Muhammad Faraj Salem Al saiy
Yaliomo
Vizuri Kuswali Kabla Ya Kutia Niyyah
Kunyanyua Sauti Katika Talbiyyah
Sa’ay Baina Ya Swafaaa Na Marwahh
Shukrani zote ni
zake Mwenyezi Mungu, tunashuhudia kuwa hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa
Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni Mtume wake.
Ameufikisha ujumbe na
kuifikisha amana, kwa hivyo tunakuomba Mola wetu umsalie na kumsalimu Mtume
wako huyu mtukufu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) na Aali yake na Masahaba wake watukufu - Aamin.
Amma baad,
Mwenyezi Mungu Anasema:
{{Na Mwenyezi Mungu
amewawajibishia watu wafanye Hijjah katika Nyumba hiyo; yule awezaye kufunga safari
kwenda huko.
Na atakayekanusha (asende na hali anaweza) basi
Mwenyezi Mungu si mhitaji kuwahitajia walimwengu.}} [Aali
‘Imraan–97]
Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Hijjah ni moja katika nguzo tano za Kiislamu, na ni fardhi
ijulikanayo kuwa ni ya lazima. Atakayekanusha kuwajibika kwake huwa ni kafiri aliyertadi na kutoka katika dini ya Kiislamu.
Wanavyuoni wengi wanasema kuwa: Hijjah
imefaradhishwa katika mwaka wa sita baada ya Hijra,
(baada Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuhamia
Madiynah).
Mwanachuoni maarufu Ibnil Qayyim, katika
kitabu chake kiitwacho Zaadul Ma-ad, yeye amesema kuwa Hijjah imefaridhishwa
mwaka wa tisa, pale ilipoteremshwa aya isemayo:
{{Na timizeni Hijjah na
Umra kwa ajili ya MwenyeziMungu.}} [Al Baqarah – 196]
Amesimulia Abu Hurayrah (Radhiya Llaahu
‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) aliulizwa:
"Amali ipi iliyo
bora?"
Akajibu:
"Imani juu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake"
Akaulizwa: “Kisha ipi?”
Akasema:
"Kisha Jihadi
katika njia ya Mwenyezi Mungu".
"Kisha ipi?"
Akasema:
"Kisha Hijjah
iliyokubaliwa".
Anasema As-Sayid Saabiq, mwandishi wa kitabu ‘Fiq-hus Sunnah’:
"Hijjah
iliyokubaliwa ni ile isiyochanganyika na maovu.”
Al-Hassan Al-Basry yeye amesema:
"Hijjah
iliyokubaliwa ni ile iliyomfanya aliyehiji anaporudi akawa anaipenda akhera
yake kuliko dunia.”
Wajumbe Wa Mwenyezi Mungu
Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Mahujaji na
wenye kufanya ‘Umrah ni wageni wa Mwenyezi Mungu.Wanachomuomba anawapa, na
wakiomba maghfira anawaghufiria.))
[Imepokewa na An-Nasai, Ibni Majah, Ibni Khuzaymah na Ibni Hibban]
Kwa hivyo kila aliyebahatika atambue kuwa
tokea siku ile alipoamua kwenda kuhiji, keshakuwa mgeni wa
Mola wake Subhanahu wa Taala, na kwa ajili hiyo anatakiwa awe mtu
anayekistahiki cheo hicho. Na anapokuwa katika Ibada hiyo tukufu asigombane
wala kuzozana na Mahujaji wenzake.
Zimepokelewa Hadiyth
nyingi zinazotufahamisha kuwa atakayehiji bila kufanya maovu wala kugombana
wala kuzozana, hapana zawadi nyingine anayoistahiki isipokuwa Pepo.
Maimamu wakubwa kama
vile Abu Hanifa na Maalik na Ahmad bin Hanbal na baadhi ya wanafunzi wa Imam
Ash-Shaafi’iy wanasema:
"Hijjah
inamwajibikia kila mtu toke pale anapokuwa na uwezo. Kwa sababu Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Anayetaka kuhiji basi aharakishe, kwa sababu huenda akaumwa, mnyama wake akazeeka au akapatwa
na shida (akazitumia pesa zake).))
Na katika hadithi nyengine amesema:
((Fanyeni haraka mkahiji, maana hajui mmoja
wenu atapatwa na nini.)) [Imepokewa na Ahmad, Al-Bayhaqiy, At-Twahaawiy na Ibn Maajah]
Kuhiji Kwa mali Ya Kukopa
Kutoka kwa
Abdullah bin Abu Auf (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:
((Nilimuuliza Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya mtu asiyewahi kuhiji
iwapo anaruhusiwa kukopa kwa ajili ya kuhiji?” Akaniambia;
“La, (asifanye hivyo)”.)) [Imepokewa na Al-Bayhaqiy]
Kamati ya kudumu ya Utafiti wa Kielimu na Utoaji Fatwa imetoa fatwa kuhusiana na suala
la Hijjah ya mwenye deni kwa kueleza yafuatayo:
Moja ya masharti ya Hijjah ni uwezo, na mtu kuwa na uwezo wa mali wa kuifanya Hijjah.
Ikiwa mtu ana deni ambalo anadaiwa na mkopeshaji na mkopeshaji akawa hakubali
yule mtu aende Hijjah bila kumlipa pesa zake, basi hatoruhusika kwenda Hijjah
hadi alipe deni analodaiwa, kwani mtu huyo atahesabika si mwenye uwezo wa
kwenda Hijjah. Lakini endapo mkopeshaji hatomshikilia alipe pesa zake na ima kamruhusu aende Hijjah hali ya kuwa ana deni lake,
basi anaweza kwenda na Hijjah yake kwa hali hiyo itakubalika.
[Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah
11/46]
Na katika Fatwa nyingine, Kamati
ya Kudumu ya Fatwa walipoulizwa swali kuhusu Hijjah ya mwenye deni la nyumba
ambalo muulizaji alisema anapaswa kulilipa kwa awamu,
ilieleza ifuatavyo:
Uwezo wa
kutekeleza Hijjah ni moja ya masharti ya kuwa kwake ni waajib. Ikiwa una uwezo wa kulilipa deni hilo kwa awamu ambayo imekutana na wakati
wa Hijjah, basi unaweza kwenda baada ya kulilipa deni katika awamu hiyo. Lakini
ikiwa huwezi kulipa deni hilo kwa awamu hiyo, basi
ahirisha Hijjah hadi utakapopata uwezo kwani Allaah Anasema:
“Na kwa
ajili ya Allaah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae
njia (mwenye uwezo) ya kwendea.” [Aal ‘Imraan
3: 97]
Na at-Tawfiyq ni
kutoka kwa Allaah
[Al-Lajnah ad-Daaimah lil Buhuuth
al-‘Ilmiyyah wal Iftaa 11/45]
Naye Mwanachuoni Shaykh Muhammad
bin Swaalih al-‘Uthaymiyn anasema:
Deni linalodaiwa linapaswa
kutangulizwa kulipa kuliko Hijjah, kwani wajibu wa
kulilipa unawekwa mbele kuliko mtu kwenda kutekeleza Hijjah. Hivyo,
anapaswa mtu kulipa kwanza deni kisha ndio kwenda Hijjah. Na ikiwa
hatobakiwa na chochote au kitakachobaki hakimtoshelezi
gharama za kwenda Hijjah, basi atasubiri hadi Allaah Amjaalie uwezo wa kwend
akuitekeleza nguzo hiyo. Lakini likiwa ni deni lenye
kuwa na muda mrefu aliopewa mkopeshwa la kulilipa siku za mbele, hivyo, kwa
hali hii hata kama mkopeshaji akimruhusu au asimruhusu kwenda Hijjah,
hatoruhusika kwenda Hijjah ikiwa hana uhakika au dhamana ya kulilipa kwa ule
muda aliopewa/waliokubaliana na mkopeshaji.
Kwa hali hiyo tunasema: Ikiwa mtu
anadaiwa deni, na anafahamu kuwa ana uwezo wa kulilipa
kwa muda aliopewa (hata ikiwa ni mbeleni baada ya Hijjah), basi Hijjah kwa hali
hiyo inakuwa ni wajibu kwake japokuwa ana deni.
[Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn, 21/96]
Imepokewa
kutoka kwa At-Tabarani kuwa Abu Hurayra (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema: kuwa
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Anapotoka
mwenye kuhiji kwa pesa njema akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama
wake, akasema: "Labbayka Allahumma labbayk", (Nakuitikia ewe
Mola wangu nakuitikia) hujibiwa na msemaji kutoka mbinguni, "Labbayka
wa Sa’adayka (Mwitikio wako umekubaliwa na utafurahi kwa amali yako njema
hii), kwa sababu zawadi yako (chakula na vifaa vyako) ni vya halali, na mnyama
wako ni wa halali, na Hijjah yako inakubaliwa na haina madhambi".
Lakini
anapotoka anayeihiji kwa pesa za haramu akauweka mguu
wake juu ya kipandio cha mnyama wake akasema, "Labbayka Allahumma
labbayk" (Nakuitikia ewe Mola wangu nakuitikia), hujibiwa kutoka
mbinguni, "Laa labbayaka walaa sa’adayka. (Hakukubaliwi kuitikia
kwako wala hutolipwa mema), kwa sababu vifaa vyako ni
vya haramu na pesa zako ni za haramu na Hijjah yako ni ya dhambi na wala
haikubaliwi".
Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) ameweka Miyqaat ‘mipaka’ maalum ambayo yeyote anayekwenda
Makka kwa nia ya kuhiji au kufanya ‘Umrah haruhusiwi kuivuka kabla ya kutia nia
ya Ihraam mwahala hapo. Amewawekea watu wa Madiynah
mji wa Dhul Hulayfah kuwa ni Mpaka wao. Mji huu unajulikana pia kwa jina la Abaar ‘Ali, nao upo Madiynah, kiasi cha
Kilomita 450 mbali na Makkah.
Akawawekea watu wa
Sham mji wa Al-Juhfa kuwa ni Miyqaat yao. Na Miyqaat ya
watu wa Najd ni Qarn al Manazil. Amma
watu wa Yemen Miyqaat yao ni mji wa Yalamlam.
Na watu wa Iraaq Miyqaat yao ni Dhaata ‘Irq.
Hii
ni mipaka aliyoiweka Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) kisha akasema:
((Hiyo
ni mipaka yao na ya kila apitae njia hizo, kwa wasio
wakazi wa miji hiyo, kwa kila atakaye kuhiji au kufanya ‘Umrah.))
Mtu anapowasili katika mipaka hiyo
anatakiwa aoge, ajisafishe, akate makucha na kujitia
manukato akitaka. (Si vizuri kujitia manukato katika vazi la
Ihraam, ingawaje si haram kufanya hivyo, isipokuwa sharti iwe kabla ya kutia
nia ya kuhiji).
Unaweza kukoga na
kuvaa Ihraam (vazi la kuhijia) pamoja na kufanya yote hayo ukiwa
nyumbani kwako, hotelini au popote ulipofikia kabla ya kuifikia mipaka hiyo,
isipokuwa nia lazima
uitie ufikapo penye mipaka hiyo.
Vizuri Kuswali Kabla Ya Kutia Niyyah
Utakapofika katika mojawapo ya mipaka
iliyotajwa ukiwa bado hujaswali Swalah ya fardhi ya wakati huo, basi ni bora kuswali kwanza kisha utie niyyah. Amma ukiwa
umekwishaswali, basi ni vizuri (si lazima) kusali
raka’ah mbili Sunnah ikiwa wakati huo si katika nyakati zinazokatazwa kuswali,
kisha unatia niyyah kwa kusema: “Labbayka ‘Umrah”
Kisha unaanza kufanya Talbiyyah kwa kusema:
“Labbayka Allaahumma Labbayk. Labbayka Laa
Shariyka Laka Labbayk, Inna Lhamda Wanni-‘mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Lak.”
Unaendelea hivyo njia yote, wanaume
wanasema kwa sauti kubwa na wanawake kwa sauti ndogo
huku ukimuomba Mwenyezi Mungu maghfira na kumdhukuru kwa wingi.
Unatakiwa pia uwe ukimswalia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam kwa wingi pamoja na kuamrisha mema na kukataza
maovu unapokuwa safarini mpaka utakapowasili Makkah.
Talbiyyah ni kutamka "Labbayka
Allaahumma Labbayk. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk, Inna Lhamda Wanni-‘mata
Laka Wal Mulk Laa Shariyka Lak.”
Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Talbiyyah
ni kitendo kilichotolewa amri juu yake.
Kutoka kwa
Ummus-Salama (Radhiya Llaahu ‘anha)
amesema:
((Nilimsikia Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) akisema: ‘Enyi watu wa nyumba ya Muhammad, anayehiji kati
yenu anyanyuwe sauti yake anapofanya Talbiyyah.)) [Imepokewa na Imam Ahmad na Ibni Hibban]
Maulamaa wamekhitilafiana katika hukmu
yake, katika wakati wake, na katika kuichelewesha.
Imam Ash-Shaafi’iy na
Imam Ahmad wanasema kuwa kitendo hicho ni Sunnah na kwamba mtu anatakiwa aanze
kufanya Talbiyyah mara baada ya kutia nia ya Ihraam. Na iwapo ametia nia ya
Hijjah kisha asifanye Talbiyyah, basi Hijjah yake inasihi na
wala haina tatizo lolote.
Imam Maalik, yeye anaona kuwa kitendo
hicho ni Wajib na mtu asipofanya Talbiyyah baada ya
kutia nia ya Ihraam, akaendelea hivyo muda mrefu bila kufanya Talbiyyah, basi
inampasa kuchinja mnyama.
Imesimuliwa na
Jaabir (Radhiya Llaahu ‘anhu)
kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Muislam yeyote atakayefanya Talbiyyah
tokea asubuhi mpaka jua linapozama, dhambi zake zitafutwa na
atarudi (akiwa hana dhambi) kama alivyokuwa siku aliozaliwa na mama yake.)) [Imepokewa na Ibni Majah]
Imesimuliwa pia na
Abu Hurayrah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Kila mwenye kuinyanyua sauti yake kwa
kufanya Talbiyyah, anapewa bishara (njema), na kila mwenye kufanya Takbir
(kutamka 'Allaahu Akbar') anapewa bishara (njema)” Akaulizwa: “Ewe Mtume
wa Mwenyezi Mungu, bishara ya Pepo?” Akasema:
“Ndiyo”)) [Imepokewa na At-Tabaraniy na Sa’iyd bin
Mansuur]
Kunyanyua Sauti Katika Talbiyyah
Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) amesema:
((Alinijia Jibriyl akaniambia: “Waamrishe
sahibu zako wanyanyuwe sauti zao katika Talbiyyah, kwani hiyo ni
katika alama za Hijjah.”)) [Imepokewa na Ibni
Majah. Imam Ahmad, Ibni Khuzaymah na Al Hakim]
Na kutoka kwa
Abubakar (Radhiya Llaahu ‘anhu)
amesema:
((Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) aliulizwa: “Amali gani iliyo bora katika Hijjah?” Akajibu: “Al
ajji wa thajji” (Kunyanyua sauti katika kufanya Talbiyyah na kuchinja).)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ibni Majah]
Unapowasili Makkah unaanza kufanya ‘Umrah kwa taratibu ifuatayo:
‘Unatufu’, kwa
kuizunguka Al-Ka’abah mizunguko saba ukianzia penye jiwe jeusi (Al Hajar al
aswad), ukiwa mbali na jiwe hilo anzia sawa na jiwe jeusi.
Kabla ya kuanza kutufu lielekee
Jiwe jeusi kisha linyoshee mkono (ukiweza kulifikia na
kulibusu au kuligusa bila ya kuumiza watu ni vizuri), la kama utasababisha
madhara kwa watu au kwa nafsi yako, inatosha kuliashiria tu kwa mkono wa kulia
kwa mbali huku ukisema: “Bismillahi Allaahu Akbar” Kisha
unaizunguka Al-Ka’abah ikiwa kushotoni kwako mizunguko saba.
Kwa wanaume ni
vizuri katika mizunguko mitatu ya mwanzo kukimbia kidogo kidogo mfano wa mtu
anayekimbia juu ya mchanga, na mizunguko minne iliyobaki unakwenda mwendo wa
kawaida. Wanawake wanakwenda mwendo wa kawaida katika
mizunguko yote saba.
Wakati wote huo
unatakiwa uwe ukisoma du’aa zozote ulizohifadhi. Hapana kisomo maalum au du’aa maalum, bali unaweza kuomba du’aa yoyote na kwa lugha yoyote, na unaweza
pia kusoma sura ulizohifadhi katika Qur-aan.
Al-Ka’abah ina
nguzo nne, na maarufu katika hizo ni nguzo ya jiwe jeusi na nguzo iliyo kabla
yake ambayo ni nguzo ya Yaman (Ar-Rukn al-Yamani). Unapoifikia nguzo ya
Yaman (Ar-Rukn al-Yamani) ni vizuri kuigusa.
Hutakiwi kuibusu wala kuiashiria kama unavyolifanyia
jiwe jeusi. Na unapokwenda baina ya nguzo hiyo ya Yamani na
Jiwe Jeusi ni vizuri kuomba na kuikariri du’aa ifuatayo.
“Rabbana Aatina
Fidduniya Hasanatan Wa Fil Aakhirati Hasanatan Wa Qinaa ‘Adhaaba Nnaar”.
Na maana yake ni:
(Mola wetu tupe katika dunia yaliyo mema, na katika akhera (tupe) yaliyo mema, na utuepushe na adhabu
ya Moto).
Unaendelea hivyo
mpaka utakapolifikia Jiwe jeusi. Hapo utakuwa umekwishamaliza mzunguko wa mwanzo, na
utaanza mzunguko wa pili kwa kunyanyua mkono wa kulia huku ukiliashiria tena
jiwe jeusi na kusema: “Allaahu akbar”, kisha utatenda yale yale
uliyotenda katika mzunguko wa mwanzo, mpaka umalize mizunguko saba.
Kila unapolifikia jiwe jeusi au unapokuwa
sawa nalo, unanyanyua mkono wa kulia na kulielekea
jiwe huku ukisema: “Allaahu Akbar”
Ukishamaliza kutufu mara saba, unakwenda kuswali raka’a mbili nyuma ya Maqaam
Ibraahiym. Katika raka’a ya mwanzo unasoma Alhamdu na
Qul ya ayyuha l kaafiruun na katika raka’a ya pili unasoma Alhamdu na
QulhuwAllaahu ahad.
Usipoweza kuswali penye Maqaam
Ibraahiym kwa sababu ya msongamano mkubwa wa watu,
unaweza kuswali popote karibu na hapo au popote mbali na hapo sharti iwe ndani
ya msikiti.
