TAARIKU SSALAAT
Sala ni ibada
iliyo katika daraja ya juu kupita ibada zote katika dini ya Kiislam na ni nguzo
muhimu sana kupita nguzo zote za dini, na ni ibada ya pekee ambayo Mwenyezi
Mungu Subhanahu wa Taala amemfaradhishia mja wake Muhammad (SAW) kwa kuzungumza
naye moja kwa moja usiku ule wa Miraji alipomnyanyua na kumfikisha juu ya
mbingu ya saba, kisha akamsogeza mpaka penye Sidratul Muntaha na huko
akamfaridhishia ibada hii ya Sala bila ya kumtumia malaika Wake Jibril (AS)
kama alivyofanya katika kuzifaridhisha ibada nyingine.
Sala ni jambo
la mwanzo atakaloulizwa mja na Mola wake siku ya kiama, na ikiwa ameitimiza
sawa kama alivyoamrishwa basi mambo yote yaliyobaki yatakuwa sawa.
Mtume (SAW)
amesema;
“Cha mwanzo
atakachoulizwa mja siku ya Kiama ni Sala, ikiwa ameitimiza basi yote yaliyobaki
yatatimia, la kama ikiharibika basi yaliyobaki yataharibika”.
Attabarani –
Attirmidhiy – Annasai na wengineo.
NGUZO YA DINI
Sala ni nguzo
ya mwanzo katika dini baada ya kuzitamka shahada mbili.
Kutoka kwa
Abdillahi bin Omar (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Uislam
umejengeka juu ya nguzo tano. Shahada ya La ilaaha illa Llah, Muhammadun Rasulu
Llah, kusimamisha Sala na Kutoa Zaka na Kufunga mwezi wa Ramadhani na Kuhiji
Makka kwa mwenye uwezo wa kufika huko.”
Na akasema
(SAW)
“Kichwa cha
jambo ni Uislam, na nguzo yake ni Sala na kilele chake ni Jihadi katika njia ya
Mwenyezi Mungu”.
Kwa vile
nyumba haiwezi kusimama bila ya nguzo, basi asiyesali anahesabiwa kuwa ni
mbomoaji wa nyumba hiyo na si mwenye kuijenga na makaazi yake ni Motoni.
Mwenyezi
Mungu Subhanahu wa Taala akituelezea juu ya sababu zitakazowaingiza watu Motoni
alisema;
“Isipokuwa watu wa
kuliani (watu wa kheri).
(Hao watakuwa)
katika Mabustani,
Wawe wanaulizana.
Juu ya watu wabaya
(wawaambie).
‘Ni kipi kilichokupelekeni
Motoni?’
Waseme;
‘Hatukuwa miongoni
mwa waliokuwa wakisali…”
Al Mudathir -
39-43
USIA WA MTUME
(SAW) KWA UMMA WAKE
Kwa ajili ya
umuhimu wake, Mtume (SAW) aliendelea kuwausia umma wake juu ya Sala mpaka pale
alipokuwa akipumua pumzi zake za mwisho.
Imepokelewa
kuwa Mtume (SAW) alipokuwa akipumua pumzi zake za mwisho kabla ya kufariki
dunia alikuwa akiusia kwa kusema;
“Salaa Salaa
na mliowamiliki kwa mikono yenu ya kulia”.
Na
imepokelewa pia kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Yatakuja
kuachwa maamrisho ya kiislamu moja baada ya jingine. Kila ikitoweka amri moja,
watu wataing’ang’ania inayofuatia. La mwanzo kuachwa itakuwa hukmu (ya Mwenyezi
Mungu) na la mwisho ni Sala”.
Ibni Haban.
Katika
hadithi hii Mtume (SAW) anatutabiria juu ya wakati wetu huu ambapo hukumu ya
Mwenyezi Mungu ishapigwa vita na kuachwa, na kwamba ibada nyingine nazo pia
zitapigwa vita moja baada ya nyingine mpaka mwisho haitobaki isipokuwa ibada ya
Sala ambayo nayo pia itapigwa vita na kuachwa.
SALA NDANI YA
QURANI
Anasema Sh.
Sayed Sabeq katika Fiqhil Sunnah;
“Atakayefuatilia
aya za Qurani atagundua kuwa Mwenyezi Mungu mara nyingi anaitaja ibada ya Sala
kwa kuipambanisha na ibada mbali mbali. Kwa mfano;
Ameipambanisha
Sala na Dhikri (kumbusho) aliposema;
“Bila shaka
Sala (ikisaliwa vilivyo) humzuiliya (huyo mwenye kusali na) mambo machafu na
maouvu, na kwa yakini kumbusho la Mwenyezi Mungu (lililomo ndani ya Sala) ni
jambo kubwa kabisa (la kumzuwilia mtu na mabaya)”.
