AQIQAH

Shukrani zote ni zake Mwenyezi Mungu, na sala na salam zimfikie Mtume wake Muhammad (SAW) pamoja na Aali zake na Sahaba zake wakarimu (Radhiyallahu anhum).

Wa baad,

Aqiqah ni mbuzi anayechinjwa pale mtu anapopata mtoto, na maulamaa wengi wanasema kuwa kitendo hicho ni Sunnah muakkadah (Sunnah iliyotiliwa nguvu).

Imeelezwa na Imam Malik katika Muwatta'a kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alisema;

"Aliyepata mtoto akataka kuchinja na achinje."

Na imepokelewa na maulamaa wa Ahlu ssunah kutoka kwa Samarah (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Kila mtoto aliyezaliwa yupo rahani kwa mbuzi wake, anachinjiwa siku ya saba kisha anakatwa nywele kisha inatolewa sadaka uzito wa nywele zake kwa fedha au kilicho mfano wake."

Mtoto wa kiume anachinjiwa mbuzi wawili na wa kike mbuzi mmoja, kama ilivyopokelewa na Attirmidhiy kutoka kwa mama wa Waislamu Bibi Aisha (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliwaamrisha wachinje kwa ajili ya mtoto wa kiume mbuzi wawili wasio na kilema na kwa ajili ya mtoto wa kike mbuzi mmoja."

Ni Sunnah kuchinja siku ya saba tokea kuzaliwa mtoto. Kutoka kwa Al Baihaqiy kutoka kwa Buraidah (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alisema;

"Aqiqah huchinjwa siku ya saba."

Na kama kutokana na sababu yoyote ile haikuwezekana katika siku ya saba, basi mtu anaweza kuchinja siku yeyote ile atakapojaaliwa, bila ya kuweka siku maalum, isipokuwa kama itawezekana kufanya haraka na kuchinja katika siku hiyo ya saba, hiyo itakuwa afadhali.

 

Aina ya Mbuzi;

Mbuzi wa aina yoyote anaweza kuchinjwa, sharti asiwe na kilema, yaani asiwe kiguru wala kipofu wala aliyekatika pembe au sikio au aliyevunjika sehemu yoyote ya mwili wake nk.

Isiuzwe nyama yake wala sufi yake wala ngozi yake wala chochote katika mwili wake.

Nyama inaliwa na watu wa nyumba na kutolewa sadaka na kugawiwa ndugu na jamaa na marafiki.

Imam Malik anaona kuwa si vizuri kupikwa nyama na kualikwa watu kuja kuila, na pia anaona kuwa inajuzu kuvunjwa mafupa yake na kupikwa na kuliwa

 

Ama ile hadithi inayosema kuwa si vizuri kuvunja mifupa kwa ajili ya usalama wa mtoto mchanga Imam watu wa madhehebu ya Imam Malik wanasema kuwa hadithi yake si sahihi, na hadithi yenyewe inasema hivi;

"Amesema Bibi Aisha (RA) kuwa Sunnah ni kuchinja mbuzi wawili wasio na kilema kwa ajili ya mtoto wa kiume na mmoja kwa ajili ya mtoto wa kike, kisha ipikwe bila kuvunjwa mafupa yake."

Na hadithi hii imetolewa na Al Baihaqiy na Al Hakim na kusimuliwa na Ataa (RA).

Anasema Imam Al Dhahabiy kuwa hadithi hii ni sahihi, lakini Imam Annawawiy katika Majmua juzuu ya 8 hadithi nambari 407 anasema;

"Hadithi hii haina nguvu na haiwezi kuwa dalili."

Al Albani yeye anasema;

"Inavyoelekea isnadi ya hadithi hii ni sahihi, isipokuwa kwangu mimi ina ila mbili;

Ya kwanza kukatika kwa isnadi, na ya pili kuongezeka kwa maneno, kwani ile kauli isemayo; "Ipikwe bila kuvunjwa mafupa", ni maneno ya Ataa (na si maneno ya Mtume (SAW)."

Irwaa lghaliyl takhrij ya hadithi za Subuli ssalaam (4\392-395).

 

Ama Imam Shafi na Imam Ahmed, wao wanaona kuwa hapana ubaya kuvunja mafupa yake, kwani hapana hadithi sahihi inayokataza, isipokuwa wao wanaona kuwa ni bora kutovunja