Baada ya kumaliza kutufu na kuswali raka’a mbili penye Maqam Ibrahim, ni
vizuri kunywa maji ya Zamzam. Unaweza kunywa kutoka katika majagi ya maji
yaliyoenezwa msikitini hapo, na unaweza pia kwenda
penye mifereji (mabomba) ya maji ya Zamzam yaliyokuwepo penye uwanja wa Swafaaa
na Marwah.
Imepokewa
kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim kuwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) alikunywa maji ya Zamzam kisha akasema: ((Maji haya yamebarikiwa, yanamshibisha
mwenye njaa na yanamponesha mgonjwa.))
Sa’ay Baina Ya Swafaaa Na Marwahh
Swafaaa na Marwah ni vilima viwili vilivyoelekezana,
vilivyomo ndani ya msikiti upande wa kisima cha Zamzam.
Ukimaliza kutufu na
kunywa maji ya Zamzam, unakwenda penye jabali Swafaaa kwa ajili ya
kuanza kufanya ibada ya Sa'ayi, baina ya majabali Swafaaa na Marwah.
Unaanza kwa
kupanda Swafaaa huku ukisema:
“Inna Swafaa
walMarwahta min shaairi llah". kisha unasema
"Abdau maa badaa llahu bihi”, na maana yake ni:
(“Hakika Swafaaa na
Marwah ni katika alama za kuadhimisha dini ya Mwenyezi Mungu. Ninaanza pale
alipoanzia Mwenyezi Mungu. (Ambaye ndani ya Qur-aan tukufu ameanza
kulitaja jabali Swafaaa kisha Marwah).
Si lazima kutamka maneno hayo, lakini hi ni kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisema na kufanya hivyo.
Unapowasili juu ya Swafaaa unaelekea
Qiblah kisha unasema:
ÇáÍãÏ
ááå -
Çááå ÇßÈÑ - áÇ Åöáåó ÅáÇøó Çááåõ æóÍúÏóåõ áÇ ÔóÑöíßó áóåõ¡ áóåõ Çáãõáúßõ æóáóåõ
ÇáÍóãúÏõ æåõæó Úóáì ßõáøö ÔóíÁò ÞóÏíÑñ¡ áÇ Åöáóåó ÅáÇ Çááåõ æóÍúÏóåõ ÃóäúÌóÒó
æóÚúÏóåõ¡ æóäóÕóÑó ÚóÈúÏóåõ æóåóÒóãó ÇáÃóÍúÒóÇÈó æóÍúÏóåõ.
“Alhamdu Lillahi
Allaahu Akbar La Ilaha Illa Llahu Wahdahu Laashariyka Lahu Wahuwa Alaa Kulli
Shay-In Qadiir. La Ilaha Illa Llahu Wahdau, Anjaza Waadahu Wanawsara ‘Abdahu Wahazamal
Ahzaaba Wahdahu” Unasema hivyo mara tatu.
Hivi
ndivyo alivyofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Kama hukuweza (kutokana na zahma au kama hujaweza
kuhifadhi vizuri) basi unasoma hata mara moja tu, au unaomba du’aa yoyote na
kusoma chochote unachoweza kusoma. Kisha teremka na ufanye
"Sa’ay ya Umra”.
Na Sa’ay ni
kwenda baina ya Swafaaa na Marwah mara saba (Kwenda, inahisabiwa
mara moja, na kurudi mara moja). Ni vizuri kukimbia kidogo kidogo kila
unapozifikia alama za kijani zilizo ukutani baina ya Swafaa na Marwah, lakini wanawake, wao wanakwenda mwendo wa
kawaida. Ukifika Marwah, unapanda juu na kusema
pamoja na kufanya yale uliyoyafanya ulipokuwa juu ya Swafaaa.
Hakuna katika Twawaafu
wala katika Sa’ay, du’aa au kisomo maalum. Soma chochote na
omba du’aa yoyote.
Ukishamaliza kufanya Sa’ay,
unapunguza nywele zako au unazinyoa zote. Kwa wanaume ni
vizuri kunyoa, kama alivyofanya na kupendekeza Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Lakini wanawake, wao wanapunguza kidogo tu.
Hapo utakuwa umekwisha maliza ibada ya ‘Umrah na unaweza
kuvua nguo za Ihraam na kuvaa nguo zako za kawaida.
Na kinakuhalalikia kila kitu
ulichoharamishiwa ulipokuwa katika Umrah, hata mkeo. (Kama
ni ‘Umrah ya Hijjah unaisubiri tarehe 8 Dhul-Hijjah
ili uanze ibada ya Hijjah.)
Kutoka kwa
Abdillahi bin ‘Umar (Radhiya Llaahu
‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((“Mwenyezi Mungu Awarehemu walionyoa
(nywele zote)” Masahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) wakasema: “Na waliopunguza je
ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: “Mwenyezi Mungu
awarehemu walionyoa (nywele zote).” Wakasema: “Na waliopunguza je ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: “Mwenyezi Mungu awarehemu
walionyoa (nywele zote).” Wakasema: “Na waliopunguza je ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: “Na waliopunguza.”))
Katika Hadiyth hii Mtume Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amewaombea rehema mara tatu walionyoa nywele zote na
akawaombea mara moja tu waliopunguza.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuingize katika
Rahmah Yake – Aamin
Tarehe nane Dhul Hijjah inaitwa "Siku ya
Attarwiyah”, nayo ni siku inayoanza Ibada za Hijjah. Likishatoka jua la siku hiyo, oga na uvae nguo zako za Ihraam ukiwa nyumbani, hotelini
au popote ulipofikia mjini Makkah au nje yake kisha sema: “Labbayka Hijjah”.
Masharti ya Ihraam ni yale yale tuliyoyataja
hapo mwanzo katika ibada ya ‘Umrah.
Asubuhi ya siku hiyo Mahujaji wanaondoka
Makkah kuelekea Minaa na wanaswali mahali hapo Swalah
ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Isha ya siku hiyo, pamoja na Swalah ya
Alfajiri ya siku ifuatayo. Kila Swalah inaswaliwa katika wakati wake Qasran
(kwa kufupisha). Unazifupisha Swalah za raka’a nne unaziswali raka’a mbili, ama Swalah ya Magharibi
unaiswali kwa ukamilifu – raka’a tatu.
Kusimama
y ni nguzo kubwa kupita zote katika nguzo za Hijjah,
na hii inatokana na Hadiyth ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema:
((Al Haju ‘Arafah – (Kusimama) Arafa ndiyo Hijjah yenyewe -
atakayewahi usiku wa kujikusanya kabla ya kuingia
alfajiri (ya siku ya ‘Arafah) basi amewahi”.)) [Imepokewa na Imam Ahmad pamoja na ma Imam wengine wa Hadyith]
Likishatoka jua la tarehe tisa Dhul Hijjah,
Mahujaji wanaondoka Minaa na kuelekea ‘Arafah kwa utulivu na tahadhari, huku
wakisema: “Allaahu akbar” – au “Laa ilaaha illa Allaah” au huku wakilabiy
kwa kusema:
“Labbayka Allahumma Labbayk Labbayka Laa
Shariyka Laka Labbayk - Inna Lhamda Wanni’mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka
Laka.”
Wanakwenda kwa
utulivu bila kuwaudhi wenzao, na wanaziswali Swalah za Adhuhuri na Alasiri
wakati mmoja hapo ‘Arafah, Qasran, zote wakati wa Adhuhuri, kwa adhana
moja na iqama mbili.
Ni vizuri kubaki katika sehemu ya Namirah,
mahali ulipo msikiti mkubwa wa Namirah na
wasiingie ‘Arafah mpaka baada ya wakati wa zawaal (Kiasi cha saa sita za
mchana).
Hii siyo lazima, hasa kutokana na zahma za hapo ‘Arafah siku hiyo, isipokuwa ni bora kama
ikiwezekana. Hakikisha kuwa umo ndani ya mipaka ya ‘Arafah, na
unapokuwa mahali hapo patakatifu, zidisha kuomba du’aa na kumtaja Mola wako huku
ukiwa umeelekea Qiblah, kwa sababu siku hiyo na mahali hapo
ndipo watu wanapoghufiriwa madhambi yao yote na kurudi makwao kama siku
waliyozaliwa.
Nyakati za jioni
tafuta sehemu za juu juu. Panda, kisha elekea Qiblah na
unyanyue mikono yako juu huku ukiomba, kama alivyofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Imesimuliwa na
Jaabir (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
amesema:
((“Hakuna siku bora
kwa Mwenyezi Mungu kuliko siku kumi za (mwanzo) za Dhul Hijjah”. Mtu mmoja akamuuliza: “Siku hizo ni bora, au
mtu anapokuwa katika Jihadi kwa muda huo?” Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) akamuambia: “Siku hizo ni bora kuliko idadi ya siku hizo
katika Jihadi fiy sabiili Llah. Na hapana siku iliyo bora kwa Mwenyezi Mungu kuliko siku ya ‘Arafah. Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala
huwaambia Malaika wake kwa fahari: “Tazameni waja wangu, wamekuja nywele zao
zikiwa zimetimka, wamejaa mavumbi, wametoka kila sehemu za mbali wakitaraji
rehema Zangu na wala hawakuwahi kuiona adhabu Yangu”. Hakuna
siku ambayo Mwenyezi Mungu anawaepusha watu wengi na moto kuliko siku hiyo”.))
