DARAJA YA SUNNAH
Imekusanywa na
kutafsiriwa na Muhammad Faraj Salem Al Saiy
Tembelea http://www.mawaidha.info/
Qurani
tukufu ni asili ya mwanzo ya utungaji wa sheria katika
Uislam, na hii ni kwa sababu Qurani ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyomteremshia
Mtume wake Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kupitia kwa Malaika
Mwaminifu Jibril (Alayhi ssalaam).
Na
yote yaliyomo ndani ya msahafu yanakubaliwa na Waislam wote kuwa ni yale yale
aliyoteremshiwa Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) bila
kubadilika chochote ndani yake, na husomwa katika Swala na katika hadhara
nyingine kama ni ibada.
Qurani
ni muujiza ambao Mwenyezi Mungu amewabishia makafiri
kuleta mfano wake tangu miaka elfu moja mia nne na ishirini iliyopita na mpaka
leo hii, baada ya kupita miaka yote hiyo, wameshindwa kuleta hata aya moja
yenye mfano wake.
Kila
kilichopokelewa kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi
wa sallam) kisichokuwa Qurani tukufu, katika yale yanayobainisha itikadi ya
dini, yanayoisherehesha sheria, yanayohimiza kuyafuata maamrisho ya Qurani
tukufu nk, yote hayo ni 'Sunnah', au huitwa 'Hadithi za Mtume (Swallah Llahu
alayhi wa sallam)' au 'Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)'.
Na yote hayo ni Wahyi aliofunuliwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na Mola wake Subhanahu wa Taala.
Mtume
wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pia
hufanya Ijtihadi katika baadhi ya Hukmu, na Mwenyezi Mungu haithibitishi hukmu
ya Ijtihadi iwapo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atakosea katika
kujitahidi kwake, na hapo hapo atatumwa Malaika Jibril na kumsahihisha. Ama
pale Mwenyezi Mungu anapoithibitisha Ijtihadi ya Mtume wake (Swallah Llahu
alayhi wa sallam), basi Ijitihadi hiyo huingia katika
hukmu ya Sunnah, na kwa ajili hiyo Sunnah yote asili yake ni Wahyi.
Baada ya vita vya
Badar kumalizika na Waislamu kurudi Madina na mateka
wao, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwataka shauri
Sahaba zake juu ya mateka wa vita hivyo vya Badar.
Abubakar (Radhiya
Llahu anhu) akamwambia:
"Mimi
naona kuwa hawa ni jamaa zetu, kwa hivyo itakuwa bora kama
tutachukua fidia kutoka kwao na pesa hizo sisi zitatusaidia katika mapambano
yetu na makafiri, na wakati huo huo huenda Mwenyezi Mungu akawahidi hawa na
kutusaidia siku za mbele."
Ama Umar (Radhiya
Llahu anhu) akasema:
"Mimi
sioni kama aonavyo Abubakar, bali naona itakuwa bora
kama utanipa (jamaa yangu) 'fulani' nimkate kichwa chake, na Aly umpe (ndugu
yake) Aqiyl amkate kichwa chake na Hamza umpe (jamaa yake) fulani amkate kichwa
chake ili Mwenyezi Mungu ajuwe kuwa nyoyoni mwetu hamna mapenzi ya washirikina.
Na hawa ni vigogo vya washirikina na viongozi wao."
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
alipendezewa na rai ya Abubakar (Radhiya Llahu anhu), akachukua fidia kutoka
kwao na kuwaacha huru baadhi
Usiku ule Jibril
akateremsha aya kutoka kwa Mwenyezi Mungu Subahanahu
wa Taala isemayo:
مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ
لَهُ أَسْرَى حَتَّى يُثْخِنَ فِي الأَرْضِ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا
وَاللّهُ يُرِيدُ الآخِرَةَ
وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {67} لَّوْلاَ كِتَابٌ مِّنَ اللّهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ
فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {68} فَكُلُواْ مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلاَلاً
طَيِّباً وَاتَّقُواْ اللّهَ إِنَّ اللّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ {69}
"Haimpasi Nabii kuwa na mateka
mpaka apigane (sana) na kushinda (barabara) katika nchi (ndipo achukue mateka). Mnataka vitu vya dunia, hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera!
