TAQWA

 

Maana ya Taqwa

Mara nyingi tunalisikia neno 'Taqwa', likitamkwa. Utamsikia mtu akisema: "Mtu fulani ni 'Taqiy' kweli" , au "Ittaqiy Llah". Leo tulidurusu neno hili na maana yake.

'Taqwa', UchaMungu, asili yake linatokana na neno la Kiarabu "Wiqaya", na maana yake ni kujikinga.

Na katika kamusi la dini, neno hili maana yake ni 'Ucha Mungu', nako ni kujikinga, kujiepusha na maasi, pamoja na kumtii Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.

Sayyidna Umar (Radhiya Llahu anhu) alipoulizwa na Ubayyi bin Kaab (Radhiya Llahu anhu):

"Nini maana ya Taqwa?".

Alisema:

"Uliwahi kupita njia iliyojaa miba?"

Akajibu:

"Ndiyo".

Umar akamuuliza:

"Ulipitapitaje?"

Ubayyi akasema:

"Nilipania nikajitahidi."

Umar akamuambia:

"Basi hiyo ndiyo Taqwa".

Na sisi katika wakati wetu huu tunatembea juu ya njia iliyojaa miba. Ukitizama kuliani miba imejaa, kushotoni utaona mitihani mikubwa, ukitizama chini au juu, kote kumejaa miba. Kwa ajili hiyo hatuna budi kupania na kujitahidi sana ili tupite kwa salama bila ya kujichoma. Kwani mdharau mwiba mguu huota tende.

 

Sayyiduna Ali (Radhiya Llahu anhu), yeye amesema:

"Taqwa ni Mwenyezi Mungu akuone pale anapotaka kukuona, na asikuone pale asipotaka kukuona."

Na akasema:

( )

"Taqwa ni kumuogopa Mwenyezi Mungu (Al Jaliyl), na kufuata wahyi ulioteremshwa (At tanziyl), na kukinai kichache (Al qaliyl), na kujitayarisha na siku ya kuondoka (Yawm al Rahiyl)."

 

Wapo wanaowaogopa wanadamu kuliko wanavyomuogopa Mwenyezi Mungu Al Jaliyl, na wapo wenye kutumia jitihada kubwa na wakati wao wote katika kujifunza mambo ya kidunia, lakini hawataki kupoteza hata wakati mchache katika kujifunza juu ya wahyi uliyoteremshwa At tanzyl, na wengi kati yetu hatukinai kichache tulichojaaliwa Al qaliyl, bali hatukinai hata kingi. Na hatujitayarishi na siku ya kuondoka Yawm al Rahiyl, bali tunajisahau na kuzama katka maasi kama kwamba tutaishi milele.

Hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni ghali sana, hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni Pepo.

 

Mwalimu na mwanafunzi wake

Baada ya kumsomesha muda usiopungua miaka 30, Sheikh alimuuliza mwanafunzi wake:

"Umejifunza nini kwangu miaka yote hii?"

Mwanafunzi akajibu:

"Kusema kweli sikujifunza isipokuwa machache tu."

Sheikh akasema kwa mshangao:

"Nimekusomesha miaka 30, kisha unaniambia hukujifunza isipokuwa machache tu! Haya nielezee hayo machache ni yepi?"

Mwanafunzi akasema:

"Niliuangalia ulimwengu. Nikaona kila kitu kinahitajia wa kukiendesha. Kisha nikawaaangalia wanadamu, nikawaona wanawategemea wengine wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Na nilipofahamu kutoka kwako ewe ustadhi wangu kuwa hapana kinachoweza kuwa bila ya Mwenyezi Mungu kutaka kiwe, nikaacha kumtegemea ye yote isipokuwa Mwenyezi Mungu."

Sheikh akasema:

"Enhe? Endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Kisha nikawaangalia viumbe. Nikaona kila mmoja ana kipenzi chake. Wanaishi pamoja, wanacheza, wanasafiri na kurudi pamoja katika safari zao zote. Lakini katika safari ile ya mwisho, mtu anapowasili kaburini pake, anaingia mle ndani peke yake, na vipenzi vyake vyote vinabaki nje. Hawawezi kumfuata. Nikaona bora nijaalie kipenzi changu kiwe amali njema zangu ili ziwe nami nitakapokuwa kaburini peke yangu."

Sheikh akasema:

"Ahsante! Ehe? Endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Kisha nikawaangalia wanadamu. Nikawaona kila mmoja pesa ikishaingia mkononi mwake haitoki. Watu wake wenye haja hawapati haki zao. Masikini hawapati haki zao. Kisha nikatafakari juu ya maneno ya Mwenyezi Mungu katika Suratul Nahl aya ya 96 isemayo:

"Mlivyonavyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu (vya jaza yenu) ndivyo vitavyobakia."

Nikawa kila kinachoingia mikononi mwangu hukitoa ili kipate kubaki huko kwa Mwenyezi Mungu."

Kwa kukifafanua zaidi kifungu hiki, tuangalie namna gani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alivyokuwa akitoa.

Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) baada ya kuchinja mbuzi na kuigawa nyama yote alimuuliza Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) kama bado pana chochote kilichosalia. Bibi Aisha akasema:

"Limebaki hili bega tu."

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akamsahihisha kwa kumuambia:

"Bali ile tuliyoigawa ndiyo iliyobaki ewe Aisha."

 

Katika hadithi nyingine, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Kipo kingine unachofaidika nacho katika mali yako isipokuwa kile unachokula kikaoza tumboni na unachokivaa kikachakaa na unachotoa sadaka kikabaki?"

Sheikh akasema:

"Enhe, endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Nikawatizama viumbe. Nikawaona kila mmoja anamuonea husuda mwenzake kwa kile alichokipata. Nikakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu katika Suratul Zukhruf aya ya 32 yasemayo:

"Je, wao wanaigawa rehema ya Mola wako (wakampa wampendae na kumnyima wamtakae?) Sisi tumewagawiya maisha yao katika uhai wa dunia na kuwainua baadhi yao daraja kubwa juu ya wengine."

"Nikaacha kuwahusudu viumbe.

Sheikh akasema:

"Ahsante. Endelea."

Mwanafunzi akasema:

"Kisha nikawatizama wanadamu. Nikaona tonge imewadhalilisha na kuwafanya wapige mbizi katika mambo ya haramu. Nikakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu katika Surat Hud aya ya 6 aliposema: "Na hakuna kiumbe cho chote katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Mwenyezi Mungu. Na anajua makao yake ya milele na mahali pake pa kupita tu.Yote yamo katika kitabu kinachodhihirisha (kila kitu)."

Nikafahamu kuwa riziki yangu hawezi kuichukua mwengine, na hapo moyo wangu ukatulia. "

Katika kukisherehesha kifungu hiki tuzingatie maneno ya Hassan Al-Basri (Radhiya Llahu anhu) mmoja katika Maulamaa wa At-Tabiina. (waliowaona Masahaba (Radhiya Llahu anhum) lakini hawakumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam).

Hassan Al Basri alisema:

"Nilipotambua kuwa amali zangu hapana mwengine anayeweza kunifanyia, nikapania kuzifanya mwenyewe. Na nilipotambua kuwa riziki yangu hawezi mwengine kuichukuwa, moyo wangu ukatulia. Na nilipotambua kuwa Mola wangu ananiona, nikaona haya asije akaniona nikiwa katika hali ya kumuasi.

Moyo

Mwenyezi Mungu anasema:

" Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.

Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi."

Ash Shua'raa- 87-89

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Hakika Mwenyezi Mungu ana vyombo vyake ndani ya viumbe vyake wanaoishi juu ya ardhi, na vyombo vya Mola wenu ni nyoyo za Wachamungu".

Hadithi hii imo katika Silsilat Alsahiha - Hadithi Nambari 1691.

Moyo unapambana na misukosuko inayoudhoofisha, na wakati huo huo unatenda amali njema zinazoupa nguvu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Kila moyo una kiwingu kama kiwingu cha mwezi. Utauona mwezi unaangaza, kisha ghafla unapitiwa na kiwingu na kuifunika nuru yake."

Sahih Al Jamea.

Moyo unapitiwa na vijiwingu vinavyoizuwia nuru yake isiweze kuangaza wala kupokea mwangaza. Na vijiwingu hivyo ni madhambi. Muislamu anapotenda dhambi, moyo wake unadhoofika na nuru yake inatoweka, na anapotubu na kuomba maghfira, moyo unarudi tena kuwa na nguvu na kuangaza. Na hii ndiyo sababu Imani ikawa inaongezeka na kupungua.

Inaongezeka kwa tw'aa na inapungua kwa maasi.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Hakika Muislamu anapotenda dhambi, linaingia katika moyo wake doa jeusi. Na akitubu na kuomba maghfira doa hilo huondoka. Akiendelea kufanya madhambi, madoa nayo yanaongezeka na kuwa mengi mpaka moyo unapiga weusi. Na hiyo ndiyo Raanna aliyoitaja Mwenyezi Mungu aliposema:

"Sivyo hivyo! Bali yametia kutu (Raanna) juu ya nyoyo zao (kwa maovu) waliyokuwa wakiyachuma ".

Al Mutaffifiyn 14

Imam Ahmad na Attirmidhy katika Al Jamia

Na akasema:

"Katika mwili mna kipande cha nyama, kikitengenea na mwili wote unatengenea, na kikiharibika na mwili wote unaharibika, kipande hicho ni Moyo".

Na akasema:

"Kwa yakini Moyo unachakaa katika kifua cha mmoja wenu kama nguo inavyochakaa ".

 

Ndugu zangu Waislamu; jueni ya kuwa hatokuwa katika amani siku ya Kiama isipokuwa yule tu atakayehudhuria mbele ya Mola wake akiwa na moyo safi.

Mwenyezi Mungu anasema:

" Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.

Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.

Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi."

Ash Shua'raa- 87-89

 

Ni upi basi Moyo safi?

Maulamaa wamekhitalifiana katika kulifasiri neno; 'Moyo safi'.

Amesema Qadata:

"Moyo safi ni ule ulioepukana na shaka pamoja na shirki. Ama dhambi ni jambo lisiloweza kuepukika."

Saeed bin Musayib amesema:

"Moyo safi ni moyo wa Muislamu aliyeamini kikweli, kwa sababu moyo wa kafiri na wa mnafiki una maradhi.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Nyoyoni mwao mna maradhi."

Al Baqarah 10

Ama Abu Uthman Al Sayaariy yeye amesema:

"Moyo safi ni ule ulioepukana na uzushi na uliotulia katika kuifuata Sunnah."

Al Dhahaak amesema:

"Moyo safi ni ule uliojitakasa."

Na kauli hii inajumuisha maana zote zilizotangulia kutajwa. Kwani moyo uliojitakasa ni ule uliojiepusha na kila kauli na kitendo kiovu, na ni ule unaosifika kwa kila sifa njema.

Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa Moyo safi ni ule wenye kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu, uliojiepusha na kila kinachokwenda kinyume na maamrisho Yake Subhanahu wa Taala. Ni Moyo uliojisalimisha kwa Mola wake ukaacha kujikurubisha na kumnyenyekea au kumuogopa yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Ni ule wenye kujiepusha na makatazo ya Mwenyezi Mungu na kufuata maamrisho Yake. Uliosalimika na shirki, kiburi kuipenda dunia, tamaa, matusi, roho mbaya. Ni Moyo wenye kuipenda akhera yake kuliko unavyooipenda dunia.

Huu ndio Moyo safi unaompendeza Mwenyezi Mungu.

Moyo huu uko Peponi tokea hapa duniani, na pia baada ya kufa unapokuwa katika maisha ya barzakh, na unaingia Peponi milele siku ya Kiama baada ya kuhesabiwa.

 

Imepokelewa kuwa mmoja katika watu wema aliwausia watoto wake kwa kuwaambia:

"Enyi wanangu msiwe wenye kulaaniana, kwa sababu Nabi Ibrahim hakuwa mwenye kuwalani watu, na Mola wake amemsifia aliposema:

"Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima."

Ass'affat 84

Anasema Sayiduna Aly (Radhiyallahu anhu):

"Jifunzeni ilimu ili muwe watu wake. Jueni kuwa dunia tunaiacha nyuma na akhera tunaikabili, na kila moja kati ya nyumba mbili hizo ina watu wake. Basi kuweni watu wa akhera na wala msiwe watu wa dunia.

Waloikinai dunia, wameijaalia ardhi yake kuwa busati, udongo kuwa tandiko, na maji kuwa pambo lao.

Mwenye kuipenda akhera lazima ajiweke mbali na matamanio, na mwenye kuuogopa moto ajiweke mbali na yaliyoharamishwa.

