DUA

Unapokuwa ndani ya chombo chako cha baharini ukakumbana na upepo mkali, dhoruba na mawimbi makubwa ya kutisha, usiingiwe na hofu, kumbuka kuwa yupo anayekuona na kukusikia, sema; "Yaa Allah".

Ukipotea njia, popote utakapokuwa, porini au jangwani na kiza kikaanza kuingia, usikubali kuvaliwa na hofu, sema; "Yaa Allah".

Unapokumbana na misiba, masaibu au matatizo yasiyokwisha, sema; "Yaa Allah".

Unapokuwa na shida ukashindwa kumpata wa kukusaidia na kila unayemuendea kwa ajili ya kumuomba msaada anakufungia mlango usoni pako, na njia zote ukazikuta zimefungwa hata ardhi ikawa dhiki kwako juu wasaa wake, sema; "Yaa Allah".

Unapoumwa, sema; "Ya Allah".

Unapolala juu ya kitanda ukijijuwa kuwa roho yako inakaribia kutoka na kurudi kwa Mola wake aliyeiumba, sema; "Ya Allah".

Unapokuwa katika hali yoyote ile, sema: "Yaa Allah".

Kwake Yeye linapanda neno jema na dua halisi na kilio cha kweli na chozi la aliyedhulumiwa.

Kwa jina Lake tu watu wanaomba na kutegema, na jina Lake tu watu wanalidhukuru ili nyoyo zilainike na ili zielekee na kupata matumaini na utulivu unaotoka Kwake.

"Ya Allah", Jina bora kupita majina yote na utajo bora kupita utajo wowote;

Mwenyezi Mungu anasema;

"Je, unamjua (mwingine) mwenye jina lake (hili la 'Allah' aliye kama Yeye)?"

MARYAM _ 65

Ushindi, hekima, nguvu na uwezo, wote ni wake Yeye tu Subhanahu wa Taala.

Mola wetu, tujaalie shida yetu igeuke kuwa ladha nzuri, na huzuni yetu iwe furaha, na hofu yetu iwe amani na matumaini.

Mola wetu ziburudishe nyoyo zetu kwa barafu ya yaqini na uuzime moto ulio ndani ya nyoyo zetu kwa maji ya Imani.

Ya Allah, tumiminie kwa jicho lako lisilolala rehma na amani itokayo Kwako, na utumimine utulivu katika nafsi zetu zilizojaa wahka na uzipe ushindi wa karibu.

Ya Allah, kwa Nuru yako waongoze waja wako ili waweze kuiona haki na kuifuata, na waongoze waliopotea mpaka waweze kuifika njia Yako.

Ya Allah, tuondolee wasiwasi uliotujaa nyoyoni mwetu na badala yake uzijaze nyoyo hizi nuru ya kweli, na utuondolee dhiki na huzuni zilizomo nafsini mwetu na utubadilishie kwa kutujaza furaha na tumaini jema, kwani hakuna wa kujikinga kwake kutokana na wasiwasi na dhiki na huzuni ila Wewe tu, Subhanahu wa Taala, na hakuna wa kumuomba na wa kumtegemea ila Wewe tu, Subhanahu wa Taala.

WALAA HAULA WALAA QUWWATA ILLA BILLAH

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY