FUNGA YA RAMADHANI, HUKUMU, FADHILA
NA ADABU ZAKE
IBRAHIM A.H.GHULAAM
ÇáÍãÏ
ááå ÑÈ ÇáÚÇáãíä æ ÇáÕáÇ É æ ÇáÓáÇ ã Úáí äÈíäÇ
ãÍãÏ æÚáì Âáå æÕÍÈå, æ ÈÚÏ:
UTANGULIZI.
Baada ya kumshukuru Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumtakia rehma na
amani Mtume wetu [Swallah Llahu alayhi wa
sallam] pamoja na Ali
zake na Maswahaba zake wote .
Basi kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu
(Subhaanahu wa Ta’ala) amejaalia kwa waja wake miongo [misimu] ya
kuzidisha ndani yake matendo mema na Mwenyezi
Mungu (Subhaanahu wa
Ta’ala) huzidisha pia malipo ya matendo
hayo kwa waja
wake , na miongoni mwa miongo hiyo ni
huu mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Basi katika makala hii nitaelezea kwa ufupi juu ya funga na yale yanayoambatana nayo ikiwa ni pamoja na hukumu, fadhila na adabu zake.
Ninamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) awanufaishe waislamu kwa yale nitakayoyaelezea, na aturuzuku
ikh-laswi [kutaka radhi zake pekee] katika matendo yetu yote, amiiin.
Na kwake pekee ndio kwenye mafanikio ya dunia na
akhera.
MAANA YA FUNGA
Neno swaumu ambalo ni funga katika lugha ya kiswahili,
kilugha lina maana ya kujizuilia . Ama katika
sheria funga [swaumu] ni kumuabudu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu
wa Ta’ala) kwa kujizuilia na vyenye kufuturisha [kufunguza] kuanzia
kudhihiri alfajiri [ya pili] mpaka kuchwa [kuzama]
kwa jua na kwa kunuilia
kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).
HISTORIA YA FUNGA
Kwa hakika funga si ibada ngeni, bali ni ibada iliyofaradhishwa kwa umati zilizotangulia na pia
kufaradhishwa katika umati huu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {{Enyi mlioamini! mmelazimishwa kufunga [saumu]
Ama katika umati huu wa Muhammad [Swallah Llahu alayhi wa sallam.] funga
ilifaradhishwa katika mwezi wa Shaabani mwaka wa pili baada ya hijrah
(2H).
HUKUMU YA FUNGA.
Funga ya mwezi wa Ramadhani
ni nguzo katika nguzo za Uislamu, nayo ni wajibu
kwa dalili ya kitabu (Qur-an), Sunnah na Ijmai (makubaliano) ya wanavyuoni
wote wa Kiislamu.
1: Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala): {{Enyi
mlioamini mmelazimishwa kufunga (saumu)
mwezi wa Ramadhani
ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Qurani ili iwe uwongozi kwa watu, na
hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi
(wa baina ya haki na batili) Atakae kuwa katika mji katika huu
mwezi (wa Ramadhani)afunge. …}(2:183-185)
.
2: Na imepokewa hadithi kutoka kwa Abdullah ibn ‘Umar (Radhiya Llahu anhu)
amesema : Nimemsikia Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam.) akisema: “Umejengwa Uislamu juu ya
nguzo tano; kushuhudia ya kwamba hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kwamba hakika ya Muhammad (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) ni mtume
wa Allah(Subhaanahu wa Ta’ala) na usimamishaji Swalah na utoaji zakah na kuhiji katika nyumba
(tukufu) ya alkaaba na funga ya ramadhani. (Al Bukhariy na
Muslim).
Na kuna hadithi nyingine nyingi
zinazojulisha wajibu huo, na wanavyuoni wote
wamewafikiana juu ya uwajibu huo.
INAE MUWAJIBIKIA FUNGA YA RAMADHANI.
Funga ya Ramadhani inamuwajibikia
kila Muislamu, baleghe, mwenye akili, alie
katika mji wake (asiwe msafiri), mwenye siha (afya- asiwe mgonjwa), asiwe na mambo yanayozuia kusihi kwa funga (
*Na inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga
watoto wao wanapofikia umri wa miaka saba(7) na kuwalazimisha hadi
ikibidi kuwapiga wanapofikia umri wa mika kumi(10), na hili inabidi
pia kuzingatia afya na ukuaji wa mtoto.
NYUDHURU ZA KUFUNGA
Nyudhuru za kuacha kufunga zinatofautiana na kila udhuru una hukumu
yake, na hapa nitazielezea nyudhuru hizo kwa ufupi.