Mwenye kuitaka Pepo akimbilie kumtii Mwenyezi Mungu, na aliyeikinai dunia hayapi umuhimu wowote masaibu yake.

Jueni kuwa Mwenyezi Mungu ana waja wake, amewahifadhi wasifanye shari, nyoyo zao za huzuni, nafsi zao zimekinai, matakwa yao machache, wamesubiri siku chache ili wapata raha za milele."

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Wataingia Peponi watu, nyoyo zao mfano wa nyoyo za ndege."

Muslim

"Imani inaongezeka na kupungua".

Maulamaa wanasema:

'Imani inaongezeka kwa kufanya mema na inapungua kwa kufanya maasi.'

Moyo uliofunikwa na kutu 'Raana', haupo tayari kuyasikiliza na kuyakubali mafundisho ya Mwenyezi Mungu, bali unadhikika kila unaposikia neno la haki. Na kinyume chake unaridhika na kufurahi kila unaposikia maneno ya batil, kwa sababu moyo huo mlinzi wake ni shetani.

Lazima utambue kuwa maadui wako wakubwa ni shetani na matamanio ya nafsi yako. Usiuendekeze wala usiudekeze, kwa sababu katika kuuendekeza ni kuihilikisha nafsi yako.

 

Luqman mwenye hekima "Luqman al Hakiym", siku moja alitakiwa achague kutoka katika mbuzi wawili waliochinjwa sehemu mbili zilizo mbaya kupita zote na sehemu mbili nzuri kupita zote. Luqman akachagua moyo na ulimi kutoka kila mbuzi. Na alipoulizwa:

"Tulikuambia uchague kutoka KILA mbuzi sehemu mbili, mbona umechagua mbili hizi tu (Moyo na ulimi)?"

Akajibu:

"Hapana vibaya kuliko hivi vinapoharibika, na hapana vizuri kuliko hivi vinapotengenea".

Ndugu zangu Waislam, jukumu letu kubwa ni kupambana na shetani anayeurandia moyo na kuulenga ili aufisidi kama alivyofisidika yeye. Ukiuendekeza na kuufuata, moyo utazowea na hatimaye kwako maasi yatageuka kuwa ni jambo la kawaida, na utajikuta kila siku unatubu toba za uongo kwa kusema: 'Astaghfirullah', huku ukiendelea kumuasi Mola wako bila ya kutia nia ya kutorudia tena maasi hayo. Na haya ni katika maradhi makubwa yenye kuangamiza.

Anasema Ibnul Qayim katika 'Al Jawab al Kafi':

"Hatimaye mtu badala ya kuona haya kumuasi Mola wake anajikuta akijisifia kwayo. Utamsikia akisema kwa fahari: "Ewe Fulani, jana nilifanya hivi na vile." Mwenyezi Mungu amemsitiri lakini yeye anajifedhehesha mwenyewe mbele za watu. Mtu wa aina hii mara nyingi anakuwa keshajifungia milango ya toba.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema: "Umati wangu wote umesalimika isipokuwa wanaojifedhehesha baada ya kufanya maasi."

Kuutibia moyo

1-Kusoma Qurani kwa kutafakari

Ndugu yangu Muislamu, soma kitabu cha ya Mwenyezi Mungu, kwani ndani yake utaipata raha na tiba ya kuitakasa nafsi na kuulainisha moyo na kuingiza furaha na matumaini ndani yake.

Hapana dawa bora ya kuusafisha moyo na kuirudishia nuru yake kuliko dawa ya kuupambanisha na maneno ya Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala.

Isome Qur'ani kwa kutafakari, kisha fuata maamrisho yake na epukana na makatazo yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Je! Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na mwenye moyo mgumu?)

Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisizomkumbuka Mwenyezi Mungu! Hao wamo katika upotofu wa dhahiri. Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumcha Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa."

Azzumar 22-23

Na akasema :

"Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kama imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi. "

Annisaa- 82

Na akasema:

"Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili."

Saad - 29

Ndugu yangu Muislam, isome Qurani tukufu kwa mazingatio sio kama chiriku, kifungue kifua chako na uyakubali yaliyomo ndani yake. Hapo tu ndipo utakapoweza kufaidika nayo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwa akiisoma Qurani kwa kutafakari na alikuwa akipenda kuzirudiarudia aya zinapomuathiri.

Imepokelewa kuwa usiku mmoja alipokuwa akisali, alikuwa usiku kucha akiirudia kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Ikiwa utawaadhibu, basi bila shaka hao ni waja wako; na ukiwasamehe basi kwa hakika wewe ndiye Mwenye nguvu (na) Mwenye hikima".

Al Maidah - 118 .

Usiku kucha alikuwa akiirudia kauli hiyo huku akilia mpaka alfajiri ilipoingia.

Haya ni maneno yatakayotamkwa na Nabii Issa (Alayhi Ssalaam) siku ya kiama. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwa akilia kwa kuwafikiria watu katika umati wake watakaoingia Motoni siku hiyo kutokana na kumuasi kwao Mwenyezi Mungu kwa kumshirikisha, kutokusali, kula riba, kudhulumu, nk.

Anasema Uthman bin Affan (Radhiya Llah anhu):

"Nyoyo zetu zingelikuwa safi, basi hii Qur'ani ingelitutosha na kutushibisha ".

 

Usiwe kama yule mwenye kuisoma Qur'ani kisha haupiti muda, huyoo keshaufunga msahafu. Anaona dhiki, haoni raha anaposoma maneno ya Mola wake, wala hafaidiki na mafundisho yake.

Huyo ni shetani anataka kukuchezea. Usikubali kuchezewa naye.

"Je! Mnamfanya yeye na kizazi chake kuwa marafiki badala yangu hali wao ni maadui zenu? Ni mbaya kabisa kwa madhalimu badala ya hii."

Al Kahf 50

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili."

Sa-ad 29

Na akasema:

"Kwa yakini tumeifanya Qurani iwe nyepesi kufahamika Lakini yuko anayekumbuka?"

Al Qamar - 22

 

Imesimuliwa kuwa mmoja katika watu wema alikuwa akisoma Qur'ani. na alipoifikia aya ya 109 Surat Bani Israil, isemayo:

"Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na (Qurani) inazidi kuwaongeza unyeyekevu".

Mtu huyo aliporomoka kifudifudi na kusujudu, kisha akasema kwa uchungu:

"Kusujudu nimesujudu lakini kilio kiko wapi?"

 

Maulamaa wanasema: "Ukitaka kumsikia Mola wako Akizungumza nawe basi soma Qur'ani, na ukitaka wewe kuzungumza na Mola wako basi funga Swala."

 

Ndugu zangu Waislam, Qur'ani ni roho itokayo kwa Mola wetu, na bila yake dunia yote inakuwa mfano wa maiti.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na namna hivi Tumekufunulia wahyi (Roho) kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini wala imani; lakini tumefanya kitabu hiki (Qur'ani) ni nuru, ambayo kwa (nuru) hiyo Tunamuongoza Tumtakaye katika waja wetu. Na kwa yakini wewe unaongoza katika njia iliyonyoka".

Ash-Shuura - 52

 

Na Qurani tukufu ndiyo katiba yetu na mafundisho kutoka kwa Mola wetu. Usalama wetu hapa duniani na huko Akhera unapatikana katika kukifuata kitabu hiki. Tukiikamata hatuwezi kupotea abadan, bali upotevu wote upo katika kukiacha kitabu hiki.

 

Kila herufi utakayosoma unapata thawabu kumi.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Na sisemi kuwa Alif laam miym ni herufi moja, bali aliif ni herufi na laam ni herufi na miym ni herufi."

 

Ndugu zangu Waislamu msiikimbie Qurani wala msiibadilishe na kilichokuwa duni kuliko hiyo, kwani masaibu yote yanatukuta kwa ajili ya kukiacha.

Katika hadith al Qudusiy, Mwenyezi Mungu anauliza:

"Je! Unafuata kilichokuwa bora kuliko Mimi au maneno yaliyo bora kuliko Yangu?"

Na katika Qurani tukufu Mwenyezi Mungu anasema:

"Mtume alikuwa akisema 'Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya Qurani hii kuwa kitu kilichoachwa (kilichohujuriwa)" Kilichohamwa".

Al Furqan 30

Katika kuifasiri aya hii anasema Ibni Kathiyr:

"Kuzungumza pale inaposomwa Qurani ukashindwa kuisikia ni katika kuihama Qurani. Kuacha kuisoma na kuisikiliza na badala yake ukafuata mashairi au nyimbo ni katika kuihama Qurani. Kutoifanyia kazi ni katika kuihama Qurani, na kuacha kutafakari juu ya maana yake pale unapoisoma ni katika kuihama Qurani."

 

Tunapata wasaa wa kufuatilia mipira na vipindi mbali mbali vya TV. Tunapata wasaa wa kusoma magazeti ya kila siku na ya kila wiki na vitabu mbali mbali, yote hayo ni mazuri. Lakini kwa nini basi tusitenge wakati mdogo kila siku angalau robo saa kwa ajili ya kusoma maneno ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala?

 

Mtu anapotaka kujua uzito wa Imani yake, basi auangalie uhusiano wake na kitabu hiki kitukufu. Akijiona kuwa anapenda kuisoma na inamfurahisha, basi amshukuru Mola wake. Ama akiona kinyume na hivyo, basi lazima ajitahidi ili nuru hii itokayo mbinguni iweze kumfikia.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) anasema:

"Mbora wenu ni mwenye kujifunza Qur'ani na kuwafunza wengine".

Na akasema:

"Mwenyezi Mungu kwa kitabu hiki atawanyanyua makundi na kuwaangusha makundi".

 

Swalaa

Ndugu yangu Muislam, usisali kama mwenye kufukuzwa. Usisujudu na kurukuu mfano wa kuku anayedokoa mtama. Kuwa mtulivu ndani ya swala yako (Tuma'aniyna), na mnyenyekevu (khushuuu). Hima yako iwe kutaka radhi za Mola wako. Usiwe mwenye kutafuta sura ndogo ndogo na kuzisoma kwa haraka ukitamani wakati gani swala imalizike ukajishughulishe na yale unayoyapenda na kustarehe nayo zaidi kuliko hiyo Swala.

Mfano wa mtu wa aina hii ni mfano wa anayekunywa dawa chungu. Anainywa haraka kisha anatafuta chungwa au kitu kitamu kitakachoiondoa ladha chungu ya dawa mdomoni mwake.

Lakini mwenye kuswali kwa utulivu na khushuu, mfano wake ni mfano wa anayekunywa kinywaji kitamu. Hatamani kimalizike. Anakunywa kidogo kidogo apate kufaidika na kustarehe nacho muda mrefu zaidi.

 

Kumbuka kuwa ndani ya Swala yanapita mazungumzo baina yako na baina ya Mola wako.

Imepokelewa kutoka kwa Muslim na Imam Ahmad na Attirimidhy na Attabarani na wengine kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenyezi Mungu Amesema: "Nimeigawa Swala baina Yangu na baina ya mja wangu sehemu mbili, na mja wangu atapata atakachoomba. Mja wangu anaposema:

Mwenyezi Mungu husema: "Amenisifia mja wangu". Na anaposema: Mwenyezi Mungu husema: "Ameniadhimisha mja wangu. Na anaposema: Anasema: "Mja wangu amenitukuza." Au husema: "Amejisalimisha kwangu mja wangu."Na anaposema:

Mwenyezi Mungu husema: "Haya ni baina yangu na baina ya mja wangu, na mja wangu atapata atakachoniomba." Na anaposema:

*

Mwenyezi Mungu anasema: "Haya ni kwa ajili ya mja wangu na mja wangu atapata atakachoniomba."

 

Kumbuka kuwa unafanya biashara na Mola wako ukitegemea kutoka kwake bidhaa yenye thamani kubwa sana

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Mwenye kuogopa kuchelewa aianze safari mapema. Na mwenye kuianza safari mapema anawasili mapema. Hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni ghali sana. Hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni Pepo."

Attirmidhy na Al Hakim

 

Ndugu yangu Muislam! Kumbuka kuwa kujishughulisha na uliyokwisha dhaminiwa (dunia) ukaacha kujishughulisha na usichokuwa na dhamana nacho (akhera), ni dalili ya kutokuona mbali.

"Je! Wakati haujafika tu kwa wale walioamini kwamba nyoyo zao zinyenyekee kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kwa mambo ya haki yaliyoteremka? Wala wasiwe kama wale waliopewa kitabu zamani (Mayahui na Manasara) na muda wao ukawa mrefu kwa hivvyo nyoyo zao zikawa ngumu na wengi wao wakawa maasi."

