FUNGA YA SITA

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

 

Shukrani zote ni zake Mwenyezi Mungu. Tunashuhudia ya kwamba hapana mola anaepaswa kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni Mtume wake. Ameufikisha ujumbe na kuituwa amana, kwa hivyo tunakuomba Mola wetu umsalie na kumsalimu Mtume wako huyu mtukufu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pamoja na Ali yake na Masahaba Wake Watukufu - Aamin.

Amma baad,

Saumu ni Ibada ambayo nguzo zake ni mbili;

Ya  Kwanza ‘Nia’

Ya Pili ni ‘Kujizuwia na kila kinachofungulisha kuanzia inapoingia Alfajiri mpaka linapozama jua.’

 

Baadhi Ya Hadithi Zinazozungumzia Juu Ya Umuhimu Wa Saumu

 

1.     Katika hadithi Al Qudsy,  Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) anasema;

"Mwenyezi Mungu anasema, 'Ibada za mwanadamu zote ni zake isipokuwa Saumu, hiyo ni Yangu, na Mimi ndiye ninaetoa jazaa yake…(Malipo yake)'

Imam Ahmed na Muslim na Annasai

 

2.     Anasema Abi Amama  (Radhiya Llahu anhu)

“Nilimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) nikamwambia, 'Niamrishe juu ya Ibada itakayoniingiza Peponi'.

Akanambia; 'Pendelea kufunga, kwa sababu (Ibada) hiyo haina mfano. Nilipomwendea mara ya pili, akanambia;

‘Endelea kufunga".

Ahmad , Annasai na Al Hakim .

 

3.     Kutoka kwa Abi Saeed Al Khodary  (Radhiya Llahu anhu) anasema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

"Mja anapofunga siku moja katika njia ya Mwenyezi Mungu (kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu), basi Mwenyezi Mungu anamuepusha  na Moto wa Jahannam umbali wa Miaka Sabini"

Maimam wote wa Hadithi isipokuwa Abu Daood.

 

4.     Imepokelewa kutoka kwa Sahal bin Saeed  (Radhiya Llahu anhu) kwamba Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

,"Hakika Pepo ina mlango uitwao Ar Rayaan. Siku ya Kiama patasemwa; "Wako wapi wafungaji?" Wakeshaingia wafungaji wote (kupitia mlango huo), mlango utafungwa".

Bukhari na Muslim.

 

Sheikh Shaarawi (Mwenyezi Mungu amrehemu) alitoa mfano wa mtu anayependa kujikurubisha kwa Mola wake kwa kupiga mfano wa baba mwenye watoto wawili. Mmoja kati yao hapendi kutumika mpaka atolewe ukali na kukaripiwa. Ama mwingine, yeye hupenda kutumika na kila mara hujipendekeza  kwa wazee wake kwa kuuliza iwapo pana utumwa wowote ule, na pale anapotumwa basi huenda haraka sana.

Anasema Sheikh Shaarawi;

"Bila shaka baba atampenda yule mtoto anayependa kujikurubisha kwake. Mfano huu ni mfano wa mtu mzito wa kutimiza Ibada zake za Fardhi. Bila shaka huyu ni bora kuliko yule asiyetimiza Ibada zake kabisa. Lakini yupo mwingine anayetimiza Ibada alizofaridhishiwa kisha huongeza kwa kufanya Ibada nyingine za Sunna.

Bila shaka huyu wa pili atapendwa  zaidi na Mola wake.”

(Mwisho wa maneno ya Sheikh Shaarawi)

 

Na hii ni tafsiri ya hadithi ya Al Qudsy ambayo ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) anasema;

"Mwenyezi Mungu anasema;

“Atakayemfanyia uadui kipenzi changu nitamtangazia vita. Na mja wangu hajisogezi kwangu kwa jambo ninalolipenda kuliko lile nililomfaridhishia. Na mja wangu huwa anaendelea kujisogeza kwangu kwa Ibada za Sunna, mpaka Nimpende, na Nitakapompenda, basi Mimi Nitakuwa ndiyo masikio yake anayosikilizia (Hatopenda kusikiliza isipokuwa Ninayoyapenda) na macho yake anyoyaonea (Hatopenda kutizama isipokuwa Ninayoyapenda) na mkono wake anaoutumia (Hatopenda kuutumilia isipokuwa katika yale Ninayoyapenda) na miguu yake anayoiendea, (Hatopenda kwenda isipokuwa katika yale Ninayoyapenda) na anaponiomba, Nitampa, na anapotaka ulinzi wangu, Nitamlinda."

Bukhari.

 

Saumu Ya Siku Sita Katika Mwezi Wa Shawaal

Tukirudi katika maudhui yetu ya Saumu ya Siku sita katika mwezi wa Shawaal, anasema Sheikh Sayed Sabiq katika kitabu chake kiitwacho ‘Fiq -hi Sunnah’ kwamba wamesimulia Maimam wote wa Hadithi isipokuwa Bukhari kuwa; Ameelezea Abu Ayoub Al Ansari  (Radhiya Llahu anhu) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

"Atakeyefunga Mwezi wa Ramadhani kisha akafuatilia (kufunga) siku sita katika mwezi wa Shawaal, (anakuwa) kama aliyefunga maisha yake yote,”

 

Na hii ni kwa sababu mtu anapofunga mwezi mmoja wa Ramadhani, anapata thawabu ya kufunga miezi kumi, kwa sababu mtu anapotenda jema moja hulipwa kumi badala yake. Na anapofunga siku sita katika Shawwal, anakuwa mfano wa aliyefunga siku sitini. Ukijumlisha funga ya Ramadhani na funga ya sita, unapata miezi kumi na miwili, na kwa ajili hiyo anakuwa mfano wa aliyefunga mwaka mzima. Na mtu anapoendelea hivyo maisha yake yote anakuwa mfano wa anayefunga maisha yake yote”.

 

NAMNA YA KUFUNGA

Imam Annawawi ambae ni katika Maulamaa wakubwa wa madhehebu ya Imam Shafi anasema;

"Ni vizuri kufunga siku sita mfululizo mara tu baada ya kumalizika sikukuu ya mwanzo, na atakayefunga siku sita mbali mbali katika mwezi wa Shawaal , pia inakubaliwa”.

Amma Imam Ahmed bin Hanbal anasema;

“Ukifunga mfululizo au ukizifunga siku sita tofauti katika mwezi wa Shawaal yote ni sawa tu.”

 

Maulamaa wanasema kuwa;

‘Lazima mtu atimize Ramadhani yake kwanza, ndiyo aweze kufunga sita. Yaani ikiwa mtu anadaiwa katika Ramadhani, basi lazima alipe kwanza deni lake lote kisha ndio afunge sita.’

Na hii ni tafsiri ya kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema;

ATAKAYEFUNGA Mwezi wa Ramadhani KISHA akafuatilia (kufunga) siku sita…”

Wakasema kuwa kutokana na kauli hii, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hapa anasisitiza kuwa mtu lazima kwanza afunge Mwezi wa Ramadhani, KISHA afunge sita. Na ikiwa mtu ana deni la kufunga, basi huyo anakuwa hakufunga mwezi wa Ramadhani, na kwa ajili hiyo ikiwa anazitaka thawabu zilizotajwa katika hadithi hiyo, basi inampasa kulipa deni lake kwanza, kisha ndiyo afunge sita.

 

Wallahu taala aalam

Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh