HASADA NA MADHARA YAKE
Na Ali Said Arafa
Katika makala hii tumeonelea tuelezane kwa mukhtasari ubaya wa hasada
na madhara yake na zaidi kwa kuwa karibuni hivi tumetoka katika mwezi mtukufu
wa Ramadhan ambao tulijituma kwa ibada mbali mbali na pia hivi sasa tumo katika
miezi mitukufu ambapo pia tunatakiwa tuwe na hima ya kutenda amali mbali mbali
wanavyuoni wametwambia: “Bora ya mawaidha ni yale yenye kumpelekea mja kumcha
Mungu na bora ya elimu ni ile yenye kumpelekea awe mnyenyekevu na mzuri wa tabia”.
Masikitiko makubwa katika nyoyo za watu wengi wanapofikiwa na mwezi wa
Ramadhan huwa na hima ya kujitakasa na maasi mbali mbali ya nyoyo n.k. lakini
baada ya kumalizika tu mwezi wa Ramadhan masikini tunatekwa na Bilisi pamoja na
nyoyo zetu kwa kutenda maasi mbali mbali na hapana dhambi ambayo Bilisi
ameipandisha katika nyoyo za watu wengi na wa matabaka mbali mbali kama hasada,
gonjwa hili la hasada limewasibu vijana wadogo baina yao, watu wazima, masikini
na matajiri, wasio kuwa na elimu na hata hao wenye elimu nao ndio zaidi.
Mtume (S.A.W) amesema katika hadithi aliyosimulia sahaba Bwana Abi Malik
(R.A) ambayo imepokewa na Imam Muslim “Twahara ni nusu
ya imani…” wanavyuoni wenye elimu za batini wemefasiri kuwa twahara
iliyokusudiwa hapo ni mtu ajisafishe na maradhi ya nyoyo nayo ni hasada, kibri,
choyo, bughudha, jeuri n.k akishajisafisha na magonjwa hayo hapo ndio mja huyo
atakuwa na nusu ya imani.
Wamesema baadhi ya watu wenye hikima kuwa “Madhambi makubwa yenye
kumuangamiza mja mwenyewe ni matatu hasada, kibri na pupa” ubaya na uzito wa
dhambi hii ya hasada ni kuwa mtu mwenyenayo anakuwa anaingilia utawala wa
Mwenyezi Mungu (S.W) pasina mwenyewe mtu huyo kujijuwa na kujitambua, kwa vile
tu kuchukiwa kwake mja huyo, kubughudhi na kuhoji kwa nini Fulani karuzukiwa
hivi na miongoni mwa sifa za Mola wetu (S.W) ni kuwa yeye hakuna wa kumuhoji na
kumtia ila kama alivyotwambia katika aya ya 16 ya Suratul-Buruji: “Yeye
Mwenyezi Mungu (S.W) ni mwingi wa kutenda alipendalo na wala hakuna wa kumuhoji
kwa hali zote”.
Maadui
wa neema za Mwenyezi Mungu (S.W).
Kila mtu mwenye hasada anahisabika mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W) kuwa ni adui wa neema zake kwa waja wake na haya ameyesema Mtume
(S.A.W): “Hakika ya neema za Mwenyezi Mungu (S.W) zina maadui” Masahaba
walimuuliza “Nani hao maadui wa Mwenyezi Mungu (S.W)” Mtume (S.A.W) aliwajibu:
“Hao ni wale ambao wanawahusudu watu katika neema walizoruzukiwa na Mwenyezi
Mungu (S.W)”. Ukirejea katika
historia za Mitume mbali mbali na wafuasi wao, historia za wanasiasa mbali
mbali na wananchi, tofauti na mabara mbali mbali utaona athari za hasada
ziliziathiri Qaumu zote hizo, mayahudi (L.A) walikataa kumuamini na kumfata
Mtume (S.A.W) si kwa lolote ila ni kwa sababu ya husda yao tu juu ya Mtume
(S.A.W) na haya ameyasimulia Mwenyezi Mungu (S.W) katika Qur-a! n aya ya 53-54 ya Suratu-Nnisai: “Au wanayo sehemu ya ufalme wa
(Mwenyezi Mungu (S.W), basi wanahamaki kwa nini kupewa mtu kitu pasina amri
Ubaya
wa hasada katika Jamii
Hasada inapotawala katika jamii yoyote kwanza jamii hiyo itambue kuwa
ishafikiwa na msiba mkubwa sana usiokuwa na mithali na athari za jamii hiyo
itasibiwa na matatizo, ya majanga yakiwemo watu, hawatopendana, hawatosaidiana,
hawatoheshimiana, hawatokuwa na maendeleo yoyote tokea mtu mmoja mmoja hadi jamii yao nzima na maisha yao
watakuwa madhalili na mafukara na mwisho jamii hiyo ima iwe katika kiambo chao,
kijiji chao au nchi yao itakuja kutawaliwa na kuongozwa na wageni ambao hawana
hata tone la ikhlsai na wao katika nyanja zote wao na vizazi vyao.
Mtume (S.A.W) kwa kuielewa uzito na madhara ya gonjwa hili la hasada
katika jamii na inavyofarikisha umoja na kufuta mapenzi katika nyoyo za waja,
na kila saa akisema “Siye katika miongoni mwangu (mtu yeyote) mwenye hasada,
msengenyi na yeyote wa watu wenye sifa hizo” baada ya kusema maneno hayo
alisema aya ya 58 ya Suratul-Ahzab: “Na wale wanaowaudhi wanaume waislam na
wanawake waislam pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka (watu hao wanye
kuwaudhi) wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri”.
Maovu ya hasada yakishakushamiri katika jamii yoyote athari yake ya
mwisho inaua na kukata udugu wa damu na wa nasaba na hii ndiyo hali katika
ulimwengu wa leo iliyozifika familia za kiislam, watu wamekatanakatana, mtoto
hamjui mjomba wala shangazi, maami nao hali kadhalika sasa mapenzi, mahaba na
huruma yatapatikana vipi ikiwa jamii yenyewe imesibiwa na hali hii?
Mtume (S.A.W) amesema: “Hawatoacha watu kuwa katika kheri (na furaha za
maisha) muda wa kwamba hawakuhusudiana”
Madhara
na maafa yatakayomfika mtu mwenye hasada duniani na
akhera.
Kwa hakika mtu mwenye hasada atafikiwa na mambo mengi ambayo
yatamfikisha na kumdumisha katika maisha yake na wala hatofikia daraja ya kuwa
mwema na wala hatokuwa ni mwenye kutunukiwa za kheri na Mwenyezi Mungu (S.W) na
yatosha maneno aliyosema Mtume (S.A.W): “Nakutahadharisheni na hasada, hakika
hasada inakula mema ya mtu kama moto uanavyokula kuni” hiyo ni alama yenye kutujulisha
kuwa mtu mwenye hasada hafikili katika utukufu na daraja za juu iwe duniani au
Akhera. Sayyidha Luqmanul-Hikma (R.A)
katika miongoni mwa wasia aliomuusia mwanawe
Mmoja wa wanavyuoni ameilezea hasada kuwa mtu mwenye kuwa nayo atafikiwa
na mambo manane: atafisidika katika umri wake wote, atakuwa na tabia mbaya na
chafu zisizo na mfano, atakosa shifaa ya Mtume (S.A.W), ataingia motoni,
atapatwa na joto la moyo(presha) na atakufa kiroho, atakuwa kipofu wa moyo
hafahamu chochote katika hukumu za Mwenyezi Mungu (S.W), atanyimwa tunuku na
neema mbali mbali na Mwenyezi Mungu (S.W) na wala hatofikia katika mustakbali
mwema katika maisha yake, hatotajwa kwa wema baada ya kufa kwake.
Kujilinda
na hasada.
Ili mtu asifikwe na gonjwa la hasada itampasa ajilee katika mwenendo
mwema, kwa kusoma elimu njema na pia asuluhiane katika maisha yake na watu
walio wema na shifa kubwa ya kuepukana
na gonjwa hilo ni wajibu awe anaizingaita sana ile hadithi ya Mtume
(S.A.W). Aliposema: “Unapoangalia neema za Mwenyezi Mungu (S.W) basi watizame
alio chini yako…” yaani usiwatizame watu waliokupita kwa
uwezo wa maisha n.k, bali unavyotakiwa uwatizame wale walio chini yako uliowapita
pengine wewe una Baskeli, laikini wangapi leo hawaimiliki, pengine wewe una saa
ya morio ambayo wewe unaiona si nzuri na si ya kisasa lakini kumbuka kuna
wangapi wanatamani sa! a hiyo hiyo uliyokuwa nayo wewe
lakini hawaimiliki hawana uwezo wa kuinunua na wangapi Mwenyezi Mungu (S.W)
amewatunuku uwezo mkubwa wa maisha na wana uwezo wa kununua saa za bei ghali
lakini masikini hawana mkono wa kuvalia saa.
Kwa hiyo ni neema kubwa
Wasia mwengine ni mtu awe na dhana nzuri na wenziwe, akimuona mwenzake
maisha mazuri basi asijenge dhana kuwa ni mustahiki wa kuwa hivyo, au pia
akisikia mwenziwe kateuliwa cheo fulani pia ajenge dhana njema kuwa imemstahiki
fulani kupata cheo hicho n.k, yaani mtu ajitahidi lisimtawale tamko la kwa nini
fulani kupata hivi na hivi katika maisha yake, ataangamia asifanye maskhara.
