Khalifa aliyezuliwa mengi 1

Nasaba yake. 1

Kutawala kwake. 2

Kupenda kwake wanavyuoni 2

Kulia kwake kila anaposikia mawaidha. 2

Misimamo isiyosahaulika. 4

Misimamo yake alipokuwa Khalifa. 4

Kifo chake. 5

 

Harun Al Rashid

Khalifa aliyezuliwa mengi

Juu ya kuwa Harun al Rashid alikuwa Khalifa wa dola ya Abbasiya aliyepigana jihadi mara nyingi zaidi kupita makhalifa wote wa utawala wa bani Abbas, akateka miji mingi zaidi kuliko makhalifa wote wa kabila lake, akajishughulisha zaidi na elimu pamoja na kuwaheshimu maulamaa kupita makhalifa wote wa dola hiyo, hata hivyo huyu ni Khalifa aliyezuliwa uongo mwingi kupita makhalifa wote wa Kiislamu.

Wamemzulia kuwa eti alikuwa akijishughulisha na wanawake na ulevi, wakamtungia visa vingi visivyosadikika isipokuwa tu kwa wale wenye maradhi ya kusadiki kila wanachokisoma.

Katika waandishi waliompa sifa zinazomsitahikia Khalifa huyu ni Ahmed bin Khalkan aliyeandika yafuatayo ndani ya kitabu chake 'Wafiyat al Aayan'. Aliandika:

"Harun al Rashid alikuwa miongoni mwa makhalifa wenye sifa njema, wanaoheshimika, mwingi wa kusali na kuhiji na kupigana jihadi na kuteka. Alikuwa shujaa na mwenye rai yenye kusibu."

 

Sifa zake njema nyingi juu ya kupenda kwake kuinusuru haki na kuwaheshimu maulamaa na kusikiliza na kufuata nasaha zao zimeandikwa ndani ya vitabu mbali mbali vya historia, na hayakanushi haya isipokuwa tu mwenye kupenda kusoma maneno yaliyobadilishwa na kugeuzwa kwa ajili ya matamanio ya nafsi.

Rudi Juu

Nasaba yake

Jina lake ni Abu Jaafar – Harun al Rashid bin al Mahdi Muhammad al Mansur Abu Jaafar Abdullah bin Muhammad bin Ali bin Abdullah bin Abbas Al Hashimy Al Abbasiy.

Alizaliwa katika mji wa al Riy katika mwaka wa 148 Hijri na wakati huo baba yake ndiye aliyekuwa gavana wa mji huo pamoja na mji wa Khurasan, na mama yake alikuwa akiitwa Um Khaizaran ambaye pia ni mama wa Al Hadiy, kaka yake Harun al Rashid.

Harun al Rashid alikuwa bado mtoto mdogo alipochukuliwa na baba yake ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa jeshi lililofanikiwa kulishinda

jeshi la Roma.

Rudi Juu

Kutawala kwake

Harun al Rashid alipewa ukhalifa baada ya kufariki ndugu yake Al Hadiy usiku wa Jumamosi tarehe 16 Rabiul Awwal mwaka wa 170 Hijri kama alivyousia baba yao, na wakati huo Harun alikuwa na umri wa miaka 22.

Ndani ya usiku huo huo Mwenyezi Mungu alimruzuku Harun al Rashid mtoto wa kiume aliyepewa jina la Abdullah al Maamun, na haijapata kutokea siku katika historia ya Kiislamu ambayo ndani yake siku hiyo hiyo alifariki Khalifa akatawazwa Khalifa na akazaliwa Khalifa.

Harun al Rashid alikuwa mfasihi wa lugha, mwenye elimu na hekima nyingi katika mambo yanayohusu uendeshaji wa nchi, na alikuwa mwingi wa kusali na mwingi wa kutoa sadaka.

Alikuwa akipenda watungaji mashairi na alikuwa akiwalipa vizuri, na alikuwa akipenda kucheza mpira, kurusha mikuki na kupanda farasi na kucheza mchezo wa sataranji 'chess', na inajulikana kuwa yeye ni khalifa wa mwanzo wa Bani Abbas kuucheza mchezo huo.

Rudi Juu

Kupenda kwake wanavyuoni                                                                                        

Harun al Rashid alikuwa akiwapenda sana maulamaa na kuwaheshimu na alikuwa akiheshima kila kinachohusiana na dini na alikuwa hapendi mijadala isiyo na maana na pia hakuwa akipenda maneno mengi yasiyo na faida.

Anasema al Qadhi al Fadhl;

"Sijapata kusikia juu ya Khalifa aliyesafiri kwa ajili ya kutafuta elimu isipokuwa Harun al Rashid aliyesafiri pamoja na wanawe wawili al Amin na Al Maamun mpaka Madina kwa Imam Malik (Mwenyezi Mungu amrehemu) kwa ajili ya kusikiliza sharhi yake ya kitabu cha Al Muwatta"..