1-
Hedhi
(damu ya mwezi) na nifasi (damu ya uzazi), huu ni
udhuru ambao unamlazimisha mwanamke kuacha kufunga, na inakuwa haramu kwake
funga na iwapo atafunga haitosihi
(haitokubaliwa) funga
yake, na ni wajibu kwake kulipa funga hiyo.
2-
Maradhi
au Safari. Na mwenye udhuru wa maradhi (yanayotibika
kwa kawaida) pamoja na msafiri wanaruhusiwa kutokufunga na itawawajibikia
kulipa. Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala):{{Atakaye kuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani)
afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi (atimize) hisabu (ya siku alizoacha kufunga) katika siku nyingine.
Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.. .}} (2:185).
Na
*Ama safari ambayo inaruhusiwa kwa sababu yake kutokufunga wanachuoni wengi wemesema: Ni safari ya siku mbili kwa ngamia au kwa mwendo wa miguu (mar-hala mbili) ambayo ni sawa na umbali wa takiribani kilomita (85km). Na ruhusa hii inapatikana kwa msafiri anayesafiri kwa chombo cha aina yoyote atakachosafiria,ijapo kwa dhahiri safari hiyo haimpi uzito wowote.
3-
Vizee (vikongwe) na wenye
maradhi sugu (yasiotarajiwa kupoa). Na haya mawili iwapo yana
msababishia madhara basi ni katika udhuru na
ruhusa ya kuacha kufunga, na itamlazimikia atoe fidia kwa kumlisha masikini
kibaba
(mudi) cha chakula (ambacho ni sawa na na uzito wa
gramu 600g takiribani)au chakula
kinacho mshibisha masikini
mmoja kwa kila siku aliyoacha kufunga.
4-
Waja wazito na wanyonyeshaji.
Nao ni katika wenye ruhusa ya kutokufunga, na
inawabidi kulipa siku walizoshindwa kufunga kwa sababu ya udhuru huo.
5:Iliemzidia njaa au kiu na akahofia
kuangamia, huu pia ni katika udhuru wa kuacha kufunga, bali wamesema wanachuoni
kwamba: yule mwenye kuhofia kuangamia
inakuwa kwake ni
wajibu kufungua, na itamuwajibikia kulipa
NGUZO ZA FUNGA
1-
Nia
nayo ni kukusudia kufunga usiku wa kuamkia funga, kwa funga
ya faradhi.
2-
Kujizuilia
na vyenye kufunguza (kufuturisha).
3-
Muda
wa kufunga (mchana kuanzia alfajiri mpaka kutwa (kuzama) kwa jua).
UNAVYOTHIBITI KUINGIA MWEZI WA RAMADHANI
1-
Kwa
kukamilika siku thelathini (30) za mwezi wa shaabani.
2-
Kwa kuonekana mwezi mwandamo siku ya 29 ya mwezi wa Shaabani,
imepokewa hadithi na Abu Hurayrah (r.a.) kwamba Mtume
(Swallah Llahu alayhi wa sallam.) amesema: {Fungeni
kwa kuonekana kwake (mwezi mwandamo) na fungueni kwa kuonekana kwake} (Al Bukhariy na Muslim).
*Na mwezi wa kuingia Ramadhani inatosha kuonekana
na Muislamu mmoja mwadilifu ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni lazima uonekane na Waislamu
waadilifu wawili au zaidi.
YANAYO BATILISHA (KUHARIBU) FUNGA
1-
Kula
au kunywa kwa kukusudia.
2-
Kila
kinachoingia tumboni au kooni kwa kukusudia.
3-
Kukutana
kimwili (kuingiliana) kati ya mume na mke.
4-
Kujitoa
manii (mbegu za uzazi) au kusababisha kutokwa na manii
(kwa kujichezea sehemu za siri, kukumbatiana au kupigana mabusu nakadhalika).
5-
Kujitapisha
kwa makusudi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah (r.a.) amesema:
amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam):
{...na
mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa.}
(wameipokea maimamu watano).
6- Kutokwa na damu ya mwezi (hedhi) au damu ya uzazi (nifasi).
*Wakati wowote yanapomtokea
mwanamke mawili hayo funga yake ya siku hio itakuwa imeharibika na itamlazimikia kuilipa siku hio baada ya mwezi wa
Ramadhani.
YASIO FUNGUZA
1-
Kula au kunywa kwa kusahau.Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Mwenye kusahau nae amefunga, basi
akala au akanywa na aikamilishe funga yake….} ( Al Bukhariy na Muslim ).
