DAIMA TUYAKUMBUKE
Limeandikwa na Swaleh Suheil Abeid
Viumbe musighurike
mukajusahauliya
Bure musipumbazike
kwa anasa za duniya
Daima tuyakumbuke
mauti yatungojeya
Zindukani walimwengu
ina ghururi duniya
Mauti yako wezangu
ketini kuzingatiya
Tumepangiwa na Mungu
hatuna pa kukimbiya
Binadamu u dhaifu
nguvu ungajinyeteya
Usione ufanifu
na furaha kila ndiya
Utakujakua mfu
ghafula ushajifiya
Huna kitu una nini
kiumbe usotuliya
Na daima umbiyoni
kwa tamaa za duniya
Kumbe wewe hujioni
mauti yakungojeya
Hebu kua na fahamu
mwisho utakufikiya
Saa yako ikitimu
hapana wa kuzuwiya
Ghafula u marehemu
watu wajakuliliya
Wako wapi makhuluki
waliyo tutanguliya
Walokua wamiliki
mengi mali na dhuriya
Mara wakitahamaki
imewatupa duniya
Mkumbuke Rahamani
utekeleze shariya
Maisha ya duniyani
matembezi wapitiya
Wajatiwa kaburini
ghafula ushangamiya
Kaditmati shairi
tosha nalohubiriya
Japokua si kathiri
yote nalohubiriya
Tujue kwake Qahari
hesabu yatungojeya