Kusamehe
Vijana watatu walikwenda mbele ya Khalifa wa Waislamu Umar bin Al Khattab (Radhiya Llahu anhu) wakiwa
wamemkamata mtu waliyemfunga kamba. Wakasema kumwambia Umar (Radhiya Llahu
anhu):
"Mtu huyu
amemuuwa baba yetu na amekiri juu ya
jambo hilo, isipokuwa ametuomba tumpe siku tatu ili aweze
kusafiri kwa wanawe kwa ajili
ya kuwajulisha juu ya hazina
aliyoifukia mahala ambapo hapana anayepajuwa
isipokuwa yeye peke yake".
Sahaba mmoja aitwae Abu Dhar Al Ghafariy (Radhiya Llahu anhu)
akamdhamini mtu huyo juu ya
kuelewa kwake vizuri kuwa iwapo
mtu huyo hatorudi basi atauliwa
yeye badala yake.
Mtu huyo hakurudi mpaka
baada ya kukaribia sana
kumalizika muda wa siku tatu
hizo, na watu wakawa na
wasi wasi asije Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)
akauliwa badala yake.
Dakika za mwisho za
siku ya tatu
akawasili mtu huyo akiwa amejaa
vumbi na
huku uso wake ukionesha dalili za kuchoka sana.
Umar (Radhiya Llahu anhu)akamuuliza:
"Ilikuwaje
ukarudi wakati ungeweza kukimbia?"
Akajibu:
"Nilihofia
pasije pakasemwa kuwa; Watu wenye
ahadi za kweli hawapo tena."
Kisha Umar (Radhiya Llahu
anhu)akamgeukia
Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)na
kumuuliza:
"Na wewe
ilikuwaje ukakubali kumdhamini mtu huyu wakati humjuwi?"
Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)akasema:
"Nilihofia
pasije pakasemwa; Wakarimu na wenye
moyo wa kishujaa
hawapo tena."
Ndipi wale vijana watatu wakasema:
"Na sisi tumemsamehe mtu huyu ili
pasije pakasemwa; 'Hawapo tena watu
wenye kusamehe juu ya kuwa
na uwezo wa kulipa kisasi."