Al Ankabuut –
45
Na akasema;
“Hakika
amekwishafaulu aliyejitakasa (na mabaya). Akakumbuka jina la Mola wake na
akasali”.
Al Alaa –
Na akasema;
“Basi niabudu
na usimamishe Sala kwa kunitaja”.
Ta Ha- 14
Ameipambanisha
na Zaka;
“Na shikeni
Sala na toeni Zaka”
Al Baqarah –
110
Akaitaja
pamoja na Subira;
“Na tafuteni
msaada kwa kusubiri na kwa kusali”.
Al Baqarah-45
Mwenyezi
Mungu pia ameitaja pamoja na ibada ya kuchinja;
“Basi sali na
uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi”.
Kauthar – 2
Na akasema;
“Sema: Hakika
Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
Hana mshirika
wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu”.
Al An
am – 162-163
Mtu hata atende mema ya namna gani, lakini akiwa
hasali, au anaposali hamnyenyekei Mola wake, basi matendo yake yote hayo
yanapotea bure na anakuwa miongoni mwa waliokula hasara.
Mwenyezi Mungu anasema;
“HAKIKA
wamefanikiwa Waumini, Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,
Na
ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,
Na
ambao wanatoa Zaka,
Na
ambao wanazilinda tupu zao,
Isipo
kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye
kulaumiwa.
Lakini
anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.
Na
ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
Na
ambao Sala zao wanazihifadhi.
Hao
ndio warithi,
Ambao
watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo milele.
Al
Muuminun – 1-11
Atakayezingatia
vizuri mfumo wa aya hizi ataona kuwa Mwenyezi Mungu ameitaja Sala mara mbili.
Mara ya mwanzo kwa ajili ya kutufahamisha umuhimu wake na unyenyekevu
unaotakiwa ndani yake, na mara ya pili kwa ajili ya kututaka tuihifadhi
(tusiiache) pamoja na kutujulisha kuwa ni watu wa aina hiyo tu ndio
watakaoirithi Pepo ya Firdausi.
POPOTE
ULIPO LAZIMA USALI
Sala
ni ibada ya pekee ambayo mja analazimika kuitimiza anapokuwa katika mazingira
ya aina yoyote. Anapokuwa safarini, wakati wa hofu, anapokuwa mgonjwa na hata
anapokuwa vitani.
Mwenyezi
Mungu anasema;
“Zilindeni
Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi
ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
Ikiwa
mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapo kuwa
katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyo kufunzeni yale mliyo
kuwa hamyajui”.
Al
Baqarah – 238-239
Na
akasema
“Na
unapo kuwa pamoja nao (vitani), ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao
wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo maliza sijida zao,
basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijasali, lisali pamoja
nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio kufuru wanapenda mghafilike
na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si
vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka
silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri
adhabu ya kudhalilisha.
Mkisha
sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha
kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni SALA kama dasturi. Kwani hakika SALA
kwa Waumini ni FARADHI iliyo wekewa nyakati maalumu”.
Annisaa
– 102-103
Mwenyezi
Mungu amewakemea sana wale wanaojaribu kuipuuza ibada hii tukufu na kufuata
matamanio ya nafsi zao.
Mwenyezi
Mungu akasema;
“Lakini
wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha SALA, na wakafuata matamanio. Basi
watakuja kupata malipo ya ubaya”.
Maryam
– 59
Na
akasema
“Basi,
ole wao wanao sali,
Ambao
wanapuuza Sala zao”.
Maaun
– 4-5
Kutokana
na umuhimu wa ibada hii, Nabii Ibrahim (AS) alimuomba Mola wake amjaalie yeye
na vizazi vyake wawe wenye kuishika.
Mwenyezi
Mungu anasema juu ya Dua ya Nabii Ibrahim;
“Mola
wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika dhuriya zangu pia.
Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu”.
Ibrahim
– 40
Katika
aya nyingine Mwenyezi Mungu amesema;
“Lakini
wakitubu na wakasimamisha Sala na wakatoka Zaka basi iacheni njia yao (waacheni
huru), hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu”.
Suratut
Tawba – 5
Na
maana yake ni asiytubu na akakataa kusimamisha Sala na akakataa kutoa Zaka
asiachwe huru.