[Imepokewa na Abu Ya’ala – Al-Bazzaar – Ibn
Khuzaymah na Ibn Hibbaan]
Imepokewa pia kuwa Anas bin Maalik (Radhiya Llaahu ‘anhu) amesema:
((“Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alisimama ‘Arafah wakati jua
linakaribia kuzama, akasema: “Ewe Bilaal! Ninyamazishie
watu.” Bilaal (Radhiya Llaahu ‘anhu), akainuka na
kuwataka watu wanyamaze. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akasema:
“Enyi watu! Alinijia Jibril hivi punde na kunipa salam zitokazo kwa Mola wangu. (Kisha) Akasema:
‘Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala amewaghufiria watu wa ‘Arafah na watu wa Masha'ari
l haraam (Muzdalifah).” Akainuka ‘Umar bin Khattab (Radhiya Llaahu ‘anhu) akauliza:
“Hizi (salam na haya maghfira) ni kwa ajili yetu peke
yetu?” Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Hizi ni zenu na za
wote watakaokuja (hapa) baada yenu mpaka siku ya Qiiyaamah.” ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akasema: “Kheri
za Mwenyezi Mungu ni nyingi na nzuri.”))
Imesimuliwa na
Ibnul Mubarak kutoka kwa Sufyaan Ath-Thawriy kuwa:
'Mtu anapokuwa hapo anatakiwa
ajishughulishe na kuomba du’aa pamoja na kumtaja
Mwenyezi Mungu sana ili arudi akiwa amefaidika na ameghufiriwa, na asiwe katika
waliokula hasara siku hiyo kwa kuyakosa maghfira ya Mwenyezi Mungu.'
Jua likishazama
Mahujaji wanaondoka ‘Arafah na kuelekea Muzdalifah. (Usiswali Magharibi
hapo ‘Arafah).
Unapokuwa Muzdalifah utaswali
Swalah ya Magharibi na ‘Ishaa wakati wa ‘Ishaa, raka’a
tatu za Magharibi kisha mbili za ‘Ishaa kwa adhana moja na Iqama mbili. Kisha utabaki hapo mpaka baada ya Swalah ya Alfajiri.
Ukiwa hapo utaomba du’aaa kwa wingi huku ukinyanyua mikono yako juu na kuelekea Qiblah
kama alivyofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Ukiwa Muzdalifah
utaokota mawe ya kupigia Jamaraat. (Jamaraat ni
milingoti mikubwa mitatu ya mawe yanayopigwa hapo Minaa ambayo watu wengine
huyaita Mashetani). Unaokota mawe saba tu, (si lazima
kuokota mawe yote hapo Muzdalifah), na mawe mengine utaweza kuokota ukiwa
Minaa. Unaweza pia kuokota mawe yote ukiwa hapo kama
ukitaka.
Utaondoka Muzdalifa kwa
utulivu na kuelekea Minaa baada ya Swalah ya Alfajiri na kabla ya kutoka jua.
Utakapowasili
Minaaa unafanya yafuatayo:
1. Unalipiga Jamaratul ‘Aqabah ambalo watu
wanaliita Shetani Mkubwa, lililo karibu na Makkah kwa
mawe saba, moja baada ya jingine. Kila unaporusha jiwe unasema:
“Allaahu Akbar".
(Haijuzu kuvurumisha mawe yote saba kwa pamoja).
‘Jamaraat’ si mashetani kama wanavyoitakidi baadhi ya watu wenye kuvurumisha mawe
kwa ghadhabu na kutukana na wengine huvurumisha mawe makubwa wakidhani kuwa wanampiga
na kumkomesha shetani. Hayo yote hayajuzu, kwa sababu
‘Jamaraat’ yamewekwa kwa ajili ya kujikumbusha tu namna gani Nabii
Ibraahiym mahali hapo alivyompiga mawe shetani aliyejaribu kumshawishi
asimchinje mwanawe kama alivyoamrishwa na Mola wake.
Kwa hivyo mtu anatakiwa arushe mawe madogo
sana na kuyapiga Jamaraat kwa nia ya kutii amri ya
Mwenyezi Mungu tu, bila ya kuingiza fikra nyingine.
Kwa wale wasiojiweza wanaweza kumwakilisha
mtu awapigie, na mtu mmoja anaweza kuwakilishwa na
wengi.
(Kumbuka siku ya mwanzo unalipiga mawe Jamarat
moja tu, tofauti na siku zilizobaki unapoyapiga mawe
Jamaraat zote tatu).
2. Chinja mnyama wako, na ni
vizuri kama utakula katika nyama hiyo na nyengine utawapa masikini.
3. Punguza au nyoa nywele zako. (kunyoa
nywele zote ni bora zaidi), na mwanamke anakata nywele zake kidogo tu.