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, (na) Mwenye hikima.
Isingalikuwa
hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu (kuwa
Mwenye kujitahidi mwisho wa jitihada yake hateswi) bila shaka ingalikupateni
adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.
Basi kuleni
katika vile mlivyoteka (vitani), ni halali (yenu sasa)
na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu."
Al Anfal
- 67 - 69
Imepokelewa kutoka kwa Abu Qatada (Radhiya Llahu anhu) kuwa siku moja Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipokuwa juu ya membari yake
akihutubia, mtu mmoja alisogea mbele akauliza:
"Iwapo nitauliwa katika jihadi nikiwa nimesubiri
nikitegemea malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu huku nikiwa nakwenda mbele na
sirudi nyuma, Mwenyezi Mungu atanisamehe madhambi yangu yote?"
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamjibu:
"Ndiyo, utasamehewa".
Yule
mtu alipoondoka, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) akaamrisha aitwe, na alipokuja akamwambia:
"Ndiyo utasamehewa, isipokuwa deni, hivi ndivyo
alivyonambia Jibril alayhi ssalaam (hivi punde)".
Annasai
Imepokelewa kutoka kwa Ibni Jariyr na Ibni Mardaweya kuwa Al Hassan al Basry amesema:
"Mwanamke mmoja
alikwenda kushitaki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) kuwa amepigwa na mumewe usoni akafanya alama.
Mtume (Swallah Llahu
alayhi wa sallam) akasema:
"Lazima na yeye (mwanamke) alipe kisasi chake".
Mwenyezi Mungu
akateremsha aya ya 34 ya Suratul Nisaa isemayo:
الرجال قوامون على النساء بما
فضل الله بعضهم على بعض وبما أنفقوا من أموالهم فالصالحات قانتات حافظات للغيب بما
حفظ الله واللاتي تخافون نشوزهن فعظوهن واهجروهن في المضاجع واضربوهن فإن أطعنكم
فلا تبغوا عليهن سبيلا إن الله كان عليا كبيرا.
"Wanaume ni
walinzi wa wanawake kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao kuliko
wengine, na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii wanaojihifadhi (hata) wasipokuwapo
(waume zao) kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha wajihifadhi. Na wanawake ambao
mnaona uasi wao kwenu, waonyeni na waacheni peke yao
katika vitanda na wapigeni. Na kama wakikutiini
msiwatafutie njia ya (ya kuwaudhi bure). Hakika Mwenyezi
Mungu ndiye Aliye juu (na) Mkuu".
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:
"Nilitaka vingine lakini Mwenyezi Mungu ametaka kinyume
chake'.
Watu wa kijiji kimoja walimdanganya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) kuwa wamesilimu, na kwamba wanataka wapelekewe watu ili
wawafundishe dini
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akawa kila
anaposwali, anapoinuka katika raka-a ya mwisho kutoka katika rukuu, anaposema 'Samia
Llahu liman hamidah", alikuwa akisoma Qunuti na kuwalani watu wa
kijiji kile cha wauaji kwa kusema:
"Allahumma
mlaani fulani na fulani.."
Akawa anaendelea
hivyo katika kila swala mpaka Jibril alipoteremsha aya kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kumtaka asiendele. Mwenyezi Mungu
anasema:
لَيْسَ لَكَ مِنَ الأَمْرِ
شَيْءٌ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ أَوْ يُعَذَّبَهُمْ فَإِنَّهُمْ ظَالِمُونَ
وَلِلّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ
وَمَا فِي الأَرْضِ يَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ
وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ
وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ
"Wewe huna lako katika shauri hii -
au (Mwenyezi Mungu) awaonee huruma au awaadhibu, maana wao ni madhalimu
(Atafanya anavyoona mwenyewe).
Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni na
vilivyomo ardhini humsamehe amtakaye na kumwadhibu amtakaye. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu".