Al Hadiyd - 16

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibnu Hibban katika sahihi yake kuwa;

"Anasema Ata-a: 'Niliingia mimi na Abdullah bin Umair nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), tukamuambia Bibi Ayesha: "Tuhadithie juu ya jambo la ajabu kabisa uliloliona kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)". Bibi Ayesha (Radhiya Llah anha) akalia sana kisha akasema: "Usiku mmoja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliinuka na kuniomba nimuache amuabudu Mola wake. Nikamuambia: "Mimi natamani kuwa pamoja nawe, lakini wakati huo huo napenda kile kinachokufurahisha". Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akainuka na kuanza kuswali. Akawa anaswali huku akilia mpaka ndevu zake zikaroa machozi. Akaendelea katika hali hiyo mpaka mahala alipokuwa akiswali pakajaa machozi. Akaendelea katika hali hiyo mpaka wakati wa alfajiri alipokuja Bilal kumuamsha. Alipomkuta katika hali ile akamuuliza: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), kwa nini unalia namna hii wakati wewe umekwisha samehewa madhambi yako yaliyotangulia na yatakayokuja?' Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema: "Basi nisiwe mja mwenye kushukuru? Nimeteremshiwa aya usiku wa leo, ole wake yule atakayezisoma na asizitafakari." (Aya zenyewe ni hizi):

"Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto. Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi; na walio dhulumu hawana wasaidizi."

Aali Imran - 190-191-192

 

Ndugu yangu Muislamu! Jicheleweshe kidogo angalau katika mojawapo wa sajda zako. Omba. Mfungulie Mola wako kifua chako. Lia. Muhadithie juu ya shida zako. Muombe akufunue kifua chako na aingize furaha na matumaini mema ndani yake. Muombe akuondolee dhiki zako na shida zako. Muombe akusahilishie mambo yako yote. Na akujaalie uwe miongoni mwa atakaowaingiza ndani ya Pepo yake. Muombe unachotaka. Shida zako zote mtolee. Au huna shida wewe?

Mwandamu anapoombwa sana hukasirika, lakini Mwenyezi Mungu asipoombwa ndiyo hukasirika.

 

Tunaishi katika neema Zake lakini tunawaabudu wengine. Riziki inatoka Kwake tunawashukuru wengine. Kheri Zake zinatuteremkia, shari zetu tunampandishia.

2- Majina na sifa za Mwenyezi Mungu

Kuyazingatia majina matukufu na sifa nzuri nzuri za Mwenyezi Mungu kunaupa uhai mpya moyo na kuulainisha na kuutuliza.

Tuchukuwe kwa mfano jina la Mwenyezi Mungu "Al Mawjud" na maana yake ni "Ambaye Yupo Milele".

Anasema Sheikh AbdulMajid Al Zindani, katika kitabu chake 'Al Iman': "Tukizingatia juu ya viumbe vinavyozaliwa kila siku katika binadamu, wanyama wadudu na mimea, na tukitizama yanayotokea kila wakati duniani katika upepo na harakati zake, mvua na faida zake, usiku na mchana. Na ukitizama mabadiliko ya kila wakati na nidhamu iliyokuwepo katika harakati za jua na mwezi pamoja na sayari nyengine pamoja na kuzingatia hekima iliyopo katika mbadiliko hayo. Akili inahakikisha kwamba yote hayo hayakuumbwa na "Asiyekuwepo", bali yameumbwa na Ambaye Yupo, (Al Mawjud) Subhaanahu wa Taala.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Jee wameumbwa "pasipo na kitu", au wao ndio waliojiumba? Au wameumba mbingu na Ardhi bali hawana yakini ( ya jambo lolote)".

At Tur- 36-37

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anawapa wale wasiomuamini, wachague moja katika sababu tatu zifuatazo za kuwepo kwao hapa duniani:-

1.                        Jee wameumbwa pasipo na kitu? Bimaana wametokea hivi hivi tu, bila ya Muumbaji Mwenye Hikma kubwa aliyewaumba kwa hikma kubwa?

2.                        Wamejiumba wenyewe?

3.                        Au wao ndio walioziumba mbingu na Ardhi ?

 

Ukitafakari juu ya Jina hili la Al Mawjud na kutafakari juu ya nidhamu ya hali ya juu inayouendesha ulimwengu huu, na ukitafakari juu ya hoja yake Subhaanahu wa Taala katika aya iliyotangulia ya Surat Attur, utaweza kuuona utukufu wake MwenyeziMungu Subhaanahu wa Taala.

 

Katika majina yake pia ni - "Al Hakiym" - Mwenye Hekima

Ukizingatia sura za viumbe, utaona kuwa Mwenyezi Mungu ameumba kila aina ya viumbe kwa namna (aina) moja kwa Hikima yake."

Kwa mfano binaadamu wote umbile lao ni namna moja. Wana macho mawili usoni, pua ipo baina ya hayo macho, mikono ipo katika pande zote mbili na miguu ipo chini.

Huwezi kuona jicho likawa gotini au mkono kutokeza juu ya kichwa.

Hii inasadikisha kwamba hii ni kazi ya Mwenye Hekima Mmoja tu aliyemuumba binaadamu kwa Hekima kubwa sana.

Ukiichunguza hewa tunayoivuta utaona kuwa unaitumia hewa safi (oxygen), na kuigeuza kuwa hewa chafu (Carbon dioxide). Lakini kiasi cha hewa safi hakipungui katika anga kwa sababu Muumbaji ameiamrisha mimea iibakishe hewa hiyo uliyoichafua ili iwe hewa safi tena kwa kiasi maalum ili kiasi cha hewa kibaki kwa kadiri maalum, kisizidi wala kisipungue.

Jee hii haithibitishi kwamba ni kazi za Mwenye Hekima "Al Hakiym"?

 

Hivyo hivyo ukichunguza kila jina au sifa zake Subhaanahu wa Taala utaona kwamba inabeba maana maalum. Na kila unapoiona hekima katika kitu chochote utajua kwamba imetokana na Al Hakiym na unapoziona nguvu basi zimetokana na Al Qawiy (Mwenye nguvu), unapoiona huruma basi juwa ya kuwa imetokana na Al Rahiym n.k.

Kutafakari juu ya mambo ya Akhera

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla llahu alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

"Zidisheni kujikumbusha juu ya (Haadhimul ladhaat) Mauti."

Na akisema:

"Nilikukatazeni kuzuru makaburi, lakini sasa yazuruni kwa sababu yanaulainisha moyo, yanalifanya jicho litoke machozi na yanakumbusha Akhera".

Imam Ahmad, Al Bayhaqy na Al Haakim.

 

Baadhi ya watu wamebadilisha kusudi la ziara ya makaburi, wakawa badala ya kuyazuru kwa ajili ya kujikumbusha, wao wakageuza makaburi kuwa ni makazi ya Mawalii na mwahali pa kuwaomba mawalii hao na pa kuweka nadhiri.

 

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla llahu alayhi wa sallam) ametaja sababu tatu tu za kuturuhusu kuyazuru makaburi, nazo ni:-

1.                        Kulainisha nyoyo.

2.                        Kutoka machozi .

3.                        Kukumbusha Akhera.

 

Ndugu yangu Muislam, jitahidi katika kujikumbusha juu ya maisha baada ya maisha yetu haya. Juu maisha ya barzakdh, mahali itakapotua roho yako baada ya kuondoka hapa duniani, na juu ya siku adhimu utakaposimamishwa mbele ya Mola wako.

Kumbuka kuwa siku hiyo patakuwepo makundi matatu tu;

La kwanza thawabu zao ni nyingi kushinda dhambi zao, na hao bila shaka ni watu wa Peponi.

La pili dhambi zao ni nyingi kupita thawabu zao, na hao bila shaka ni watu wa Motoni.

Na kundi la tatu ni lile ambalo thawabu zao na dhambi zao zimekuwa sawa juu ya mezani. 'Nus bin nus'. Mtu atatamani apate thawabu moja tu itakayoongeza uzito na kuingizwa Peponi.

Mwenyezi Mungu amelipa kundi hilo la tatu jina la Watu wa 'Al Aaraf,' (As'haabul Aaraf). Na neno 'Al Aaraf' maana yake ni 'Mnyanyuko'. Na watu hawa kwa kuwa thawabu zao na dhambi zao zimekuwa sawa, wamezuilika wasiingizwe Peponi wala Motoni. Watasimamishwa mahali maalum wakingoja rehema ya Mola wao.

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala katika Surat al Aaraf anasema:

"Na baina ya makundi mawili hayo patakuwapo pazia. Na juu ya Mnyanyuko patakuwa watu watakao wajua wote kwa alama zao, na wao watawaita watu wa Peponi: Assalamu Alaykum, Amani juu yenu! Wao bado hawajaingia humo, lakini wanatumai.

Na yanapo geuzwa macho yao kuelekea watu wa Motoni, watasema: Mola Mlezi wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu walio dhulumu."

Al Aaraf 46-47

 

Katika kuifasiri aya hii anasema Ibn Kathir:

"Abdillahi bin Masaaod amesema: 'Hakika mja anapotenda jema huandikiwa thawabu kumi, na akitenda baya haandikiwi isipokuwa dhambi moja tu!" Kisha akasema: "Ameangamia yule ambaye moja zake (dhambi zake) zitashinda kumi zake (thawabu zake)".

Imepokelewa na Ibn Jariry

 

Imepokelewa kuwa siku moja Abubakar (Radhiya Llah anhu) alimuambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla llahu alayhi wa sallam):

"Ninakuona unaanza kuzeeka ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Mtume (Swalla llahu alayhi wa sallam) akamuambia:

"Zimenizeesha (Surat) Huud na ndugu zake ewe Abubakar".

Surat Huud na ndugu zake ni Huud, al Mursalaat, Al Waqiah, Amma yatasaalun na Idha Shamsu Kuwwirat.

Sura hizi zilimkongesha (zilimzeesha) Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla llahu alayhi wa sallam) kutokana na habari nzito zilizomo ndani yake juu ya walioishi kabla yetu, nguvu walizokuwa nazo, kiburi walichokuwa nacho, uwezo waliokuwa nao, namna walivyomuasi Mola wao na juu ya Adhabu kali zilizowateremkia hapa duniani kabla ya kesho Kiama.

Katika Sura hizi mna habari za Siku ya Kiama na maelezo ya kusisimua juu ya Pepo na watu wake na neema zake, na maelezo ya kutisha juu ya Moto na watu wake na adhabu zake.

 

Imepokelewa pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla llahu alayhi wa sallam) alikuwa akipenda usomaji Qurani wa Abdullah bin Masaud (Radhiya Llah anhu) na alikuwa akiwaambia Masahaba:

"Anayetaka kuisikia Qurani ikisomwa kama ilivyoteremshwa basi asikilize usomaje wa Abdullah bin Masaud ".

Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alimtaka Abdullah bin Masaood (Radhiya Llah anhu) amsomee Qurani, na Ibni Masaud akamuambia:

"Nikusomee na wewe ndiye uliyeteremshiwa?

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akamuambia:

"Mimi napenda kumsikiliza mwengine akinisomea."

Abdullah bin Masaood (Radhiya Llah anhu) akaisoma Surat Anisaa na alipoifikia aya ya 41 pale Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala aliposema:

"Basi itakuwaje (siku hiyo) tutakapoleta shahidi katika kila Umma, na tukakuleta wewe (Nabii Muhammad) uwe shahidi juu yao (Umma wako)?

Anasema Abdullah bin Masaood (Radhiya Llah anhu):

Nilipofika hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akaniambia:

"Basi, hapo hapo, inatosha."

Nikamuangalia usoni, nikaona macho yake yanatoka machozi ".

Kuyadharau madhambi

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Msije mkayadharau madhambi".

 

MchaMungu wa kweli anaiona dhambi ndogo kuwa mfano wa jabali juu ya shingo yake, lakini mtu asi anaiona dhambi kubwa mfano wa nzi mdogo juu ya pua yake, anaweza kumfukuza wakati wowote kwa mikono yake.

Maulamaa wanasema:

"Usitizame udogo wa dhambi bali tizama ukubwa wa Yule unayemuasi."

 

Mtu anaendelea kurimbika madhambi mpaka anazoweana nayo na hatimaye kwake, kuasi kunageuka kuwa ni jambo la kawaida tu.

Wingi wa madhambi unaondoa heshima ya mja mbele ya Mwenyezi Mungu.

Anasema Hassan al Basry (Mwenyezi Mungu amrehemu):

"Wingi wa maasi ni sababu ya kufedheheka mja na kutokuwa na thamani yoyote mbele ya Mola wake.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na ambaye Mwenyezi Mungu amemfedhehesha, basi hakuna atakayempa hishima."