Utaratibu huu ni
bora zaidi ingawaje unaweza kutanguliza hiki kabla ya kile. Ukimaliza kupiga
mawe, kuchinja na kunyoa, unakuwa umekwisha
jihalalisha uhalalisho mdogo na unaweza kuvaa nguo zako za kawaida na kufanya
yote uliyokatazwa ulipokuwa na Ihraam, isipokuwa tu huwezi kumwingilia mkeo
mpaka umalize Twawaaful Ifaadhwah (Twawaafu ya Hijjah).
Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Twawaaful
Ifaadhwah (Twawaafu ya Hijjah) ni katika nguzo za
Hijjah, na kwamba asiyetufu Twawaafu hiyo Hijjah yake inabatilika.
Na hii inatokana na
kauli Yake Subhanahu wa Taala
Aliposema:
{{Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na waizungike Nyumba ya Kale
(Nyumba kongwe – Al-Ka’abah).}} [Al Hajj – 29]
Ukishamaliza shughuli za hapo Minaa,
unakwenda Makkah na unafanya Twawaaful Ifaadhwah, nako ni kuizunguka Al-Ka’abah mara
saba na kufanya kama ulivyofanya katika Twawaafu ya ‘Umrah. Kisha unafanya Sa’ay,
kutembea baina ya Swafaaa na Marwah na kufanya kama
ulivyofanya mara ya mwanzo ulipofanya ‘Umrah.
Ukishamaliza, unakuwa umekwisha
jihalalishia halalisho kubwa na kwa hivyo, hata mkeo
anakuhalalikia. Unaweza kuiahirisha Twawaafu ya Ifaadhwah
mpaka baada ya kumaliza shughuli zote za Minaa.
Ukishamaliza Twawaafu ya Ifaadhwah
unarudi Minaa na unabaki hapo usiku wa tarehe 11, 12
na 13 kwa wasiokuwa na haraka. Hizo zinaitwa siku za Tashriyq.
Inatosha kama utabaki hapo usiku wa tarehe 11 na wa 12
tu. Katika siku 2 au 3 hizo unapiga mawe Jamaraat
zote tatu kila siku kwa mpangilio ufuatao:
Anza kupiga Jamaraat la mbali na Makkah, (Jamaraat dogo) kisha la kati, kisha Kubwa
(Jamarat al Aqaba). Kila moja piga kwa mawe
saba huku ukisema: "Allaahu Akbar", kila unaporusha jiwe. Hii ni kwa siku tatu zilizobaki.
Siku ya An-Nahr – Sikukuu mosi,
usipige mawe mpaka jua lichomoze:
((Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) alipokuwa Muzdalifah
aliwatanguliza Minaa watu dhaifu na wazee na wanawake, akawaambia: “Musirushe
mawe mpaka jua litoke”)) [Imepokewa na
At-Tirmidhiy]
Mwenye udhuru anaweza kuchelewesha mpaka
kabla ya Magharibi, lakini ni vizuri kupiga mawe baada
ya kutoka jua na kabla haijaingia Magharibi kwa asiyekuwa na udhuru. (Baadhi ya
Maulamaa wanajuzisha kupiga mawe baada ya Magharibi kwa
udhuru, lakini bora ujaribu kupiga kabla jua kuzama).
Wakati wa kurusha
mawe kwa siku mbili zilizobaki au siku tatu kwa wale wasiotaka kuharakisha, ni
baada ya Zawal (wakati wa adhuhuri pale jua linaposogea kidogo baada ya
kuwa katikati).
Ni vizuri kuelekea Qiblah na kuomba du’aa baada ya kumaliza kupiga kila Jamaraat
isipokuwa Jamaraat la mwisho. Hadiyth iliyosimuliwa na
Al-Bukhaariy na Imam Ahmad
inasema:
((Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akeshapiga kila Jamaraat
kwa mawe saba akisimama na kuelekea Qiblah na kuomba du’aa, isipokuwa baada ya
kulipiga Jamaraat la mwisho hakusimama.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Imam Ahmad]
Ikiwa unataka kubaki hapo kwa mda wa siku mbili tu, basi siku ya tarehe Kumi na mbili Dhul
Hijjah ambayo hujulikana kama ni "Yawmul isti’ijaal" -
Siku ya Kuharakisha – unapiga mawe na kuondoka Minaa kabla ya jua kuzama, na
ikiwa utakawia kuondoka ukawepo hapo baada ya juwa kuzama itakubidi ubaki hapo
siku moja zaidi. Ni vizuri kubaki usiku wa tatu ikiwa
huna cha kukushughulisha.
Unapotaka
kurudi nchini kwako baada ya kumaliza shughuli za Hijjah, unatufu Twawaaful
wida’a, (Twawaafu ya kuaga) nayo ni kama
ifuatavyo:
Unatufu
Al-Ka’abah mara saba na kufanya kama ulivyofanya
katika Twawaafu za mwanzo, lakini mara hii bila ya kufanya Sa’ay baina ya
Swafaa na Marwah.