Aali
Imran - 128 - 129
Bukhari – Imam Ahmed
na wengineo
Qurani
tukufu ni Wahyi. Unasomwa katika Swala na imepangiwa idadi ya thawabu katika kusoma kwake.
Mtume
wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
من قرأ حرفا من كتاب الله فله به حسنة والحسنة بعشر أمثالها لا
أقول الم حرف ولكن ألف
حرف ولام حرف وميم حرف
Atakayesoma
herufi katika kitabu cha Mwenyezi Mungu atapata kwa
kila herufi moja thawabu, na thawabu moja kwa kumi za mfano wake. Sisemi Aliyf
laam miym’ kuwa ni herufi (moja), bali aliyf ni
herufi moja na laam ni herufi moja na miym ni herufi moja
Lakini
Sunnah ni Wahyi usiosomwa katika Swala, na si ibada
katika kuisoma. Na zote mbili (Qurani na Sunnah)
zinakwenda sambamba, kazi yake ni moja na wala hapana hitilafu baina yake. Zote
hizo zinatufundisha yale Mola wetu anayoyataka kutoka
kwetu. Ya kwanza (Qurani) inatoka moja kwa moja kwa
Mwenyezi Mungu, na ya pili (Sunnah) inatoka kwa Mtume wake (Swallah Llahu
alayhi wa sallam).
Yanayosadikisha haya ni kauli Yake Subhanahu wa Taala aliposema:
وَأَنْزَلْنَا
إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ![]()
"Na tumekuteremshia mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, na ili wapate
kufikiri".
An Nahl - 44
Na
maana ya aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha mawaidha,
nayo ni Qurani tukufu, ili Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) awabainishie
watu yaliyomo ndani ya Qurani kutokana na elimu nyingine aliyopewa, nayo ni
Sunnah yake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) iliyotwahirika.
Kwa hivyo Qurani ni asili ya mwanzo ya sheria ya Mwenyezi Mungu, na Sunnah ni
asili ya pili.
Kwa
hivyo Qurani na Sunnah ni asili mbili zinazoambatana,
zisizohitilafiana katika kutimiza sheria ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa taala,
na Muislam hawezi kuijuwa sheria ya Mwenyezi Mungu bila ya mojawapo ya asili
mbili hizi. Na Mwanachuoni yeyote au hata mwenye kufanya
Ijtihadi hana budi kutafuta hoja zake kutoka katika asili mbili hizi.
Anasema Ibni l Qayim
Al Jawziy:
"Mwenyezi Mungu
anasema:
يَا
أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللّهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي
الأَمْرِ مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللّهِ
وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ ذَلِكَ خَيْرٌ
وَأَحْسَنُ تَأْوِيلاً (59)
"Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume
na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye
mwisho mwema."
AnNisaa -
59
Mwenye kuichunguza
aya hii ataona kuwa Mwenyezi Mungu anatuamrisha kumtii Yeye na
kumtii Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa ukamilifu. Bimaana kuwa
iwapo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
atatuamrisha au kutukataza jambo, basi inatuwajibikia kumtii kwa ukamilifu hata
kama amri hiyo haimo ndani ya Qurani, kwani yeye (Swallah Llahu alayhi wa
sallam) kama alivyosema katika hadithi:
ألا
أني أوتيت هذا الكتاب ومثله معه"
"Hakika
mimi nimepewa hiki Kitabu na (nimepewa) nyingine yenye
mfano wake pamoja nayo". (Nayo ni Sunnah yake)".
Abu Daud na ImamMalik katika Muwata’a
Ukiichunguza tena aya
ya Annisaa -59 utaona kuwa Mwenyezi Mungu hakutuamrisha kumfuata mwenye
madaraka moja kwa moja kama alivyotuamrisha kumfuata
Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Bali Mwenyezi Mungu amesema:
"Mt'iini
Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume"
Na hakusema
"Mtiini wenye madaraka katika nyinyi", bali
amesema:
"Na
wenye madaraka katika nyinyi" – bila
kuingiza neno 'Mtiini' kama
ilivyo katika twa- a Yake na ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Kwa ajili hiyo, ili mwenye madaraka atiiwe lazima amri yake ikubaliane na
maamrisho ya Mwenyezi Mungu au ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Na kama amri ya mwenye madaraka itakwenda kinyume na
amri ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam), basi
hapana utiifu katika kumuasi Muumbaji.
