FUNGA/ SAUMU

Na Hamzah Z. Rijaal

 

Wengi wetu wanajiuliza kawanini tunafunga? Wengine hufika hadi ya kusema kuwa kama itawezekana kutoa fidia yupo tayari kufanya hivyo, kwani kufunga ni kazi kubwa. Funga ya kiislam inatafautiyana na funga nyenginezo ambazo tuite watu kukaa na njaa, kwani yale ambayo mtu anatakiwa kuyafanya katika funga huwa nusu nusu. Ramadhani ni funga ya lazima kwa yule ambaye amefikia balighi, hana wazimu, hayupo kwenye siku zake, sio mgonjwa, hayumo kwenye nifasi n.k.

Baada ya Ramadhani kuna funga nyenginezo amabazo mtu akifunga hupata jazaa kubwa kwa Mola wake.

“Enyi mloamini! Mmelazimishwa kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”

(Al- Baqarah 2:183).

Kuna hadithi vile vile ya Bwana Mtume isemayo “Fungeni mtapata siha”

“Yule ambaye hatakuwa tayari kuwacha kusema uwongo, Allah hatompa kitu, na kukaa kwake na njaa na kiu huwa ni bure.’

Vile vile Bwana Mtume ameeleza kuwa:

“Kuna wengi hukaa na njaa na kutokunywa vinywaji huwa hawana funga sawa na wale ambao husali usiku kucha bila ya kupata chochote kile ila kukaa bila ya usingizi”

 

Funga ina mambo mengi na katika makala haya nitazungumzia mambo hayo kwa mukhtasar.

Wataalamu wa sayansi hutuelezea kuwa mtu anapotia chakula kinywani na kufikia hatua ya mwisho (mouth to the end of large intestine /clon) huchukua masaa 14, na nchi nyingi saumu huwa baina ya masaa 14, hiyo ni kusema mashine ya tumbo husita na kupumzishwa sawa na wenye vyombo vya moto pale wanaposema kuwa wanapeleka chombo chake ‘service’.

 

Masaa 14 bila ya kula katika mwezi nisawa na masaa 420 mashine yako ya kufanya kazi ya kusagia chakula huwa imesita, hizo ni sawa na siku 17.5 yaani siku 18 umekaa mashine yako haifanyi kazi ni faida kubwa sana ambayo hivi sasa watalamu wamaekuja kutambua na kutibu baadhi ya maradhi kuwataka wawele wawe hawali sana.

Wapingao saumu husema kuwa waislamu wanajiumiza na kupoteza nguvu nyingi wakati wanapofunga na kupoteza sukari kiwiliwilini mwao ‘hypoglycemia’ na kuhatarisha maisha yao. Jawabu imepatikana kuwa pengo hilo huzibwa kwa njia nyenginezo.

Katika Ramadhani au katika funga hutakiwa tujitahidi na viungo vyetu kwa mfano:

Ulimi:

Tujiepushe kusema uwongo, kusengenya, kuchongea, kutukana, kutongoza na yale yote yatakupelekea wewe kusema na kuiharibu saumu yako. Ulimi ndio nguvu kuu ya ushetani wa kila aina.

Mkono:

Mkono nao unachangia mengi, kudhulumu mali za yatima, mali za wengine, kuiba, kutesa watu, yote hayo yanatendwa na mkono, ni vyema ikawa mtu anautumia mkono wake kwa kutoa sadaka, na kutoutumia mkono wake kwa kufanya madhila.

Miguu:

Miguu ndio tunayoiringia kwenda kila tunakokutaka, ndani ya funga mtu ajilinde zaidi na miguu yake. Mtu awe anakwenda msikitini kwa darsa, kwa kusali na kwenda kusoma Quran.

Macho:

Macho ndio yenye kutizama na kutoa maamuzi ya kila kitu, kwenda kuiba, kumfwata mwanamke kwa njia za shari, n.k.

Funga inatupa fursa na kuwa ni chuo kinachomtengeneza mtu kuweza kuwa mtu mwema na kuweza kubaki na taratibu za uwema kwa mwaka mzima. Kinyume chetu ni kuwa mwezi ukiandama huwa ndio mfungwa kafunguliwa na kuanza uafriti wa kila aina, Disco, ulevi, vimwana, na kila aina ya ufirauni na upashkuki.