Al Hajj 18

"Hawakumuadhimisha Mola wao ndiyo maana wakaendelea kumuasi." Anaendelea kusema Al Hassan al Basry: "Lau kama wangelimuheshimu basi wangejiepusha nayo. Mja asiyekuwa na thamani yoyote mbele ya Mola wake ataenziwa na nani?"

 

Miongoni mwa madhambi ambayo watu wanayaona kuwa ni madogo na ambayo yanaacha athari mbaya nyoyoni ni madhambi ya kutizama yale Mwenyezi Mungu aliyoharamisha. Mtu anapokuwa peke yake akadhani kuwa hapana anayemuona, hutizama kila cha haramu kinachopita mbele yake.

Mwenyezi Mungu anasema :

"Anayajua khiyana ya macho na yanayoficha vifua".

Al Muuminun 19

Na akasema:

"Na anayemuogopa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa kurehemu, na hali ya kuwa hamuoni na akaja kwa moyo ulioelekea (kwa Mwenyezi Mungu)".

Qaf - 33

 

Imepokelewa kuwa mtu mmoja aliingia kwa Imam Ahmad bin Hanbal akamuambia:

"Nini rai yako juu ya shairi hili?"

Imam akamuuliza:

"Shairi lipi?"

Yule mtu akasoma:

"
"

Na maana yake ni: "Atakaponiambia Mola wangu; 'Hunistahi unaniasi, unajificha waja wangu wasikuone wakati mbele yangu unanijia kwa maasi?"

Imepokelewa kuwa Imam Ahmad aliposomewa shairi hilo aliingia chumbani kwake huku akilia.

 

Mtu anapokuwa peke yake mbele ya television, anaweka station anayoitaka, lakini anaposikia mlango ukifunguliwa, au hatua za mtu anayekuja, kwa haraka utamuona huyo anabadilisha station. Kwa nini? Asije akajulikana kuwa anatizama station zisizokuwa na adabu. Anasahau maskini yule kuwa Mola wake anamuona.

Kumbuka ndugu yangu Muislam kuwa unao pia Malaika wawili waliowakilishwa kuandika matendo na maneno yako.

 

Kumbuka pia kuwa macho ni neema uliyopewa na Mola wako, kwa hivyo umlipe kwa kumshukuru badala ya kumuasi. Kumbuka kuwa vidole vyao ni neema aliyokupa Mola wako, kwa hivyo umshukuru kwavyo badala ya kuvitumia katika kumuasi. Kumbuka kuwa mali iliyokuwezesha kumiliki vyombo hivyo ni neema iliyotoka kwa Mola wako.

 

Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhuma):

"Ewe mwenye kufanya dhambi usiaminishe kwamba hutolipwa kwa madhambi yako, na kwamba hutoyaona matokeo ya ubaya wa dhambi. Na kule kuifuatilia kwako hiyo dhambi, dhambi yake ni kubwa zaidi kuliko kukifanya hicho kitendo cha dhambi. Na kutokuona haya ukiwa unafanya dhambi wakati Malaika yuko kuliani kwako na mwengine kushotoni kwako, ni kubaya zaidi kuliko hiyo dhambi. Na kufanya kwako hiyo dhambi huku unacheka wala hujali nini Mwenyezi Mungu keshakutayarishia kwa dhambi yako hiyo, ni kubaya kuliko hiyo dhambi. Na kukifurahia kitendo cha dhambi ni kubaya zaidi kuliko kuitenda hiyo dhambi. Na kuhuzunika kwako unapokosa kuifanya dhambi, ni makubwa zaidi kuliko hiyo dhambi. Na unapouogopa upepo unapotikisa mlango wakati unapofanya kitendo cha madhambi, wakati moyo wako wala hausituki juu ya kuwa Mola wako anakuona ni kubaya zaidi kuliko hiyo dhambi."

 

Ndugu yangu Muislamu, acha kutizama ya haramu na utaiona athari yake ndani ya moyo wako.

Katika hadith al Qudsiy Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema:

"Kutizama (yaliyoharamishwa), ni mkuki katika mikuki ya sumu ya Ibilisi. Atakayeacha (kutizama) kwa kuniogopa, nitamlipa badala yake Imani atakayoinea raha ndani ya moyo mwake".

 

Miongoni mwa dhambi inayodhaniwa kuwa ni ndogo ni kule baadhi ya watu kuazima vitu kutoka kwa wenzao kisha wasivirudishe. Wengi hufanya hivyo bila kujali na wengine hudhania kuwa ni katika dhambi ndogo, na kwa ajili hiyo wakaliona hilo kuwa ni jepesi.

Huko ni katika kudharau madhambi

Mwenyezi Mungu anasema:

"Hakika MwenyeziMungu anakuamrisheni kuzirudisha amana kwa wenyewe".

An Nisa 58

Neno la Haki

Mwenyezi Mungu anasema:

"Enyi mlioamini! Muogopeni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya haki."

Al Ahzab- 70

Neno la Haki ni 'Neno la kweli'. Na kinyume chake ni 'Neno la Uongo'. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Na mja ataendelea kusema uongo mpaka ataandikwa kwa Mwenyezi Mungu kuwa 'fulani' Muongo. Na mja ataendelea kusema kweli mpaka ataandikwa kwa Mwenyezi Mungu kuwa 'fulani' Mkweli'.

Muslim na Attirmidhy na wengine

Kupenda kusema kweli ni dalili ya ucha Mungu Katika aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu ametumia neno 'Taqwa' aliposema: " ".na maana yake ni; (Muogopeni Mwenyezi Mungu).

Mwenyezi Mungu Anasema:

"Kwake hupanda maneno mazuri na kitendo Kizuri huyapandisha (Hayo maneno mazuri)."

Faatir - 10

Na maana ya kauli Yake Subhaanahu wa Taala aliposema: "Na kitendo kizuri huyapandisha," ni kuwa mtu anapotamka maneno mazuri anatakiwa ayafuatilie kwa vitendo vizuri. Asiwe anawakataza watu kufanya mabaya kisha yeye anayaendea.

Zimepokelewa riwaya nyingi kuwa; wa mwanzo kuadhibishwa Siku ya Kiama ni wale wanaosoma Qurani kwa ajili ya kutaka kusifiwa, na wenye kulingania watu ili pasemwe kuwa wanajuwa kusema, na wenye kutoa sadaka kwa ajili ya kusifiwa ukarimu wao.

Mwenyezi Mungu siku hiyo atawaambia:

"Mulilingania ili musifiwe, basi mumekwisha sifiwa. Na wewe ulisoma ili usifiwe kuwa sauti yako ni nzuri, basi umekwisha sifiwa. Na wewe ulitoa ili uambiwe mkarimu, basi umekwishaambiwa."

Kumbuka kuwa Mwenyezi Mungu haikubali amali yoyote isipokuwa ile tu iliyotendwa halisi kwa ajili Yake Subhanahu wa Taala. Na hapana jambo Mwenyezi Mungu analolichukia kuliko mtu kufanya kitendo kwa ajili ya 'Riyaa' (kujionyesha). Na Mwenyezi Mungu ameitaja Riyaa kuwa ni shirki ndogo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Hapana ninachokuogopeeni kuliko shirki ndogo." Wakamuuliza: "Ni nini hii shiriki ndogo?". Akasema: "Riyaa. Siku ya Kiama baada ya Mwenyezi Mungu kuwalipa watu wote jaza zao, atawaambia (waliotenda kwa ajili ya Riyaa): "Nendeni kwa wale mliokuwa mkijionyesha kwao duniani kisha muone iwapo mtaweza kupata chochote kutoka kwao."

Imam Ahmed

Tumeumbwa na macho mawili ili tuweze kuona mazuri na mabaya, masikio mawili ili tuweze kusikia mazuri na mabaya, na tundu mbili puani ili tuweze kunusa harufu nzuri na mbaya. Lakini tumeumbwa na ulimi mmoja tu, ili tusitamke isipokuwa mema peke yake. Tusitamke isipokuwa maneno ya kweli yenye kumridhisha Mola wetu Subhanahu wa Taala.

Kumbuka kuwa utakalotamka linaandikwa. Hapana kitakachopotea bure.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Hatoi kauli yoyote isipokuwa karibu nae yuko mngojeaji tayari (kuandika)".

Qaf -18

 

Muislamu anatakiwa atangulize akili kabla ya Ulimi. Afikiri kabla ya kutamka. Asitamke isipokuwa yale tu yatakayomridhisha Mola wake. Asiwe akijishughulisha na makosa ya watu. Hana la kusema isipokuwa huyu kafanya hivi na yule kafanya vile, kama kwamba yeye ni mtu nadhifu sana asiye na makosa yoyote. Kama hana la kusema bora anyamaze.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenye kuamini kuwepo kwa siku ya Akhera basi aseme maneno ya kheri au anyamaze".

Bukhari na Muslim.

Na akasema:

"Mtu bila kuhisi anaweza kutamka neno litakalomridhisha Mwenyezi Mungu, na kwa neno hilo Mwenyezi Mungu akamnyanyua daraja nyingi. Na mtu bila kuhisi anaweza kutamka neno litakalomghadhibisha Mwenyezi Mungu, na kwa neno hilo akaporomoshwa ndani ya mashimo ya moto wa Jahannam".

Bukhari

Ulimi unaunguza thawabu

Kutoka kwa Muadh bin Jabal (Radhiya Llahu anhu) amesema:

"Nilisema: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; nijulishe juu ya matendo yatakayoniingiza Peponi na yatakayoniweka mbali na Moto."

Akaniambia:

"Hakika umeuliza kubwa mno, nalo ni jepesi kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu aliyetukuka atamwepesishia; Umuabudu Mwenyezi Mungu na usimshirikishe na chochote, na Usimamishe Swala na Utoe Zaka na ufunge Ramadhani na uikusudie kwa Hijja nyumba (ya Mwenyezi Mungu ukiweza kuiendea)."

"Kisha akasema:

"Je nikujulishe na milango ya kheri? Funga, (Saumu) inakukinga na moto, na Sadaka inafuta madhambi kama maji yanavyozima Moto, na Swala ya mtu nyakati za usiku))."

Kisha akaisoma (aya Ya 16 suratul Sajdah):

    "Huinua mbavu zao kutoka vitandani wakati wa usiku ili kumuabudu Mola wao kwa kuogopa moto na kutaraji Pepo na kutoa katika yale tuliyowapa, nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho (huko Peponi) ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyafanya".

 

Kisha akasema:

"((Je nikujulishe nini kichwa cha jambo, na nguzo yake na kilele chake?))."

Nikasema:

"Ndiyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu".

Akasema:

"Kichwa cha Jambo ni Uislamu na Nguzo yake ni Swala na kilele chake ni Jihadi."

Kisha akasema:

"Je nikujulishe kisimamio cha yote hayo?"

Nikasema:

"Ndiyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu."

Akaushika ulimi wake akasema:

"Ufunge huu juu yako."

Nikasema:

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kwani sisi ni wenye kuhesabiwa kwa tunayoyasema?"

Akasema:

"Amekukosa mama yako, kwani watu kwa sababu gani watatupwa katika moto kwa (kutangulizwa) nyuso zao isipokuwa kwa chumo za Ndimi zao?.

Attirmidhy na akasema ni hadithi njema.

 

...

Chunga ulimi chunga lisije kukuponyoka

Neno baya linadunga lina sumu kama nyoka

 

Ndugu yangu Muislam. Hata ukijitahidi namna gani kuchuma thawabu kwa kufanya ibada za kila namna, lakini kama hna uwezo wa kuzihifadhi thawabu zako kwa kuuchunga ulimi, basi utazipoteza bure. Zinakwenda arijojo.

 

Kumbuka kuwa siku ya Kiyama hakutokuwa na kuhesabiana kwa mali wala pesa.

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) siku moja aliwauliza Masahaba:

"Mnamjua nani aliyefilisika?"

Masahaba wakasema:

"Aliyefilisika tunayemjua sisi ni yule asiyekuwa na Dirham wala chochote".

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akasema:

"Aliyefilisika katika umati wangu ni yule atakayekuja siku ya Kiyama (akiwa na Thawabu nyingi alizozichuma (kutokana) na Swala zake na Saumu na Zaka, kisha anakuja akiwa amemtukana huyu na kumsingizia uongo huyu. Amekula mali ya huyu na kamwaga damu ya huyu na amempiga huyu. Kisha thawabu zake zinachukuliwa na kugaiwa huyu na yule, na zikeshamalizika kabla hajamaliza mashtaka yake anabebeshwa madhambi yao, yanamjalia kisha anatumbukizwa Motoni."