2- Kusukutua au kupandisha maji puani wakati wa
udhu (bila ya kubalighisha).
3-
Kuoga au kujiburudisha kwa kujimwagia maji
katika kiwiliwili (hasa katika maeneo yenye joto kali).
4-
Kuonja chakula kwa mpishi (kwa sharti ya kutokumeza alichokionja).
5-
Kutokwa na mbegu za uzazi (manii)katika usingizi (ndoto) au bila ya kukusudia.
6-
Kuamka na janaba.Imepokewa hadithi kutoka kwa
Mamama `Aishah na Ummu Salamah (Radhiya
Llahu anhuma) kwamba Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akiamka na janaba
kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anaoga na kufunga (Al Bukhariy
na Muslim).
7-
Kupiga mswaki (wakati wowote).
8-
Kuchoma sindano ya kawaida ya tiba.
9-
Kung`oa jino na mfano wake.
10-
Mwanamke kuamka kabla ya kuoga kwa hedhi au
nifasi.
ADABU ZA FUNGA
BAADHI YANAYOSUNIWA KWA MFUNGAJI
1-
Kula daku. Imepokewa hadithi kutoka kwa Anas ibn Maalik (Radhiya Llahu
anhu) amesema:
amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Kuleni daku kwani hakika chakula cha daku
kina baraka ndani yake} (Al Bukhariy na Muslim).
*Na inasuniwa kuchelewesha kula daku mpaka kukaribia alfajiri.
2-Kuharakisha kufutari (mara tu likizama jua). Imepokewa hadithi kutoka kwa
Sahl ibn Saad (Radhiya
Llahu anhu),
Hakika Mjumbe wa Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema: {Watu watakuwa bado wapo katika
kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari}.( Al Bukhariy na Muslim).
*Na inasuniwa (kuanza)
kufutari kwa tende au maji. Imepokewa hadithi
kutoka kwa Salmaan ibn`Aamir (Radhiya Llahu anhu) kutoka
kwa Mtume
(Swallah Llahu alayhi wa
sallam.)amesema: {Anapofutari mmoja wenu basi na afuturu kwa tende na kama hakupata (tende) basi na afutari
kwa maji kwani hakika ya maji ni kitoharisho (kisafisho)
( Wameipokea Maimamu
watano).
*Na pia inasuniwa kwa mfungaji kuzidisha kuomba dua na hasa wakati wa kufutari,kwani dua ya mfungaji na hasa wakati wa
kufutari ni katika dua zinazokubaliwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).
BAADHI YANAYOTAKIWA AYAKITHIRISHE MUISLAMU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI
1-
Kisimamo
cha usiku (Swalah ya tarawehe), amesema Mtume
(Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Mwenye kusimama (kwa ibada) katika mwezi wa Ramadhani
kwa imani (thabiti) na hali ya kutaraji malipo toka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa yale aliyoyafanya katika madhambi yake}. (Al Bukhariy na
Muslim).
*Na inafaa kwa wanawake kuhudhuria Swalah katika misikiti maadamu watachunga na
kufuata taratibu za dini (sharia), amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Msivizuilie
vijakazi vya Mwenyezi Mungu (wanawake) (kuhudhuria ibada) katika misikiti ya Mungu}.(Al Bukhariy na
Muslim).
Na haifai kwa wanaume kuwazuilia wanawake walio katika
usimamizi wao kuhudhuria ibada hizo bila ya kuwa na sababu
za kimsingi zinazo kubalika
kisheria, amesema Mtume(Swallah Llahu alayhi wa sallam):
{wakiwaombeni ruhusa wanawake zenu kwenda msikitini basi waruhusuni}. (Muslim).
2-
Kuzidisha
kusoma Quran.
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Quran
na ndio mwezi ulioteremshwa ndani yake Quran, Amesema
Allah(Subhaanahu wa Ta’ala):{{Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika laylatul-Qadr
(usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa ramadhani).}} (97:1). Na {{(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni
mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii
Qurani…}} (2:185).
3-
Sadaka. Pamoja na fadhila zake katika masiku yote
huzidi fadhila na thawabu zake katika mwezi wa Ramadhani. Amesema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llahu anhu): Alikuwa Mtume (Swallah
Llahu alayhi wa sallam.) mkarimu (mtoaji) na
alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi wa Ramadhani
wakati anapokutana na Jibriyl (a.s.) (Al
Bukhariy na Muslim).