 

Faida za kufunga katika nyanja za kiafya na sayansi

Sayansi ilivyokuwa ni elimu ya mwanadamu, kwa hivyo siku zote haiko thabiti na inabadilika pale uvumbuzi mwipya unapotolewa. Wengi husema kuwa Saumu humuumiza mwenye kufunga na huumia sana na ni jambo la khatari.

Nini watalamu wa Tiba walichokiona?

v                Kile kinachofanya damu ‘haematology or serum’ haibadiliki wala haiathiriki kwa funga

v                “Metabolic rate” haibadiliki, yaani harakati mbali mbali za kutengeneza mwili nazo haziathiriki

v                Uzito nao wa mtu haubadiliki na kuna wengi katika Ramadhani huongezeka uzito kutokana na maanjumati na jazba za kula

v                Nnitrogin ipatikanayo kwenye mkojo huwa ni ya kawaida ‘blood urea nitrogen is normal’

v                Sukari ndani ya kiwiliwili hubakia 80 mgms %

 

Funga na madini ya Magnesium

Madini ya magnesium husaidia katika kuulinda moyo.

Kwenye saumu magnesium hutoka kidogo, na mtu akipatwa na mshtuko wa moyo husaidiwa kwa magnesium.

Magnesium hutumika katika ‘mitochondria’ nyezo moja ya “cell”  ambayo ndio ipayo nguvu chembe za uhai, na mtu akifunga, magnesium hufanya kazi vizuri, mishipa ya damu huchakaa lakini magnesium husaidia pakubwa kuweka sawa mambo.

Funga na malaji madogo au machache

Imeonekana kuwa wanyama walishwao kidogo bila kuvimbiana huishi sana koliko wale wanaolishwa kwa nguvu.

Watu wauguwao maradhi kama ya kisukari, shindikizo la damu (blood pressure), kitipwa tipwa (obesity) hutakiwa wapunguze kula na hiyo huwa mmoja ya dawa yao.

 

Bwana Mtume Muhammad S.A.W hajawahi kula akashiba na kuvimbiwa.

Bwana Mtume amesisitiza kuwa tule kwa kiasi. Amefika kusema;

"Sahani moja ailayo mtu mmoja inatosha kushibisha watu wawili’, na aliwahi kuulizwa Bwana Mtume kuwa kwanini kabila fulani inaishi umri mrefu? Alijibu;

"Watu wa kabila lile huwa hawali ila wanapokuwa na njaa na wanapokula wanapoanza kukaribia kushiba humaliza kula.”

Bwana Mtume alikuwa akila futari nyepesi na akila daku jepesi kinyume na wengi wa watu ambao hula  useme kesho ndio watakufa.

Funga inasaidia mengi mfano wa akili kuwa madhubuti ingawa wengi wakifunga huwa dhaifu kwa kujiregeza wenyewe.

 

Funga nyenginezo zisokuwa Ramadhani na Sunnah Kufunga

1. Funga ya siku 6 baada ya Ramadhani, yaani sitatul shawal.

Funga hii ina faida kubwa, Bwana Mtume anatuambia;

“Mwenye kufunga Ramadhani kisha akaifuatilia kwa kufunga siku 6 za mfungo mosi sawa na mtu aliyofuga mwaka mzima."

Wewe mwenzangu umezungukwa na mambo ya uchafu wa kila aina, hiyo ni fursa kubwa kwako kujiweka katika njia ya kuipata Pepo.

 

2.Funga ya Ashura ya mfungo 4

Funga hii Bwana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ametusisitiza tuifunge na iwe siku mbili badala ya siku tarehe 9, iwe 9 na 10, au 10 na 11, ili isiwe kama wafungavyo Mayahudi. Na Ashuraa ina matokeo mengi.

 

3.Funga ya Arafa katika mfungo tatu, mwezi tisa

4.Funga ya Ijumatatu na Alkhamisi, Siku aliyozaliwa Mtume

5.”Ayam Bidh” Masiku Meupe tarehe 13, 14, 15

6.”Ayam Sud” Masiku Meusi 27, 28, 29

7.Shaaban

8.Rajab

9.Ashhurul Hurum - Dhulkaad, Dhul Hijja, Muharam na Rajab

10.Sunatil Daud (kufunga siku moja na kula siku moja)

11.Siku tatu zozote zile katika kila mwezi.

 

Tujitahidi baada ya mafunzo haya ya mwezi wa Ramadhani kuweza kustahmili na kufunga, na pia tujitahidi miezi ifwatayo nayo tuwe tunafunga.

Tusiwache kufunga kutokana na fadhila zake, pamoja na kuwa na afya nzuri.