MAANA YA NENO 'SAUMU'

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

Neno Saumu katika lugha ya kiarabu maana yake ni 'Kujizuwia'. Yote sawa ikiwa kujizuwia na kula au kujizuwia na kusema, nk.

Bibi Maryam baada ya kumzaa Nabii Issa (Alayhas Salaam), alisema;

"Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema ya kufunga, kwa hivyo leo sitasema na mtu".

Maryam - 26

Kwa hivyo hapa Bibi Maryam (Alayhas Salaam) ametumia neno 'Sauma' pale aliposema ((Inniy nadhartu lilrahmani 'Sauma')), si kwa maana ya kujizuwia na kula, bali kwa maana ya kujizuwia na kusema.

Anasema Abu Ubaidah (Radhiya Llahu anhu);

"Neno 'Saumu' katika lugha ya kiarabu, maana yake ni 'Kujizuwia na kula au kujizuwia na kusema au na kwenda".

Lakini neno Saumu katika lugha inayotumika ndani ya vitabu vya elimu ya dini, maana yake ni moja tu, nayo ni;

"Kujizuwia na kula, kunywa na kumuingilia mtu mkewe, tokea inapoingia alfajiri mpaka juwa linapozama pamoja na kutia Nia".

 

SHERIA YA KUFUNGA

  1. Saumu katika dini zilizotangulia

  2.  

    Saumu ni miongoni mwa nguzo muhimu za dini, ambayo kwa hiyo watu waliotutangulia walikuwa wakimuabudu Mola wao kutokana na mafundisho ya Mitume yao na vitabu walivyokuja navyo.

    Imenukuliwa kutoka katika tafsiri ya Al Qurtubiy kuwa Mujahid amesema;

    "Mwenyezi Mungu amewafaradhishia umma zote kuufunga mwezi wa Ramadhani".

    Al Qurtubiy mwenyewe amesema;

    "Waandishi wa historia wameandika kuwa;

    'Wa mwanzo kuufunga mwezi wa Ramadhani ni Nabii Nuh alayhi ssalaam mara baada ya kutoka katika jahazi lake".

    Dalili inayotujulisha kuwa waliokuja kabla yetu nao pia walifaradhishiwa kuufunga mwezi huu mtukufu ni kauli yake Subhanahu wa Taala aliposema;

    "Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu"

    Al Baqarah - 183

    Ili kuwahamasisha waja Wake katika kuitimiza ibada hiyo kwa moyo mkunjufu, Mwenyezi Mungu katika aya hii anatujulisha juu ya kutufaradhishia sisi ibada ya saumu, na anatujulisha pia kuwa; Kama alivyotufaradhishia sisi, alikwishawafaradhishia pia wenzetu waliokuja kabla yetu, na hii ni kwa sababu kwa kawaida mwanadamu anapojuwa kuwa ibada anayoitenda ilikuwa pia ikifanywa na Mitume iliyotangulia pamoja na ummati wao, itawafanya waione nyepesi zaidi na kuwa na shauku nayo zaidi, na pia kuongeza juhudi pamoja na kuingiwa na hima katika kuikamilisha ibada hiyo.

    Haya yote ni katika hekima ya Mwenyezi Mungu pale anapoleta sheria zake;

    Mwenyezi Mungu anasema;

    "Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoa. Basi fuata uwongozi wao".

    Al An-am - 90

    Na akasema;

    "Na tunakusimulia zote katika khabari za Mitume ambazo kwa hizo tunauthubutisha moyo wako".

    Hud - 120

    Mwenyezi Mungu anatujulisha pia kuwa sababu ya kuifaradhisha ibada hii ni kujenga mwenendeo mwema 'Tabia njema' katika nafsi zetu, kama alivyowafanyia watu wema waliokuja kabla yetu, kwa sababu ibada ya Saumu inaingiza katika nafsi ya mwanadamu Taqwa (Uchamungu) na Tabia njema, tabia ambayo kwa sababu yake Mitume (Alayhim u Salaam) imeletwa.

    Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

    "Nimeletwa ili kuukamilisha mwenendo mwema".

    Imam Ahmed na Al Bazzar

    Mwenyezi Mungu ameiashiria sababu hiyo pale alipoikamilisha aya hiyo kwa kusema;

    "Ili mpate kumcha Mungu".

    Na maana yake ni kuwa; Ili mpate kumcha Mungu katika kufuata maamrisho na kuepukana na makatazo.

    Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

    "Funga ni kinga"

    Bukhari

    Na hii ni kwa sababu Ibada ya Funga inamkinga mtu kutokana na matamanio ya nafsi pamoja na maasi yanayosababisha ghadhabu za Mwenyezi Mungu

     

    MWANZO WA KUFUNGA

    Kwa vile ibada ya Funga ilikuwa ikifanywa na watu wa Ahlul Kitab waliotangulia, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kuzifanya ibada zilizokuwa zikifanywa nao kabla ya kufunuliwa Wahyi juu yake, na hasa kwa vile Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akiuelewa umuhimu wa ibada ya Funga, basi yeye (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akifunga kabla ya kuletewa Wahyi juu yake kwa hiari yake mwenyewe kabla ya kufaradhishiwa ibada hiyo.

    Imesimuliwa na Maimam Bukhari na Muslim kuwa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) amesema;

    "Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliamrisha watu wafunge siku ya Ashura, na ilipofaradhishwa saumu ya Ramadhani ikawa anayetaka anafunga (As) na asiyanakula".

    Bukhari na Muslim

    Katika riwaya nyengine;

    "Walikuwa wakifunga siku ya Ashura kabla ya kufaridhishwa Ramadhani na ilikuwa ni siku inayovalishwa Al Kaaba (siku maalum inayobadilishwa na kufunikwa kitambaa kipya) akasema (Bibni Aisha); "na ilipofaridhishwa Ramadhani, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema; ' Anayetaka kufunga (Ashura) na afunge na anayetaka kuacha aache".r

    Bukhari

    Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) amesema;

    "Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipoingia mji wa Madina aliwakuta Mayahudi wakifunga siku ya Ashura, akasema;

    "Nini hiki?" (Kwa nini mnafanya hivi?)

    Wakasema;

    "Hii ni siku njema ambayo Mwenyezi Mungu alimuokoa ndani yake Musa na wana wa Israeli (Bani Israil) kutokana na adui yao (Firauni)".

    (Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)) akawa anaifunga, na akasema;

    "Mimi ananistahiki zaidi Musa kuliko nyinyi".

    Akafunga na akaamrisha watu kufunga".

    Bukhari na Muslim

    Kwa hivyo ibada ya Funga ilikuwepo tokea mwanzo, na Waislam walikuwa wakifunga hata kabla ya kufaridhishwa, lakini mara baada ya kufaridhishwa Funga ya Mwezi wa Ramadhani, ikaachwa Funga ya siku ya Ashura na ikawa anayetaka anaifunga na asiyetaka anaiacha.

    Saumu ya Ramadhani ilifaradhishwa katika mwaka wa pili baada ya Hijra pale ilipoteremka kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo;

    "Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.

    Siku chache tu (kufunga huko). Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (atafunga baadhi ya siku), basi (atimize) hisabu katika siku nyingine. Na wale wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini"

    Al Baqarah - 183 - 184

    Tokea siku hiyo Saumu ikawa ni wajibu kwa kuhiyarishwa. Ilikuwa mtu anayetaka anafunga, na hiyo ni bora zaidi kutokana na kauli Yake Subhanahu wa Taala alipoikamilisha aya iliyotangulia kwa kusema;

    "Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake. Na (huku) kufunga ni bora kwenu. Ikiwa mnajua (haya sasa basi fuateni)".

