UKEWENZA
Mwenyezi Mungu anasema;
“Na kama mkiogopa kutowafanyia uadilifu
mayatima (basi ogopeni vile vile kutowafanyia uadilifu wanawake). Basi oeni
mnaowapeda katika wanawake (maadamu mtawafanyia insafu). Wawili au watatu au
wane (tu). Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi (oeni) mmoja tu.”
Surat an Nisa - 3
Mwenye kuichunguza aya hii vizuri
ataona kuwa Mwenyezi Mungu hapa hakutufaridhishia kuoa zaidi ya mke mmoja,
isipokuwa ameruhusu (ametowa rukhsa) kufanya hivyo kwa mwenye uwezo wa kutimiza
masharti yake, nikimaanisha kuwa katika lugha ya fiq-hi, kufaridhisha na
kuruhusu ni mambo mawili tofauti.
Bila shaka anayekijuwa zaidi chombo
chochote kile ni yule aliyekitengeneza chombo hicho, na bila shaka mwenye
kumiliki kitu chochote kile, ndiye mwenye haki ya kukifanya vile anavyoona
sawa.
Kwa vile Mwenyezi Mungu ndiye
aliyetutengeneza (aliyetuumba), basi
bila shaka Subhanahu wa Taala ndiye Mwenye kutujuwa zaidi kuliko
mwengine, na kwa vile Yeye ndiye Mwenye kutumiliki, basi bila shaka Yeye ndiye
Mwenye haki ya kutuwekea sheria yoyote ile anayoiona kuwa ndiyo sawa kwa ajili
yetu, na bila shaka Mwenyezi Mungu hamdhulumu mja wake isipokuwa waja ndio
wenye kudhulumu nafsi zao.
Makala yafuatayo nimeyafasiri kutoka
katika kitabu kiitwacho; ‘Nahwa thaqaafa Islamiyah Asiylah’, kilichoandikwa na
mwanachuoni maarufu Dr. Omar Suleiman Al Ashqar:
Katika kitabu chake hicho Dr. Al Ashqar
anasema;
“Maadui wa Uislamu wanadai kuwa kuoa
mke zaidi ya mmoja ni dhulma kwa wanawake na kwamba si jambo la haki na kwamba
rukhsa hii ya kuowa zaidi ya mke mmoja ni dharau kwa kinamama na kwamba wanaume
wanapewa haki zaidi ambazo kina mama nao hawapewi haki hizo na kwamba rukhsa
hii ni sababu kubwa ya kutengana kwa familia nk.
Kwanza - Ningependa kuwajulisha ndugu
zangu kuwa jambo hili limewekewa sheria na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala
katika kitabu chake na kwamba Mtume (SAW) ametenda hivyo, yeye na Sahaba zake
(RA) halikadhalika, na kwamba umma wote umekubaliana juu ya usahihi wake, na
Muislamu lazima aitakidi kuwa sheria za Mwenyezi Mungu amezileta kwa maslahi ya
viumbe vyake, na kwamba hapana sheria nyingine yoyote ile inayoweza kuwafaa
wanadamu kuliko sheria waliyowekewa na Mola wao Subhanahau wa Taala na kwamba
sheria yoyote ile inayokwenda kinyume na sheria ya Mwenyezi Mungu ni batil na
yenye kupotosha.
Pili - Kuoa mke zaidi ya mmoja ni jambo
la dharura katika jamii na hii ni kwa sababu takwimu zote zinaonyesha kuwa
idadi ya wanawake ni kubwa zaidi kuliko idadi ya wanaume, na kwa ajili hiyo
kukataza kuoa mke zaidi ya mmoja kutaifanya idadi kubwa ya wanawake kukaa bila
kuolewa, jambo litakaloifanya idadi hiyo kubwa ya wanawake hao kusukumwa katika
ulimwengu wa zina na kufanya yale yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, na
kutokana na hayo mwanamke atageuka kuwa ni chombo cha kuchezewa mikononi mwa
wanaume na kugeuka kuwa mwenye kumstarehesha kila mwenye uwezo wa kumlipa, na
ataishi bila ya kupata haki anazopata mke.