Muslim

Mfano wa neno zuri

Mwenyezi Mungu anasema:

. .

Je! Hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake imara, na matawi yake yako Mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano Ili wapate kukumbuka.

Na mfano wa neno Ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa juu ya ardhi. Hauna imara. Mwenyezi Mungu huwathubutisha wenye Kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo".

Ibrahim 24-27

 

Ndugu zangu Waislamu, tunaposoma Qurani tukufu tunatakiwa kuyazingatia maneno kama haya na tusiyapitie juu juu tu.

Maulamaa wa mambo ya anga wanakadiria kuwa miaka milioni nyingi iliyopita mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha ukatokea mripuko (mlipuko) mkubwa walioupa jina la 'The big bang' uliosababisha kuziambua. Kisha moshi mwingi sana ukaanza kujizungusha, na kutokana na moshi huo sayari na nyota zikaanza kujitengeneza.

Ule ndio wakati Mwenyezi Mungu aliposema "" "Kuwa" - na ikawa.

 

Anasema Sheikh Abdul Majeed Al Zindani katika mojawapo ya hotuba zake:

"Hapo mwanzo wanasayansi waliusanifu mripuko huo kama ni 'Nadharia (theory) ya kisayansi', lakini hivi sasa umekwishakuwa ni uhakika (scientific fact)."

Qurani tukufu ilizungumza juu ya uhakika huo tokea miaka elfu na mia nne iliyopita, kabla ya hao wanasayansi kuwa na fikra yoyote juu ya jambo hili. Hii ikituthibitishia kuwa Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni Mtume wa kweli aliyeletwa na Mola wake Mwenye kujuwa siri zote za kuumbika kwa ulimwengu huu.

Mwenyezi Mungu anasema:

( -30)

"Je! Hawakuona wale Waliokufuru ya kwamba mbingu na ardhi vilikuwa vimeambatana kisha tukaviambua (tukavipambanua). Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai. Basi jee hawaamini?"

Al Anbiyaa - 30

 

Wanasayansi wanasema:

"Sayari na nyota hizo zilianza kujifuma (kujiungaunga) na kuenea huku zikijitenga na kujipanga katika mifumo mbali mbali (galaxies), na baada ya kupita kiasi cha miaka 180,000 sayari na nyota hizo zilizokuwa na joto kali sana zilianza kupoa na kufikia daraja la joto la jua.

Wanasayansi hao wanaendelea kusema kuwa; nyota iliyo karibu kabisa na sisi ipo umbali wa miaka minne na miezi mitatu ikiwa tutasafiri kwa kasi ya mwanga (light years).

Wanasema kuwa mwanga, unasafiri maili 186,000 kwa dakika moja, na unasafiri Maili 11,160,000 kwa saa, na maili 160,070,400,000 kwa siku.

 

Ardhi yetu imo ndani ya mfumo uitwao "Milky Way Galaxy", uliokusanya zaidi ya nyota na sayari milioni 100. Na mfumo ulio karibu kabisa na mfumo wetu wa Milk Way upo umbali wa safari ya miaka milioni 2 kwa kasi ya mwanga (2 million light years), na unaitwa "Andromeida Galaxy",.

Watalamu hao wanasema pia kuwa Galaxy iliyo mbali kabisa na sisi inaitwa 'NGC Galaxy', nayo ipo umbali wa '20 million light years'.

 

Ndugu yangu Muislamu, sayari zote hizo ni pambo tu la mbingu ya dunia.

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema:

"Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu hii (ya dunia) kwa mataa."

Al Mulk - 5.

 

Na maana yake ni kuwa; ukiweza kusafiri miaka milioni yote hiyo kuzifikia sayari na nyota hizo, utakuwa umelifikia pambo tu la mbingu ya mwanzo, na kwamba bado utakuwa hujaifikia mbingu ya mwanzo tu, wachilia mbali mbingu ya saba.

Anasema mmoja katika maulamaa:

"Hebu jaribu kutafakari ndugu yangu Muislam juu ya Neno jema, litakalosafiri umbali wote huo hadi kuifikia mbingu ya Saba, kisha likavuka mbingu ya saba na kuifikia 'Sidratul Muntahaa' na kutoa matunda yake huko."

Mwenyezi Mungu anasema:

Je! Hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako Mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano".

 

Kwa nini basi ujinyime yote hayo wakati funguo za milango ya kheri ipo mdomoni mwako. Tamka ya kheri utayakuta matunda yake yakikusubiri kwa Mola wako. Sema neno jema ujiongezee uzito wa thawabu juu ya mizani yako.

 

Neno zuri purutangi mbinguni linapepea

Neno zuri kama mwangi mwenyewe lakurudia

Neno zuri lina rangi lakupamba wavutia

Neno zuri lina mengi Mola analiridhia

Neno zuri "Laa Ilaaha ila Llah"

Mwenyezi Mungu anasema:

{70}

{71}

"Enyi mlioamini! Muogopeni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya haki.

Atakutengenezeeni vizuri vitendo vyenu na Atakusameheni madhambi yenu; Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, bila shaka amefanikiwa mafanikio makubwa".

Al Ahzab - 70 - 71

 

1-           Laa Ilaaha Illa Llah

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wassalaam) amesema: "Yule ambaye neno lake la mwisho duniani litakuwa Laa Ilaaha ilaa Llah, ataingia Peponi ".

Hapana neno bora, zuri na lenye uzito mkubwa juu ya mezani kupita neno hili lenye kutofautisha baina ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu.

Imepokelewa kuwa siku moja Nabi Musa (Alayhi ssalaam) alimuomba Mwenyezi Mungu akasema:

"Ewe Mola wangu, nifundishe neno jema niwe nikilisema, na neno hilo liwe bora kuliko maneno yote yaliowahi kusemwa na waja wako."

Mwenyezi Mungu akamuambia: "Sema Laa ilaaha illa Llah".

Nabii Musa akasema: "Mola wangu, waja Wako wote wanasema Laa ilaaha illa Llah".

Mwenyezi Mungu akasema: "Ewe Musa, zikiwekwa mbingu zote saba pamoja na ardhi saba juu ya upande mmoja wa mizani, kisha ikawekwa "Laa ilaaha illa Llah" upande mwengine wa mezani, basi uzito wa Laa ilaaha illa Llah ndio utakaozidi."

 

Laa ilaaha illa Llah ni tamko la Tawhidi, na wataalam wa elimu hiyo ya Tawhidi wanasema kuwa maana ya neno hili limegawika sehemu mbili:

1-           Nafyun (kukanusha)

2-           Ithbaat (kuthibitisha)

 

Mtu anapotamka: 'La ilaaha' (hapana Mola). Huwa anakikanusha kila kinachoabudiwa au kutiiwa amri zake, kuombwa na kutegemewa kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

Na anapotamka: 'Illa Llah' (isipokuwa Mwenyezi Mungu) huwa anathibitisha kuwa hapana anayepasa kuabudiwa, kutiiwa amri zake, kuombwa na kutegemewa isipokuwa Allah Subhanahu wa Taala.

Kuwategemea wachawi, kuomba katika mizimu au kuomba penye makaburi ya wanaoitwa Mawalii au hata wasiokuwa hao. Kuipenda dunia kuliko Mola wako, kuyafuata matamanio ya nafsi kinyume na mafundisho yaliyotoka kwa Mola wako nk. Vyote hivyo vinakwenda kinyume na mafundisho ya kauli ya 'Laa ilaaha illa Llah'. Na hii ni kwa sababu mwenye Tawhidi ya kweli anaamini kuwa yote yaliyotangulia hayapaswi kuelekezwa isipokuwa kwake Subhanahu wa Taala.

Kwa hivyo mtu anapolitamka neno hili la Tawhidi "Laa ilaaha illa Llah" na maana yake ni "Hapana anayepasa kuabudiwa isipokuwa Allah", anatakiwa alifahamu na kulielewa vizuri, na afahamu pia juu ya kila kinachoambatana na kauli hii.

Anatakiwa alisimamishe na kulisimamia vizuri katika maisha yake, katika watu wa nyumba yake na baina ya Waislamu wenzake.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Sema; Hakika Swala yangu, na Ibada zangu na uzima wangu na kufa kwangu (zote) ni kwa Mwenyezi Mungu Muumba wa walimwengu wote."

Al An am - 162.

Anasema Ibni Kathiyr:

"Imepokelewa kutoka kwa Al Hafidh Abi Yaala, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alisema:

"Zidisheni kuitamka kauli ya Laa ilaaha illa Llah na kuomba Maghufira, maana Ibilisi amesema: 'Kwa hakika nimewaangamiza watu kwa madhambi, na wao wameniangamiza kwa kuitamka kauli ya "Laa ilaaha illa Llah" na nilipowaona katika hali hiyo, basi nikawaangamiza kwa kuwaacha wafuate matamanio, na wao wanapofuata matamanio wanajiona kuwa wameongoka".

Laa ilaha illa Llahu Ya Rabi Mola Wadudi

Laa ilaha illa Llahu Mkwasi ulo Faridi

Laa ilaha illa Llahu Idumishe tawhidi

Iwe twa'a kwa Allahu Pekeo tukuhimidi

 

3- Kumtaja (kumkumbuka) Mwenyezi Mungu (Dhikr)

Mwenyezi Mungu anasema:

.

"Na nikumbukeni (Nami) nitakukumbukeni na nishukuruni wala msinikufuru."

Al Baqarah - 152

Anasema Ibni Kathiyr katika kuifasiri aya hii kuwa Hassan Al Basry amesema:

"Nikumbukeni nami nitakukumbukeni; "Maana yake "Nikumbukeni katika yale niliyokufaridhishieni na mimi nitakukumbukeni katika yale niliyojifaridhisha juu yenu."

Na katika hadithi ya Al Qudusy iliyopokelewa na Bukhari na Imam Ahmad bin Hanbal anasema Mtume wa Mwenyezi (Mungu Swalla Llahu alayhi wa sallam):

"Mwenyezi Mungu anasema: 'Ewe Mwanadamu ukinitaja katika nafsi yako na Mimi nitakutaja katika nafsi yangu, na ukinitaja mbele ya watu na Mimi nitakutaja mbele ya Malaika wengi, na ukijikurubisha kwangu kipimo cha shubiri na Mimi nitakukaribia dhiraa, na ukinikaribia dhiraa, na Mimi nitakukaribia pima, na ukinijia ukiwa unakwenda (mwendo wa kawaida) na Mimi nitakukimbilia".

 

Kumtaja Mwenyezi Mungu ni dalili ya kumpenda Subhanahu wa Taala na kumtaka awe pamoja nawe. Maulamaa wanasema: "Ikiwa Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja nawe, nani atakayethubutu kuwa dhidi yako?"

 

Tofauti iliyopo baina ya aliyeamini kikweli na mnafiki ni kumtaja Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema juu ya wanafiki:

"Wanafiki hutaka kumdanganya (hata) Mwenyezi Mungu. Naye atawaadhibu kwa sababu ya kudanganya kwao (huko). Na wanaposimama kusali husimama kwa uvivu. Wanaonyesha watu (kuwa wanasali) wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo."

Annisaa - 142

Ama juu ya walioamini, Mwenyezi Mungu anasema:

"Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na watiifu wanaume na watiifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wenye subira wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanaofunga wanaume na wanawake, na wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa."

Al Ahzab - 35

Alipoulizwa Sheikh Shaarawi juu ya siri iliyomfanya awe anapendwa sana na watu, alijibu:

"Dhikru llaah" - Kumtaja Mwenyezi Mungu kila wakati."

 

Maulamaa wameugawa utajo wa Mwenyezi Mungu katika sehemu tano:

1- Kumtaja Mwenyezi Mungu pale unapolazimika kumtaja

Kwa mfano katika kuitikia adhana tunapoisikia, takbira ndani ya Sala, kupiga Bismillah kabla ya kula, kumshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kila neema nk.

 

2- Kumtaja Mwenyezi Mungu unapoiona batili

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na ambao wanapofanya uchafu au kudhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha kwa dhambi zao. Na ni nani anyeghufiria madhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu? Na hawaendelei na (na maovu) waliyoyafanya hali wanajua".

Aali Imran 135

Anasema Anas (Radhiya Llahu anhu):

"Nimeambiwa kuwa; Ilipoteremka aya hii Ibilisi alilia."

Na maana ya kauli yake Subhanahu wa Taala:

"Humkumbuka Mwenyezi Mungu," ni kuukumbuka utukufu Wake na kumuomba maghfira na hapo hapo husamehewa.