Nani hasa gonjwa hili la hasada limewakabili?
Gonjwa la hasada limewasibu watu wote ila hasa lilowakabili na saa
yoyote linaweza kuwadhuru kwa upesi sana ni wanavyuoni pamoja na kuwa wao ni
wajuzi sana na haya ameyathibitisha Mwenyezi Mungu (S.W) tokea katika Zaburi ya
Sayyidna Daud (A.S) na pia Mtume (S.A.W) ametwambia katika hadithi mbali mbali,
hasa katika ile hadithi iliyotaja aina sita za watu na sababu za wao kuingizwa
motoni: “Aina sita za watu wataingizwa motoni kabla ya hisabu” masahaba
walimuuliza : “Nani hao ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.W)” Mtume (S.A.W)
aliwajibu: “…Wanavyuoni wataingia motoni kwa sababu ya hasadi”. Ama katika
kitabu cha Mawaidhaul-baligha, Mwenyezi Mungu (S.W) amesema “Ewe mtoto wa adamu inapokuwa vingozi wataingia motoni kwa sababu ya
jeuri, na watu wanaokaa nje ya mji (ndani mashamba huko) wataingia motoni kwa
maasi, na wanavyuoni kwa hasada, na wafanya biash! ara kwa khiyana, na
wapiganaji kwa ujinga, na mafundi kwa ghushi, n a wafanya ibada kwa riya, na
matajiri kwa kibri na amafukara kwa kusema uongo, basi nani ataipata pepo
(yangu) na wala hamuingii peponi ila isipokuwa kwa rehma zangu”.
Hapa tuanpata faida kuwa Iblisi kila kundi la waja amewauzia bidhaa zake
za uovu sasa cha kufanya ni kuwa kila mtu ajitahidi awe kila saa anausafisha
moyo wake ili hili gonjwa la hasada pamoja na maradhi mengine yote ya moyo
yamuepuke Inshaallah kwa rehma za Mwenyezi Mungu (s.W) na kwa jaha ya Mtume
(S.A.W).
Maneno waliyoyasema baadhi ya MaBwana
wema kuhusu hasada akiwemo Bwana wetu, shifaa wa nyoyo
zetu na Mtume wetu Sayyidna Muhammad (S.A.W) ili iwe ni ibra na mazingatio kwa
kila msomaji wa makala hii:
Mtume (S.A.W) amesema: “Haikusanyiki
katika moyo wa muislam imani na hasada”
Imam Sayyidna Hasan bin Al bin Abitalib (R.A) amesema: “Maangamizi ya
watu yapo katika vitu vitatu; kibri, pupa na hasada, kibir ndio maangamizi ya dini
na kwa hili amelaaniwa Iblisi (L.A), pupa ni adui wa roho na kwa hili alitolewa
Sayyidina Adam (A.S) peponi na hasada ndio kiongozi wa maovu yote na kwa hili
Kaabil alimuuwa Habil”.
Imam Sufyan bin Uyayna (R.A) amesema: “Usiwe hasidi utapata baraka na furaha ya maisha na utakuwa mwepesi wa kufahamu
elimu mbali mbali na mambo tofauti”.
Imam Shafi (R.A) amesema: “Watu wote nilioishi nao nimewafurahisha ila
mahasidi zangu sijui niwafanyie nini ili niwafurahishe”.
Sayyid Abdulwarith
(R.A) kila saa akitawambia: “Hasidi hafuzu”.
Maalim Shaaban Robert, mwanawe mwanamke na kuolewa alimtungia utenzi wa
kumuawidh kuhusu maisha na jinsi ya kujiepusha na maradhi ya moyo ili awe nuru
kwa watu, kwa wakwe zake, kwa watoto wake na kwa jamii nzima katika baadhi ya
beti alimuusia kwa kumumbia hivi:
Majivuno hayafai
Yanaleta uadui
Japo mtu humjui
Kumdunisha hatia
Usishiriki uongo
Ijara upate hongo
Mtu muongo msungo
Masuto mengi hupewa
Masuto si mazuri
Yanapunguza kadiri
Jitihada kujibariki
Mbali na madoa.
Inshaallah Mwenyezi Mungu (S.W) atuwafikishe tuwe na
akhlaqi na atutunuku ilhamu ya kujitengeneza nyoyo zetu ili tufikilie katika
ukamilifu wa tabia njema kwa jaha ya Mtume (S.A.W) Amin.