Zakat ul-Fitr

Na: Qur'an wa Sunnah Society

Imefasiriwa Na Abufarida Muhammad A. Basawad

 

UFAFANUZI:

Maana ya Zakat-ul-Fitr au Sadaqat-ul-Fitr ni "Sadaqa ya utakaso wa kufungua Saumu. Nacho ni kiwango fulani cha chakula kinachotolewa na waislamu katika siku chache za mwisho wa Ramadhan au siku ya 'Idd asubuhi, kabla ya kuswaliwa Swala ya 'Idd.

HEKIMA:

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) ametuamrisha kutoa zakat-ul-fitr kwa sababu mbili:

a. Kuwatakasa wale waliofunga, kuzisafisha saumu zao kutokamana na mambo ya upuzi, kama vile mazungumzo yasiofaa na madhambi madogo.

b. Kuwalisha waislamu masikini ili nao wawe na chakula cha kuwatosha siku ya 'Idd.

Ibn 'Abbas  (Radhiya Llahu anhu) akasema: "Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ametuamrisha kutoa Zakat-ul-Fitr ili mwenye kufunga ajitakase kutokamana na maneno machafu au vitendo vibaya na pia kuwalisha wanaohitaji. Hukubaliwa kama Zaka kwa yule atoae kabla ya swala ya 'Idd, lakini huwa ni sadaqa kama sadaqa ya kawaida kwa yule anaetoa baada ya swala ya 'Idd"[1]

HUKUMU YAKE:

Zakat-ul-fitr ni Faradhi (wajib) kwa wale wenye uwezo wa kutoa. Imeelezwa hii waziwazi kwenye Hadith ya Ibn 'Umar  (Radhiya Llahu anhu): "Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ameamrisha zakat-ul-fitr itolewe kwa kiwango cha Sa'[2] moja ya tende au Sa' moja ya shayiri (Barley), kwa Waislamu (Mtumwa au alie huru mume au mke, mdogo au mkubwa). Na akaamrisha itolewe kabla ya watu kwenda kuswali swala ya 'Idd".[3]

Hadithi hii inazidi kudhihirisha ya kwamba ni wajib juu ya kila muislamu (mwenye uwezo) bila ya kujali umri wala hali ya kijamii.

Jukumu la kutoa zakat ul-fitr ni juu ya kiongozi wa nyumba; inampasa kutoa kwa niaba yake mwenyewe na wale walio chini ya usimamizi wake: wadogo kwa wakubwa, waume na wake, watumwa na waungwana. Ibn Umar  (Radhiya Llahu anhu) akasema:

"Ameamrisha Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) sadaqat ul-fitr itolewe kwa walio chini ya usimamizi wako: wadogo na wakubwa, waungwana na watumwa."[4]

Ama kwa yule asokuwa na uwezo wa kifedha, huyo amesamehewa kwa sababu ya Nas' kutoka kwenye Qur'ani na Sunna, kama vile maneno ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) alivyosema: "Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote illa yaliyo sawa na uwezo wake..."[5]

Na Hadithi iliyopokewa na Abu Huraira: "Ninapowaamrisha kitu chochote, fanyeni kadiri ya uwezo wenu."[6]

Baadhi ya wanavyuoni waonelea kuwa hata kijusu (mtoto kabla ya kuzaliwa) nae alipiwe kwa niaba yake. Hata hivyo, hapana ushahidi wa hayo; na huyo kijusu hachukuliwi kuwa ni kijana - si katika lugha wala kawaida za watu.

AINA ZA ZAKAT-UL-FITR

Alivyokuwa akifanya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na Maswahaba zake ni kutoa zakat-ul-fitr kwa njia ya chakula. Akapokea Abu Sa'id al-Khudri (r.a): "(Katika wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) tulikuwa tukitoa zakat-ul-fitr kama Sa' moja ya twa'am (Chakula), Sa' moja ya Shayiri, Sa' moja ya Tende, Sa' moja ya Aqit (dried yogurt), au Sa' moja ya Zabibu kavu. Wakati huo chakula chetu cha kawaida kilikuwa ni Shayiri, Zabibu kavu, Aqit (dried yogurt) na Tende."[7]

Imepatikana ikhtilafu baina ya wanavyuoni kuhusu neno "twa'am" (chakula) lililotajwa kwenye riwaya iliyotangulia hapo juu. Vile vile ni rahisi kutambua yakuwa neno hilo limehusu nafaka na aina nyengine ya chakula kinachoweza kupimwa kwa chombo. Jambo hilo limedhihirishwa na baadhi ya riwaya kutoka kwa maswahaba. Kwa mfano Ibn 'Abbas  (Radhiya Llahu anhu) amesema:

"Sadaqa ya Ramadhan ni Sa' moja ya chakula, kwa hivyo yule atakaeleta ngano, atakubaliwa nayo; kwa yule atakaeleta shayiri, atakubaliwa nayo; kwa yule atakaeleta tende, atakubaliwa nayo; kwa yule atakaeleta nafaka (kama ngano) atakubaliwa nayo; kwa yule atakaeleta zabibu kavu, atakubaliwa nayo..."[8]

Hadithi hizo zilizopita zimezidi kudhihirisha yakuwa haifai mtu kutoa kwa njia ya pesa; wala kutoa kwa kutumia aina nyengine ya chakula kama vile nyama au mafuta, maadamu hilo ni jambo la ibada, ni lazima litekelezwe kulingana na Sunna.

Hata hivyo, mtu anaweza kukadiria kiwango cha fedha cha gharama ya mali alokusudia kutoa, na akampa mtu au chama ambacho anakiamini kuwa watanunuwa aina (ya chakula) inayofaa. Ni muhimu yakwamba itakapomfikia anaepasa kupokea hiyo zakat ul-fitr, iwe katika hali inayoruhusiwa kwenye Sunna.