Anasema Sayiduna Aly bin Abi Talib (Radhiya Llahu anhu):

"Amenihadithia Abubakar kwamba amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Mungu Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisema:

"Mtu anapofanya dhambi kisha akatawadha vizuri na kusali rakaa mbili na kuomba maghfira, Mwenyezi Mungu Humghufiria".

Imepokelewa na Imam Ahmad na Maimam wa Sunnah.

 

3- Kumtaja Mwenyezi Mungu katika nyakati maalum au kwa sababu maalum

Kwa mfano mtu anapoamka akasema:

( ).

'Alhamdu lillahi lladhi ahyaana baada ma amaatanaa wa ilayhi nnushuur.'

 

Au mtu anapoingia chooni akasema:

"Allahumma inniy audhu bika minal khubuthi wa l khabaith."

 

Au anapotoka nyumbani akasema:

"Bismillah, tawakkaltu ala Llah."

 

Utajo wa Mwenyezi Mungu ndani ya Sala, unapotoka msikitini, unapoingia nyumbani, unapokula nk.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na umtukuze Mola wako pamoja na kumsifu kabla halijatoka jua na kabla halijatua, na nyakati za usiku pia umtukuze, na katikati ya mchana ili upate ya kukuridhisha (siku ya Kiama)."

Ta ha- 30.

 

4- Kumtaja Mwenyezi Mungu kwa idadi maalum

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema: "Atakayesema kila siku mara 100;

"La Ilaaha Illa Llah Wahdahu La Sharika Lahu Lahu Lmulk Wa Lahu L- Hamdu Wahuwa alaa Kulli Shay'in Qadiyr."

Anakuwa mfano wa aliyeacha huru watumwa 10 na akaandikiwa thawabu 100 na kughufuriwa madhambi 100 na inakuwa kinga kwake na shetani, na hatokuja na lililo bora kuliko hilo isipokuwa mtu aliyesema kama alivyosema kisha akazidisha."

 

Kumdhukuru Mwenyezi Mungu kwa hesabu baada ya Sala unaposoma:

Subhaana llah mara 33

Alhamdulillah mara 33

Allahu Akbar mara 33

 

Dhikri kama hizi zinatakiwa lazima ziwe kwa hesabu zilizotolewa amri juu yake.

 

5- Dhikri Mutlaq, na maana yake ni Kumtaja wakati wowote na mahali popote na katika mazingara yoyote

Muislamu anatakiwa ulimi wake uwe laini katika kumtaja Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala wakati wote na mahali popote sipokuwa chooni ambapo unaweza kumtaja moyoni mwako ukitaka.

 

Tunatakiwa kila wakati tuwe tukimsabih kwa kusema: 'Subhaana Llah'

Imepokelewa na Attirmidhy, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) siku ya Miraji aliambiwa:

'Mchanga wa Peponi ni mzuri, na maji yake ni mazuri, na Pepo ni kubwa sana na mbegu zake (za miti ya Peponi) ni;

"Subhaana Llah wal Hamdulillah wa Laailaha illa Llah wa Llaahu Akbar".

Ukiwa u mahamumu au hata u bukheri

Jina Lake Muadhamu litaje na kukariri

Litakukinga na ghamu na dhiki hata na shari

Jina la Mola Karimu funguo la kila kheri

Kuwalingania watu

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye (viumbe) kwa Mwenyezi Mungu, na (mwenyewe) akafanya vitendo vizuri na husema (kwa maneno yake na vitendo vyake): "Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu."

Fussilat - 33.

Mwenyezi Mungu katika aya hii anauliza kwa maana ya kutuhakikishia. Kwa kusema: 'Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye (viumbe) kwa Mwenyezi Mungu.?' Akikusudia kutuhakikishia kuwa hapana kauli bora kupita hiyo ya kuwaita watu katika njia Yake Subhaanahu wa Taala., huku akitutaka tuambatanishe kuita huko na matendo yanayolingana nayo.

Katika kuifasiri aya hii anasema Ibn Kathir ambaye ni mwanachuoni na mfasiri maarufu wa Qurani tukufu:

"Bibi Ayesha (Radhiya Llahu anha) amesema: 'Hao (waitaji) ni Waadhini wanaposema "Hayya ala Swalaa", huwa wanawaita watu kwa Mwenyezi Mungu'. Akaendelea Ibn Kathiir: "Lakini si waadhini peke yao wanaowaita watu, bali kila anayeamrisha mema na kukataza mabaya yumo katika waitaji".

 

Katika hadithi sahihi, imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Atakayewaita watu katika uongofu atapata thawabu za kila aliyemfuata bila ya kupungua cho chote katika thawabu zao. Na atakayewaita watu katika upotofu (upotevu) atapata dhambi za kila aliyemfuata bila kupungua cho chote katika dhambi zao."

Muslim

Ndugu zangu Waislam, manufaa ya kuwaita watu katika njia ya Mwenyezi Mungu ni ya milele. Faida yake ni yenye kuendelea. Mti wake haukauki wala hausiti kutoa matunda. Kila anapoingiza thawabu yule uliyemuokoa, na kwako inaingia idadi ile ile ya thawabu bila ya yeye kupunguziwa.

Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako Mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake.

Na kama huyo uliyemungoza ataweza kumuongoza mwingine, basi hesabu itaendelea kuongezeka, na kila mtu huyo anapotenda mema, nyote kwa pamoja mnapata fungu lenu bila kupungua katika thawabu za mmojawapo.

Neema iliyoje na biashara njema iliyoje ambayo wengi wanajiepusha nayo.

 

Fardhi kifaya

Kuwaita watu katika njia ya Mwenyezi Mungu ni 'Fardhi kifaya', na maana yake ni; "Fardhi inayotosheleza". Iwapo litatokea kundi miongoni mwa Waislamu watakaoitekeleza fardhi hii, waliobaki watasamehewa. Na kama watu wote wataiacha, basi wote watapata madhambi.

 

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri (Uislamu) na wanaoamrisha mema na wakakataza maovu. Na hao ndio wataotengenekewa."

Al Imraan - 104.

Na maana ya 'kulingania kheri' ni kuwalingania watu katika kufuata mafundisho ya Qurani tukufu pamoja na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam).

 

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Kheri yote ipo katika kufuata Qurani na mafundisho yangu".

Ibn Mardaweya

Na katika hadithi iliyopokelewa na Iman Ahmad na Attirmidhiy na Ibn Majah, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake; mtaamrisha mema na mtakataza maovu, ama sivyo Mwenyezi Mungu hivi karibuni atakuleteeni adhabu itokayo kwake, kisha mtakuja kumuomba na asikukubalieni."

Mojawapo ya sababu kubwa ya kupatwa na masaibu tuliyonayo umma huu hata makafiri wakaweza kutudhalilisha, ni kuiacha kazi hii tukufu.
Mwenyezi Mungu ameweka masharti maalum ambayo tukiyafuata atazikubali dua zetu.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao.."

Al Raad - 11.

Na Katika hadithi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Ikiwa watu katika kijiji au katika nyumba wataendelea kuwemo katika kumtii Mola wao kisha wabadilike na kuanza kuwa watu wanaoasi, basi Mwenyezi Mungu atawabadilishia kile wanachokipenda wawe wanakichukia".

Imenyanyuliwa na Ibn Abi Hatim na Ibn Abi Sheyba.


Ndugu zangu Waislam, wakati bado upo wa kuzibadilisha hali zetu. Muda bado tunao wa kuyaondoa masaibu. Kila mmoja wetu aianze kazi hii nyumbani kwake leo kabla ya kesho. Kila nyumba iwe mfano wa tufali lenye kuunganisha tufali jingine kwa ajili ya kuisimamaisha nyumba kubwa ya Kiislam.

Swala tuzisali misikitini. Tunapokwenda tuwachukue na watoto wetu. Tuwahimize kusoma Qurani. Tufuatilie kujua habari zao za skuli na juu ya sahibu zao wa mitaani. Kwani mtu na sahibu yake. Tusiwaache hivi hivi tu wakawindwa kwa urahisi na mashetani wa kila aina walioenea kila mahali kuanzia katika mitandao ya internet, ndani ya television na katika kila kichochoro.

Masuali yetu yawe: "Unakwenda wapi, umetoka wapi, umesali Sala ya asubuhi leo au adhuhuri nk. umesoma sura ngapi za Qurani leo au hata aya ngapi?" Nk.

Ndugu zangu Waislam, ikiwa hatukujitahidi wenyewe hapana atakayetusaidia. Sisi ndio wenye uchungu wa watoto wetu.

Hata wake zetu wanazichelewesha Sala na kuzisali kwa pamoja au kuzikurubisha. (hii ikiwa wanaume nao wanasali kama inavyotakiwa).

 

Tuache tabia ya kukaa chini ya TV kutwa kucha tukifuatilia vipindi baada ya vipindi.

Tutawezaje kuzibadilisha hali zetu ikiwa majumbani mwetu Mwenyezi Mungu hatajwi isipokuwa kwa nadra? Na mazungumzo makubwa majumbani na mabarazani ni kusengenyana (kusemana) Waislamu wenyewe kwa wenyewe?

Tutawezaje kuzibadilisha hali zetu ikiwa tunavaa kila tunacholetewa na mafundi wa ushoni ulimwenguni, hata kama mavazi hayo yanakwenda kinyume na mafundisho ya dini?

Tutawezaje kuzibadilisha hali zetu ikiwa ndugu wa nasaba hawakamatani wala hata hawaendeani? Bali ndugu anakuwa na shida au dhiki na hapati katika ndugu zake wenye kumsaidia au kumpunguzia dhiki zake?

Tutawezaje kuzibadilisha hali zetu wakati Waislamu hawataki kujifunza dini yao? Wengi wetu tukiulizwa juu ya jambo la kidunia tunajibu haraka pamoja na kusherehesha kwa dalili mbali mbali, na majumbani mwetu yamejaa kila aina ya mabuku. Hii ni dalili nzuri ya kupenda elimu. Lakini ingelikuwa vizuri kama na mabuku ya dini pia yangepewa nafasi katika rafu za majumba yetu na kusomwa pia.

Mwenyezi Mungu hampendi mwenye kujifunza mambo ya kidunia tu asijifunze na ya akhera yake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenyezi Mungu anamchukia kila mjeuri kupindukia. Mpiga kelele masokoni na mwenye kulala usiku mfano wa maiti na mchana anahangaika kama punda. Na (anamchukia) mjuzi katika mambo ya kidunia mjinga katika mambo ya Akhera".

Imepokelewa na kusahihishwa na Ibn Hibban na Al Bayhaqi.

 

Nyumba ya kiislamu ni nyumba ya ibada, siyo ya kumuasi Mwenyezi Mungu.

Muislamu anatakiwa awe anawaita watu katika kheri na isiwe kinyume cha hivyo. Na jukumu hili si la Maulamaa peke yao, bali ni la kila Mwislamu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Nifikishieni ujumbe wangu japo kwa aya moja."

Bukhari.

Tujaribu kuhifadhi baadhi ya sura au hata aya za Qurani tukufu na pia baadhi ya hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam). Tusome juu ya sira ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na sira ya Watu wa nyumba yake na Masahaba wake (Radhiyallahu anhum jamiy'an). Tujifunze baadhi ya hukmu za Fiq-hi. Tununuwe vitabu vya dini na kuvifungua na kuvisoma.

Ulinganiaji uanze nyumbani kwa wake zetu, watoto wetu na walio karibu nasi. Ikiwa hutowaita katika njia ya kheri, tutamuachia nani atufanyie kazi hiyo? Huko nje kumejaa mashetani watakaowaita katika njia za shari ambazo kwa wakati huu zimejaa tele.

Tusipoanza kuitimiza fardhi hii tutaingia katika hatari kubwa zaidi ya kukosa radhi zake Subhaanahu wa Taala na kupata ghadhabu zake.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Walilaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israili kwa ulimi wa Daudi na wa Issa bin Maryam. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakapindukia mipaka.

Hawakuwa wenye kuzuwiana (kukatazana) mambo mabaya waliyokuwa wakiyafanya. Uovu ulioje wa jambo hilo waliokuwa wakilifanya."

Al Maida - 78-79.

Katika kuifasiri aya hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Katika maasi ya mwanzo yaliyofanywa na wana wa Israili ni kuwa mmoja wao anapokutana na mwenzake alikuwa akimuambia: "Ewe mwenzangu muogope Mwenyezi Mungu acha kumuasi, si halali kwako kutenda hayo. Kisha siku ifuatayo anapokutana naye akiwa katika hali ile ile ya kumuasi Mwenyezi Mungu huwa haoni vibaya kula, kunywa na kukaa pamoja naye. Kwa kufanya kwao hivyo Mwenyezi Mungu akazipiganisha nyoyo zao".

Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akasema:

"Sivyo Wallahi! Lazima muamrishe mema na mukataze maovu na mumuonyeshe dhalimu njia ya haki ama sivyo Mwenyezi Mungu atazipiganisha nyoyo zenu na atakulaanini kama alivyowalani."

Abu Daud. 

Kupatanisha watu

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema:

.

"Hakuna kheri katika mengi wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa (mashauri ya) wale wanaoamrisha kutoa sadaka au kufanya mema au kupatanisha baina ya watu. Na atakayefanya hivi kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutampa ujira mkubwa."

Annisaa -114

Waislamu ni mfano wa ukoo mkubwa ambao unapotokea mzozo wowote baina yao, wale wenye hekima na utambuzi huingilia na kupatanisha.

Kupatanisha wanaogombana na wasiosikilizana ndio mwenendo wa Waislamu tokea hapo zamani, na sio kugombanisha au kuchochea panapotokea ugomvi na kutokuelewana.

 

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) ametufahamisha katika hadithi nyingi juu ya umuhimu wa kupatanisha watu, na pia juu ya ghadhabu za Mwenyezi Mungu zinazowafikia wenye kuchochea ugomvi baina ya watu.

Kwa vile kugombanisha watu siyo maudhui yetu hapa, kwa hivyo tutaisoma hadithi moja tu katika maudhui hayo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Haingii Peponi Nam-maam".

Nam-maam, ni mwenye kupenda kusikiliza habari za huku na kuzipeleka kule kwa nia ya kugombanisha. Na kwa mujibu wa hadithi hii mtu wa aina hii hatoingia Peponi.

Katika aya niliyotangulia kuitaja, Mwenyezi Mungu anatujulisha kuwa; mengi ya maneno yanayozungumzwa mabarazani, mikutanoni au majumbani, huwa hayana maana isipokuwa yafuatayo, nayo ni:-

a - Kutoa sadaka (kwa ajili ya kusaidia masikini na wenye shida)

b - Kufanya mema (kila analolipenda Mwenyezi Mungu na kuridhika nalo)

c - Kupatanisha baina ya watu.

Kisha Mwenyezi Mungu akaikamilisha aya kwa kusema:

"Na atakayefanya hivi kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutampa ujira mkubwa".

Na hii ni kwa sababu kitendo chochote kile ili kikubaliwe na ili upatikane ujira wake, lazima kiwe halisi kwa ajili ya kutaka radhi zake Subhanahu wa Taala, na lisiwe kwa ajili ya kutaka kusifiwa na watu. Kwa sababu atakayetenda jambo akitarajia kusifiwa na watu, basi Mwenyezi Mungu humsukumia amali yake hiyo huko huko alikotegemea ujira wake.

 

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Maneno yote ya mwanadamu ni dhidi yake isipokuwa Kumtaja Mwenyezi Mungu au kuamrisha mema au kukataza maovu".

Imepokelewa na Ibn Mardaweya na kusimuliwa na Um Habiyba.

 

Na katika hadithi iliyopokelewa na Imam Ahmad bin Hanbal, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Je! Nikujulisheni juu ya daraja iliyo bora kuliko (ibada ya) Funga na Sala na (kutoa) Sadaka?

Masahaba wakasema: "Tujulishe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu",

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akasema: "Kupatanisha watu, kwa sababu kugombanisha watu ndiko kunakonyoa". (kunainyoa dini)

Imepokelwea na Abu Daud na Attirmidhiy.

 

Nguvu ya Waislamu inadhoofika na kupungua, na mifarakano inatokea pale watu wanapoanza kusengenyana, kugombana na kuhitalifiana,

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane (msigombane), msije mkaharibikiwa na kupotea nguvu zenu, na vumilieni (mstahamiliane). Bila shaka Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaovumilia."

Al Anfal- 46

Masahaba (Radhiya Llahu anhum) waliifuata amri hii, wakafanikiwa kuueneza Uislamu katika pembe zote za ulimwengu.

Anasema Imam Malik (Radhiya Llahu anhu):

"Hautofanikiwa Umma huu ikiwa hawatofuata waliyofanya waliokuja kabla yao".

 

Imepokelewa kuwa jambo la mwanzo alilofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alipowasili Madina lilikuwa ni ni kuyapatanisha makabila mawili makubwa ya hapo Al Awus na Al Khazraj, na pia kuwafunga undugu watu wa Makka na wa Madina.

Alimchagulia kila mtu wa Makka ndugu yake katika watu wa Madina ili Waislamu wawe kitu kimoja, nguvu moja na ili waweze kuyakabili matatizo yao wakiwa kama ukoo moja mkubwa. Na matokeo yake wakawa wakipendeleana kuliko nafsi zao.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na (pia wapewe) wale waliofanya maskani yao hapa (yaani Madina) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya (kuja) hao (Muhajiri huko Madina) na wakawapenda hao waliohamia kwao, wala hawapati, hawaoni dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa (hao Muhajiri), na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo. Na waepushwao na ubakhili wa nafsi zao hao ndio wenye kufaulu kweli kweli."

Al-Hashr 9

Imepokelewa kuwa baada ya kumalizika vita vya Yarmuk mtu mmoja alimuendea bin ammi yake aliyekuwa amelala baina ya uhai na umauti pamoja na waliojeruhiwa katika vita hivyo. Alipomuona akamsogezea kiriba cha maji mdomoni mwake na kumuambia: "Kunywa". Lakini bin ammi yake yule alipotaka kunywa akasikia sauti karibu yake ikilia: "Aah Aah". Akamuambia mwenye maji: "Bora mpe mwenzangu huyu, maana yeye anaonyesha hali yake taabani zaidi kuliko mimi". Alipotaka kumpa maji yule mtu mwengine akasikia sauti ya aliye karibu yake ikilia: "Aah Aah", na yule mtu mwengine naye pia akamuambia: "Bora mpe mwenzangu huyu maana anaonyesha ana shida zaidi kuliko mimi". Hivyo hivyo aliendelea kila anapotaka kumpa maji mmoja anamuomba ampe aliye karibu naye, na alipomrudia yule wa kabla yake akamkuta kesha kufa, na alipomrudia wa pili akamkuta kesha kufa na alipomrudia bin Ammi yake akamkuta naye pia kesha kufa.

Wanapendeleana mpaka mauti (Radhia Llahu anhum).

 

Imepokelewa pia kuwa siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) ilibidi aikose swala ya jamaa na badala yake Abubakar (Radhiya Llahu anhu) alisalisha, kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikwenda kupatanisha ukoo wa Amru bin Auf (Radhiya Llahu anhu).

Bukhari na Muslim

 

Mwenyezi Mungu anasema:

"..Basi Muogopeni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni katika wanoamini (kweli)."

Al Anfal -1

Katika hadithi iliyosimuliwa na Abu Yaala Al Mousali, anasema Anas bin Malik (Radhiya Llahu anhu).

"Tulikuwa tumekaa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), kisha ghafla akacheka mpaka yakaanza kuonekana magego yake. Umar (Radhiya Llahu anhu) akamuuliza: 'Kipi kilichokuchekesha ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?'

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akasema:

"(Siku ya Kiyama) Watu wawili watagombana mbele ya Mwenyezi Mungu, mmoja wao atasema: 'Mola wangu nidaie haki yangu kutoka kwa mwenzangu huyu", Mwenyezi Mungu atasema: "Mlipe ndugu yako haki yake uliyomdhulumu". Mja atasema: "Mola wangu, thawabu zangu zote zimemalizika sina cha kumlipa'. Yule mja mwenye kudai atasema: "Basi na abebe dhambi zangu".

Anas (Radhiya Llahu anhu) akasema: "Machozi yakaanza kumlenga Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) huku akilia. Kisha akasema: "Hiyo ni siku kubwa sana. Siku ambayo kila mtu atamtafuta wa kumbebea madhambi yake. Kisha Mwenyezi Mungu atamuambia mwenye kudai: "Nyanyua macho yako uangalie Peponi". Atanyanyua na kusema: "Mola wangu naona miji iliyotengenezwa kwa fedha na maqasri yaliyojengwa kwa dhahabu na kupambwa kwa lulu, ni ya Mtume gani haya? Ya Msemakweli gani haya? Ya Shahidi gani haya?" Mwenyezi Mungu atasema: "Ni ya yule atakaelipa thamani yake." Yule mtu atauliza: "Ni nani huyo anaemiliki thamani yake?", Mwenyezi Mungu atajibu: "Wewe ndie mwenye kuimiliki." Yule mtu atauliza: "Nini thamani yake?" Mwenyezi Mungu atasema: "Ni kumsamehe ndugu yako huyu." Yule mtu atasema: "Nimekwisha msamehe Ewe Mola wangu." Na Mwenyezi Mungu atasema: "Shikaneni mikono muingie Peponi pamoja."

Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) akasema:

"Mcheni Mwenyezi Mungu na mpatanishe baina ya watu kwani Mwenyezi Mungu atapatanisha baina yenu siku ya Kiama.''

Istighfar

Mwenyezi Mungu anasema:

.

"Sema (uwaulize): 'Ni vya nani vilivyomo mbinguni na ardhini?' Useme (tena kujibu) 'Ni vya Mwenyezi Mungu'.Yeye amejilazimisha kuwafanyia rehma waja wake."

An-Am - 12

Katika kuisherehesha aya hii, anasema Ibn Kathiyr:

"Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi na kila kilichokuwemo ndani yake. Mwenye uwezo wa kufanya atakalo juu ya waja wake, lakini juu ya yote hayo amejilazimisha mwenyewe kuwarehemu waja wake."

Na katika hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim na kusimuliwa na Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu), anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam):

"Mwenyezi Mungu baada ya kuwaumba viumbe, aliandika juu ya Arshi Yake: Hakika huruma Yangu imezishinda ghadhabu Zangu."

Mwenyezi Mungu hawadhulumu waja wake, lakini watu ndio wenye kujidhulumu nafsi zao, na uadilifu haupatikani ikiwa mwenye kufanya maasi na mwenye kutii wote watalipwa sawa sawa.

Kila mwenye akili timamu anatambua kuwa mtu dhalimu lazima ahukumiwe na kutiwa adabu, ama sivyo dhulma na ufisadi vitaenea ulimwenguni, na Mwenyezi Mungu ambaye ni Muadilifu hatowafanya watu waasi na watiifu wote wawe sawa mbele Yake bila ya kuwaadhibu madhalimu na kuwalipa mema wanaomtii.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Je! Wanafikiri wale waliofanya maovu kuwa tutawafanya kama wale walioamini na kutenda mema - kwamba maisha yao na mauti yao yawe sawa? Ni hukumu mbaya wanayoihukumu.

Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na ili kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma; na wala hawatadhulumiwa".

Al - Jaathiyah -21-22

 

Pamoja na hayo Mwenyezi Mungu ameufungua mlango ambao aliyedhulumu au aliyejidhulumu nafsi yake anaweza kupita wakati wowote anapotaka, sharti usiwe wakati wa kukata roho. Mwenyezi Mungu anautandaza mkono Wake wakati wa mchana kwa ajili ya kuwasamehe wanaotenda madhambi usiku na anautandaza mkono Wake wakati wa usiku kwa ajili ya kuwasamehe watendao madhambi mchana.

Na katika hadith Al-Qudsy, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenyezi Mungu anasema: 'Ewe mwanadamu utakapoomba maghfira nitakusamehe madhambi yote uliyonayo bila kujali. Ewe mwanadamu madhambi yako hata yawe yenye kufika mawinguni lakini utakaponiomba maghfira nitakusamehe bila ya kujali. Ewe mwanadamu ukinijia na madhambi yenye kuijaza ardhi yote, ikiwa hujanishirikisha na cho chote nitakupa maghfira kiasi cha kuijaza ardhi yote".

Attirmidhy

Na katika Surat Az-Zumar aya ya 53 Mwenyezi Mungu akasema:

"Sema, 'Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; bila shaka Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu".

 

Watu wema waliotangulia walikuwa mwingi katika wakati wao wa usiku wakiswali, na kabla ya kuingia alfajiri walikuwa wakiomba maghfira.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Walikuwa wakilala kidogo tu usiku .Na wakiomba maghfira nyakati za alfajiri".

Adhariyaat 17-18

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) ametuamrisha kuomba maghfira. Kusema 'Astaghfirullah' mara tatu baada ya kumaliza kila Swala. Hii ni baada ya kufanya ibada ambayo ni kitendo cha utiifu. Na hii ina mana kuwa tunatakiwa kuomba maghfira zaidi baada ya kufanya kitendo cha kuasi. Bali maulamaa wanasema kuwa; mwanadamu anapaswa kuomba maghfira kwa kila kitendo cha maasi.