*Na katika sadaka zinazotiliwa mkazo katika mwezi wa Ramadhani ni kuwafuturisha
waliofunga, amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Mwenye
kumfutarisha aliyefunga anakuwa na malipo mfano
wa malipo ya aliyemfutarisha na hayapungui
malipo ya aliyefunga kitu chochote}. (Ahmad na Annasaiy).
4-
Kufanya
Umrah, amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Umrah katika mwezi wa Ramadhani una malipo
sawa na Hijjah}. (Muslim).
5-
Itikafu
(nako ni kubaki msikitini bila ya kutoka ukijishughulisha
na ibada mbalimbali), inasuniwa kufanya itikafu na
hasa katika
kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Imepokewa hadithi
kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Llahu anhu) amesema: Alikuwa Mtume(Swallah Llahu
alayhi wa sallam.)
akifanya itikafu siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhani.(Al
Bukhariy na Muslim).
6- Kuutafuta
usiku wa cheo (laylatul-qadr), na zaidi katika kumi la
mwisho la Ramadhani, imepokewa hadithi kutoka
kwa Mama ‘Aishah (Radhiya Llahu anha) amesema: Amesema Mtume
(Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Utafuteni usiku wa cheo (laylatul-qadri) katika siku kumi za mwisho
za Ramadhani}
(Al Bukhariy na Muslim).
Na amepokea Abu Hurayrah (Radhiya
Llahu anhu) kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa
sallam) amesema: {Mwenye kusimama
katika usiku wa cheo (laylatul-qadri) kwa imani thabiti na kwa kutaraji malipo
kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa madhambi alioyafanya (kabla ya
hapo)}. (AlBukhariy na Muslim).
7- Toba. Nako ni kurudi kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na makosa aliyoyatenda mja na kuomba msamaha kutoka kwake, kujuta na kuazimia kutokuyarudia tena makosa hayo).
*Tukumbuke ya
kwamba Mwanaadamu si mkamilifu daima yupo katika hatari ya kufanya makosa, sawa
makosa hayo ikiwa ni makosa ambayo ameyahisi au hakuyahisi wakati
wa kuyafanya kwake, toba ndio njia ya kujikosha na madhambi ya makosa hayo,na kipindi cha mwezi wa Ramadhani
ni fursa muhimu ya
kutubia.
* Ikiwa katika makosa yake kuna haki za
wanaadamu inamlazimu kuzirejesha
kwa wenyewe
haki
hizo.
FADHILA ZA FUNGA
Zimepokewa Hadithi nyingi
1- Amesema Mtume(Swallah Llahu alayhi wa sallam): {Mwenye kufunga Ramadhani
kwa imani na kutarajia malipo (toka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)) husamehewa madhambi
aliyoyatanguliza}. (Al Bukhariy na Muslim).
2-
Na amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): {amesema Allah (Subhaanahu
wa Ta’ala): Kila amali ya
mwanaadamu (aifanyayo) ni yake,
wema (mmoja) hulipwa kwa mfano wake mara
kumi mpaka mara mia saba, isipokuwa funga,
hakika ya funga ni Yangu
mimi, na Mimi
najua namna gani Nimlipe kwa funga hiyo, ameacha matamanio yake na chakula
chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu,
mfungaji ana furaha mbili, furaha wakati wa kufutari kwake na furaha
nyengine pale atapokukutana na Mola wake. Harufu yakinywa cha mfungaji
inapendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko
harufu ya miski}. (Al Bukhariy na Muslim).
YANAYOPASWA KUJIEPUSHA NAYO
MFUNGAJI.
1- Tabia chafu na maneno maovu,
2-
Kuzidisha usingizi (kulala kupita kiasi) ambao unampotezea
Muislamu fursa ya kufanya ibada zaidi.
3-
Kupoteza wakati mwingi katika michezo na
maongezi yasiyo na faida, na kuacha kuutumia wakati huo katika kazi na ibada
mbali mbali.
4-
Kuacha kula daku au kuchelewa kufuturu baada ya kutwa kwa
jua.
5-
Kufanya israfu katika vyakula na vinywaji
wakati wa kufutari.
6-
Kufutari kwa vyakula vyenye harufu ya
kuchukiza,
7- Kutokuswali tarawehe kwa utulivu na
unyenyekevu.
YANAYOTAKIWA
KWA KUMALIZIKA RAMADHANI.
