FADHILA ZA KUFUTARISHA

Sameer Zulfikar

       

FADHILA ZA KUFUTARISHA.

Imepokewa na Imam Tirmidhy kutoka kwa

Sahaba Zayd bin Khalid Al-Juhany  (Radhiya Llahu anhu) kuwa amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akisema;

“Mwenye kumfutarisha aliyefunga atapata ujira kama ule ujira wa aliyefunga bila ya kupungua  ujira wake (aliyefunga).”

(Tirmidhy).

Pia imepokewa hadithi na Ibni Khuzayma kutoka kwa sahaba Salman  (Radhiya Llahu anhu), kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

“Mwenye kumfutarisha aliyefunga katika mwezi wa ramadhani atasamehewa madhambi yake na ataepushwa na moto na atapata ujira kama anaopata aliyefunga bila ya kumpunguzia mfungaji ujirawake,” Masaahaba wakasema; 'sio kila mmoja wetu anayeweza kumiliki cha kumfutarisha aliyefunga', akasema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam); “Allah humpa thawabu hizi mwenye kumfutarisha aliyefunga (hata) kwa kokwa ya tende au kwa kumpatia maji, au kumpatia maziwa”. 

 

Hizi hi hadithi maarufu zilizopokelewa kuelezea fadhila za kufutarisha ingawa zipo nyengine lakini madhumuni yake huwa ni moja hivyo tutosheke na hizi mbili.

Maana ya hadithi ni kwamba yoyote atakayemfutarisha mtu aliyefunga sio kwa kujionyesha kuwa anatoa sadaka bali anafanya hayo kwa kutaraji kupata thawabu kutoka kwa Aallah (Subhaanahu wa Ta’ala), basi atalipwa ujira ulio sawa na ujira wa yule aliyefunga, na jambo linalojulikana kuwa aliyefunga ujira wake haujulikani na yeyote isipokuwa Aallah (Subhaanahu wa Ta’ala), hayo ni kutokanao na wingi wa fadhila zake, hapo hapo yule aliyefunga ana fungu lake pale.

Tusije tukafanya mchezo katika ibada kwa kusema kuwa  nikimpa aliyefunga kokwa ya tende afutarie nitakuwa ni sawa na aliyefunga basi hakutokuwa na haja ya kufunga. Afahamu mtu huyo kuwa hajafahamu makusudio yake na atapata dhambi nyingi kwa kuifanyia mchezo sheria ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

WAKATI WA KUFUTARI  

Ama wakati wa kufutari ni ule wakati jua linapozama, au tuseme pale utapomsikia mwadhini wa magharibi, na wale ambao vyote hivyo vinashindikana, juu yao ni kufwata jadweli ya kuzama jua waliopewa Misikitini au katika jumuia za kiislam zinazoaminika.

Kutoka kwa Abu Hurayra, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

“Hakika mja ampendaye Allah  ni yule anayefutari mapema.”

 

Na maana ya kufutari mapema sio kufutari kabla ya wakati, bali iwe mwanzo wa wakati baada ya kuingia kwake tu. Lakini kuna watu wengi hukosa fadhila hizi za kufutari mapema na si kwa jengine illa kutokujuwa umuhimu wa jambo lenyewe na utawaona wakisha maliza kusali magharibi ndio hutafuta  tende. Haya ni makosa, nayo ni katika mambo yanayochukizwa katika funga na yule anayetaka kumfuata Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) basi na afahamu kuwa alikuwa akifutari kwa tende kabla ya kusali sala ya magharibi.     

 

Kwa hivyo kama kuna mtu ataalikwa na mwenzake akafutari kwake basi na afahamu kuwa anatakiwaa afike kwake kabla  ya magharibi ili afutari kwa tende za huyo aliyemualika kisha ndio akasali, tena baada ya hapo kama kutafuatia chakula ni masuala mengine. Ama kama aliyekualika hakutaka uende kwake wakati huo, basi nae afahamu kuwa fadhila khasa za kufutarisha amezikosa na atapata fadhila za kumlisha muislam mwenzake tu ambazo fadhila zake sio kama tulizokwisha zieleza.

Hali kadhalika katika mambo muhimu yanayopaswa  kufanyiwa kazi ni kuomba dua wakati wakufutari na hii inatokana na maneno ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ya kuwa dua hupokelewa haraka wakati wakufutari, hivyo watu wasiwe wanazungumza mambo ya kipuuzi wakati huu kwani wanajikosesha fadhila za bure ambazo hawawezi kuzidiriki illa mwaka mara moja na unatakiwa useme;

“Ewe Mola hakika mimi nimefunga kwa ajili yako na kutokana na riziki hii uliyonipa nafutari.” Kisha uombe maghfira.

 

CHAKULA CHA KUFUTARIA

Chakula gani aliyefunga anatakiwa afutarie?

Ama chakula cha kufutaria na kiwe chakula cha aina yeyote ile, la muhimu kiwe cha halali yaani kimechumwa kwa njia za halali kuliwa, iwe kwa maji au vyakula vikavu, muhimu kiwe ni kitu chenye kuliwa. Chakula hasa kinachopendezewa kwa kufungua kinywa ni tende na ukipata zinazoitwa Rutab (nusu mbichi nusu mbivu) ni bora zaidi maana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ndizo alizozitumia, na kama huzipati basi ni tende za kawaida inatosha, na ukizikosa hizo basi ufutarie kwa chakula cha sukari au maji lakini mwenye kujitahidi kufungua kinywa kwa tende hupata daraja ya kwanza katika fadhila na iwe kwa njia za witri (odd number) moja, tatu, tano, saba tisa, n.k yaani kwa idadi isiyogawika kwa mbili.         

Hivyo watu wasikimbilie kula vyenginevyo wakaacha tende, kwani kuna hikma maalumu Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuhimiza kufungua kwa tende na itoshe kumfuata Mtume wako ambaye tumetakiwa matendo yetu yaambatane na yale aliyoyatenda yeye.

Pia la muhimu kuzingatiwa ni kuwa mtu kama ataamua kupeleka tende msikitini ili watu wafutarie, basi wale wahudumu wa msikiti wahakikishe kuwa tende hiyo wanapewa walengwa, tena katika wakati unaostahiki. Hali kadhalika mtoaji asitafute tende mbovu ndio akaamua kuzitolea sadaka, kwani Allah (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hafurahishwi na sadaka isiyo nzuri. Kama mtu anavyopenda kupokeaa vizuri  basi na anapotowaa atoe vilivyo vizuri