UHUSIANO WA BABA NA MTOTO WA ZINA AU NA MTOTO WA KULAANI
Anasema Sayed Sabeq katika
Fiqhil Sunnah;
"Mwana wa zina ni yule
aliyezaliwa nje ya ndoa ya kisheria, na mtoto wa kulaani ni yule ambaye mume
ameikataa mimba kuwa si yake".
Mume anaweza kuikataa mimba
kuwa si yake ikiwa atakuwa na mashahidi wanaoweza kuthibitisha hayo, au ikiwa
ataapa viapo vinne kuwa yeye anasema kweli na mara ya tano aape kuwa laana ya
Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa anasema uongo.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Na wale
wanaowasingizia wake zao (kuwa wamezini) na hawana mashahidhi ila nafsi zao,
basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi
Mungu ; ya kwamba bila shaka yeye ni mmoja wa wanaosema kweli.
Na mara ya tano (aape)
kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.
Na (mke) itamuondokea
adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba (huyu
mume) ni miongoni mwa waongo.
Na mara ya tano (aape) ya
kwamba hasira ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama (mumewe) yu miongoni mwa
wanosema kweli, (na yeye mke ndiye muongo)".
ANNUR-6-9
Mwana wa zina (aliyezaliwa
nje ya ndoa na mwana wa kulaani ambaye mzee wake amemkataa, hawa hawarithiani
na baba zao, yaani baba hamrithi mwana wala mwana hamrithi baba, na mtoto huyo
anaungana na mama yake moja kwa moja na kurithiana naye.
Kuhusu hukumu hii hakuna
hitilafu baina ya maulamaa wa Kiislam, kutokana na kutokuwepo kwa uhusiano wa
kisheria baina yao.
Kutoka kwa Ibni Omar (RA)
kuwa katika wakati wa Mtume (SAW) mtu mmoja aliapa kwa njia ya kulaani kuwa
mtoto si wake, na Mtume (SAW) akawatenganisha baina yao na kumhusisha mtoto
huyo moja kwa moja na mama yake.
Bukhari na Abu Daud
Lafdhi ya hadithi inasema
hivi;
"Mtume (SAW) amehukumu
kuwa mtoto aliyekataliwa na baba yake kwa njia ya kulaani kuwa (hatorithiana na
babake, bali) atarithiana na mamake na atarithiana pia na wale wanaoweza
kumrithi mama yake".
Kifungu nabari 47 cha
sheria ya mirathi ya nchi ya Misri kinasema;
"Mwana aliyezaliwa nje
ya ndoa, na mwana aliyekataliwa kwa njia ya kulaani, anarithiana na mamake na
jamaa za mamake".
Muhammad Faraj Salem