Kisha itakuwaje hali ya watoto
waliozaliwa nje ya ndoa?
Bila shaka baba zao hawatawatambua wala
kuwakubali na watageuka kuwa mizigo kwa mama zao.
Mwanamke ataweza kuepukana na mtoto wa
aina hiyo kwa njia ya kutoa mimba, au baada ya kumzaa kwa njia ya kumweka mtoto
mahali popote ili aokotwe na mtu yeyote yule, au kwa njia ya kumwacha katika
sehemu za kulea mayatima mahali atakapokosa ulezi wa kibinadamu na kukosa
mapenzi ya mama na malezi ya baba na kwa ajili hiyo mtoto huyo hatokuwa na raha
katika nafsi yake.
Takwimu zinazotolewa na nchi
zinazokataza mtu kuowa zaidi ya mke mmoja zinastusha sana. Katika mwaka 1901 ulifanywa
mkutano kwa ajili ya kuzungumzia tatizo la watoto wachanga wanaotupwa, na pia
juu ya mimba zinazotolewa na juu ya sababu za kuongezeka kwa tatizo hilo, na
takwimu iliyotolewa juu ya mji mmoja tu katika miji ya Kifaransa nchi ambayo
watoto wanalelewa kwa msaada wa serikali, basi idadi ya watoto hao wanaotupwa
ilifikia idadi ya elfu hamsini.
Na katika ripoti ya Umoja wa mataifa
iliyotolewa katika mwaka 1959 imeeleza kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya
ndoa katika ulimwengu imefikia sitini katika mia 60%, na katika dola nyingine
mfano nchi ya Panama, idadi hiyo imepindukia sabini na tano katika mia 75%.
Hii ndiyo athari ya kukataza watu kuowa
zaidi ya mke mmoja. Si ingekuwa bora kwa mwanamke kuolewa akawa mke wa pili au
wa tatu na akawa ana mahali pake katika jamii, na watoto wake wakawa na nasaba
yao na wakaweza kujinasibisha na kulelewa na baba yao bila upendeleo baina ya
ndugu zao?
Bila shaka katika kuruhusu kuowa zaidi
ya mke mmoja mna faida kubwa kwa wanawake, ama katika kuharimisha jambo hili,
ndani yake mna hasara kubwa.
Tatu - Ukiuchunguza uwezo wa kupata
mtoto, utaona kuwa mwanamke anapofikia umri wa miaka hamsini au hata kabla ya
hapo, uwezo wake wa kuzaa unasimama. Amma mwanamume anaendelea kuwa na uwezo wa
kuzaa hata kama ataishi miaka mia.
Mwanamke hujiwa na damu ya hedhi kila
mwezi kwa muda unaofikia siku saba mara nyingine, na uwezo wake wa kuingiliana
na mumewe unapungua sana pale anapopata mimba kwa muda wote wa miezi tisa,
kisha huzaa na hatimaye huwa katika nifasi kwa muda unaofikia siku arubaini, na
bila shaka ni haramu kwa mwanamume kumsogelea mwenye hedhi au mwenye nifasi.
Ukizihesabu siku ambazo mwanamke hawi
na uwezo wa kukutana na mumewe, utaona kuwa ni siku nyingi sana zinazofikia
theluthi nzima ya umri wake, wakati mwanamume hafikiwa na yote haya.
Kuwakataza wanaume kuowa zaidi ya mke
mmoja ni kuwadhulumu wanaume hao, kwa sababu mwanamume kimaumbile hakumbani na
yale anayokumbana nayo mwanamke, na pia kwa sababu yeye anakuwa na uwezo na
nguvu za kupata mtoto wakati mwanamke anapokuwa hana uwezo huo, na kwa ajili
hiyo unapomkataza kuoa zaidi ya mke mmoja unaunyima umma wa Kiislamu kupata
ongezeko la watu.
