayoibatilisha ni riba yetu, riba ya
Abbas bin Abdul Muttalib, ishabatilika yote, na muogopeni Mwenyezi Mungu katika
wake zenu, kwani nyinyi mumewachukuwa kwa dhamana ya Mwenyezi Mungu, na
mkahalalishiwa tupu zao kwa neno la Mwenyezi Mungu, na nyinyi mna haki zenu juu
yao. Wasiwaingize nyumbani kwenu yeyote msiyempenda (awe mwanamume au
mwanamke), na wakifanya hivyo, mnayo haki ya kuwapiga
kipigo kisichoumiza. Na haki yao juu yenu ni kuwalisha
na kuwavisha kwa wema. Na nimekuwachieni ambayo hamtopotea
baada yake ikiwa mtashikamana nayo, kitabu cha Mwenyezi Mungu. Mkiulizwa juu yangu mtasema nini?"
Wakasema:
"Tutashuhudia kuwa
umefikisha na umekamilisha na umenasihi".
Akanyanyua kidole cha shahada akawa mara
anakielekeza mbinguni mara anakielekeza kwa watu,
akasema:
"Mola wangu
shuhudia - (mara tatu)".
Kisha akaadhini, akakimu na kuswali Swala ya adhuhuri, kisha akakimu tena na kuswali Swala
ya alasiri bila kuswali Sunnah baina yao. Kisha akampanda ngamia wake na kuelekea naye moja kwa moja mpaka mahali pa kusimama
(katika uwanja wa Arafat), akamuelekeza ngamia wake Al Qaswaa penye majabali na
yeye akaelekea kibla.
Akasimama mahali hapo mpaka wakati wa magharibi ulipoingia na umanjano wa juwa kutoweka na juwa
kuzama kabisa, ndipo alipoondoka akiwa amempakia Usama nyuma yake.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akampanda ngamia wake Al Qaswaa na kuianza
safari ya kwenda Muzdalifa. Akawa anazikaza kamba za hatamu za ngamia wake na kumbana nazo ili asiweze kwenda mbio kwa ajili ya zahma
ya watu. Akawa anaashiria watu kwa mkono wake wa kulia
huku akiwaambia:
"Enyi watu! (nendeni kwa)
utulivu (nendeni kwa) utulivu".
Na kila anapolifikia jabali akawa
anailegeza kamba ili mnyama wake aweze kupanda kwa
wepesi. Akawa anafanya hivyo mpaka alipowasili Muzdalifa, akaswali hapo Swala
ya Magharibi na Isha kwa adhana moja na iqama mbili,
bila ya kusabih baina ya Swala hizo.
Kisha Mtume wa
Mwenyezi Mungu akapumzika mahala hapo mpaka alfajiri ilipoingia, akaswali
Alfajiri pale ilipombainikia kuwa wakati wa Swala ya alfajiri ushaingia, kwa
adhana na iqama.
Kisha akampanda Al Qaswaa
mpaka alipowasili Mashaaril haraam - (jabali lililopo hapo hapo
Muzdalifa), akaelekea kibla na kuomba dua huku
akikabir na kumtukuza na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Akawa
katika hali hiyo mpaka kulipopambazuka.
Kisha akaondoka na
kuianza safari ya kuelekea Mina kabla ya jua kupanda akiwa amempakia Al Fadhal
bin Abbas aliyekuwa kijana mwenye nywele nzuri, mweupe, na mwenye sura nzuri.
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipokuwa
akiondoka naye, akapita mbele yao ngamia aliyebeba wanawake wawili, na Al
Fadhal akawa anawaangalia wanawake hao. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
akauweka mkono wake usoni pa Al Fadhal ili asiweze kuwatizama, lakini Al Fadhal
aliugeuza uso wake upande wa pili na kuendelea kuwatizama, na Mtume (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) akaukamata uso wa Al Fadhal na kuugeuza upande
mwingine. Akaendelea na safari yake mpaka alipolifikia
bonde la Muhsir akaongeza mwendo kidogo, kisha akapita njia ya kati inayopeleka
moja kwa moja mpaka penye Jamarat kubwa (shetani mkubwa), na alipolifikia
Jamarat (hilo) lililokuwa karibu na mti akalipiga kwa mawe saba huku akikabir
kila anaporusha jiwe.
Kisha akaondoka kuelekea mahali pa
kuchinja, akachinja (ngamia) sitini na tatu kwa mkono
wake, kisha akampa Aliy achinje waliobaki, kisha akaamrisha nyama ikatwe katwe,
ikatiwa ndani ya vyungu vya kupikia, ikapikwa, wakala katika nyama ile na
kunywa supu yake.
Kisha Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akampanda ngamia wake na kuelekea penye Al Kaaba,
akaswali adhuhuri alipowasili Makka.
Baada ya kuswali akawaendea watu wa kabila la Bani Abdul Muttalib waliokuwa na jukumu la
kuwahudumia watu katika kunywa maji ya Zamzam, akawaambia:
"Wanywisheni maji enyi watu wa kabila la Bani Abdul Muttalib, ingekuwa sikuogopeeni watu
kukuchukulieni kazi hii ya kunywesha maji, basi ningelikusaidieni".
Wakampa maji (ya
Zamzam), akanywa.