1-
Kutoa zakatul-fitri,nayo ni wajibu kwa kila Muislamu, (mwanamume,
mwanamke, mkubwa, mdogo, muungwana (huru) au mtumwa).*Watoto wadogo,Watumwa na
pia Wanawake waliochini ya usimamizi wa Wanaume itawalazimikia zakah hio
wasimamizi wao, ama Wanawake wanaojitegemea itawalazimikia wao wenyewe.
*Na inatakikana itolewe zakatul-fitri
kabla ya Swalah ya iddi.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Llahu anhu) amesema: Amefaradhisha
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam.) Zaka ya fitri (ya kumalizika Ramadhani) pishi ya tende au pishi ya shairi kwa
mtumwa na huru (muungwana), mume na mke, mdogo na mkubwa katika waislamu, na
akaamrisha (hiyo zakah ya fitri)
itolewe kabla ya kutoka watu kuelekea katika Swalah
(ya iddi). (Al
Bukhariy na Muslim).
*Na
wajibu ni kutoa pishi ya chakula maarufu
katika mji uliopo
(ambayo ni sawa na uzito wa kilo mbili na gramu mia nne (2.4 kg) takribani kwa
nafaka kama mchele na mfano wake) (au thamani
yake kwa baadhi ya wanachuoni).
2-
Takbir, inasuniwa kuleta takbir baada ya kuandama (kuonekana) mwezi wa kumalizika Ramadhani,
kuanzia kuchwa (kuzama) kwa jua mpaka wakati wa Swalah
ya iddi. Na inasuniwa kunyanyua sauti kwa wanaume njiani, masokoni na hata majumbani.
3- Swalah ya iddi, kwa wanaume na wanawake.
*Na inasuniwa ifanyike
katika viwanja, na hata akina mama walio katika siku
zao (hedhi) inasuniwa na wao wahudhurie ingawa
wao hawatoshiriki katika kuswali.
4-
Na inasuniwa kula tende kwa idadi ya (witri) au chakula chengine hafifu kabla ya kutoka kwa ajili ya Swalah ya iddi al-fitri.
5-
Pia inasuniwa kubadilisha njia wakati wa kwenda
na kurudi kwenye Swalah ya iddi. Imepokewa
hadithi kutoka kwa Jaabir (Radhiya Llahu anhu) amesema: Alikuwa Mjumbe wa Allah (Swallah Llahu alayhi wa sallam) inapokuwa siku ya iddi
akibadilisha njia (ya kwenda na ya kurudia). (Al Bukhary).
6-
Kuvaa
mavazi bora zaidi anayoyamiliki Muislamu.
*Na inatakikana kwa wale
wenye familia kuwaandalia mavazi mazuri watu wa familia zao (bila ya kufanya
israfu).
7-
Na pia inasuniwa baada ya kumalizika Ramadhani
kufunga siku sita katika mwezi wa mfunguo mosi
(shawwali). Amesema Mtume (Swallah Llahu alayhi
wa sallam): {Mwenye kufunga Ramadhani kisha akaifuatilizia siku
sita katika mwezi wa shawwali (mfunguo mosi)
inakuwa
8- Na tukumbuke ya kwamba siku hii ya iddi inakatazwa (ni haramu) kufunga ndani yake. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Said Al khudriy (Radhiya Llahu anhu):( Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amekataza kufunga katika siku mbili: Siku ya (iddi) alfitri na siku ya (iddi) ya kuchinja (iddi l-adh`ha)).(Al Bukhariy na Muslim).
MWISHO.
Namalizia makala hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) alie niwezesha kufanikisha lengo langu hili.
Na kisha natoa shukurani zangu za dhati kwa wale wote waliochangia kwa njia moja au nyengine kukamilika kwa makala hii.
Na ninamuomba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) atupe kila la kheri hapa duniani na kesho akhera. Amiin.
æÕáì Çááå Úáì äÈíäÇ ãÍãÏ æÚáì  áå æÕÍÈå æÓáã .
*KILA MTU ANAYO HAKI NA ANASHAJIISHWA KUSAMBAZA MAKALA HII KWA NJIA YEYOTE ITAKAYO KUWA RAHISI KWAKE KWA SHARTI LA KUTO KUIFANYIA MAREKEBISHO YEYOTE KABLA YA KUWASILIANA NA MTAYARISHAJI WA MAKALA HII.
*UKIWA NA MASWALI MAPENDEKEZO MAREKEBISHO AU AINA YEYOTE YA USHAURI, WASILIANA NAMI KWA ANUANI IFUATAYO:
IBRAHIM
ALLY HAMAD GHULAAM
P.O
SIMU NAMBARI:
BARUA PEPE: ibralhamd2000@yahoo.co