(Mwisho wa maneno ya Ibnul Jawzi).
Kisha Mwenyezi Mungu
akaikamilisha aya hiyo kwa kusema:
"Na
mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi
Mungu na Mtume".
Kauli hii
inatujulisha kwa uwazi kabisa kuwa marejeo yetu sisi
Waislam katika
kuhukumu ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake (Swallah
Llahu alayhi wa sallam).
Katika kamusi la
Fiq-hi, neno 'Sunnah', maana yake ni; 'kila
kilichothibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa
sallam) kuwa Amekitamka, Amekitenda au Amekikubali.
Na mfano wake ni
1.
Aliyotamka; Ni yale maneno aliyotamka katika matukio
mbali mbali yanayohusiana na Itikadi, Adabu na mengineyo. Kwa mfano kauli yake (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) pale aliposema:
إنما الأعمال بالنيات
"Hakika ya matendo hufuatana
na nia"
Au aliposema:
لا ضرر ولا ضرار
"Hairuhusiwi kudhuru wala
kujidhuru"
2- Aliyotenda;
Nayo ni yale matendo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) tuliyojulishwa na Masahaba (Radhiya Llahu anhu), kama
vile namna alivyokuwa Akitawadha, Akiswali Akihiji nk.
3- Aliyoyakubali;
Ni zile kauli au matendo waliyokuwa wakitamka na kutenda Masahaba (Radhiya
Llahu anhum) mbele yake, na yeye (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akayakubali
au akayanyamazia ikiwa ni dalili kuwa ameridhika nayo.
Na mfano wake
unapatikana katika hadithi iliyopokelewa kutoka kwa
Annasai na kusimuliwa na Abu Saeed al Khudhary (Radhiya Llahu anhu) kuwa;
Watu wawili waliokuwa
safarini uliwafikia wakati wa swala na hawakupata
maji, wakatayammam na kuswali. Baada ya kuswali wakapata
maji. Mmoja wao akatawadha na kuswali tena,
lakini mwenzake hakurudia kuswali. Waliporudi kwa
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kumuuliza juu ya hukmu yao, Mtume (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) akasema kumwambia yule asiyerudia kuswali; "Wewe umeisibu Sunnah sawa sawa",
na akamwambia yule aliyerudia; "Wewe
umepata thawabu mara mbili".
Baadhi ya watu
wanaojinasibisha na Uislam wamejaribu kuishambulia
Sunnah - (Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa hoja
mbali mbali. Wapo miongoni mwao wanaoikataa moja kwa
moja, na wengine wanazikataa baadhi ya Hadithi, hasa zile ambazo katika elimu
ya Hadithi zinazoitwa Hadithi za Aahad, na wapo wanaozikataa hadithi za aina
hiyo zile tu zinazozungumzia mambo ya Itikadi nk.
Wale wanaokataa moja kwa moja kuwajibika kufuata Sunnah za Mtume (Swallah Llahu
alayhi wa sallam) ni watu wenye kusudi la kutaka kuifasiri Qurani kwa namna
waitakayo wao, kwa sababu Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
ndiyo yanayotufasiria Qurani na kutubainishia. Ikiwa watafanikiwa kuipiga vita
Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), basi
itakuwa wepesi kwao kuipiga vita Qurani Tukufu kwa kuzitumia zile aya
zinazobeba maana nyingi (Mutashabihaat) na zile hukmu zilizoachiwa huru
(Mutlaq), kwani wao wataweza kuzibebesha hukmu hizo maana wanayotaka, na
si kwa maana anayotaka Mola wetu Subhanahu wa Taala. Kwa sababu katika
Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
pana vizuizi vinavyozuwia mtu asiweze kucheza na maana ya Aya.
Jambo linaloshangaza ni kwamba hao wanaoipinga Sunnah ya Mtume (Swallah Llahu
alayhi wa sallam) eti wanajiita 'Al Qur-aniyyun' (wenye kuifuata Qurani tu),
wakati anayechunguza hali zao ataona kuwa kujinasibisha kwao huko na Qurani ni
uongo mtupu, kwa sababu kwa kupinga kwao Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu
alayhi wa sallam) wao wanakwenda kinyume na mafundisho ya Qurani Tukufu.
Kwa sababu katika
Qurani Mwenyezi Mungu anasema:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ
عَنْهُ فَانتَهُو
"Na
anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho".
Al Hashar
- 7
Na anasema:
وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى
اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْراً أَن يَكُونَ لَهُمُ
الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ
ضَلَالاً مُّبِيناً
"Haiwi
kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini,
Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanapokata shauri wawe na hiari katika shauri lao.
Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hakika
amepotea upotofu (upotevu) ulio wazi (kabisa)".
Al Ahzab
- 36
Katika shuruti za
Imani, ni kuyakubali yote aliyokuja nayo Mtume wetu
Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam), kwa sababu Mwenyezi Mungu amemchagua
na kumwaminisha Mtume huyu mtukufu atufikishie maamrisho Yake kwetu.
Na Mwenyezi Mungu
anasema:
{واللّه أعلم حيث يجعل رسالته}
"Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi
kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake."
Al
An-an-am124
Na akasema:
فَهَلْ عَلَى الرُّسُلِ إِلاَّ الْبَلاغُ الْمُبِينُ
"Basi lipo lolote juu ya Mitume
isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi?"
An Nahl - 35
Na akasema:
} يَا
أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ آمِنُواْ بِاللّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي
نَزَّلَ عَلَى رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِيَ أَنزَلَ مِن
قَبْلُ وَمَن يَكْفُرْ بِاللّهِ وَمَلاَئِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ
فَقَدْ ضَلَّ
ضَلاَلاً
بَعِيداً}
"Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake,
na Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha
kabla yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika
wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha
potelea mbali."
AnNisaa -
136
Na akasema:
فَآمِنُواْ بِاللّهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ
الأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللّهِ وَكَلِمَاتِهِ
وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ
"Basi
muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma
na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka".
Al Aaraf
- 158
Hizi ni dalili zilizo wazi zinazotuamrisha kufuata mafundisho ya
Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Anasema Imam Shafi
Rahimahu Llah:
"Mwenyezi
Mungu amejaalia ukamilifu wa Imani katika kumuamini
Yeye kisha katika kumuamini Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam)."
Kitabul
Umm
Katika Qurani tukufu
mna aya nyingi zinazoelezea juu ya kuwajibika kuti na kufuata
Mafundisho ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Mwenyezi Mungu
anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللّهَ
وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي الأَمْرِ
مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللّهِ وَالرَّسُولِ إِن
كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ
بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ ذَلِكَ خَيْرٌ َأَحْسَنُ تَأْوِيلاً
"Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume
na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye
mwisho mwema."
An Nisaa - 59
Kumtii Mwenyezi Mungu
ni kukifuata kitabu Chake, na kumtii Mtume ni kufuata
mafudisho yake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).
Mwenyezi Mungu pia
amesema:
وما آتاكم الرسول
فخذوه وما نهاكم عنه فانتهوا
"Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni
jiepusheni nacho".
Al Hashar
- 7
Na katika aya
ifuatayo, Mwenyezi Mungu ameliweka wazi kabisa kusudi Lake, pale aliposema:
فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّىَ
يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لاَ يَجِدُواْ فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجاً مِّمَّا قَضَيْتَ
وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيماً
"La!
Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye
WEWE ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana,
kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee
kabisa ".
An Nisaa - 65
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
تركت فيكم
أمرين لن تضلوا ما تمسكتم بهما كتاب اللّه وسنتي
"Nimekuachieni amri mbili
hamtopotea mkizishika; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na
Sunnah yangu (Mafundisho yangu)".
Imam
Malik - Al Hakim
Na akasema:
عليكم بسنتي
وسنة الخلفاء الراشدين عضوا عليها بالنواجذ
"Mzifuate
Sunnah zangu na (Sunnah) za Makhalifa waongofu, mzikamate vizuri kwa magego
yenu".
Sunan Abu Daud
Hadithi hizi ni dalili kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi
wa sallam) amepewa Kitabu na Sunnah, na kwamba inatuwajibikia kuvifuata na
kuvikamata vizuri, kuvitii na kuvifanyia kazi vyote viwili bila ya
kuvitenganisha.
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)
ametutahadharisha juu wale watakaokuja baada yake watakaokataa kufuata
mafundisho yake wakidai kuwa eti Qurani peke yake inatosha.
Mtume (Swallah Llahu
alayhi wa sallam) amesema:
يُوشِكُ
الرَّجُلُ مُتَّكِئًا عَلَى أَرِيكَتِهِ يُحَدَّثُ بِحَدِيثٍ مِنْ حَدِيثِي
فَيَقُولُ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ كِتَابُ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ مَا وَجَدْنَا
فِيهِ مِنْ حَلَالٍ اسْتَحْلَلْنَاهُ وَمَا وَجَدْنَا فِيهِ مِنْ حَرَامٍ
حَرَّمْنَاهُ أَلَّا وَإِنَّ مَا حَرَّمَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ
عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مِثْلُ مَا حَرَّمَ اللَّهُ "
"Hivi
karibuni (mtaona ya kushangaza) utamkuta mtu ameegemea tandiko lake,
anahadithiwa Hadithi katika hadithi zangu, anasema: "Baina yetu na baina yenu ni kitabu cha Mwenyezi Mungu (peke yake),
tutakayoyaona yamehalalishwa ndani yake tutayahalalisha na tutakayoyaona
yameharamishwa ndani yake tutayaharamisha" - Mjuwe kuwa yaliyoharamishwa
na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni sawa na
yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu".
Ibni Majah - Al Baihaqiy - Abu Daud.
Na katika hadithi
nyingine, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu
alayhi wa sallam) amesema:
مَن بلغه عني
حديث, فكذب به, فقد كذب ثلاثة: الله, ورسوله , والذي حدث به
"Mtu atakapojulishwa juu ya hadithi yangu akaikadhibisha,
(basi) amekadhibisha watatu. Mwenyezi Mungu, Mtume wake na yule aliyemfikishia hadithi
hiyo".
Attabarani
Bila shaka hapa
panakusudiwa zile hadithi sahihi
Umma wote wa Kiislam
kwa ujumla umekubaliana juu ya kuwajibika kuifanyia kazi Sunnah ya Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) katika sheria ya Mwenyezi
Mungu, na hii inatokana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) yanayotutaka tuisimamishe hukmu ya Mwenyezi Mungu kwa
kufuata Kitabu Chake na Mafundisho ya Mtume Wake (Swallah Llahu alayhi wa
sallam), kwa sababu hizi ni asili mbili za sheria kwa Umma wa Kiislam, asili
ambazo Mwenyezi Mungu ametujulisha nazo na kushuhudia Mwenyewe kuwa Mtume wake (Swallah
Llahu alayhi wa sallam) hasemi isipokuwa yale aliyofunuliwa.
Mwenyezi Mungu
anasema:
قُل لاَّ أَقُولُ لَكُمْ عِندِي
خَزَآئِنُ اللّهِ وَلا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ إِنْ
أَتَّبِعُ إِلاَّ مَا يُوحَى إِلَيَّ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الأَعْمَى وَالْبَصِيرُ أَفَلاَ
تَتَفَكَّرُونَ {50}
"Sema; "Mimi sikwambieni kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu wala (sikwambieni kuwa) najua mambo ya siri (ya Mwenyezi Mungu). Wala sikwambieni kuwa Mimi ni Malaika