    Ama asiyetaka kufunga alikuwa akiruhusiwa kula, lakini lazima atoe badala yake fidia kwa kuwalisha masikini katika kila siku anayokula. Iliendelea hivyo mpaka ilipoteremshwa aya iliyofuatilia, Mwenyezi Mungu aliposema;

    "(Mwezi huo mlioambiwa mfunge ni) Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qurani ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi na uwongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili).

    Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge".

    Al Baqarah - 185

    Bukhari

    Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu);

    "Baada ya kuteremka aya hii, ile hukmu ya kuhiyarishwa ikafutwa na badala yake ikawajibika kufunga kwa kila anayeweza kufunga isipokuwa kwa mgonjwa na mtu mwenye umri mkubwa sana."

    Ama ile kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema;

    "Na wale wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini", anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu);

    "Hukmu hii haikufutwa, bali ni kwa ajili ya mwanamume mtu mzima na mwanamke mtu mzima asiyeweza kufunga, wawalishe masikini kila siku badala ya Funga yao", kisha akasoma;

    "Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge".

     

    HEKIMA YA KUFARIDHISHWA KUFUNGA

    Mwenyezi Mungu haifaridhishi ibada yoyote ile isipokuwa kwa ajili ya hekima kubwa sana yenye manufaa kwa waja wake. Hutujulisha baadhi tu ya hekima hizo na mara nyengine hatujulishi, na hii ni kwa ajili ya kutupa mitihani sisi waja wake, 'Jee tutatii (au tutakuwa tukizijadili hukumu za Mwenyezi Mungu kisha tuamue kufuata au kutofuata)?"

    Saumu ni katika zile ibada ambazo Mwenyezi Mungu ametubainishia hekima yake, na miongoni mwa hekima hizo ni hizi zifuatazo;

    1- TAQWA

    Saumu ni miongoni mwa ibada tukufu sana ambayo athari yake huonekana wazi kabisa hapa hapa duniani na pia huko akhera. Athari yake inaonekana katika mwenendo wa mtu, tabia zake na katika kutengenea kwa umma.

    Mwenyezi Mungu aliashiria hayo aliposema;

    "Ili mpate kumcha Mungu".

    Yaani ili muifikie daraja hii ya Taqwa kutokana na kufunga kwenu.

    Na hii ni kwa sababu saumu ni njia inayomfikisha mtu katika daraja hiyo ya Taqwa kutokana na kufuata kwake amri ya Mwenyezi Mungu na kuepukana na makatazo Yake, kwa sababu Mwenyezi Mungu anataka amkute mja wake pale anapomtaka awepo na asimkute pale alipomkataza.

    Maana nyingine ya Taqwa ni mtu kufanya matendo yake yote kama alivyoamrishwa katika Wahyi na pia kumuogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu na awe siku zote akijitayarisha na siku ya kuondoka hapa duniani, na hii ni tafsiri ya ile kauli ya Mwenyezi Mungu pale aliposema;

    "Na chukueni masurufu. Na hakika masurufu bora ni yale yanayomfanya mtu asiombe. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili".

    Al Baqarah - 197

    Mwenyezi Mungu aliwapa wasia huu huu watu wema waliotangulia na wale watakaokuja.

    Mwenyezi Mungu anasema;

    "Na kwa yakini tuliwausia waliopewa Kitabu kabla yenu, na nyinyi (pia) kwamba mumche Mwenyezi Mungu".

    An Nisaa - 131

    Na akasema;

    "Enyi milioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atakupeni tamyizi ya kupambana baina ya haki na batili na atakufutieni makosa yenu na kukusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenyezi fadhila kubwa kabisa."

    Al Anfal - 29

    Bila shaka ibada ya Funga inamsaidia sana mtu katika kuifikia daraja hii ya Taqwa, na ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasema;

    "Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu"

    Al Baqarah - 183

    Mtu aliyefunga, huwa wakati wote na kwa hisia zake zote anajihisi yuko karibu sana na Mola wake na anajaribu kila mara kuepukana na kumuasi kwa moyo wake na kwa viungo vyake, yote sawa anapokuwa peke yake au anapokuwa na wenzake, kwa sababu wakati wote anakumbuka kuwa yeye amefunga. Hata kama mtu atamkosea, basi yeye hawezi kulipiza kisasi isipokuwa husema

    "Mimi nimefunga".

    Yote haya akiogopa asije akafanya jambo au kutamka neno litakalombatilishia Saumu yake.

    Hivi ndivyo alivyofundishwa na Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema;

    'Saumu ni kinga, basi asifanye (mtu) maasi wala asimdharau mwenzake, na mtu akigombana naye au akimtukana basi aseme;

    "Mimi nimefunga".

    Bukhari

    Yote haya yanamsaidia aliyefunga katika kuifikia daraja hiyo ya Taqwa, na hii ni kwa sababu aliyefunga anaelewa vizuri kuwa ikiwa hakujizuwia na yote hayo, basi hatoambulia kitu kutokana na saumu yake isipokuwa atakuwa amejitaabisha bure kwa kujiweka na njaa pamoja na kiu,

    Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

    "Asiyeacha kusema uongo na kuufanyia kazi (uwongo huo), basi Mwenyezi Mungu hana haja ya kujiweka kwake na njaa na kujizuwia kwake kunywa maji".

    Bukhari

    Na hii ni kwa sababu aliyefunga kama inavyojulikana ni kuwa anafunga kwa vitendo na kwa mwenendo. Kwa hivyo ikiwa mtu hatoacha kusema uongo nk. anakuwa amejizuwia na yale yanayofunguza kwa vitendo tu wakati ilimbidi ajizuwie na yale yanayofunguza kwa mwenenendo pia ambayo ni maasi, ili aweze kuifikia daraja ya Taqwa, kwa sababu kinyume na hivyo, Mwenyezi Mungu hana haja ya kumuadhibisha mja wake kwa kumweka na njaa pamoja na kiu.

    Na bila shaka aliyefunga anapoijuwa vizuri maana ya ibada hii ya Funga, atajiepusha na maasi yote kwa ujumla, kwa ajili hiyo saumu yake itamweka karibu zaidi na daraja hii ya Taqwa.

    Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliashiria haya aliposema;

    "Saumu ni kinga" na maana yake ni kuwa Saumu inamkinga mtu kutokana na maasi na kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu anaridhika naye na kujiepusha nafsi yake na Moto wa Jahanam uliotayarishwa kwa ajili ya wanaomuasi Mwenyezi Mungu.

  3. FUNGA INAMKUMBUSHA MWANADAMU NEEMA ZA MOLA WAKE NA KUMFANYA AMSHUKURU

Mwanadamu kwa kawaida hakumbuki kuwa anaishi katika neema kubwa alizoneemeshwa na Mola wake pamoja na fadhila Zake kwa sababu keshazowea kuziona neema hizo na kwa ajili hiyo anayaona kuwa ni mambo ya kawaida tu, na kwamba neema hizo ni sehemu ya maisha yake yasiyoweza kumbanduka.

Lakini mara neema hizo zitakapomuondokea, hapo ndipo anapoutambua utukufu wa neema hizo. Na hii ni kwa sababu siku zote umuhimu wa kitu unajulikana pale kinapokosekana.

Imepokelewa katika Athari kuwa Omar bin Khattab (Radhiya Llahu anhu) alisema;

"Hautambuwi (utukufu) wa Uislam yule asiyeujua (upotovu) wa Ujahilia"

Na mtu aliyefunga anapoona njaa na kiu au akawa anamtamani mkewe, hapo ndipo anapokumbuka na kutambua kuwa kumbe yote yale ni neema alizoneemeshwa na Mola wake Mkarimu, na kwa ajili hiyo atazidisha katika kumshukuru Mola wake.