Istighfar ni 'Neno la haki'. Mfano wake ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako Mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi, na ni neno ambalo Muislamu anatakiwa wakati wote liwe kinywani mwake akilitamka.

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) alikuwa akiomba maghfira kila siku zaidi ya mara mia.

 

Sheikh Mohammad Ghazali katika kitabu chake kiitwacho 'Jaddid Hayatak' anasema:

"Kila jambo muhimu lenye faida au hasara huwekewa mabuku ya kudhibiti hesabu zake, ili ijulikane faida na hasara zake. Ili ijulikane ngapi zimetoka na ngapi zimeingia. Nani kachukua na nani kaingiza nk.

Juu ya kuwa maisha ya mwanadamu na mustaqbal wake wa huko anakoelekea ni muhimu zaidi kupita mambo haya ya kidunia, lakini utamuona anayaacha matendo yake yaende ovyo bila ya kuyadhibiti wala kujihesabia.

Yupo kati yetu aliyefikiria kuchukua daftari na kujifanyia hesabu ya kila alilotenda katika mabaya na kila aliloacha katika mema ili kila wakati aweze kujua amefanya mangapi katika mambo ya shari na kuomba maghfira kwa Mola wake?"

Kusingekuwa na tatizo lau kama tungeachiliwa tufanye tutakavyo hapa duniani bila kudhibitiwa wala kuhesabiwa kheri wala shari. Kusingekuwa na tatizo lolote kwa mtu kuyapoteza maisha yake ovyo mfano wa mjinga anayetupa mali yake huku na kule.

Lakini Mwenyezi Mungu ametuwekea Malaika wenye kuhesabu kila neno na kila tendo. Malaika wasioacha hata kitendo chenye uzito wa punje ndogo isipokuwa wataliingiza katika daftari lao. Malaika wenye kutayarisha madaftari yenye hesabu ndefu sana."

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na madaftari yatawekwa (mbele yao). Utawaona wabaya wanavyoogopa kwa sababu ya yale yaliyomo (madaftarini) na watasema: "Ole wetu! Eee kuangamia kwetu leo! Namna gani madaftari haya! Haliachi dogo wala kubwa ila yamelidhibiti (yameliandika). "Na watakuta yote yale waliyoyafanya yamehudhuria hapo; na Mola wako hamdhulmu yoyote."

Al Kahf - 49

 

Ndugu zangu Waislam, lazima tujifanyie hesabu kabla ya kuhesabiwa, na lazima tuvipime vitendo vyetu kabla ya kupimiwa, kwani siku hiyo hesabu yake ni nzito sana.

Imesimuliwa na Ibnul Qayyim katika baadhi ya vitabu vyake kuwa; baadhi ya watu wema waliotangulia walikuwa wakichimba makaburi ndani ya nyumba zao na kuingia humo baadhi ya wakati katika nyakati za usiku wakiwa na madaftari yao na kujihesabia yale waliyotenda siku hiyo huku wakimuomba maghfira Mola wao ambaye hapana mwenye kusamehe madhambi isipokuwa Yeye Subhanahu wa Taala.

 

"Yachunge mabaya yako," amesema Abdillahi bin Masaood (Radhiya Llahu anhu), "nami natoa ahadi kuwa Mola wako hatokupotezea mema yako".

Na katika hadithi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Jifanyieni hesabu nafsi zenu kabla hamjahesabiwa, na pimeni amali zenu kabla hamjapimiwa."

Attirmidhy

Na akasema:

"Atakayejishughulisna na Istighfar, Mwenyezi Mungu atamfarijia shida zake na atamuondolea dhiki zake na atamruzuku kupitia njia asiyoitegemea".

Na akasema:

"Enyi watu, tubuni kwa Mola wenu na muombeni maghufira kwani mimi ninatubu kwake kila siku mara mia".

Bukhari

 

Kila mwanadamu ni mtenda madhambi, na mbora wao ni mwenye kutubu na kurudi kwa Mola wake.

Imepokelewa kuwa siku moja mtu aliingia katika majlis ya Hassan Al Basry (Radhiya Llahu anhu) akamuuliza:

"Mvua haijatunyeshea muda mrefu na majani yameanza kukauka. Tufanye nini?"

Al Hassan akasema:

"Ombeni maghfira kwa Mola wenu".

Mwingine akaingia kwenye majlis hiyo hiyo akasema:

"Umasikini umezidi na shida zimekuwa nyingi kwetu ewe Al Hassan".

Al Hassan akasema:

"Ombeni maghfira kwa Mola wenu"

Wa tatu akaingia akasema:

"Sijapata mtoto mpaka sasa ewe al Hassan. Nifanyeje?"

Al Hassan akamuambia:

"Omba maghfira kwa Mola wako."

Watu wakashangazwa na majibu hayo, wakamuuliza:

"Sheikh, watu hawa wamekuuliza juu ya masaala mbali mbali na wewe umewapa wote dawa moja tu, nayo ni Istighfar?"

Al Hassan akawaambia:

"Kweni hamkuisoma kauli ya Mola wenu katika Surat Nuh aliposema:

'Nikawaambia: Ombeni msamaha kwa Mola wenu. Hakika yeye ni Mwingi wa msamaha. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi. Na atakupeni mali na watoto, na atakupeni mabustani, na atakufanyieni mito?"

Masharti ya Toba

Mwenyezi Mungu anasema:

 

.

"Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu."

Az Zumar - 53

Hii ni rehema kubwa iliyojumuisha msamaha wa madhambi yote. Hata yawe makubwa namna gani.

Huu ni mwito kutoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi kwa wote wenye kumuasi Mola wao, na wale waliozama na kufurutu mpaka katika maasi hata wakakata tamaa kuwa hawatoweza tena kusamehewa. Huu ni mwito kutoka kwa Muumba wa kila kitu, Mwenye kuzijua vizuri nafsi za viumbe. Mwenye kujua kuwa shetani amemkalia mja wake katika kila njia, na kwamba shetani huyo anao uwezo wa kumshinda nguvu mja masikini kwa kujipenyeza kupitia sehemu za udhaifu wake akamchezea na kumtelezesha, hasa pale mja anapoiacha kamba ya Mwenyezi Mungu akaishikilia kamba ya dunia.

Mwenyezi Mungu kwa kuuelewa vizuri udhaifu wa mja Wake, anamnyoshea mkono wa msaada na rehma, ili asikate tamaa baada ya kuzama akadhani kuwa hapana tena tumaini.

Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote.

Ewe Mola mwingi wa kusamehe,

Niruzuku ghufurani Niepushe na maasi

Nakuomba ya Manani Dhamiri inanighasi

Naungua kifuani Kama moto wa nuhasi

Rabbi nighufurie Ewe Ghafuru Rahimu

 

Kheri ukinishushia Nasahau kwa wepesi

Mitihani yanijia Mimi nazidisha kasi

Wewe wanichukulia Miye nazidi kuasi

Rabbi nighufurie Ewe Ghafuru Rahimu

 

Maulamaa wanasema kuwa toba zipo aina mbili;

1.            Toba ya mtu aliyetenda dhambi baina yake na Mola wake.

2.            Toba ya dhambi yenye uhusiano na mwanadamu mwengine.

 

Mtu anapotenda dhambi baina yake na Mola wake, na dhambi hiyo ikawa haina uhusiano na mwanadamu mwengine, basi masharti ya kutubu kwake ni matatu:-

3.            Ayaache maasi hayo

4.            Ajute kwa kuyafanya maasi hayo.

5.            Atie nia ya kutoyarudia tena.

Toba ya kweli haisihi likikosekana mojawapo ya masharti hayo.

 

 

Maulamaa wanasema kuwa inamuwajibikia mtu kutubu kwa kila dhambi aliyotenda na atie nia ya kutoirudia tena.

Mtu anapomuibia mwenzake kitu, kisha akajuta na akaamua kumrudishia mwenyewe kitu chake hicho na kumuomba msamaha, je mtu huyo atakirudisha akiwa na nia ya kukiibia tena?

Bila shaka hatokuwa na nia hiyo. Na hivyo ndivyo ilivyo wakati mtu anapomuasi Mola wake kisha akajuta na akaamua kutubu, bila shaka hatotubu huku akitia nia ya kulirudia tena kosa hilo.

 

Masharti ya kutubia dhambi yenye kuhusiana na haki za mwanadamu mwingne, kama vile kumdhulumu au kumuibia au kumsengenya ni manne

Masharti matatu yaliyotangulia kutajwa, na la nne ni 'kuirudisha haki ya aliyedhulumiwa.'

Ikiwa ni ya kumvunjia heshima au kumsengenya, hapo litaongezeka sharti la kuomba msamaha.

Baadhi ya Maulamaa wanasema kuwa; kwa vile mambo ya kusengenya huenda yakasababisha matatizo mkubwa zaidi pale mtu anapoendewa kuombwa msamaha, basi inatosha badala yake uwe ukimuombea dua mtu huyo kila wakati na ni vizuri zaidi kama kama utakwenda katika vikao ulivyokuwa ukimsengenya ukazungumza juu ya mema yake, huku ukiwajulisha watu kuwa ulikuwa ukikosea pale ulipokuwa ukimsema vibaya.

Maulamaa wanasema kuwa mtu akifanya hivyo huenda Mwenyezi Mungu akamghufiria madhambi yake.

Wengine wakasema kuwa toba sahihi haipatikani mpaka umuendee mtu huyo na kumtaka radhi kwa maovu uliyokuwa ukizungumza juu yake.

 

Kwa mtu aliyemdhulumu mwenzake mali kwa njia ya hiana nk. akaona vigumu kumrudishia mwenyewe haki yake na kumuambia ukweli, basi inatosha ikiwa badala yake atanunuliwa zawadi kiasi cha thamani ya mali yake na kumpa yeye au wanawe kama zawadi bila kumjulisha sababu ya zawadi hiyo.

Na kama haiwezekani kufanya hivyo basi inatosha kuchukuwa thamani ya mali hiyo na kufanya kila hila ili uweze kuifikisha nyumbani kwake na kuiweka mahali popote, na kama hilo pa haliwezekani basi inatosha kuiweka japo ndani ya uwa wa nyumba yake au mahali popote ikiwa pana uhakika wa kumfikia mwenyewe haki yake.

Iwapo hapana njia yo yote ya kumfikishia mdhulumiwa haki yake, kwa mfano mtu huyo amesafiri na anwani yake haijulikani, au amekwisha fariki dunia na haijawezekana kumpata mrithi wake nk. basi thamani ya haki yake inaweza kutolewa sadaka kwa jina lake.

Kumbukeni ndugu zangu kuwa dhambi yoyote baina ya mtu na Mola wake inafutika, lakini baina ya mtu na mwenzake, haifutiki isipokuwa kwa mojawapo ya njia zilizotajwa au zilizo mfano wake.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Yaendeeni upesi upesi maghufira ya Mola wenu na Pepo (Yake) ambayo upana wake (tu) ni (sawa na) mbingu na ardhi, (Pepo) iliyowekewa wamchao Mungu."

Aali Imran - 133

Na katika hadithi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenyezi Mungu hufurahi sana kwa toba ya mja wake kuliko msafiri aliyepanda mnyama kisha mnyama wake akamuangusha na kumkimbia akiwa amebeba chakula chake na maji yake, akakata tamaa ya kumuona mnyama huyo tena, akaenda chini ya mti na kujinyosha chini ya kivuli chake, keshakata tamaa, na alipozindukana akamuona mnyama wake mbele yake na vifaa vyake kamili, kisha akasema kwa furaha (bila kujijua), 'Mola wangu, wewe ni mja wangu na mimi ni mola wako', kwa furaha nyingi akakosea."

Bukhari na Muslim

Kwa vile bado muda unao, na hujui kama muda huo utakuwa nao kwa muda mrefu au mfupi, kwa nini basi hayakimbilii maghfira ya Mola wako kabla haujafika wakati wa kujuta na majuto yasiweze kusaidia kitu?

Mwenyezi Mungu anasema:

"Au ikasema (nafsi); 'Kama Mwenyezi Mungu angeniokoa bila shaka ningekuwa miongoni mwa wenye kumcha Menyezi Mungu.'

Au ikasema ionapo adhabu; 'Kama ningepata marejeo (ya kurejea tena duniani) ningekuwa miongoni mwa wafanyao mema.'

(Ataambiwa); 'Kwa nini! Bila shaka zilikujia Aya zangu ukazikadhibisha na ukajivuna na ukawa miongoni mwa makafiri."

Az Zumar 57-59