KIWANGO:

Hadithi zilizotangulia zina ashiria yakwamba kiwango cha zakat ul-fitr ni Sa' moja ya aina mbali mbali ya chakula kinachoweza kupimika. Isipokuwa tu kwa jambo moja: kuhusu ngano, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwaamrisha watu watoe 'madd' mbili, zilizo sawa na nusu Sa'.[9] Na hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Mu'awiyah (r.a) huko Damascus.

Sa' ilikuwa ni kipimo kisichobadilika au sehemu ya ndani ya chombo kilichowazi. Ilikuwa ikibadilika kulingana na pahali, lakini Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaisawazisha kwa kusema: "Uzani ni kulingana an uzani wa Makkah; na vipimo ni kulingana na vipimo vya Madinah."[10]

Kwa hivyo, kipimo nakikadiriwe kulingana na kipimo cha Sa' ya Madinah, ambacho mpaka leo chapatikana. Walaakin kipimo hicho hakiwezi kufikiwa na watu wengi.Kwa sababu hiyo, wanavyuoni wengi wamekadiria karibu kuwa sawa sawa na miteko mine iliyojaa (kwa kushikanisha mikono miwili pamoja) ya mtu wastani.[11]

Hii inathibitisha ya kwamba ni makosa kupima zakat ul-fitr kwa uzani, kwa sababu uzani wa Sa' moja hubadilika kulingana na vitu tafauti. Hata hivyo, iwapo uhusiano baina ya uzani wa kitu chochote na kipimo kwenye chombo utathibitika, basi uzani wa Sa' moja wa kitu hicho unaweza kutumika.

 

WAKATI WA KUTOA:

Kama ilivyo wazi kutokamana na riwaya ya Ibn 'Abbas  (Radhiya Llahu anhu) iliyotangulia, zakat-ul-fitr inatakikana kutolewa siku ya 'Idd, kabla ya Swala ya Idd.

Ikazidi kupokewa yakuwa Ibn 'Umar  (Radhiya Llahu anhu) alikuwa akitoa siku moja au mbili kabla ya siku ya 'Idd.[12] Kutokamana na hayo imepatikana misingi ya ushahidi wa kutoa kwa siku chache kabla ya 'Idd. Lakini ni makosa kutoa mapema mno katika mwezi wa Ramadhan. Na kufanya hivyo itakuwa ni kwenda kinyume na hikima yake ya kuwa kafara ya madhambi wakati wa mwezi (wa Ramadhan), na kuwalisha wanaohitaji siku ya 'Idd, na zaidi itakuwa ni kwenda kinyume na walivyokuwa wakifanya Maswahaba na Ma-Salaf (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote).

Hata hivyo. Inaruhusiwa kuwapa mapema wale wanaokusanya, ukiamini yakwamba hawatozifikisha kwa wanaohitaji kabla ya mwisho wa mwezi (wa Ramadhan). Hivyo ndivyo ilivyokuwa ikifanywa wakati wa maswahaba, ilipokuwa wakusanyaji wakimaliza kukusanya siku moja au mbili kabla ya 'Idd.[13]

UKUSANYAJI:

Inaruhusiwa kuchagua watu kukusanya zakat-ul-fitr miongoni mwao. Vile vile inaruhusiwa kuwapa (hiyo zaka) hao wakusanyaji iwapo wanahitaji na wanastahiki. Ibn 'Umar  (Radhiya Llahu anhu) alikuwa akifanya hivyo.[14]

Ikazidi kusisitizwa kumchagua mtu kulinda zakat-ul-fitr iliyokusanywa. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alimchagua Abu Hurairah (r.a) kwa kazi hii; kama alivyosema  (Radhiya Llahu anhu): "Mtume wa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) amenikabidhi mimi kuchunza Zaka ya Ramadhan."[15]

WANAOSTAHIKI KUPEWA:

Zakat-ul-fitr inapasa kugawanyiwa masikini (wanaohitaji) kama ilivyosemwa kwenye hadithi ya Ibn 'Abbas. Haistahiki kupewa miongoni mwa aina nane za watu wanaopewa Zaka ya kawaida. Mtu miskin si mtu alie kwenye hali ya ufukara wa hali ya mwisho, lakini ni mtu ambae hali yake ya kifedha ni kiasi cha haja.

Nukta Ya Maelezo:

[1] Abu Dawud, an-Nasa'i na wengineo, imepewa hukmu ya hasan (al-Hilaali).
[2] Miteko mine, na kila mteko mmoja, ni kwa mikono miwili kwa pamoja. Mikono ya mtu wa umri wastani. Tazama chini kwa maelezo.
[3] Al-Bukhari na Muslim.
[4] Ad-Daraqutni na wengineo. Imepewa hukmu ya hasan kwa mkusanyiko wa riwaya.
[5] Al-Baqarah 2:286.
[6] Al-Bukhari na Muslim.
[7] Al-Bukhari.
[8] Ibn Khuzaymah kwa upokezi sahih (al-Hilaali).
[9] Amenukuu maneno hayo at-Tahawi; akapokea Sa'id Bin al-Musayyib na wengineo miongoni mwa ma-Taabi'in. Ikapewa hukmu kuwa ni riwaya nzuri ('Abdullah Bin Yusuf).
[10] Abu Dawud na wengineo kutoka kwa Ibn 'Umar, Sahih (al-Hilaali).
[11] An-Nawawi katika al-Majmu' 6:69.
[12] Ibn Khuzaymah (al-Hilaali).
[13] Ibn Khuzaymah (al-Hilaali).
[14] Ibn Khuzaymah (al-Hilaali).
[15] Al-Bukhari.