Haya ni mojawapo ya matunda ya ibada hii ya Funga ambayo Mwenyezi Mungu aliashiria pale a;

"(Mwezi huo mlioammfunge ni) Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qurani ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi na uwongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili).

Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini bai (atimize) hisabu (ya siku alizowacha kufunga) katika siku nyingine.

Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na pia mtimize hisabu hiyo, na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongozeni, ili mpate KUMSHUKURU".

Al Baqarah - 185

Na maana yake ni kuwa; Ikiwa mtafunga kama alivyokuamrisheni Mwenyezi Mungu na kujiepusha na yale aliyokuharimisheni pamoja na kuilinda mipaka Yake, basi mtakuwa miongoni mwa Wanaomshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, ambao Mwenyezi Mungu amewasifia katika aya ya saba ya Suratul Zumar aliposema;

"Na kama mkimshukuru, hayo yanamridhisha kwenu".

Na hapana kitu mtu anachotamani kuliko kuzipata radhi za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaomshukuru".

Aali Imran

Na akasema;

"Kama mkinishukuru nitakuzidishieni; na kama mkikufuru (jueni) kuwa adhabu Yangu ni kali sana".

Ibrahim - 7

Na akasema;

"Na ni wachache wanaoshukuru katika waja wangu".

Na hii ni kwa sababu kumshukuru Mwenyezi Mungu maana yake ni kutumia mtu nguvu zake, viungo vyake pamoja na hisia zake zote katika yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala. Na bila shaka mtu aliyefunga akajizuwia na yote yale aliyoyaharamisha Mola wake wakati wa mchana, anakuwa amezitumia nguvu zake hizo, hisia zake pamoja na viungo vyake katika kumtii Mola wake, na kwa ajili hiyo anakuwa miongoni mwa wale wanaostahiki kupata fadhila za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.

Mwenyezi Mungu hakusema ni malipo gani atakayowalipa waja wake wanaofunga, kwa sababu jazaa yake ni kubwa sana, na kwa ajili hiyo akasema;

"Amali zote za binadamu ni kwa ajili yake isipokuwa Saumu (Funga), kwa hakika hiyo ni kwa ajili yangu na mimi ndiye nitakayemlipa kwa ajili yake".

Bukhari

Na katika riwaya nyingine imepokelewa kama ifuatavyo;

"Amali zote za wanadamu huwalipa mara kumi katika kila jema analotenda na kufikia mara mia saba" Mwenyezi Mungu amesema; "Isipokuwa Funga, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu, na mimi ndiye nitakayelipa kwa ajili yake. (mwanadamu) Anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu".

Bukhari na Muslim

Kutokana na haya tunaona kuwa Mwenyezi Mungu ametututayarishia Yeye mwenyewe jazaa ya Funga tofauti na ibada nyingine, kwani jazaa ya Funga hawaijuwi hata Malaika watukufu, na yote haya yanatokana na daraja kubwa ya 'Shukrani', kwa vile aliyefunga anaifikia daraja hiyo, ndiyo maana akastahiki kutunukiwa zawadi hiyo na Mwenyezi Mungu mwenyewe Subhanahu wa Taala.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

"Imani imegawika sehemu mbili, nusu moja ni Subira na ya pili Kushukuru"

Al Baihaqi

(Anasema Sh. Dr. Ahmed bin Abdul Aziz al Haddad - Mufti wa Dubai katika kitabu chake 'Fiqhul Siyam' kuwa hadithi hii ina udhaifu ndani yake).

Na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema;

"Saumu ni nusu ya Subira"

Attirmidhiy

Ama ujira wa Subira ni mkubwa sana na Mwenyezi Mungu ameutaja katika Qurani tukufu aliposema;

"Na bila shaka wafanyao Subira (wakajizuilia na maasia na wakaendelea kufanya ya taa) watapewa ujira wao pasipo hisabu."

Az Zumar - 10

 

ITAENDELEA INSHAALLAH