Alihuzunika sana zilipomfikia habari za kifo cha Abdullah bin Al Mubarak, na mmoja katika maulamaa aitwae Abu Muawiya ambaye ni kipofu alisema;

"Kila ninapomtaja Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) mbele ya Harun al Rashid humsikia akimsalia akisema 'Allahumma salliy alaa sayidiy', na siku ile nilipomsomea hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) inayosema; 'Natamani nipigane vita katika njia ya Mwenyezi Mungu, kisha niuliwe kisha nihuishwe tena ili nipigane tena na niuliwe tena', Harun al Rashid alilia kwa huzuni sana."

"Siku moja baada ya kumaliza kula", anaendelea kusema Abu Muawiya (Kipofu), "mtu mmoja alikimbilia kunimiminia maji kwa ajili ya kuosha mikono yangu huku akiniuliza; "Unajuwa nani anakumiminia maji? Ni Mimi Harun al Rashid, kwa kwa ajili ya kuiheshimu elimu yako."

Rudi Juu

Kulia kwake kila anaposikia mawaidha

Anasema Mansur bin Ammar; "Sijapa kuona mtu anayelia sana anaposikia mawaidha kupita watu watatu hawa, Al Fudhail bin Iyadh na Harun al Rashid na mtu mmoja mwingine."

Na siku ile Al Fudhali bin Iyadh alipomwambia Harun al Rashid; 'Wewe ndiye mbebaji jukumu la umma huu." Harun alilia sana mpaka akawa anahema.

 

Imenukuliwa kutoka kwa Imam al Qurtuby katika tafsiri yake kuwa mwanamke wa kiyahudi aliyekuwa na shida alijaribu mara nyingi sana kutaka ruhusa ya kuingia  katika kasri ya Khalifa Harun al Rashid apate kumuelezea shida zake, lakini walinzi hawakumruhusu kuingia, na siku moja akabahatika kumuona Haruna al Rashid akitoka akiwa juu ya farasi, akamsogelea na kumwambia; "Muogope Mwenyezi Mungu ewe Harun al Rashid!"

Kusikia maneno hayo Harun al Rashid akateremka moja kwa moja kutoka juu ya farasi wake na kusujudu, kisha akaamrisha mwanamke huyo akidhiwe haja zake zote.

Watu wakamuuliza;

"Ewe Amiri wa Waislamu, umeteremka kutoka juu ya farasi wako kwa ajili ya maneno ya mwanamke wa kiyahudi?"

Harun akasema;

"Sivyo, bali nimeteremka nilipoikumbuka kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo; 'Na wanapoambiwa. "Mcheni Mwenyezi Mungu," mori wao huwapeleka zaidi kwenda kufanya madhambi hayo. Basi Jahannam inawatosha (kuwatia adabu). Napo ni mahali pabaya kabisa pa kutengenezewa  kiumbe."

Al Baqarah – 206

 

Imepokelewa kuwa siku moja Ibni Sammak alipokuwa akimimina maji katika gilasi ya Harun al Rashid akamuuliza;

"Ewe Khalifa wa Waislamu! Iwapo duniani hapana maji mengine isipokuwa haya utakuwa tayari kuyanunua kwa kiasi gani?"

Harun al Rashid akasema;

"Nusu ya mali yangu yote."

Akamwambia;

"Kunywa Mwenyezi Mungu akubariki nayo."

Na alipomaliza kunywa akamuuliza:

"Ikiwa maji haya uliyokunywa yatazuilikia tumboni mwako yasiweze kutoka utakuwa tayari kutoa kiasi gani ili yatolewe?"

Akasema;

"Ufalme wangu wote."

Akamwambia;

"Ufalme thamani yake maji na mkojo sina haja nao."

Harun al Rashid akalia sana.

 

Anasema Ibni l Jawzi;

"Siku moja Harun al Rashid alimwambia Sheiban; 'Niwaidhi.' Sheiban akamwambia;

'Upae sahibu mwenye kukutisha ukasalimika ni bora kuliko kuwa na sahibu mwenye kukusifia akakutia mashakani.'

Haruna al Rashid akamwambia;

"Nishereheshee."

Akamwambia;

"Mwenye kukuambia; Wewe ndiye mbebaji jukumu la raia hawa kwa hivyo muogope Mwenyezi Mungu ni bora kwako kuliko mwenye kukuambia; Nyinyi watu wa Ahlul Bayt mumekwisha samehewa madhambi yenu na kwamba nyinyi ndiyo wenye haki ya kutawala."

Harun akalia kwa furaha.

Rudi Juu

Misimamo isiyosahaulika

Katika mwaka wa mia na themanini na saba ilimfikia Harun al Rashid barua kutoka kwa mfalme wa Waroma Naghfur ikivunja mkataba na ahadi waliyokubaliana baina ya Harun al Rashid na mfalme wa Roma mwanamke aitwae Rene aliyetawala kabla yake.