Nne – Wakati mwengine mwanamke hupata
maradhi ya kuondokewa na hamu ya kuingiliana na mwanamume, lakini wakati huo
huo mume na mke hupendelea kuendelea na uhusiano wao wa mtu na mkewe na
kuendelea kuyahifadhi mapenzi na huruma iliyopo baina yao. Ikiwa itawekwa
sheria ya kukataza kuowa mke zaidi ya mmoja, basi mwanamume atajikuta
amelazimika kumtaliki mke huyo ili aruhusiwe kuowa mke mwingine.
Tano – Kuowa zaidi ya mke mmoja ni
nidhamu iliyokuwepo tokea hapo zamani, kwani katika Taurati imeandikwa kuwa
Nabii Ibrahim na Nabii Yaakubu na Nabii Suleiman na Nabii Daud , wote hawa
waliowa zaidi ya mke mmoja, na katika Injili hakuna mahali palipokataza
ukewenza, bali sheria zilizotangulia juu ya kuowa mke zaidi ya mmoja hazikuwa
zimefungwa na masharti yoyote, lakini Qurani ikaja na msimamo wa kati na kati,
ikaruhusu kuowa, lakini wakati huo huo ikaweka idadi maalum na masharti maalum.
DHULMA KWA WANAWAKE?
Miongoni mwa wanawake wapo ambao
hawakubali waume zao kuwaolea juu yao wake wengine, na jambo hili linasababisha
matatizo mengi na hitilafu nyingi.
Sisi hatukatai kuwa jambo hili linaweza
kuleta matatizo na hitilafu, lakini maslahi yanayopatikana ndani yake ni
makubwa sana kuliko madhara yake, bali madhara hayo hayafikii hata asilimia
moja katika elfu (moja juu ya elfu) ya faida inayopatikana ndani yake. Isitoshe
Uislamu haukuyapuuza matatizo yanayoweza kupatikana, na kwa ajili hiyo hakubaliwi
mtu kuowa mke mwingine ikiwa hana uwezo wa kuwasimamia wake zake hao, kisha
mwanamume akaamrishwa kuwa muadilifu baina ya wake zake katika makazi na
chakula na mavazi na pia ukamuamrisha mwanamume awe muadilifu baina ya watoto
wake, kwani haijuzu kwa mwanamume kuwabaguwa wanawe kwa hali yoyote ile. Yote
haya kwa ajili ya kuzuwia mtafaruku wowote ule unaoweza kupatikana katika kuowa
mke zaidi ya mmoja.
KWA NINI MWANAMKE NAYE HARUHUSIWI
KUOLEWA NA MUME ZAIDI YA MMOJA?
Kwa mwanamke kuolewa na mume zaidi ya
mmoja ni jambo lililoharimishwa kisheria, ni jambo ovu ki khulqa hata kwa
kulifikiria tu, kwani mwanamke ni mahali pa uzazi, na ikiwa atakuwa na waume
wengi, basi maji ya uzazi yatachanganyika na nasaba zitapotea.
Mwanamume anaweza kuwa na wake wengi na
akawa na uhakika kuwa watoto wote ni wake, lakini kwa upande wa mwanamke jambo
hilo haliwezekani.
Kisha mwanamume ndiye mwenye kumsimamia
mwanamke, sasa ikiwa mwanamke mmoja atakuwa na waume wengi, atamtii yupi kati
ya waume wote hao?
Isitoshe wanawake wengi hawana uwezo wa
kutimiza mahitajio ya mwanamume mmoja tu. Vipi basi atakuwa na uwezo wa
kutimiza mahitajio ya wanaume wengi?”
Mwisho wa maneno ya Sheikh Al Ashqar
Wallahu taala aalam
Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa
Barakatuh
Ndugu yenu
Muhammad Faraj Salem