Na
katika Sura hiyo hiyo ya Attawba aya ya 11 Mwenyezi Mungu anasema;
“Kama
wakitubu na wakasimamisha Sala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika
dini”.
Na
kinyume chake ni kuwa; Yule asiyetubu na akakataa kusimamisha Sala na akakataa
kutoka Zaka, basi huyo si ndugu yetu katika dini.
HUKMU
YA MWENYE KUACHA KUSALI (TAARIKU SALAAT)
Maulamaa
wote bila hitilafu yoyote baina yao wamekubaliana kuwa mwenye kuiacha Sala
kusudi kwa jeuri na kwa kuikanusha, huyo anakuwa kafiri aliyekwisha toka katika
dini ya Kiislam.
Isipokuwa
wamehitalifiana juu ya yule mwenye kuiacha kwa uvivu tu au kwa kujishughulisha
na dunia lakini haikanushi na anaamini kuwa ni fardhi juu yake.
Wapo
wanaosema hata huyu naye pia anakuwa kafiri aliyekwishatoka katika dini ya
Kiislam, na dalili walizoziegemea maulamaa hao ni hadithi za Mtume (SAW)
zifuatazo;
“Kutoka kwa
Jabir (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Baina ya mtu
(kuwa Muislam) na baina ya (kuwa) kafiri, ni kuacha Sala”.
Muslim –
Ahmed – Atttirmidhiy na wengineo
Na kutoka kwa
Buraida (RA) kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Ahadi iliyopo
baina yetu na baina yao ni Sala, atakayeacha (kusali) kesha kufuru”.
Ahmed na
wengineo
Na kutoka kwa
Abdillahi bin Amru bin Al Aas (RA) kuwa Mtume (SAW) siku moja alizungumza juu
ya Sala kisha akasema;
“Atakayeisimamisha
atakuwa na nuru na dalili na ataokoka siku ya Kiama, ama asiyeisimamisha
hatokuwa na nuru wala dalili wala hatookoka, na atakuwa siku ya Kiama pamoja na
Qaruni na Firauni na Hamana na Ubaya bin Khalaf”.
Imam Ahmed na
Attabarani na wengineo
Katika kuifasiri hadithi hii, anasema
mwanachuoni maarufu Ibnul Qayim al Jouzi kuwa;
“Mwenye
kuacha Sala huwa ameshuhgulika na mojawapo kati ya yafuatayo; ama atakuwa
imemshughulisha mali yake au ufalme wake au cheo chake au biashara zake. Yule
aliyeshughulika na mali yake, atafufuliwa pamoja na Qaruni, na aliyeshughulika
na ufalme wake, huyo atakuwa pamoja na Firauni, na aliyeshughulika na cheo
chake atakuwa pamoja na Hamana na yule aliyeshughulika na biashara zake
(akaacha kusali), huyo atakuwa pamoja na Ubaya bin Khalaf”.
Kutoka kwa
Abdillahi bin Shaqiq Al Aqliy anasema;
“Masahaba wa
Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) hawakuwa wakiona amali yoyote nyingine mtu
akiiacha anakuwa kafiri isipokuwa Sala”.
Attirmidhiy
na Al Hakim
Anasema Ibni
Hazm;
“Imepokelewa
kutoka kwa Omar bin Khatab na Abdul Rahman bin Auf na Muadh bin Jabal na Abu
Huraira na Masahaba wengi (RA) kuwa;
“Atakayeacha
kusali (Sala moja tu ya) fardhi kusudi (bila ya udhuru wowote) mpaka wakati
wake (Sala hiyo) ukatoka, anakuwa kafiri”.
Hadithi
zifuatazo zinaelezea juu ya hukmu ya kuuliwa kwa Taariku ssalaat (Asiyesali);
Kutoka kwa
Ibni Abbas (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
“Heshima ya
Uislam na misingi ya dini ni mitatu, juu yake misingi hiyo umejengeka Uislam.
Atakayeacha mojawapo anakuwa kafiri na damu yake halali;
Kushuhudia
kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah,
Na Sala
zilizofaradhishwa,
Na Funga ya
Ramadhani”.
Abu Yaala
Na kutoka kwa
Ibni Omar (Abdillahi bin Omar bin Khattab (Radhiyallahu anhum) kuwa Mtume (SAW)
amesema;
“Nimeamrishwa
nipigane vita mpaka pashuhudiwe kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa
Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na isimamishwe Sala
na itolewe Zaka, watakapofanya
hivyo, itakingika kwangu damu zao na mali zao ila kwa haki ya Uislam na hesabu
yao iko kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka”.
Bukhari na
Muslim”
RAI ZA BAADHI
YA WANAVYUONI
Anaendela
kusema Sayed Sabeq kuwa;
“Kutokana na
Aya pamoja na Hadithi zilizotangulia, inatubainikia kuwa Asiyesali ni kafiri na
kwamba damu yake ni halali. Hata hivyo baadhi ya maulamaa waliotangulia na wa
siku hizi wakiwemo Imam Abu Hanifa na Imam Shafi na Imam Ahmed wanasema kuwa
hawi kafiri moja kwa moja, bali anahesabiwa kuwa ni mtu fasiq na anakamatwa na
kutubishwa na akikataa kutubu basi maulamaa wote hao wanasema kuwa mtu huyo anahukumiwa
kuuliwa.
Anasema
Annawawi katika Sharhi Muslim;
“Anakatwa
kichwa chake kwa upanga”.
Imam Abu
Hanifa anaona kuwa aliyertadi na akastahiki kuhukumiwa kuuliwa ni yule tu
anayeikanusha Ibada hiyo ya Sala, lakini yule anayeacha kusali kwa uvivu tu au kwa
kujishughulisha na dunia, huyo si kafiri bali ni fasiq na hukmu yake ni
kumhamisha mbali na mji wake, wakiegemea dalili zinazobeba maana kwa ujumla
kama vile kauli Yake Subhanahu wa Taala aliposema;
“Hakika
Mwenyezi Mungu hasamehe(dhambi ya) kushirikishwa na kitu, lakini Yeye husamehe
yasiyokuwa hayo kwa amtakaye”.
Annisaa - 114
Na hadithi
iliyosimuliwa na Abu Huraira kuwa Mtume (SAW) amesema;
“Kila Mtume
ana dua yake inayokubaliwa. Kila Mtume akafanya haraka kuiomba dua yake hiyo.
Ama mimi nimeiweka dua yangu kwa ajili ya kuwaombea shafaa ummati wangu siku ya
Kiama, ataipata Inshaallah kila aliyekufa na asimshirikishe Mwenyezi Mungu na
chochote”.
Na hadithi
nyingine za mfano huo.
Maulamaa
wengine wakasema kuwa hauliwi mtu kwa ajili ya kutosali, na hawa wameegemeza
hoja zao kutokana na hadithi iliyomo ndani ya Bukhari na Muslim isemayo;
“Si halali
kumwaga damu ya Muislamu ila kwa mojawapo ya matatu; Mzinzi aliyekwishaoa,
nafsi kwa nafsi (aliyeuwa auwawe) na aliyertadi (aliyetoka katika dini) na
kujitoa katika jamii ya Kiislam”.
Wanasema kuwa
hapa Mtume (SAW) hakumtaja asiyesali kuwa ni miongoni wa waliohalalishwa damu
yao.
MAJADILIANO
BAINA YA IMAM SHAFI NA IMAM AHMED
Imepokelewa
kuwa Maimam waiwili wakubwa, Imam Shafi na mwanafunzi wake Imam Ahmed bin Hanbal
walijadiliana juu ya maudhui haya ya mtu asiyesali, na majadiliano hayo
yalikwenda kama ifuatavyo;
Imam Shafi;
“Ewe Ahmed!
Unasema kuwa anayeacha kusali anakuwa kafiri?”
Imam Ahmed;
“Ndiyo nasema
hivyo”.
Imam Shafi;
“Ikiwa
atakuwa kafiri, vipi atarudi katika Uislam?”
Imam Ahmed;
“Kwa kutamka;
‘Ash-hadu an laa ilaaha illa Llah Muhammadan Rasulu Llah”.
Imam Shafi;
“Lakini mtu
huyo hajaikanusha shahada hiyo”.
Imam Ahmed;
“Anarudi
katika Uislam kwa kusali”.
Imam Shafi;
“Sala ya
kafiri haikubaliwi, na kafiri hahesabiwi kuwa ni Muislamu hata kama atasali”.
Imam Ahmed
akanyamaza.
TAHAKIKI YA
IMAM ASHAUKANI
Anasema
Ashaukani kuwa;
Kwa hakika
asiyesali ni Kafiri, kwa sababu hadithi zote zilizopokelewa katika maudhui haya
zinamwita hivyo (kuwa ni kafiri), na mpaka uliowekwa baina ya mtu anayestahiki
kuitwa kafiri na yule asiyestahiki kuitwa kafiri ni ‘Sala’.
MUHAMMAD
FARAJ SALEM AL SAIY