Barua hiyo iliandikwa ifuatavyo;

"Kutoka kwa Naghfur mfalme wa Roma kumfikia Harun al Rashid mfalme wa Waarabu. Amma baad, kwa hakika mfalme aliyetawala kabla yangu alikuwa akikupa wewe mali nyingi na akijipa nafsi yake starehe nyingi, kama unavyojuwa udhaifu wa wanawake na ujinga wao, basi ukeshaisoma barua yangu rudisha mali yote aliyokuletea, ama sivyo basi kitakachohukumu baina yetu ni panga."

Uso wa Harun al Rashid ulibadilika kwa ghadhabu baada ya kuisoma barua hiyo hata waliokuwa pamoja naye katika majlis ile walianza kutawanyika kwa hofu, baada ya kumuona Harun al Rashid akiinuka, na kumwita waziri wake huku akimuambia:

"Lete kidawati cha uwino na kalamu kisha andika yafuatayo;

"Bismillahi Rahmani Rahiym, kutoka kwa Harun al Rashid Khalifa wa Waislamu, imfikie Naghfur Mbwa wa Roma! Nimeisoma barua yako ewe mwana wa kikafiri na jawabu utaiona na wala hutoisikia."

Harun al Rashid akatayarisha jeshi kubwa na kuondoka nalo mpaka alipoufikia mji wa Heracles na kuuteka , kisha akamlazimisha Naghfur atie sahihi ya kulipa fidia kila mwaka.

 

Imepokelewa kutoka kwa Al Sauly kutoka kwa Yakub bin Jaafar kuwa katika mwaka alotawazwa Harun al Rashid alimuota Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akimwambia;

"Mambo yatakuendea vizuri, kwa hivyo teka miji, nenda kahiji na uwagawie mali watu wa Makka na Madina .

Harun al Rashid akafanya kama alivyoambiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), akaifunga safari katika mwezi wa Shaabani mwaka wa mwanzo wa ukhalifa wake, akateka miji mingi ya Roma kisha akaelekea moja kwa moja mpaka Makka kwa ajili ya kuhiji, kisha akenda Madina, na kote huko aligawa mali nyingi sana kwa wote wanaostahiki

Rudi Juu

Misimamo yake alipokuwa Khalifa

Amehiji mara nyingi na ameteka miji mingi ya makafiri.

Anasema Al Masuudiy katika kitabu chake 'Muruuj al Dhahab':

"Harun al Rashid alikuwa na nia ya kuendelea kuteka na kuifanya dola ya Kiislamu kuwa kubwa kuanzia bahari ya Roma hadi bahari ya Qalzam."

 

Katika mwaka wa 175Hijri alimchaguwa Al Ghatrif bin Ataa kuwa gavana wa Khurasan na akamchaguwa Jaafar Barmaki kuwa gavana wa Misri, na katika mwaka huo vilishtadi vita baina ya makabila ya Al Qisiya na Al Yamaniya katika nchi ya Sham na chuki baina yao iliongezeka.

Majeshi ya Harun al Rashid yakiongozwa na Yahya al Barmaki yalifanikiwa kuiteka miji ya Qazwin na miji iliyo karibu na nchi ya Urusi.

Katika Ramadhani ya mwaka 179 H. Harun al Rashid alifanya Umra na akabaki Makka mpaka musimu wa Hijja, akahiji akitembea kwa miguu kutoka Makka mpaka Arafat na Muzdalifa na Mina nk.

Kutoka hapo akaingia vitani tena na kufanikiwa kuiteka miji mingine ya Roma, akauteka mji wa Safsaf na Ankara, kisha mwaka uliofuata akahiji tena akifuatana na wanawe wawili Al Amin na Al Maaamun, na baada ya hapo Jaafar al Barmaki pamoja baba yake wakafanya khiana juu ya kuwa Haruna al Rashid aliwaokowa walipotaka kuuliwa kisha akawapa vyeo vikubwa katika ukhalifa wake, akahukumu Jaafar auliwe na baba yake atiwe jela.

Na katika mwaka huo huo majeshi ya Harun al Rashid chini ya uongozi wa Abdul Rahman bin Abdul Malik bin Saleh al Abbasi yaliuteka mji wa Dibsah.

Na katika Ramadhani ya mwaka 179 Harun al Rashid alifanya tena Umra na akabaki na nguo zake za Ihram mpaka ulipoingia musimu wa Hija, akahiji tena kwa miguu yake kutoka Makka hadi Arafat na kurudi tena Makka.

Kifo chake

Harun al Rashid alifariki dunia akiwa vitani katika mji wa Al Tuss uliopo Khurasan siku ya tarehe tatu mwezi wa Jamadil Akhira mwaka wa 193H akiwa na umri wa miaka 45 na zipo riwaya zinazosema kuwa alikuwa na umri wa miaka 48, akazikwa huko na kusaliwa na mwanawe Al Saleh.

Rudi Juu